Mashahidi wa Yehova Wasaidia Katika Maendeleo ya Upasuaji wa Moyo
DAILY NEWS la New York la Agosti 27, 1995, liliweka katika kichwa kikuu ripoti yao, “Upasuaji Bila Damu.” Lilitaarifu kwamba Kitovu cha Kitiba cha Hospitali ya Cornell ya New York kilikuwa “kifunue njia yenye badiliko kubwa ya kufanya upasuaji wa moyo kwa kuelekeza damu njia nyingine—upasuaji ambao hivi majuzi ulihitajiwa na aliyekuwa hapo awali Meya David Dinkins—bila kupoteza hata tone la damu.”
“Ikichochewa na mahangaiko ya Mashahidi wa Yehova,” hilo gazeti likasema, “ajabu ya hiyo taratibu mpya . . . itaonyeshwa katika kuokoa mamia ya maelfu ya dola kwa hospitali kukiwa na hatari za chini zaidi za ambukizo la damu kwa wagonjwa.” Dakt. Todd Rosengart, mkurugenzi wa programu ya hospitali ya upasuaji bila damu, alisema hivi: “Sasa twaweza kupunguza kiasi cha utiaji-damu mishipani kinachohitajiwa wakati wa upasuaji huu kutoka kile cha kawaida cha kati ya painti mbili na nne hadi sufuri.”
Dakt. Karl Kreiger, mpasuaji wa moyo wa hiyo hospitali, ambaye alisaidia kuanzisha upasuaji huo, alisema hivi: “Kwa kuondoa uhitaji wa damu ya wanaotoa damu na vifanyizo vya damu, twapunguza pia hatari ya homa nyinginezo za baada ya upasuaji na maambukizo yanayohusianishwa kwa ukawaida na utiaji-damu.”
Wataalamu wengine wanasema kwamba “uelekezaji damu njia nyingine bila utumizi wa damu hupunguza wakati unaotumiwa katika utunzaji wa kipekee baada ya upasuaji—kutoka muda wa saa 24 au zaidi hadi muda wa saa sita tu. Wagonjwa walioteuliwa kwa ajili ya upasuaji bila damu waliweza kupata nafuu na kutoka hospitalini muda wa saa 48 mapema zaidi.” Hilo lamaanisha kuokoa fedha nyingi za hospitali nyingi, serikali, na makampuni ya bima. Dakt. Rosengart alikadiria kwamba “upasuaji huu waweza kuokoa angalau dola 1,600 kwa kila mgonjwa.”
Daily News liliendelea hivi:
“Kwa kinyume, huo upasuaji mpya ulichochewa si na uhitaji wa kiuchumi au hata kitiba, bali na juhudi nyingi za kidini. Jamii ya Mashahidi wa Yehova—ambayo itikadi zayo hukataza utiaji-damu—ilikuwa ikitafuta msaada kwa washiriki wazee-wazee wenye kupatwa na maradhi ya moyo. . . .
“Kwa sihi la jamii ya Mashahidi wa Yehova, madaktari waliunganisha ufundi wao wa kuokoa damu kwa madawa mapya. Walipata pia njia mpya ya kutumia mashine ya kidesturi ya moyo na mapafu inayotumiwa kufanya wagonjwa waendelee kuwa hai wakati wa upasuaji wa moyo.
“Kuongezea wagonjwa 40 walio Mashahidi wa Yehova waliokubali uchunguzi wa mwanzoni wa kitiba, miezi sita iliyopita kikundi cha New York-Cornell kilianzisha huo upasuaji kwa wagonjwa wengine kwa ujumla. ‘Tangu wakati huo, wamekamilisha pasuaji 100 mfululizo kwa kuelekeza damu njia nyingine bila kuongeza damu na hakukuwa na vifo vyovyote,’ akasema Krieger. Kiwango cha kifo kwa upasuaji wa kawaida ni asilimia 2.3.”
Ulimwenguni pote hospitali 102 zimeongeza programu za upasuaji bila damu kwa vifaa vyazo, zikifanya taratibu hizi za upasuaji zilizo salama zaidi zipatikane kwa wagonjwa wote kwa ujumla duniani pote.