Upasuaji Bila Damu—Manufaa Yake Yatambuliwa
KATIKA mwaka wa 1996 chuo cha Royal College of Surgeons cha Uingereza kilichapisha kijitabu kinachoitwa Code of Practice for the Surgical Management of Jehovah’s Witnesses. Katika kijitabu hicho madaktari-wapasuaji wasema hivi: “Hatari za upasuaji wa kutumia damu zafanya itakikane kufikiria hatua za badala inapowezekana.”
Gazeti AHA NEWS, linalochapishwa na Shirika la Hospitali la Marekani, pia liliripoti kwa nini manufaa za upasuaji bila damu zimetambuliwa. “Kilichoanza kama itikadi ya kidini kimekuwa uchaguzi wa kitiba na tekinolojia ya hali ya juu,” likasema jarida hilo la kila juma. “Matibabu na upasuaji bila damu, uliochochewa kwa sehemu na mafundisho ya Mashahidi wa Yehova, sasa hautumiki tu kwa mahitaji ya kiroho ya jamii fulani bali unatumika sana kwenye vyumba vya upasuaji katika taifa lote.”
Nyongeza ya chapa ya miezi ya mwisho-mwisho ya 1997 ya gazeti Time ilikuwa na habari iliyokazia kwa nini madaktari wanapendekeza upasuaji bila damu. Makala hiyo ilisema, “Sababu moja pekee ni kuhofu UKIMWI.” Makala hiyo iliripoti hasa kazi inayofanywa katika Hospitali ya Englewood Hospital’s New Jersey Institute for the Advancement of Bloodless Medicine and Surgery, katika Englewood, New Jersey.
Gazeti Time lilisema hivi: “Taasisi hii ndiyo inayoongoza kati ya hospitali zaidi ya 50 katika Marekani ambazo sasa hufanya upasuaji bila damu. Bila kutumia damu yoyote iliyochangwa, zinatoa huduma mbalimbali za upasuaji ambazo kwa kawaida zingehusisha damu, pamoja na mbinu ambazo hupunguza sana, au hukomesha kabisa, kupoteza damu.”
Ni Wenye Matokeo na Salama
Utangulizi wa makala ya gazeti Time ulikazia simulizi la Henry Jackson, ambaye alivuja damu nyingi sana na kupoteza asilimia 90 ya damu yake na hivyo kiwango cha himoglobini yake kikapungua na kufikia hali yenye kuhatarisha ya gramu 1.7 kwa kila desilita. Jackson alipelekwa Englewood Hospital kutoka hospitali nyingine ya New Jersey, ambayo haingemtibu bila kumtia damu.
Akiwa katika hospitali hiyo ya Englewood, akitibiwa na Dakt. Aryeh Shander, Jackson alipewa “dawa zenye nguvu za chuma na vitamini, pamoja na ‘dawa zenye nguvu’ za kuongeza damu, ambazo huchochea uboho utokeze chembe nyekundu za damu. Hatimaye, alipewa umajimaji wenye kupitishwa mishipani ili kuchochea mzunguko mdogo wa damu uliokuwa umebaki.”
Gazeti Time liliripoti kwamba siku chache baadaye, “ile hospitali ya kwanza ilipiga simu ikitaka kujua kama Jackson alikuwa amekufa. Akiwa ameridhika kikweli, Shander aliwaambia, ‘Licha ya kwamba hajafa, ni mzima na yuko tayari kwenda nyumbani, na karibuni atarudia shughuli zake za kawaida.’”
Katika mahojiano ya televisheni mnamo Novemba 28, 1997, Dakt. Edwin Deitch, mkurugenzi wa kitiba wa mradi wa kutotumia damu katika University Hospital, Newark, New Jersey, alieleza namna utafiti wa upasuaji bila damu ulivyositawi: “Mashahidi wa Yehova . . . walifanya jitihada nyingi sana za kutafuta watu ambao wangewafanyia upasuaji bila damu. Baadhi ya matokeo ya uchunguzi huo yalionyesha kwamba walifanikiwa zaidi ya ilivyotarajiwa, [kuliko] watu waliotiwa damu.”
Dakt. Deitch aliongezea hivi: “Damu yaweza kupunguza uwezo wa mfumo wa kinga na kusababisha matatizo ya ambukizo baada ya upasuaji; yaweza kuongeza hatari ya mtu kurudiwa na kansa, kwa hiyo damu, ijapokuwa ilinufaisha katika hali fulani, ina madhara.” Kuhusu upasuaji bila damu, Dakt. Deitch alifikia mkataa huu: “Kwa wazi unaboresha hali ya baadaye ya mgonjwa kukiwa na matatizo machache, na [una] gharama nafuu. Na kwa hiyo, ni wenye manufaa katika hali zote.”
Hivyo, kama lilivyosema gazeti Time, “wagonjwa wengi zaidi na zaidi wanadai njia za badala zilizo salama zaidi na zenye matokeo zaidi kuliko tiba ya kutia damu mishipani.” Pia gazeti hilo liliripoti hivi: “Kulingana na makadirio fulani, asilimia 25 ya visa vya kutiwa damu mishipani katika Marekani si vya lazima. Pia kuna dalili kwamba wagonjwa hawawezi kuvumilia viwango vya juu vya himoglobini kama ilivyofikiriwa hapo awali na kwamba vijana hasa wana akiba ya kiasili ya damu. . . . [Shander] anasadiki kwamba kutotumia damu ni uchaguzi unaowezekana na unaopendelewa na wagonjwa wengi zaidi.”
Kuna hatari nyinginezo licha ya hatari kubwa ya kupatwa na maradhi yanayopitishwa kwa kutiwa damu mishipani. “Baada ya damu iliyohifadhiwa kupoa, haina uwezo sawa na damu ya kawaida katika kusafirisha oksijeni,” akaeleza Dakt. Shander. “Ndipo tu tuanzapo kuelewa kinachotukia hasa tunapomtia mtu damu mishipani.”
“Kiwango cha Kipimo”
“Hatimaye,” Time lilimalizia, “kuna gharama: karibu dola 500 kwa kila kisa cha kutiwa damu mishipani, na kwa kuongezea gharama za ziada, gharama ya jumla inafikia kati ya dola bilioni 1 na bilioni 2 kila mwaka, jambo linalochochea kutafuta matibabu ya badala.” Sasa inaonekana kwamba sababu kubwa inayofanya upasuaji bila damu upendwe ni kwa kuwa upasuaji unaohusisha kutia damu mishipani umekuwa wa gharama ya juu sana.
Sharon Vernon, mkurugenzi wa Kituo cha Matibabu na Upasuaji Bila Damu katika St. Vincent Charity Hospital, Cleveland, Ohio, alisema hivi kuhusu kutibu wagonjwa bila damu: “Utibabu huu unakua kwa sababu matabibu wanatambua kwamba matibabu bila damu ndicho kiwango cha kipimo katika hali ya kupunguza gharama. Tumeona kwamba hata makampuni ya bima ambayo kwa kawaida hayashirikiani nasi kikazi, yanawatuma watu kwetu, kwa sababu wanaokoa pesa zao.”
Kwa wazi, kuna sababu nyingi zinazofanya upasuaji bila damu utambuliwe haraka katika jumuiya ya kitiba.
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Maamuzi ya Majuzi ya Mahakama
Maamuzi mawili ya mahakama yaliyotolewa katika jimbo la Illinois, Marekani, katika Novemba na Desemba mwaka wa 1997 yalikuwa yenye maana. Katika uamuzi wa kwanza, Mary Jones, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alilipwa fidia ya dola 150,000 kwa sababu katika mwaka wa 1993 alitiwa damu painti mbili licha ya kupinga waziwazi aina hii ya matibabu. Hiki kilikuwa kiasi kikubwa zaidi cha fedha kupewa Shahidi kwa sababu ya madhara ya kihisia-moyo yaliyosababishwa na kutiwa damu mishipani bila kutaka.
Kesi ya pili ilihusisha Shahidi aliyekuwa mjamzito aliyeitwa Darlene Brown, ambaye alitiwa damu kwa nguvu ili kuokoa kijusi chake kilichokuwa na majuma 34. Mnamo Desemba 31, 1997, Mahakama ya Rufani ya Illinois ilifafanua uamuzi wake kwa kusema kwamba “kutiwa damu mishipani ni njia ya kitiba ya uvamizi ambayo huvuruga hali bora ya mtu mzima.” Mahakama ya Rufani ilitoa muhtasari wa uamuzi wake kwa kusema kwamba “chini ya sheria ya Jimbo hili, . . . hatuwezi kuweka sheria ya kumlazimisha mwanamke mjamzito akubaliane na njia ya uvamizi ya kitiba.”
Mnamo Februari 9, 1998, Mahakama Kuu ya Tokyo ilitangua uamuzi wa mahakama ndogo, iliyoamua kwamba daktari alikuwa na haki ya kumtia damu Misae Takeda wakati alipofanyiwa upasuaji katika mwaka wa 1992. Mahakama Kuu ilitangaza kwamba “haki ya mgonjwa ya kuchagua matibabu yapasa kuheshimiwa. Ilikuwa kinyume cha sheria kutia damu mishipani.” Misae Takeda alilipwa fidia ya yen 550,000 (dola 4,200).