Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 9/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kashfa ya Damu Yaongezeka Katika Ufaransa
  • “Ibilisi” Mmoja Kapungua
  • Hasira na Magonjwa ya Ghafula ya Moyo
  • Usingizi Si Mzuri kwa Miwani Ivaliwayo Ndani ya Macho
  • Mzoroto wa Lugha
  • Somo Lenye Kuua
  • Kudhibiti Vijidudu Viambukizi vya Mavumbini
  • Mafanikio au Afya?
  • Uhalifu Walipa?
  • Sababu Ifanyayo Majaribio ya Kuleta Amani Yashindwe
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2012
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Je, Kweli Unahitaji Kufanya Mazoezi?
    Amkeni!—2005
  • Vita Vimebadilika Siku Hizi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 9/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kashfa ya Damu Yaongezeka Katika Ufaransa

Machunguzi ya kashfa ya damu katika Ufaransa yametokeza hati zinazoonyesha kwamba ni wazi kuwa maofisa wa serikali hutanguliza mambo ya uchumi mbele ya afya na usalama wa wagonjwa Wafaransa. Kulingana na International Herald Tribune ya Paris, hati hizo zafunua kwamba maabara moja ya Marekani ilipogundua namna ya kuchunguza damu kuona kama ina virusi ya UKIMWI katika ugavi wa damu, maofisa Wafaransa, wakihofu kwamba kifanyizo hicho cha Marekani kingesambazwa katika soko la Ufaransa, wakazuia mauzo “ili kumpa mtengenezaji fulani Mfaransa wakati wa kufikilia kusitawisha kifanyizo kama hicho.” Tokeo ni kwamba, mamia ya watu walipatwa na UKIMWI baada ya kupokea mitio-damu yenye viini vibaya muda ule wa karibu miezi saba ambao ilichukua kampuni hiyo ya Ufaransa kutengeneza kifanyizo chayo.

“Ibilisi” Mmoja Kapungua

Mume na mke wa Tokyo waliita mtoto wao mgeni Akuma, kumaanisha “Ibilisi.” “Ni jina la kishindo sana hivi kwamba ukiisha kulisikia, hulisahau kamwe,” akasema baba. “Ni jina litakalowezesha mwanangu akutane na watu wengi akuapo.” Kwanza wenye mamlaka huko walikubali kuandikisha jina hilo, lakini baadaye wakalifuta kuwa lisilokubalika na la kutumia vibaya haki za kiuzazi, wakisema lingekaribisha kudhihakiwa na kubaguliwa. Baada ya miezi ya kupambana katika mahakama mbalimbali, wazazi waliacha nia yao wakasema wangeandikisha mwana wao kwa jina jingine, ili waendelee kuishi bila kusumbuliwa na wasiache mvulana huyo bila jina rasmi. Hata hivyo mambo hayakubadilika nyumbani. “Tutaendelea kumwita Akuma kuwa ndilo jina lake la kila siku,” baba huyo akasema, na hilo ndilo jina aitikialo mtoto mchanga huyo.

Hasira na Magonjwa ya Ghafula ya Moyo

“Watu wenye maradhi ya moyo huongezea zaidi ya maradufu hatari yao ya kupatwa na magonjwa ya ghafula ya moyo wakasirikapo, na hatari hiyo hukaa muda wa saa mbili,” laripoti The New York Times. Ingawa machunguzi yaliyotangulia yameonyesha uhusiano kati ya hasira na ongezeko la mpigo wa moyo, ongezeko la msongo mwingi wa damu, na kuzibika kwa mishipa-ateri, uchunguzi mpya huu ndio wa kwanza kutoa ithibati ya kisayansi kwamba hasira yaweza kuleta ugonjwa wa ghafula wa moyo papohapo. Hatari hiyo yaweza kupunguzwa kwa kujaribu kubaki mtulivu unapokabili migogoro ya hisiamoyo, akasema Dakt. Murray Mittleman, mwanzishi mkuu wa uchunguzi huo. “Watafiti hao wameona pia kwamba watu watumiao aspirini, ambayo hupunguza hatari za magonjwa ya ghafula ya moyo, walilindwa kwa kadiri fulani na athari za mifoko ya hasira,” ikasema makala hiyo, yawezekana kwa sababu aspirini hupunguza uwezo wa visahani vya damu kufanyiza migando ya damu na huziba mishipa-ateri. Hivyo huenda ikawa kwamba hasira huathiri visahani vya damu, Dakt. Mittleman akasema.

Usingizi Si Mzuri kwa Miwani Ivaliwayo Ndani ya Macho

Watu wavaao miwani yao ya ndani ya macho wakiwa wamelala huelekea mara nane zaidi kupatwa na ambukizo la macho kuliko wale wasiofanya hivyo, kulingana na uchunguzi mmoja wa karibuni. Watafiti hao walipata kwamba hata usafi wa kutunza miwani hiyo kwa uangalifu hautoi ulinzi dhidi ya ile hatari nyingi mno ya kuvaa miwani ya ndani ya macho usiku kucha, laripoti International Herald Tribune. Kuivaa usiku kucha kwaweza kufanya konea, ule ufuniko wa jicho wa nje-nje, iambukizwe na viini na bakteria, bila kujali miwani ni ya namna gani. Kwa kuondoa miwani ya ndani ya macho kabla ya kulala, wavaaji waweza kupunguza uelekeo wa kuvimba kwa konea kwa kiasi cha asilimia 74.

Mzoroto wa Lugha

Mnamo miaka 100, nusu ya zile lugha 6,000 zilizopo leo zitaelekea kutokomea, ndivyo itabirivyo Atlas of the World’s Languages. Ndimi zipatazo 1,000 tayari zimetokomea muda wa miaka 500 iliyopita, sana-sana katika kontinenti za Amerika na Australia. Lugha nyingi hazifundishwi tena kwa bidii. Katika Alaska, ambako kuna ndimi 20 za kienyeji, ni 2 tu ambazo bado watoto hujifunza. Papua New Guinea ina lugha 155 ambazo chini ya waongeaji 300 husema kila moja, hali katika Australia 135 kati ya zile lugha 200 za Kiasili zilizobakia huongewa na chini ya watu 10 kila moja. “Si lugha zenyewe tu zinazotokomea,” laripoti gazeti Independent la London. “Kawaida nzima za fasihi, za mapokeo ya mdomo na ya maandishi pia; mifumo isiyo na kifani ya sarufi na msamiati inayoonyesha mifumo isiyo na kifani pia ya mawazo na mitindo-maisha; lugha ambayo ndiyo msingi mkuu wa maelfu ya tamaduni za kibinadamu: yote hayo yatatoweka, yaachie ulimwengu umaskini wa kitamaduni ulio mwingi zaidi ajabu.”

Somo Lenye Kuua

Maofisa wa Urusi wa urukaji wa ndege wamekiri kwamba mshirika wa kundi la Aeroflot alikuwa akifundisha watoto wake jinsi ya kuruka wakati jeti hiyo ilipogonga mlima mmoja wa Siberia katika Machi, ikiua watu wote 75 waliokuwamo. “Mgongano huo ulitendeka kwa sababu rubani alitaka kuonyesha watoto wake jinsi ya kurusha ndege,” shirika la habari la Kirusi Itar-Tass likasema. Maofisa wa Magharibi wa urukaji wa ndege, walipokuwa wakichunguza virekodi vya mruko wa ndege katika Ufaransa, walisema kwamba “sauti za watoto zingeweza kusikiwa na kwamba hakukuwa na marubani kwenye mitambo ya udhibiti wakati ndege hiyo ilipoanguka,” laripoti The New York Times. “Mirekodi ya chumba cha rubani yathibitisha kwamba bila kukusudia mtoto mmoja au wengi zaidi katika viti vya rubani walifungulia kwa aksidenti mitambo yenye kujiendesha yenyewe na kuitosa jeti chini kwenye msiba,” likasema Times.

Kudhibiti Vijidudu Viambukizi vya Mavumbini

Ugonjwa wa pumu na mizio imekuwa ikiongezeka Uingereza, laripoti The Times la London. Kisababishi ni nini? Ni vijidudu vya mavumbini. “Makao ya kibinadamu hayajawa kamwe na ukosefu wa nafasi za kuingizia hewa kama ilivyo sasa—yamejaa hewa chafu, chepechepe, yenye mizio mingi,” asema Dakt. John Maunder wa Kitovu cha Cambridge cha Kutibu Maradhi Yaletwayo na Vijidudu vya Mavumbini. Vijidudu vya mavumbini huishi kwa kutegemea vijipande vya ngozi na huendelea vizuri sana nyumbani katika mazingira chepechepe ya vitanda visivyoingiwa na hewa ya kutosha. Vijidudu vya mavumbini vilivyo hai na vilivyokufa pamoja na samadi yavyo, na magamba ya ngozi na kuvu, vyaweza kujumlika kuwa sehemu moja ya kumi ya uzito wa mto wa kulalia usiotunzwa vizuri. Mavi ya vijidudu hivyo vya mavumbini yaweza kuwa na protini iaminiwayo kuchochea kushikwa-shikwa ghafula na ugonjwa wa pumu na pia kuwa kisababishi kikuu cha kuwashawasha kwa kiwambo cha ute wa pua kutokana na mizio—pua yenye kuziba. Nyumba za ki-siku-hizi zilizozibwa mianya haziingizi hewa safi ya kutosha kukandamiza vijidudu hivyo vya mavumbini. Kwa maisha yenye afya zaidi, Dakt. Maunder apendekeza kulala madirisha yakiwa wazi iwezekanapo, kuacha vitanda viingiwe na hewa kila siku, na kuisafisha kwa kawaida mito ya kulalia, magodoro, na blanketi.

Mafanikio au Afya?

“Kwa jumla, michezo ya kiwango cha juu huwa ya kuhangaikia hasa kuboresha mafanikio ya wanariadha wayo, si sana kuboresha afya yao,” asema daktari wa mifupa Victor Matsudo, kama alivyonukuliwa katika Veja. “Hakuna mtu ahitajiye kuwa mwanariadha ili kuboresha afya yake.” Kwa kweli, asema Dakt. Matsudo, “mtu afanyaye mazoezi kupita kiasi huelekea kufa mapema kuliko mtu akaaye mahali pamoja.” Aongezea hivi: “Watu wengi bado wanafikiri kwamba mazoezi yafaayo yapasa kuwa jambo gumu, linalosababisha kutoa jasho na kuteseka. Hii si kweli. Mazoezi yafaayo ni ya kiasi, yasiyosababisha wala maumivu, usumbufu wala mafundo ya misuli. . . . Kutembea ndilo jambo la kwanza lipendekezwalo kwa mtu akaaye mahali pamoja na atakaye kuanza jitihada ya kuwa na hali njema ya kimwili.” Mtu atembeaye kwa nusu-saa, mara mbili au tatu kwa juma, ana fursa ya asilimia 15 ya kutoelekea sana kufa kama mtu akaaye mahali pamoja. Dakt. Matsudo adokeza kwamba matembezi hayo yafanywe katika ardhi yenye usawa na kwa mwendo uruhusuo mtu kupumua kwa urahisi na kuongea na mtu mwingine.

Uhalifu Walipa?

Muuaji wa mfululizo katika Marekani alikiri kuua na kuwakata maungo wavulana na wanaume 17. Kwa kufanya vitendo hivyo vya uhalifu anatumika kifungo cha maisha gerezani. Lakini rekodi za gereza zaonyesha kwamba kufikia Machi mwaka huu, amepokea zaidi ya dola 12,000 kutoka kwa waandikaji barua ulimwenguni pote hata kutoka kule mbali Ufaransa na Afrika Kusini, kutia na msaada wa dola 5,920 kutoka kwa mwanamke mmoja wa London. “Mwanamke mmoja alisema alitaka ku[m]fundisha juu ya Yesu, kwa hiyo akampelekea dola 350, pamoja na fasihi fulani ya Biblia,” lasema The New York Times. “Mwanamke mwingine alipeleka dola 50 ili [mwanamume huyo] aweze kununua ‘sigareti, stampu na bahasha’ gerezani.” Mwanamume huyo alitumia nyingi za fedha hizo, hata ingawa watu wa ukoo wa wale waliodhulumiwa naye hawajapokea hata senti moja kati ya zile dola milioni 80 za mahukumio yaliyofanywa dhidi yake. Kulingana na mtunza-gereza, hakuna sheria ikatazayo wafungwa kuomba usaidizi wa kifedha, mradi hakuna upunjaji ufanywao.

Sababu Ifanyayo Majaribio ya Kuleta Amani Yashindwe

“Vile vita 35 vilivyoendelea kuwako ulimwenguni hadi 1994 vyathibitisha ule utabiri wa Maandiko wa kukosesha matumaini usemapo kwamba sikuzote kutakuwa na vita na matetesi ya vita,” yasema makala moja ya Toronto Star. (Taarifa hii si sahihi. Kwa kweli Biblia hutabiri kwamba karibuni vita vitakoma. Ona Isaya 2:2-4) “Vita vyote dazani tatu vinavyovuma ulimwenguni leo ni mapigano yanayofanyika ndani ya nchi moja-moja—hakuna lolote lililo pigano kati ya nchi na nchi.” Kuongezeka nguvu kwa vita hivi vya wenyewe kwa wenyewe kwaonyesha kwamba mashirika ya ulimwengu hayawezi kusuluhisha magomvi kwa amani. “Mradi vikundi vilivyoudhiwa vyajua kwamba UM hauwezi kudhibiti nchi zilizo washirika wao ili zifuate hata viwango vya chini tu vya mwenendo na haki za kibinadamu, vitaendelea kufanya jeuri ili kuzidi kudai haki zao,” yasema makala hiyo. “Baada ya Vita ya Ulimwengu 2 ni kama hakuna kabisa visa vya kutumia nguvu nyingi za kijeshi za nchi za Kaskazini kufanikiwa kukomesha mapigano ya nchi na nchi au ya wenyewe kwa wenyewe katika Ulimwengu wa Tatu au kwingineko.” Kwa kweli, fedha ambazo bado zinatumiwa kutayarisha vita vya nchi na nchi husaidia hasa kuchangia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa kutumia fedha ambazo zingaliweza kutumiwa kuboresha hali ziletazo vita vya wenyewe kwa wenyewe.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki