Kuutazama Ulimwengu
Uongozi Bora Watakwa
Watu ulimwenguni pote hawaridhiki na viongozi wao. “Wengine wasema,” lasema The Wall Street Journal, “kwamba viongozi wa ulimwengu wanaotawala sasa hawana uwezo wa kufanya kazi yao.” Aliyekuwa rais wa Ufaransa Valéry Giscard d’Estaing asema: “Tunashuhudia taabu kubwa ya demokrasia wakilishi.” Kwa nini umma unazidi kutoridhika? Kwa sababu watu “huudhiwa na viongozi wanaoonekana wanyonge wakati ambapo matatizo yanayowakabili ni makubwa sana,” lajibu Journal. Liliendelea kusema: “Wanachukizwa kwa kutopata jawabu na kupata ufisadi wanapotafuta uelekezo. Na si wanasiasa mmoja-mmoja tu ambao hupatwa na ule mfadhaiko wa umma: Katika mahali kama Japan na Italia, watu hawapendi mfumo mzima wa kisiasa.” Ingawa serikali haipendwi na wengi katika nyakati ngumu kiuchumi “hali hiyo ni isiyo ya kawaida kwa sababu inapatikana katika mahali pengi wakati uleule, na kwa sababu haihusu watawala tu bali pia yahusu vyama vya upinzani.” Zaidi ya badiliko la kiuchumi litahitajiwa ikiwa hali ya kutazamia mema itarudishwa, asema Bwa. Giscard d’Estaing. “Jamii zetu zahitaji kuwa na mwono wa wakati ujao.”
Mashahidi wa Yehova Watambuliwa Kisheria Katika Meksiko
Mnamo Mei 7, Mashahidi wa Yehova walihalalishwa kuwa dini katika Meksiko. Wao walipewa hati iliyowahakikishia kutambuliwa huko na Katibu-mdogo wa Idara ya Mambo ya Ndani ya Serikali mnamo Mei 31. Hivyo hatua nyingine mbele ilichukuliwa kuelekea uhuru wa kidini katika Meksiko. Ilikuwa katika Aprili 1, 1989, kwamba Mashahidi wa Yehova waliweza kwa mara ya kwanza kutoa sala kwa uhuru kwenye mikutano yao ya kutaniko na kutumia Biblia katika huduma yao ya mlango kwa mlango. Kuna Mashahidi zaidi ya 370,000 katika Meksiko. Serikali ya Meksiko ilirekebisha sheria zayo mwaka uliopita na ikaanza kutambua kisheria mashirika ya kidini katika nchi hiyo.
Haki za Kibinadamu Hazifai Kitu
Kituo cha UM cha Haki za Kibinadamu katika Geneva, Uswisi, chakadiria kwamba “nusu ya jamii ya wanadamu wana matatizo makubwa ya kuvunjwa kwa haki zao za kibinadamu,” laripoti gazeti la Ujerumani Süddeutsche Zeitung. Mabaya hayo yalitia ndani mateso, unajisi, na kuuawa hadi kuchukuliwa utumwa, njaa, na kutenda watoto vibaya. Kituo hicho chakadiria kwamba kati ya watoto milioni 150 na milioni 200 hulazimishwa kufanya kazi ngumu wakiwa watoto katika mabara zaidi ya 50. Zaidi ya hayo mamilioni ya watu hupatwa na ubaguzi wa rangi na uhasama kuelekea wageni. “Katika hali ya umaskini na upungufu, haki za kibinadamu hazifai kitu,” akasema Bwa. Ibrahime Fall, msimamizi wa kituo hicho. “Ni kweli kwamba tumepeleka mwanadamu mwezini, lakini ulimwengu tunamoishi waendelea kuwa mgumu, hatari, na mara nyingi wenye kufisha.”
Umalaya wa Watoto Waenea
“Madaktari, maofisa wa polisi, wafanyakazi wa jamii . . . waripoti kwamba watoto na wabalehe wazidi kuhitajiwa kuwa malaya kwa sababu wateja wawaona kuwa ‘salama zaidi’ na wakielekea kuwa bila UKIMWI,” yasema International Herald Tribune ya Paris. Kwenye mjadala wa hivi karibuni wa UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni) juu ya “biashara ya ngono na haki za kibinadamu” uliofanywa katika Brussels, Ubelgiji, wastadi walithibitisha kwamba wateja walikuwa tayari kulipa bei kubwa zaidi kwa watoto wanaofikiriwa kuwa bikira. Ingawa wakubali kwamba mweneo wa UKIMWI wa tufeni pote ulikuwa jambo kuu, wastadi hao walisema pia kwamba zile pande nyingi za biashara hiyo yenye faida nyingi “zimefanya iwe kawaida kununua na kuuza ngono waziwazi na kumeondoa miiko dhidi ya kuwatumia vibaya watoto kingono kwa faida za kichoyo.” Uchunguzi mbalimbali wa UNESCO waonyesha tatizo hilo kuwa limeenea hasa katika Benin, Brazili, Kolombia, Thailandi, na Ufilipino. Kadirio la 800,000 kati ya malaya wanawake Wathailandi milioni 2 ni watoto na wabalehe, na zaidi ya wavulana 10,000 wa umri wa kutoka 6 hadi 14 wasemekana kuwa hufanya kazi wakiwa makahaba katika Sri Lanka.
Kazi za Mke wa Nyumbani
“Yeye hufanya kazi kama mkimbiaji wa mbio ndefu . . . lakini hata hapati medali,” lasema gazeti la kila siku la Italia Il Messaggero katika kuzungumza juu ya mke wa nyumbani wa kawaida. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Roma ya Sayansi ya Michezo waonyesha kwamba nishati itumiwayo na mke wa nyumbani wa kawaida katika kazi yake ya nyumbani (zaidi ya kalori 200 kwa saa) yaweza “kulinganishwa na ile ya michezo kadhaa.” Ingawa michezo fulani kwa wazi hutumia kalori nyingi zaidi, takwimu hizo zatumika zaidi “unapofikiria kwamba utendaji wa mke wa nyumbani huendelezwa kwa karibu saa nane kila siku.” Mkimbiaji wa mbio fupi anayeshikilia rekodi Marisa Masullo akiri hivi: “Mimi huchoka zaidi ninapofanya kazi nyumbani kuliko vile ninavyochoshwa ninapojizoeza.”
Sayari ya Maji
Kama maji yangeenezwa kwa usawa juu ya sayari, maji ya ulimwengu yangefanyiza bahari ya tufeni pote yenye kina cha kilometa 2.5, lasema gazeti People & the Planet. Kwa kweli, sehemu zote za bara za dunia zingeweza kutoshea ndani ya Bahari Pasifiki kukiwa na nafasi kubwa ya ziada. Lakini, kati ya hifadhi zote kubwa za maji ya dunia, ni asilimia 3 tu ya maji hayo ambayo ni safi bila kuwa na chumvi. Na ni asilimia 1 tu ya maji safi ya sayari yapatikanayo kwa urahisi kwa jamii ya wanadamu. Mengine yote yamefungwa katika mito ya barafu na sehemu za barafu au yamo chini ya ardhi. Hata hivyo, hiyo asilimia 1 yatosha kutegemeza mara mbili au tatu ya idadi ya sasa ya watu wote ulimwenguni. “Kwa kusikitisha,” laomboleza gazeti hilo, “maji safi yamegawanywa katika hali isiyo sawa kabisa na hutumiwa vibaya kila mahali.” Kama tokeo, kulingana na kadirio moja, wakazi wa dunia wapatao bilioni mbili huishi katika maeneo ambayo maji ni nadra sana kupatikana.
Maisha Marefu ya Takataka
Takataka ya kawaida huchukua muda gani ili kuoza? Kulingana na tarakimu zilizochapwa katika gazeti la Italia Focus, huchukua kuanzia miezi mitatu hadi sita kwa vitambaa vya karatasi au takataka za mboga kuharibiwa, kuanzia mwaka 1 hadi 2 kwa miisho ya sigareti, miaka 5 kwa peremende ya kutafuna, na kuanzia miaka 10 hadi 100 kwa mikebe ya aluminiamu. Lakini baadhi ya vyombo vya plastiki “hudumu kwa karne nyingi bila kuharibika . . . Haviyeyushwi kwa maji . . . , na hakuna vijiumbe vinavyoweza kuvila.” Polystyrene, ambayo kwa kawaida hutumiwa kupakia vitu na kutengenezea vitu vya kuwekea chakula na vinywaji, labda itaharibika katika muda wa miaka elfu, na ni lazima miaka 4,000 ipite kabla chupa za glasi kurudi mahali pazo katika hali ya asili.
Matundu ya Meno Huambukizwa
“Kuoza kwa meno kwaweza kuambukizwa.” Ndivyo inavyosema ripoti moja ya huduma za habari za Agence France-Presse juu ya uchunguzi uliofanywa na shule ya meno ya Uswisi na Shirika la Afya Ulimwenguni. Utafiti wao wafunua kwamba Streptococcus mutans, ile bakteria inayosababisha kuoza kwa meno, mara nyingi hupitishwa kutoka mdomoni mwa mshiriki mmoja wa familia hadi mwingine, kama vile wakati wazazi wanapotumia kijiko kilekile na mtoto wao au wanapoonja chupa ya mtoto kabla ya wakati wa kumlisha. Hatari huongezeka kulingana na kiasi cha bakteria kilichopo katika mate ya mtu. Bakteria hiyo, inayobadili sukari kuwa asidi inayoshambulia meno, yaonekana husitawi hasa katika midomo ya watoto kati ya umri wa mwaka mmoja na miaka minne—wakati ambapo meno ya watoto hasa huoza kwa urahisi.
Kofia za Chuma kwa Waendesha Baiskeli
Vaa kifaa cha kulinda kichwa! Hilo ndilo shauri ambalo WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) lawapa waendesha baiskeli. Ingawa kofia za chuma hupunguza majeraha ya kichwa kwa asilimia 75, Australia ndiyo nchi pekee ambayo kwa sasa hutaka waendesha baiskeli wazivae. Katika United States, sehemu mbili kwa tatu ya vifo vyote vya waendesha baiskeli husababishwa na majeraha ya kichwa na ubongo, huku watoto wa kati ya umri wa miaka 6 hadi 14 wakiwa kwenye hatari kubwa zaidi. WHO laomboleza: “Kutopenda [kuvaa kofia za chuma] kunakoonyeshwa na baadhi ya waendesha baiskeli ni kugumu kueleweka, kwa kufikiria kwamba hakuna mtu anayekataa tena kwamba waendesha pikipiki hulindwa kwa kufaa na kofia za chuma.”
Vijidudu vya Vumbini
“Hakuna mtu ajuaye kikweli jinsi wanavyofika hapo, lakini vijidudu vya vumbini vya nyumba huishi katika karibu kila nyumba,” lasema gazeti Science News. Vikiwa havionwi kwa macho ya kibinadamu, vijidudu hivyo visivyo na mifupa hujilisha ngozi ya wanadamu ambayo huambuka kila mara. Vijidudu hao waweza kupatikana katika matandiko ya kitanda, mazulia, na fanicha yenye matakia. Wangapi? Watafiti wakiwa na kisafishatupu na darubini kali walichunguza vumbi katika nyumba mbili zilizoambukizwa. Kiti kimoja chenye matakia katika nyumba moja kilikuwa na vijidudu 7,454 kwa kila gramu ya vumbi, kukiwa na vijidudu 2,361 zaidi kwa kila gramu kwenye zulia chini ya kiti hicho.
Mbaya Zaidi ya Kifo Cheusi
“Katika Ulaya ya karne ya 14, Kifo Cheusi kiliua karibu watu milioni 25, au mmoja kati ya kila wanne,” lasema gazeti American Health. “Data mpya yaonyesha kwamba ikiwa watu wataendelea kuvuta sigareti katika viwango vya sasa, sigareti zitaua mara 10 ya idadi hiyo: angalau milioni 250, au mtu mmoja kati ya kila watu watano walio hai sasa katika nchi zilizositawi.” Ugunduzi huo, ukitegemea uchunguzi mkubwa wa watu zaidi ya milioni moja, ulionyesha kwamba kuvuta sigareti kulikuwa hatari hata zaidi kuliko vile ilivyodhaniwa hapo mwanzoni. “Tulikuwa tumeamini kwamba karibu mvutaji mmoja kati ya wanne huuawa kwa sababu ya zoea lao,” akasema Dakt. Richard Peto, profesa katika Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza. “Lakini sasa tunajua kwamba angalau theluthi moja—na labda wengi zaidi—ya wavutaji wote hufa kwa sababu ya kuvuta sigareti. Athari ya kuvuta sigareti katika vifo vya taifa hupita kwa mbali athari ya jambo jingine lolote.” Kati ya vifo milioni 250 vinavyotazamiwa, zaidi ya nusu yavyo vitakuwa vya watu wa umri wa kutoka miaka 35 hadi 69, ambao watakuwa wamepunguza uhai wao kwa wastani wa miaka 23 kwa sababu ya kuvuta sigareti.