Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 7/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Njaa Yatesa Sehemu Kubwa za Jamii ya Wanadamu
  • Kuongezea Mapato kwa Njia ya Kushangaza Sana
  • Kazi za Kuajiri Watoto
  • Idadi ya Watu Ulimwenguni Yaharibiwa na UKIMWI
  • Uzuizi wa Kuvuta Sigareti Waongezwa
  • Mashine-Binadamu ya Kuchuma Matunda
  • Mahali Ambapo Magugu Hupendwa na Wengi
  • Kuuzima Moto wa Helo
  • Utamaduni wa Karaoke
  • Haki za Kibinadamu Hali: ‘Ya Kusononesha’
  • Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?
    Amkeni!—1996
  • Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini
    Amkeni!—1995
  • Wauzaji wa Kifo—Je! Wewe Ni Mnunuzi?
    Amkeni!—1990
  • Mataraja Kutoka Orofa ya 29
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 7/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Njaa Yatesa Sehemu Kubwa za Jamii ya Wanadamu

Dunia haijapata kamwe kuzaa chakula kingi sana cha kulisha jamii ya wanadamu kama ilivyo sasa; hata hivyo, hakujapata kamwe kuwa na wakati ambapo jamii ya kibinadamu imeteswa sana na njaa kama ilivyo sasa. Shirika la habari la France-Presse laripoti kwamba kulingana na takwimu za karibuni zaidi kutoka Benki ya Ulimwengu, njaa ilibana sana maisha za watu kama bilioni 1.13 katika 1990, wengi zaidi ya ilivyopata kuwa wakati wowote uliotangulia. Iliathiri karibu asilimia 30 ya watu wanaoishi katika nchi zinazositawi. Maeneo ya ulimwengu yenye kuathiriwa vibaya zaidi yalikuwa Asia ya kusini, ambako watu milioni 562 hutaabishwa na njaa (asilimia 49 ya idadi ya watu); Afrika, ikiwa na milioni 216 (asilimia 47.8 ya idadi ya watu); Mashariki ya Karibu na Afrika Kaskazini, zikiwa na milioni 73 (asilimia 33.1 ya idadi ya watu); na Amerika ya Latini na eneo la Karibea, zikiwa na milioni 108 (asilimia 25.2 ya idadi ya watu). Tarakimu hizi hazitii ndani karibu bilioni nyingine moja ya watu wataabishwao na utapiamlo.

Kuongezea Mapato kwa Njia ya Kushangaza Sana

Mwanzoni mwa 1993, Shirika la Utafiti wa Kisayansi wa Mambo Yasiyojulikana na Sayansi katika Ujerumani lilikusanya matabiri 70 yaliyofanywa na wanajimu kisha likakadiria matokeo mwishoni mwa mwaka. Kwa kufikiria kutofanikiwa kwa matabiri ya miaka iliyotangulia (ona Amkeni! la Juni 8, 1992 [Kiingereza], ukurasa 29, na Julai 8, 1993, ukurasa 29), je, wanajimu walifua dafu katika 1993? ‘Walisema uwongo mtupu,’ yaripoti Nassauische Neue Presse. “Wanajimu walio wengi hata hawaamini matabiri yao wenyewe ya kila mwaka,” asema msemaji wa shirika hilo. Lakini unajimu ni biashara kubwa katika Ujerumani, nayo huingiza mapato ya dola milioni 57. Watabiri wengi huchukua matabiri ya kuamsha msisimko kuwa “njia yenye matokeo ya kuweza kutambuliwa kwa kuchapishwa katika vichwa vya habari” ili kuongezea mapato, laripoti gazeti hilo.

Kazi za Kuajiri Watoto

Watoto wakadiriwao kuwa milioni nane wako kazini katika Brazili, laripoti O Estado de S. Paulo. Watoto hawa huenda wakafanya kazi ileile ambayo watu wazima hufanya. Hata hivyo, wao hawachangii sana mapato ya familia kwa sababu ya kupewa malipo ya chini. Yaelekea kwamba, kwa sababu wafanyakazi wachanga hawa hawakupata masomo ya kutosha, wao hubaki wakiwa na elimu ndogo tu na wakiwa maskini kama wazazi wao. Isitoshe, Luiz Cláudio de Vasconcelos wa Wizara ya Wafanyakazi asema, “mtoto afanyaye kazi huondoa uhitaji wa kuajiri kazi vichwa vingine vya familia, kwa kuwa yuko tayari kupokea theluthi ya mshahara wa mtu mzima.”

Idadi ya Watu Ulimwenguni Yaharibiwa na UKIMWI

◻ “UKIMWI utafyeka maisha za wanadamu katika zile nchi 15 zenye mweneo mkubwa zaidi wa HIV,” laonya Populi, gazeti la Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa. Kwa kutegemea ripoti ya hivi majuzi ya UM, World Population Prospects: The 1992 Revision, gazeti hilo latabiri kwamba kama miaka kumi kutoka sasa, “ukuzi wa idadi ya watu katika nchi hizi utapungua kwa milioni 12 kwa sababu ya UKIMWI. Karibu watu zaidi ya milioni 9 watakufa kutokana na UKIMWI katika nchi hizi, na watoto wachache zaidi watazaliwa kwa sababu ya vifo vya wanawake wakiwa katika miaka yao ya kuzaa.”

◻ Siku ya UKIMWI Ulimwenguni ilisherehekewa Desemba 1, 1993. Lakini matokeo ya kampeni za kupambana na ugonjwa hazikutoa sababu ya kutosha ya kusherehekea. Ofisa mmoja wa WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) alikiri hivi: “Kusema kweli mimi sifikiri tumekuwa na mafanikio yoyote makubwa ya kupambana na Ukimwi katika Afrika.” Alikiri uhitaji wa kukazia umaana wa uaminifu katika ndoa ili kupambana na ugonjwa huo. Gazeti Cape Times lilitaarifu kwamba Afrika “ina theluthi moja ya visa vilivyoripotiwa.” Kulingana na WHO, visa vya UKIMWI katika watu wazima vinavyokadiriwa kuwa milioni moja vimo katika Afrika iliyo ya chini ya Sahara.

Uzuizi wa Kuvuta Sigareti Waongezwa

Sheria mpya zinazotaka maonyo ya wazi yatolewe juu ya hatari za kuvuta sigareti zimepitishwa katika Eneo la Jiji Kuu la Australia. Kuanzia Aprili 1, 1994, pakiti zote za sigareti ni lazima ziwe na maonyo yenye kuonekana wazi, kama vile: “Kuvuta Sigareti Huua,” “Kuvuta Kwako Sigareti Kwaweza Kudhuru Wengine,” “Kuvuta Sigareti Hutia Mtu Uraibu,” na “Kuvuta Sigareti Ukiwa Mjamzito Hudhuru Mtoto Wako.” Kulingana na The Canberra Times, ni lazima maonyo hayo yachukue nafasi isiyopungua asilimia 25 ya upande wa mbele wa pakiti. Upande wa nyuma wa pakiti ni lazima ufunikwe angalau theluthi moja kwa taarifa inayofuata: “Moshi wa tumbako una kemikali nyingi zinazosababisha kansa. Wakati ule moshi uvutwapo, kemikali hizo zaweza kudhuru mapafu, na zaweza kusababisha kansa. Kansa ya mapafu ndiyo kansa iliyo ya kawaida zaidi isababishwayo na kuvuta sigareti. Kwa kawaida kansa ya mapafu huongezeka na kuenea kabla haijaonekana. Katika visa vilivyo vingi hiyo huua upesi. [Kuvuta sigareti] huua karibu mara tatu zaidi ya watu ambao huuawa na kileo na dawa nyingine zote za kulevya, zikijumlishwa pamoja. Watu mara sita zaidi hufa kutokana na athari za kuvuta sigareti kila mwaka kuliko wale wafao kutokana na aksidenti za magari.”

Mashine-Binadamu ya Kuchuma Matunda

Uvumbuzi wa karibuni zaidi katika ufundi wa ukulima wa Italia ni mashine-binadamu iwezayo kuchuma “kufikia machungwa 2,500 kwa saa moja kutoka kwenye michungwa moja-kwa-moja.” Mashine hiyo ina mikono minane ya kujiendesha yenyewe “iliyo myepesi sana kugundua vitu,” kila mkono ukiwa na jicho la elektroni, nayo imepangiliwa utaratibu wa ‘kufahamu ukolevu wa rangi mbalimbali’ na kuchagua “tunda lililoiva, ikipita lile lisiloiva bila kukosea, baada ya kuyagusa kwa wepesi sana,” kulingana na La Stampa. Mashine-binadamu hiyo yenye vifaa vya kuhisi mapito yafaayo, “yenye kuendeshwa na injini ya dizeli yaweza kufanya kazi usiku na mchana hata katika hali mbaya ya hewa na kuchuma machungwa kwenye miti ya kimo cha kufikia meta tatu na nusu . . . Wakati wa kuchuma, mashine hiyo husogea kwa mwendo wa juu zaidi wa kilometa nane kwa saa na ina mwendo wa kusafiri ufikao kilometa 14 kwa saa moja, ikivuta gari-mkokoteni liwezalo kubeba uzito wa kufikia kilo 500.”

Mahali Ambapo Magugu Hupendwa na Wengi

“Magugu yamefunika uwanja wote wa starehe, na kuna miti mingi ya matunda na ya chestnati,” lasema Asahi Evening News juu ya uwanja wa starehe wa namna mpya katika Tokyo. Hakuna nafasi za wazi za mapito yaliyotandazwa, na “vile vitu vya kawaida katika nyanja za starehe kama pembea, vitelezo, na masanduku ya mchanga ya watoto kuchezea havipatikani.” Wakaaji wa hapo karibu wafurahishwa na jambo hilo. Miaka miwili iliyopita walidokezea baraza la jiji la kwao kwamba uwanja fulani wa starehe “wapaswa kuwa na majani yenye kukua na uwe na wadudu na wanyama wadogo” na kwamba “watoto wapaswa waweze kuchimba mashimo na kuchezea matope, na hakupaswi kuwa na ishara za kupiga marufuku kitu chochote.” Tangu wakati huo, bustani ya pili, ambayo pia yaelezwa kuwa “yakaribia kuwa ya hali ya asili, ikiwa imejawa mno na magugu” imejengwa katika Tokyo. Kotekote taifani wabuni wa nyanja za starehe wamestaajabu kuona wakazi wa majiji wakitaka sana uwanja wa starehe wa namna hii, wakaona kwamba waupatapo uwanja wa starehe, wao hushiriki kwa hamu nyingi katika kuusafisha na kuutunza.

Kuuzima Moto wa Helo

“Makanisa hayakazii sana yale mahubiri ya moto na kibiriti” kama vile yamefanya wakati uliopita, asema Robert Wuthnow, mtaalamu wa mambo ya kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Princeton. Kwa nini sivyo? “Adhabu ya mateso ya milele haiko vile ilivyokuwa zamani,” laripoti The Edmonton Journal, gazeti la Kanada. Uchunguzi wa Gallup wa kutafuta maoni ya watu uliofanywa hivi majuzi ulionyesha kwamba ingawa asilimia 60 ya Waamerika walisema wao huamini kuna helo yenye moto, ni asilimia 4 tu watarajiao kwenda huko. Katika Kanada, asilimia 38 ya wale waliochunguzwa huamini kuna moto wa helo; katika Hispania, ni asilimia 27; na katika Sweden, ni asilimia 7. “Wazo la helo halionekani likichochea watu ama watumikie Mungu ama wakubali Kristo kuwa mwokozi wao,” adai kasisi Mpentekoste Bruce Klepp. Lile “fundisho [la moto wa helo] halina matokeo ya kuboresha maadili hata kidogo,” adai Tom Harpur wa The Toronto Star.

Utamaduni wa Karaoke

Mmojapo miingizo ya maneno yaliyo katika Merriam-Webster’s Collegiate Dictionary, chapa ya kumi, ni neno “karaoke.” Neno hili hurejezea “ala itoayo midundo ya kuambatanishwa na nyimbo teule ambazo mtumia-ala huimba anapoendelea kupiga ala hiyo” nalo latokana na neno la Kijapani lililofanyizwa kutokana na kara, likimaanisha “tupu,” na oke, ufupisho wa “okestra.” Ala hiyo humfanya mtumizi ajisikie raha kwa kumwezesha kuimba na mipigo kamili kama okestra kamili. Kwa mara ya kwanza katika Japani, karaoke ilionwa na ilikubaliwa katika “ripoti ya elimu” kuwa “somo la kitamaduni,” tena lenye kupendwa na wengi zaidi nchini. Yastajaabisha kwamba asilimia 74 kati ya wale wa rika la miaka 19 hadi 29 walilishiriki katika kile kipindi cha mwaka mmoja kilichotangulia uchunguzi mmoja. Akitoa elezo juu ya badiliko la hali ya kufikiri miongoni mwa Wajapani, Tetsuo Sakurai, profesa mmoja wa mambo ya kijamii, alisema hivi katika Mainichi Daily News: “Sasa watu wana hamu ya kujieleza kwa uhuru na peupe.”

Haki za Kibinadamu Hali: ‘Ya Kusononesha’

“Ni jambo la maana sana kustahi haki za kibinadamu ili jamii ya kibinadamu iwe na hali njema wakati ujao,” ndivyo alivyotaarifu Ibrahima Fall, msaidizi wa katibu mkuu wa haki za kibinadamu kwenye Kongamano la Ulimwengu la UM Kuhusu Haki za Kibinadamu. “Lakini katika [nchi] nyingi,” alisema, “kiwango cha uvunjaji wa haki za kibinadamu ni cha kusononesha.” World Conference on Human Rights, ambayo ni barua ya UM ya kujulisha habari kwa wahusika, yathibitisha kwamba angalau nusu ya idadi ya watu wa ulimwengu huteseka kwa kuvunjiwa haki za kibinadamu leo. Aongezea hivi Bw. Fall: “Mamilioni ya maisha ya watu hubaki katika laana ya kila siku kwa kupatwa na kifo, uharibifu, ubaguzi, umaskini, mnyanyaso, unajisi, utumwa, kufa-njaa na kudumaa-ukuzi au kusinyaa.” Na vibaya zaidi, laana hiyo inaenea kwa sababu “matatizo ya kutofanyiwa haki,” UM latoa onyo, “yanaongezeka sana.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki