Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/22 kur. 6-7
  • Mataraja Kutoka Orofa ya 29

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mataraja Kutoka Orofa ya 29
  • Amkeni!—1998
  • Habari Zinazolingana
  • “Kazi ya Muda Mrefu Yamalizika”
    Amkeni!—1998
  • Haki za Kibinadamu kwa Wote—Uhalisi wa Ulimwenguni Pote!
    Amkeni!—1998
  • Haki za Kibinadamu na Makosa Leo
    Amkeni!—1998
  • Je, Ni Haki Bila Madaraka?
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/22 kur. 6-7

Mataraja Kutoka Orofa ya 29

UNAPOTOKA katika lifti kwenye orofa ya 29 ya jengo la Umoja wa Mataifa katika New York City, ishara ndogo ya samawati huonyesha njia inayoelekeza kwenye Ofisi ya Mjumbe Mkuu wa Haki za Kibinadamu (OHCHR). Ofisi hii ya upatanisho huwakilisha makao makuu ya OHCHR katika Geneva, Uswisi—kitovu cha utendaji wa UM wa haki za kibinadamu. Huku Mary Robinson, Mjumbe Mkuu wa Haki za Kibinadamu, akisimamia ofisi za OHCHR katika Geneva, Elsa Stamatopoulou mzaliwa wa Ugiriki ndiye msimamizi wa ofisi ya New York. Mapema mwaka huu, Bi. Stamatopoulou alimpokea vizuri mwandishi wa Amkeni! wakachunguza utendaji wa haki za kibinadamu katika miongo mitano iliyopita. Yafuatayo ni madondoo ya mahojiano hayo.

Swali. Unahisi ni maendeleo gani yamefanywa kuendeleza haki za kibinadamu?

Jibu. Nitakupa mifano mitatu ya maendeleo: Kwanza, miaka 50 iliyopita hakukuwa na wazo la haki za kibinadamu katika ajenda ya kimataifa; leo linapatikana kila mahali na linatenda. Serikali ambazo hazikupata kusikia juu ya haki za kibinadamu miongo kadhaa iliyopita sasa zinazungumza juu yake. Pili, sasa tuna mfumo wa sheria wa kimataifa, au kitabu cha sheria, chenye mikataba mingi ya kimataifa inayoambia serikali kwa maandishi daraka lake kuelekea raia zake. [Ona sanduku “Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu,” katika ukurasa wa 7.] Ilichukua muda wa miaka mingi kubuni mfumo huu wa sheria. Tunauonea fahari sana. Kielelezo cha tatu ni kwamba leo watu wako tayari kuliko wakati mwingine wowote kujiunga na harakati za haki za kibinadamu na wanaweza kujieleza wenyewe waziwazi kuhusu masuala ya haki za kibinadamu.

Swali. Kuna vizuizi vipi?

Jibu. Bila shaka, baada ya kufanya kazi na mashirika ya UM ya haki za kibinadamu kwa miaka 17, natambua kwamba tunakabili matatizo yenye kuvunja moyo. Tatizo kubwa zaidi ni kwamba mara nyingi serikali huona haki za kibinadamu kuwa suala la kisiasa badala ya suala la kibinadamu. Huenda zisiwe tayari kutekeleza mikataba ya haki za kibinadamu kwa sababu zinahisi kuwa zinatishwa kisiasa. Katika visa hivyo, mikataba ya haki za kibinadamu haitumiki. Kizuizi kingine kimekuwa kushindwa kwa UM kuzuia ukiukaji mzito wa haki za kibinadamu katika sehemu kama vile ile iliyokuwa Yugoslavia, Rwanda na hivi karibuni zaidi, Algeria. Kushindwa kwa UM kuzuia mauaji ya kinyama yaliyotokea katika nchi hizi ni kosa kubwa sana. Kuna njia za kutekeleza haki za kibinadamu, lakini mtu fulani apaswa kuzitekeleza. Ni nani atakayezitekeleza? Ikiwa faida za nchi ambazo zingeandaa ulinzi hazihatarishwi, mara nyingi nchi hizo hukosa nia ya kisiasa ya kujitokeza kukomesha ukiukaji.

Swali. Ni nini unachotazamia?

Jibu. Ninaona tisho na ahadi kwenye barabara inayoelekeza kwenye haki za kibinadamu kwa wote. Kinachonitia wasiwasi ni tisho linalotokezwa na uchumi wa tufeni pote unaochochea mashirika makubwa yaanze kutenda katika nchi ambako ni rahisi kupata wafanyakazi wa malipo ya chini. Leo, ikihitajika, tunaweza kuzilaumu serikali kwa ukiukaji wa haki za binadamu na kuziwekea msongo mkubwa. Lakini ni nani tunayeweza kumlaumu kwa ukiukaji huu wakati ambapo mikataba ya kibiashara inayohusisha pande nyingi inapozidi kupunguza nguvu za serikali na kuimarisha mashirika ya kiuchumi? Kwa kuwa hatudhibiti mashirika haya ya kiuchumi, inadhoofisha msimamo wa mashirika baina ya serikali mbalimbali kama vile UM. Kuhusu haki za kibinadamu, mwelekeo huu ni wenye kudhuru. Sasa ni jambo muhimu kuhusisha mashirika ya kibiashara katika haki za kibinadamu.

Swali. Vipi juu ya ahadi uliyotaja?

Jibu. Ukuzi wa utamaduni wa haki za kibinadamu wa tufeni pote. Namaanisha kwamba kupitia elimu twapaswa kufahamisha watu juu ya haki za kibinadamu. Bila shaka, hilo ni tatizo gumu kwa sababu linatia ndani badiliko la akili. Ndiyo sababu, miaka kumi iliyopita, UM ulianzisha kampeni ya habari ya peupe ya ulimwenguni pote ili kuelimisha watu kuhusu haki zao na kuelimisha nchi juu ya madaraka yao. Kwa kuongezea, UM umechagua miaka ya 1995 hadi 2004 kuwa “Mwongo wa Elimu ya Haki za Kibinadamu.” Inatumainiwa kwamba huenda elimu ikabadili akili na mioyo ya watu. Huenda jambo hili likasikika kuwa Gospeli, lakini inapohusu elimu ya haki za kibinadamu, mimi ni mwamini wa kweli. Ninatumaini ulimwengu utatumia utamaduni wa haki za kibinadamu kuwa itikadi yake katika karne inayofuata.

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu

Mbali na Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu, pia kuna Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu. Zinahusianaje?

Naam, ukilinganisha Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu na kitabu chenye sura tano, basi Azimio kwa Wote laweza kulinganishwa na sura ya 1. Sura ya 2 na ya 3 ni Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni. Na kila moja ya sura ya 4 na ya 5 ina Itifaki ya Hiari.

Ingawa Azimio kwa Wote linaonwa kuwa lina mafaa ya maadili, likiyaambia mataifa mambo yapaswayo kufanya, hati hizi nne za ziada ni makubaliano ya kisheria, zikiambia mataifa mambo ambayo ni lazima yafanye. Ingawa kazi kuhusu hati hizi ilianza katika mwaka wa 1949, ilichukua miongo kadhaa kabla hazijaanza kutenda. Leo, hati hizi nne pamoja na Azimio kwa Wote hufanyiza Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu.

Mbali na huu Mswada wa Kimataifa, UM umeidhinisha zaidi ya mikataba mingine 80 ya haki za kibinadamu. “Kwa hiyo ni kosa kufikiri kwamba mikataba ya haki za kibinadamu katika Mswada wa Kimataifa ndiyo ya maana zaidi,” asema mtaalamu mmoja wa haki za kibinadamu. “Kwa kielelezo, Mkataba wa 1990 juu ya Haki za Mtoto ndiyo hati ambayo imekubaliwa zaidi na ya ulimwenguni pote ya UM, na bado hiyo si sehemu ya Mswada wa Kimataifa. Usemi ‘Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu’ ulitungwa kwa makusudi ya kujulikana badala ya kuwa dhana rasmi. Na utakubali kwamba ni usemi wenye kuvutia.”a

[Maelezo ya Chini]

a Kufikia wakati wa kuandika, mataifa 191 (mataifa wanachama 183 wa UM pamoja na mataifa 8 yasiyokuwa wanachama) yameidhinisha Mkataba wa Haki za Mtoto. Ni nchi mbili tu ambazo hazijauidhinisha: Somalia na Marekani.

[Picha katika ukurasa wa 6]

Elsa Stamatopoulou

[Hisani]

UN/DPI photo by J. Isaac

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki