“Kazi ya Muda Mrefu Yamalizika”
MIAKA 50 iliyopita, mwanamke aliyekuwa katika umri wa miaka 60 alizungumza, ulimwengu ukasikiliza. Ilitukia Paris mnamo Desemba 10, 1948. Kusanyiko Kuu la Umoja wa Mataifa lilikuwa limekusanyika katika jengo la Palais Chaillot lililokuwa limejengwa karibuni wakati msimamizi wa Tume ya UM ya Haki za Kibinadamu alipoamka ili kutoa hotuba. Kwa sauti yenye nguvu, Eleanor Roosevelt, mjane mrefu wa aliyekuwa Rais wa Marekani Franklin D. Roosevelt, aliwaambia hivi wale waliokusanyika: “Leo tumefikia tukio kuu la Umoja wa Mataifa na maisha ya wanadamu, yaani idhini ya Kusanyiko Kuu la Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu.”
Baada ya kusoma mafungu yaliyo wazi sana ya dibaji ya Azimio hilo na mafungu yake 30, Kusanyiko Kuu liliidhinisha hati hiyo.a Kisha, ili kutoa heshima kwa uongozi usio na kifani wa Bi. Roosevelt, washiriki wa UM walimpa heshima huyo “Bibi wa Kwanza wa Dunia,” kama alivyokuwa akiitwa, kwa kumshangilia. Mwishoni mwa siku hiyo, aliandika: “Kazi ya muda mrefu yamalizika.”
Kutoka Maoni Mengi Hadi Azimio Moja
Miaka miwili awali, mnamo Januari 1947, punde tu baada ya kazi ya tume ya UM kuanza, ilikuwa dhahiri kwamba kutunga hati ya haki za kibinadamu ambayo ingekubaliwa na washiriki wote wa UM kungekuwa kazi ngumu sana. Kutoka mwanzo, kutokubaliana kwingi kuliingiza tume hiyo yenye washiriki 18 kwenye mabishano mengi. Mjumbe wa Wachina alihisi kwamba hati hiyo ilipaswa kutia ndani falsafa za Confucius, mshiriki Mkatoliki wa tume hiyo aliendeleza mafundisho ya Thomas Aquinas, Marekani iliunga mkono Mswada wa Haki wa Marekani, na Wasovieti walitaka mawazo ya Karl Marx yatiwe ndani—na haya yalikuwa baadhi ya maoni machache tu yenye kushikiliwa sana yaliyotajwa!
Bi. Roosevelt alivumilia mabishano yenye kuendelea baina ya washiriki wa tume hiyo. Mnamo 1948, wakati alipokuwa akitoa hotuba katika Paris, Sorbonne, alitaja kwamba alifikiri kwamba kulea familia yake kubwa kulimfanya avumilie mpaka mwisho. Hata hivyo, inaripotiwa kuwa aliwafurahisha wasikilizaji kwa kusema kwamba, “kusimamia Tume ya Haki za Kibinadamu kulihitaji saburi hata zaidi.”
Ijapokuwa hivyo, ni wazi kwamba uzoefu aliokuwa nao akiwa mama ulisaidia. Wakati huo, ripota mmoja aliandika kwamba namna Bi. Roosevelt alivyoshughulika na washiriki wa tume ilimkumbusha mama “anayesimamia familia kubwa yenye wavulana wenye kelele, ambao nyakati nyingine ni watukutu lakini wenye moyo mzuri, ambao pindi kwa pindi huhitaji nidhamu imara.” (Eleanor Roosevelt—A Personal and Public Life) Ingawa hivyo, kwa kuongezea uthabiti kwenye uzuri wake, aliweza kuwasadikisha wengine bila kufanya wapinzani wake kuwa maadui.
Tokeo likawa kwamba baada ya miaka miwili ya mikutano, mamia ya marekebisho, maelfu ya taarifa, na duru 1,400 za kupigia kura karibu kila neno na kila kifungu, tume hiyo iliweza kutokeza hati iliyoorodhesha haki za kibinadamu ambazo iliamini kwamba wanaume na wanawake wote ulimwenguni, wanapaswa kuwa nazo. Hati hiyo iliitwa Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu. Hivyo kazi ambayo nyakati fulani ilionekana kuwa haiwezekani, ikakamilishwa.
Mataraja Makuu
Bila shaka, haikutazamiwa kwamba uonezi ungemalizika kwa kuanzishwa kwa hili azimio la haki za kibinadamu. Na bado, kuidhinishwa kwa hilo Azimio kwa Wote kulitokeza mataraja makuu. Msimamizi wa Kusanyiko Kuu la UM wakati huo, Dakt. Herbert V. Evatt wa Australia, alitabiri kwamba “mamilioni ya wanaume, wanawake, na watoto ulimwenguni pote, wanaoishi mbali sana na Paris na New York, wataendea hati hii kwa msaada, mwongozo, na kichocheo.”
Miaka 50 imepita tangu Dakt. Evatt aseme maneno hayo. Katika kipindi hicho, kwa kweli wengi wameliona Azimio hilo kuwa mwongozo na wamelitumia kupima kiwango cha kuheshimu haki za kibinadamu ulimwenguni pote. Walipofanya hivyo, walipata nini? Je, mataifa wanachama wa UM wanafikia kipimo hiki? Hali ya haki za kibinadamu ikoje ulimwenguni leo?
[Maelezo ya Chini]
a Nchi 48 ziliunga mkono uamuzi huo, hakuna iliyopinga. Hata hivyo, leo, mataifa yote 185 ambayo ni wanachama wa UM, kutia ndani yale yaliyojiondoa katika mwaka wa 1948, yameidhinisha Azimio hilo.
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Haki za Kibinadamu Ni Nini?
Umoja wa Mataifa wafasili haki za kibinadamu kuwa “zile haki ambazo tumerithi kiasili na ambazo bila hizo hatuwezi kuishi kama binadamu.” Pia haki za kibinadamu zimefafanuliwa kuwa “lugha ya kawaida ya binadamu”—na kwa kufaa. Kama vile uwezo wa kusema lugha ulivyo sifa ya kurithi ambayo hututofautisha sisi wanadamu, kuna mahitaji na sifa nyingine za kuzaliwa ambazo hututofautisha na viumbe vinginevyo duniani. Mathalani, wanadamu wana uhitaji wa ujuzi, kujieleza vizuri, na hali ya kiroho. Binadamu ambaye ananyimwa kutimiza mahitaji haya ya msingi hulazimika kuishi maisha yasiyostahili binadamu. Ili kuwalinda wanadamu wasinyimwe uhitaji huo, aeleza wakili mmoja wa haki za kibinadamu, “sisi hutumia neno ‘haki za kibinadamu’ badala ya ‘mahitaji ya binadamu’ kwa sababu kwa kusema kisheria neno ‘uhitaji’ si nzito kama neno ‘haki.’ Kwa kutumia neno ‘haki’ tunakuza utoshelezaji wa haki za kibinadamu kuwa kitu ambacho kila binadamu anapaswa kuwa nacho kiadili na kisheria.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]
Azimio la Haki za Kibinadamu kwa Wote
Mwandishi aliye pia mshindi wa Tuzo la Nobel Aleksandr Solzhenitsyn alitaja Azimio kwa Wote kuwa “hati bora kabisa” iliyopata kuandikwa na UM. Kutazama kifupi yaliyomo huonyesha kwa nini wengi hukubaliana naye.
Falsafa ya msingi ya Azimio hilo inapatikana katika Kifungu cha 1: “Wanadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na sawa katika adhama na haki. Wamejaliwa kuwa na uwezo wa kusababu na dhamiri na wanapaswa kutendeana kwa roho ya udugu.”
Kwenye msingi huu, wenye kubuni Azimio hilo walipata vikundi viwili vya haki za kibinadamu. Kikundi cha kwanza kinaonyeshwa katika Kifungu cha 3: “Kila mtu ana haki ya kuishi, kuwa na uhuru na usalama.” Kifungu hiki chaweka msingi wa haki za mtu za kiraia na kisiasa zinazoorodheshwa katika Kifungu cha 4 hadi cha 21. Kikundi cha pili chategemea Kifungu cha 22, ambacho kwa sehemu chasema kwamba kila mtu ana haki za kutambua haki “za lazima za kukuza adhama yake na kuendeleza uhuru wa utu wake.” Kinaunga mkono Kifungu cha 23 hadi 27, kinachoonyesha waziwazi haki za mwanadamu za kiuchumi, kijamii, na kitamaduni. Azimio kwa Wote lilikuwa hati ya kwanza ya kimataifa kutambua kikundi hiki cha pili cha haki kuwa kimetiwa ndani ya haki za msingi za kibinadamu. Pia lilikuwa hati ya kwanza kabisa ya kimataifa kutumia usemi “haki za kibinadamu.”
Mwanasoshiolojia Mbrazili Ruth Rocha aeleza waziwazi kile ambacho Azimio kwa Wote lituambiavyo: “Haidhuru wewe ni wa jamii gani. Haidhuru kama wewe ni mwanamume au mwanamke. Haidhuru unasema lugha gani, dini yako ni gani, maoni yako ya kisiasa ni gani, wewe ni wa nchi gani au familia yako ni gani. Haidhuru kama u tajiri au maskini. Haidhuru unatoka sehemu gani ya ulimwengu; kama nchi yako ni ufalme au ni jamhuri. Haki hizi na uhuru huu wapaswa kufurahiwa na kila mmoja.”
Tangu lianze kutumiwa, Azimio kwa Wote limetafsiriwa katika lugha 200 na limekuwa sehemu ya katiba za nchi nyingi. Hata hivyo, leo, viongozi fulani wanahisi kwamba Azimio hilo lapaswa kuandikwa upya. Lakini Katibu Mkuu wa UM Kofi Annan anapinga jambo hilo. Ofisa mmoja wa UM anamnukuu akisema: “Kama vile hakuna uhitaji wa kuandika upya Biblia au Korani, hakuna uhitaji wa kurekebisha Azimio hilo. Kinachohitaji kurekebishwa, si maandishi ya Azimio kwa Wote, bali mwenendo wa wafuasi wake.”
Katibu Mkuu wa UM Koffi Annan
[Hisani]
UN/DPI photo by Evan Schneider (Feb97)
[Picha katika ukurasa wa 3]
Bi. Roosevelt akishikilia Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu
[Hisani]
Bi. Roosevelt na ishara kwenye ukurasa wa 3, 5, na 7: UN photo