Je, Ni Haki Bila Madaraka?
“KUTAMBUA adhama ya asili na haki sawa na zisizoweza kutenganishwa za washiriki wote wa familia ya kibinadamu ndio msingi wa uhuru, haki na amani ulimwenguni.” Ndivyo isemavyo dibaji ya Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu, ambalo liliadhimisha ukumbusho wake wa miaka 50 mnamo Desemba 1998. Ingawa hivyo, hivi majuzi, marais wa zamani na mawaziri wakuu 24, wanaowakilisha mabara yote, wamependekeza kwamba kwa kuongezea azimio hilo, azimio kwa wote la madaraka ya kibinadamu lapasa kuanzishwa na Umoja wa Mataifa. Kwa nini wengi wanaona uhitaji wa mradi kama huo?
“Haki na madaraka ni mambo yasiyoweza kutenganishwa. Kwa kusikitisha, baada ya nusu karne, jambo hili limesahauliwa au likakosa mafaa. Wengi hudai haki zao bila kuona uhitaji wa kutunza madaraka yanayohusiana nazo,” akaeleza Profesa Jean-Claude Soyer, mshiriki wa Tume ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Athari za kupuuzwa kwa madaraka ni jambo linalohisiwa na wengi. “Kuna tamaa iliyo dhahiri hasa miongoni mwa vijana, ya ono la kupanga kuhusu wakati ujao, namna ya mawazo yanayokubalika ambayo kupitia kwake pupa, ubinafsi na ukosefu wa udugu, mambo ambayo yanaonekana yakiutawala ulimwengu. . . . yatashughulikiwa na kutiishwa. Mjadala huu unaoongezeka kuhusu uhitaji wa maadili ya tufeni pote ni udhihirisho wa wazi kwamba kitu fulani kinakosekana,” lasema gazeti la habari la kila siku la Paris International Herald Tribune. Kwa sababu hiyo, wanasiasa, wanatheolojia, na wanafalsafa wamekuwa wakizungumzia kuhusu “mradi wa maadili kwa wote,” kama uitwavyo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni, ili kujazia pengo na kuamua madaraka ya kibinadamu ni yapi. Hata hivyo, wamekabili magumu fulani.
Ingawa kwa kiasi fulani ni rahisi kuamua ni haki zipi za kibinadamu zipasazo kulindwa, mara nyingi si rahisi kufasiri madaraka ya kibinadamu yapasayo kukubaliwa kwa wote. Hata hivyo, baadhi ya kanuni katika Azimio lililopendekezwa la Madaraka zaweza kupatikana kwenye Kanuni Bora ya sikuzote ambayo hutumika kila mahali iliyotolewa na Yesu miaka ipatayo elfu mbili iliyopita: “Kwa hiyo, mambo yote mtakayo watu wawafanyie nyinyi, lazima mwafanyie wao pia hivyohivyo.”—Mathayo 7:12.
Ingawa mara nyingi Biblia imekuwa ikichochea kulindwa kwa haki za kibinadamu, inakazia wazo la kuchukua daraka la kibinafsi. Mtume Yakobo alitangaza hivi: “Ikiwa mtu ajua jinsi ya kufanya lililo sawa na bado halifanyi, hiyo ni dhambi kwake.” (Yakobo 4:17) Kama vile Yesu alivyotafuta njia za kuwatendea wengine mema, Wakristo wa kweli pia hujaribu kuwatendea mema binadamu wenzao. Bila kuridhika tu na kudhihirisha haki zao, wanaelewa kwamba haki huambatana na madaraka na kwamba kila mmoja wetu ana daraka mbele za Mungu kwa matendo yake mwenyewe.