Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/22 kur. 8-11
  • Haki za Kibinadamu na Makosa Leo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Haki za Kibinadamu na Makosa Leo
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Usawa kwa Wote?
  • Watoto Wasioweza Kufurahia Utoto wa Kawaida
  • Kuchagua na Kubadili Dini
  • Kazi Nyingi Mshahara Kidogo
  • Matibabu ya Kitiba kwa Wote?
  • Mataraja Kutoka Orofa ya 29
    Amkeni!—1998
  • “Kazi ya Muda Mrefu Yamalizika”
    Amkeni!—1998
  • Haki za Kibinadamu kwa Wote—Uhalisi wa Ulimwenguni Pote!
    Amkeni!—1998
  • Je, Ni Haki Bila Madaraka?
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/22 kur. 8-11

Haki za Kibinadamu na Makosa Leo

HIVI karibuni watetezi wa haki za kibinadamu walitimiza jambo kubwa. Kwanza, waliunganisha mashirika zaidi ya 1,000 katika nchi 60 katika harakati iliyoitwa Kampeni ya Kimataifa ya Kupiga Marufuku Makombora ya Ardhini (ICBL). Kisha, wakahimiza mkataba wa kimataifa wa kupiga marufuku silaha hizi. Baada ya hilo, harakati ya ICBL na mkurugenzi wake asiyechoka, mtetezi Mmarekani Jody Williams, akashinda Tuzo la Amani la Nobel la 1997.

Ingawa hivyo, mafanikio kama haya, hufuatana na matangazo yenye kuamsha fikira. Kama lisemavyo Human Rights Watch World Report 1998, haki za kibinadamu za kotekote zingali “zinashambuliwa.” Na si kwamba udikteta wa hali ya chini na usiofaa ndio unaolaumiwa tu. “Mataifa yenye nguvu,” yasema ripoti hiyo, “yalionyesha mwelekeo dhahiri wa kupuuza haki za kibinadamu zilipohitilafiana na mapendezi yao ya kiuchumi—taabu iliyo kawaida katika Ulaya na Marekani.”

Kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote, ni vigumu kupuuza ukiukaji wa haki za kibinadamu. Hali yao mbaya ya kila siku ingali ina ubaguzi, umaskini, njaa, mnyanyaso, kubakwa, kutenda watoto vibaya, utumwa, na kifo chenye jeuri. Kwa wahasiriwa hawa hali zenye kutumainiwa zilizoahidiwa katika mikataba mingi ya haki za kibinadamu haziwezi kufikiwa wala hazina maana yoyote kwao. Kwa kweli, kwa wanadamu wengi, hata haki za msingi zinazoorodheshwa katika vifungu 30 vya Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu zimekosa kutimizwa. Kwa kielelezo, fikiria kifupi jinsi haki nyingine bora zilizotajwa katika Azimio zinavyotumika katika maisha ya kila siku.

Usawa kwa Wote?

Wanadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na sawa katika adhama na haki.—Kifungu cha 1.

Mswada wa kwanza wa Kifungu cha 1 cha Azimio kwa Wote ulisema: “Wanaume wote . . . ni sawa.” Hata hivyo, ili kuhakikisha kwamba taarifa hii haitaeleweka kumaanisha kwamba wanawake hawatiwi ndani, washiriki wa kike kwenye tume iliyotayarisha mswada huu walisisitiza kwamba lugha hiyo ibadilishwe. Walishinda, na “wanaume wote . . . ni sawa” ikawa “wanadamu wote . . . ni sawa.” (Italiki ni zetu.) Lakini je, kubadilishwa kwa lugha ya kifungu hiki kulibadili fungu la wanawake?

Mnamo Desemba 10, 1997, Siku ya Haki za Kibinadamu, Mke wa Rais wa Marekani, Hillary Clinton, aliuambia UM kwamba ulimwengu unaendelea “kuwatenda wanawake kama raia duni.” Alitoa vielelezo kadhaa: Kati ya watu maskini ulimwenguni, asilimia 70 ni wanawake. Thuluthi mbili ya watoto milioni 130 ulimwenguni wasio na uwezo wa kwenda shuleni ni wasichana. Thuluthi mbili za watu milioni 96 wasiojua kusoma na kuandika ni wanawake. Pia wanawake huteseka sana kutokana na jeuri ya kinyumbani na ya kingono, ambayo ingali, aongezea Bi. Clinton, “mmojawapo wa ukiukaji wa haki za kibinadamu usioripotiwa zaidi na ulioenea sana ulimwenguni.”

Wanawake fulani hufanyiwa jeuri hata kabla hawajazaliwa. Hasa katika nchi fulani za Asia, mama fulani hutoa mimba za watoto wa kike kwa sababu wanapendelea wana badala ya mabinti. Katika sehemu fulani kupendelea wana kumefanya mbinu ya kutambua jinsia ya mtoto iwe biashara inayovuma. Kliniki moja ya kugundua jinsia ilitangaza huduma zake kwa kudokeza kwamba ilikuwa bora kutumia dola 38 sasa ili kuharibu kijusu cha kike kuliko kutumia dola 3,800 baadaye kumlipia mahari. Matangazo ya biashara kama hayo hufanya kazi. Uchunguzi mmoja uliofanywa katika hospitali moja kubwa ya Asia ulipata kwamba asilimia 95.5 ya vijusu vilivyotambuliwa kuwa vya kike vilitolewa. Kupendelea wana ni zoea lililoko katika sehemu nyingine za ulimwengu vilevile. Mtu mmoja aliyekuwa bingwa wa zamani wa ndondi Marekani alipoulizwa alikuwa baba wa watoto wangapi, alijibu: “Mvulana mmoja na makosa saba.” Kichapo cha UM Women and Violence chasema kwamba “kubadili mtazamo na nia ya watu kuelekea wanawake kutachukua muda mrefu—wengi wanaamini angalau kizazi kimoja, na labda muda mrefu zaidi.”

Watoto Wasioweza Kufurahia Utoto wa Kawaida

Hakuna mtu atakayewekwa utumwani au kutumikishwa; utumwa na biashara ya utumwa itazuiwa katika namna zake zote.—Kifungu cha 4.

Kinadharia, utumwa umekwisha. Serikali zimetia sahihi mikataba mingi sana inayofanya utumwa uwe haramu. Hata hivyo, kulingana na Shirika la Uingereza la Kupinga Utumwa, linalojulikana kuwa shirika la haki za kibinadamu la zamani zaidi, “kuna watumwa wengi leo kuliko wakati mwingine wowote.” Utumwa wa siku hizi unatia ndani ukiukaji wa namna mbalimbali wa haki za kibinadamu. Kulazimisha watoto wafanye kazi kunasemekana kuwa namna moja ya utumwa wa siku hizi.

Kielelezo kimoja chenye kuhuzunisha ni cha mvulana mmoja wa Amerika Kusini anayeitwa Derivan. ‘Mikono yake midogo imechunika ngozi kwa kushughulika na majani magumu ya mkonge, ambao hutokeza katani za kutengenezea magodoro. Kazi yake ni kubeba majani mpaka kwenye ghala na kuyabeba hadi kwenye mashine ya utengenezaji kwa umbali wa meta 90. Ufikapo mwisho wa kila siku ya kazi ya saa 12, anakuwa amebeba tani moja ya majani. Derivan alianza kufanya kazi alipokuwa na umri wa miaka mitano. Leo ana umri wa miaka 11.’—World Press Review.

Ofisi ya Shirika la Kimataifa la Wafanyakazi inakadiria kwamba watoto robo bilioni walio na umri wa kati ya miaka 5 na 14 hufanyizwa kazi leo—wafanyakazi wadogo wengi wanaokaribia kutoshana na jumla ya idadi ya watu wa Brazili na Mexico! Wengi wa watoto hawa wasiofurahia utoto humenyeka kwenye migodi, wakikokota karai zilizojaa makaa ya mawe; hutembea kwa taabu katikati ya matope ili kuvuna mazao; au huinama kwenye vitanda vya kufuma ili kutengeneza mazulia manene madogo. Hata watoto wanaoanza kutembea—wenye umri wa miaka mitatu, minne, na mitano—hufungwa pamoja katika vikundi ili kulima kwa plau, kupanda mbegu, na kuokota masazo ya mashamba kuanzia mapambazuko hadi machweo. “Watoto,” asema mwenye shamba mmoja katika nchi fulani ya Asia, “wanagharimu kiasi kidogo kuliko trekta na wana akili kuliko fahali.”

Kuchagua na Kubadili Dini

Kila mtu ana haki ya uhuru wa kuwaza, dhamiri na dini; haki hii yatia ndani uhuru wa kubadili dini.—Kifungu cha 18.

Mnamo Oktoba 16, 1997, Kusanyiko Kuu la UM lilipokea “ripoti ya muda juu ya kuondolewa kwa kila namna ya kutovumilia dini.” Ripoti hiyo iliyotayarishwa na Mwandishi Maalumu wa Tume ya Haki za Kibinadamu, Abdelfattah Amor, yaorodhesha ukiukaji unaoendelea wa Kifungu cha 18. Ikizungumza kuhusu nchi nyingi, ripoti hiyo yanukuu visa vingi sana vya ‘kusumbuliwa, kutishwa, kutendwa vibaya, kukamatwa, vizuizi, kutoweka, na mauaji.’

Vivyo hivyo, 1997 Human Rights Reports, iliyokusanywa na shirika la Marekani la Demokrasia, Haki za Kibinadamu, na Wafanyakazi, yataja kwamba hata nchi ambazo zimezoea demokrasia kwa muda mrefu “zimejaribu kuzuia uhuru wa mchanganyiko wa vikundi vidogo-vidogo vya kidini, wakivijumlisha pamoja kuwa ‘madhehebu.’” Mielekeo kama hiyo inatokeza hangaiko. Willy Fautré, msimamizi wa shirika la Haki za Kibinadamu Lisilo na Mipaka lenye makao makuu Brussels, asema: “Uhuru wa kidini ni mmojawapo wa vionyeshi bora vya hali ya ujumla ya uhuru wa kibinadamu katika jamii yoyote.”

Kazi Nyingi Mshahara Kidogo

Kila mtu anayefanya kazi ana haki ya kulipwa ifaavyo ili apate kujiruzuku pamoja na familia yake katika njia inayofaa adhama ya binadamu.—Kifungu cha 23.

Wakataji wa miwa katika Karibea waweza kuchuma dola tatu kwa siku, lakini gharama ya kukodi nyumba na vifaa huwafanya wawe na deni la wenye mashamba hayo. Kwa kuongezea, hawalipwi pesa taslimu bali kwa vocha. Na kwa kuwa duka la kampuni ya wenye mashamba ndilo duka la pekee ambalo wakataji wa miwa wanaweza kuliendea, wanalazimika kununua mafuta yao ya kupikia, mchele, na maharagwe huko. Hata hivyo, kama gharama za huduma za kukubali vocha za wafanyakazi, duka hilo hupunguza thamani ya vocha hiyo kwa kiwango cha asilimia 10 hadi 20. Bill O’Neill, naibu wa mkurugenzi wa Kamati ya Mawakili ya Haki za Kibinadamu, alisema hivi kwenye tangazo la redio ya UM: “Mwishoni mwa msimu, hawana pesa zozote zilizosalia kwa majuma na miezi ya kazi ngumu sana yenye jasho. Hawana akiba yoyote, na wameweza tu kujiruzuku kwenye huo.”

Matibabu ya Kitiba kwa Wote?

Kila mtu ana haki ya kuwa na kiwango cha maisha kinachofaa kwa ajili ya afya na hali njema yake na familia yake, kutia ndani chakula, makao, na matibabu.—Kifungu cha 25.

‘Ricardo na Justina ni wakulima maskini wa Amerika ya Latini wanaoishi kilometa zipatazo 80 kutoka jiji lililo karibu. Wakati binti yao mchanga Gemma alipougua, walimpeleka kwenye kliniki ya kibinafsi iliyokuwa karibu, lakini wafanyakazi wa huko walikataa kumtibu mtoto huyo kwa sababu ilikuwa wazi kwamba Ricardo hangeweza kulipia gharama hiyo. Siku iliyofuata, Justina alikopa pesa kutoka kwa majirani ili asafiri kwa magari ya umma kwenda kwenye jiji. Hatimaye Justina na mtoto huyo walipofika kwenye hospitali ya serikali ya jiji hilo, Justina aliambiwa kwamba hakuna vitanda na kwamba arudi keshoye asubuhi. Kwa kuwa hakuwa na jamaa zake walioishi katika jiji hilo na hakuwa na pesa za kukodisha chumba, usiku alijilaza juu ya meza katika soko la umma. Justina alimshikilia mtoto huyo kwa ukaribu ili amfariji na kumtunza, lakini haikusaidia. Usiku huo Gemma mchanga alikufa.’—Human Rights and Social Work.

Ulimwenguni pote, mtu 1 kati ya 4 hujikimu kwa dola moja (ya Marekani) kwa siku. Wanakabili utatanishi uleule kama Ricardo na Justina: Matibabu ya kibinafsi yanapatikana lakini hayawezi kugharimiwa, huku matibabu ya umma yanaweza kugharimiwa lakini hayapatikani. Kwa kuhuzunisha, ingawa zaidi ya watu bilioni moja ulimwenguni walio maskini wamepokea ‘haki ya kupata matibabu,’ bado hawawezi kupata manufaa za kitiba.

Orodha ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu haina mwisho. Hali kama hizo zilizotajwa juu zaweza kuzidishwa mara mamia ya mamilioni. Licha ya jitihada kubwa sana za mashirika ya haki za kibinadamu na licha ya kujitoa kwa maelfu ya watetezi ambao kwa kweli huhatarisha uhai wao ili kuboresha hali ya wanaume, wanawake, na watoto ulimwenguni pote, haki za kibinadamu kwa wote zingali ndoto tu. Je, zitapata kuwa halisi? Bila shaka zitakuwa hivyo, lakini lazima mabadiliko fulani yatukie kwanza. Makala ifuatayo itachunguza mabadiliko mawili.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]

Courtesy MgM Stiftung Menschen gegen Minen (www.mgm.org)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]

UN PHOTO 148051/J. P. Laffont—SYGMA

WHO photo/PAHO by J. Vizcarra

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki