Vijana Huuliza. . .
Akina Mama Wasioolewa Waweza Kushughulikiaje Hali Yao Vizuri Iwezekanavyo?
HISIA-MOYO za Linda zilitia ndani kushtuka, kukana, kuhofu, kukasirika, kuwa hoi, na kukata tamaa.a Uchunguzi ukawa umethibitisha alichohofia zaidi—alikuwa na mimba ya miezi mitatu. Akiwa hajaolewa na mwenye miaka 15 tu, Linda ni mmoja tu wa matineja milioni moja kila mwaka katika Marekani wapatao mimba. Hata hivyo, mimba za matineja ni tatizo la tufeni pote, linalohusu makabila yote na tabaka zote za uchumi na jamii.
Wasichana fulani matineja huwazia kwamba mimba itawaokoa na maisha ya nyumbani yasiyofurahisha au iimarishe uhusiano na mvulana-rafiki. Wengine huona mtoto mchanga kuwa ishara ya hadhi au kitu chao wenyewe cha kushika na kupenda. Hata hivyo, utambuzi wa magumu halisi ya kuwa mzazi mmoja tu huondosha upesi mawazo hayo ya kudhaniadhania. Mama asiyeolewa hulazimika kufanya machaguo magumu, mara nyingi yenye maumivu makali. Huenda pia akaminyana na matatizo ya kiuchumi, mtamauko wa kihisia-moyo, upweke, na mikazo ya kulea mtoto bila mwenzi wa ndoa. Basi, Muumba wetu ana sababu nzuri aamurupo Wakristo ‘wakimbie uasherati,’ kutia na ngono kabla ya ndoa.—1 Wakorintho 6:18, NW; Isaya 48:17.
Ukosefu wa adili katika ngono hauvumiliwi miongoni mwa Mashahidi wa Yehova. (1 Wakorintho 5:11-13) Hata hivyo, miongoni mwao mna akina mama wachanga wasioolewa. Wengine wao walipata mimba kabla ya kujifunza viwango vya Mungu. Wengine walilelewa wakiwa Wakristo, lakini wakatumbukia katika ukosefu wa adili. Wengine wao, wakiisha kutiwa nidhamu na kutaniko, hutubu juu ya makosa yao. Ni msaada na mwelekezo gani ambao Neno la Mungu latolea vijana hao?b
Je, Nifunge Ndoa na Baba-Mtoto?
Biblia huelewesha wazi kwamba kutoa mimba ni dhidi ya sheria ya Mungu. (Kutoka 20:13; linganisha Kutoka 21:22, 23; Zaburi 139:14-16.) Pia hufundisha kwamba mama aliye peke yake ana daraka la kuandalia mtoto wake, ijapokuwa hali zilizofanya achukue mimba si za kutamanika. (1 Timotheo 5:8) Katika visa vilivyo vingi, ni bora zaidi yule msichana ajilelee mtoto mwenyewe badala ya kumtoa achukuliwe na watunzaji wa malezi ya kujichagulia.c
Kwa sababu ya magumu ambayo kujilelea mtoto kwaweza kuleta, mama fulani huenda wakahisi lingekuwa jambo la hekima kufunga ndoa na baba-mtoto. Lakini baba wengi matineja hawahisi wakiwa sana na wajibu wa kutunza mtoto wala mama yake. Zaidi ya hilo, baba wachanga walio wengi bado ni wa umri wa kwenda shuleni na hawajaajiriwa kazi. Kuingilia kile ambacho mtafiti mmoja hukiita “ndoa iwezayo kukosa uthabiti ifungwayo ili tu kuzuia uzazi wa nje ya ndoa” huenda kukaharibu mambo zaidi. Kumbuka pia kwamba Biblia huelekeza Wakristo wafunge ndoa “katika Bwana tu.” (1 Wakorintho 7:39) Akitambua hili, Linda (aliyetajwa mwanzoni) aliamua dhidi ya kufunga ndoa na baba mwenye miaka 18 wa mtoto wake. “Mvulana huyo hakupendezwa kamwe na Mungu wala Biblia.”
Hii haimaanishi kwa lazima kutohusisha kabisa baba huyo. Kadiri mtoto awavyo na umri mkubwa zaidi, huenda akataka kumjua baba yake mzazi. Au huenda ikawa kwamba yule baba mchanga au wazazi wake wahisi wajibu fulani wa kiadili kuwa na uhusiano fulani na mtoto au kuandaa utegemezo wa kifedha. Hata hivyo, huenda wazazi wa msichana wakapendelea kwamba asionane tena na yule mwanamume kijana. (1 Wathesalonike 4:3) Ingawa hivyo, katika mabara fulani mahakama zimewapa baba wazazi wasiofunga ndoa haki za kisheria kama zile za baba waliofunga ndoa. Kwa hiyo kudumisha uhusiano wenye uungwana pamoja na baba asiyefunga ndoa na familia yake huenda kukaepusha pambano kali la kutetea haki ya kutunza mtoto.d Ingawa mwonano fulani na yule baba mchanga huenda ukawa lazima, haupasi kuwa katika kikao cha kimahaba au kiwezacho kuchangia kuharibu maadili. Kwa kawaida yafaa kuwe na usimamizi mkomavu.
Kupata Msaada
Chasema hivi kitabu Surviving Teen Pregnancy: “Uamuapo kukaa na mtoto wako na kumlea, papohapo umechagua utu mzima. . . . Wachagua kuacha nyuma sehemu yako mwenyewe iliyokuwa ya kutojali zaidi, iliyokuwa na wajibu au madaraka machache zaidi.” Hivyo mzazi tineja huhitaji msaada na utegemezo. Kusoma fasihi ya kitiba ifaayo (ambayo huenda ikapatikana kwa urahisi katika maktaba ya umma) huenda kukasaidia sana mama mchanga mwenye wasiwasi asitawishe uhakika katika stadi zake za kutunza mtoto.
Utegemezo wa wazazi hasa ni wa thamani kubwa. Mama ya mtu huenda akawa mgodi hakika wa kuendea ili kufukua maarifa ya kulea mtoto. Ni kweli, huenda ikawa hisia ngumu kuomba msaada. Huenda wazazi wa msichana wakawa bado wameumia hisia na wamekasirika. Huenda pia wakahofu kwamba ile mimba itakuwa na matokeo hasi juu ya mtindo-maisha wao wenyewe. “Wazazi wangu waliudhika kwa sababu walikuwa na mambo mengi sana waliyotaka kufanya,” akumbuka Donna mwenye miaka 17. “Sasa wao wasema hawawezi kwa sababu ya mimi kupata mtoto huyu.” Baada ya muda wazazi walio wengi humudu hisia-moyo zao zenye maumivu na huwa na nia ya kusaidia kwa njia fulani. Kijana mwenye toba aweza kupunguza sana mahangaiko kwa kukubali kwamba amesababisha maumivu na kuomba radhi kwa moyo mweupe.—Linganisha Luka 15:21.
Namna gani wazazi wa msichana wakikataa kusaidia au ikiwa hawana kabisa uwezo wa kumruhusu aendelee kuishi nao? Katika mabara fulani ambako umma huandaliwa usaidizi wa serikali, mama asiyeolewa huenda asiwe sana na la kufanya ila kujifaidi na huo—angalau pale mwanzoni. Biblia huruhusu Wakristo watumie maandalizi hayo. Hata hivyo, hii itamaanisha kuishi kwa kufuata sana utumizi wa fedha uliopangwa kwa uthabiti sana. “Yaonekana tatizo langu kubwa zaidi ni fedha,” asema Sharon mwenye miaka 17. “Naweza kununua chakula na nepi, na basi.” Baada ya muda huenda ikawezekana kufanya kazi ya kuajiriwa. Haitakuwa rahisi kusawazisha umama, kazi, na utendaji mbalimbali wa kiroho, lakini wengine wameweza kufanya hivyo.
Kutumia Hekima na Utambuzi Katika Kukaa Pamoja
Wazazi wa mtu wakikubali, huenda kukawa na faida halisi za kukaa nyumbani badala ya yeye kujasiria kwenda kukaa peke yake. Kwa kawaida kuishi nyumbani huwa na gharama chache zaidi. Zaidi ya hilo, mazingira ya nyumbani yaliyozoelewa huenda yakatoa hisia ya usalama na himaya. Pia kukaa nyumbani huenda kukafanya iwe rahisi zaidi msichana kuendelea na shule. Kwa kuhitimu shule ya sekondari, msichana huboresha sana nafasi zake za kuepuka maisha ya umaskini.e
Bila shaka, kushiriki nyumba moja na vizazi vitatu kwaweza kufanyiza mkazo na mbano kwa kila mtu ahusikaye. Mama aliye peke yake huenda akalazimika kukabiliana na makao yaliyosongamana. Wazazi na ndugu za mtu huenda wakalazimika kuzoea kukatizwa usingizi na kilio cha mtoto mchanga. Huenda kawaida ya familia ile ikavurugwa. Lakini Mithali 24:3 husema: “Nyumba hujengwa kwa hekima, na kwa ufahamu huthibitika.” Ndiyo, wahusika wote wakionyesha upendo na ufikirio usio na ubinafsi, mkwaruzano ndani ya familia waweza kupunguzwa.
Pia matatizo yatatokea yule mama mchanga akijaribu kuepuka kubeba furushi lake mwenyewe la madaraka na kumtarajia nyanya ndiye afanye kazi yote. (Linganisha Wagalatia 6:5.) Au huenda ikawa kwamba nyanya mwenye makusudi mazuri ajitwalia mwenyewe utunzaji wa mjukuu wake. Chasema hivi kitabu Facing Teenage Pregnancy: “Akina nyanya waleao mtoto wa binti asiyeolewa kama kwamba ni wao wenyewe huenda wakaongezea kutopatana kwa familia na kufanya mtoto avurugike juu ya aliye mzazi wake halisi.” Ingawa msaada na utegemezo wa mzazi-mkuu ni wa thamani kubwa, Maandiko hugawia wazazi daraka la kulea mtoto. (Waefeso 6:1, 4) Basi uwasiliano wa wazi na ushirikiano waweza kusaidia sana kuzuia hali za kutoelewana.—Mithali 15:22.
Si Wewe Peke Yako
Ingawa kuwa na mtoto bila ndoa ni jambo gumu, huo sio mwisho wa maisha ya mtu. Mungu ‘husamehe kabisa’ wale watubuo juu ya makosa yao. (Isaya 55:7) Kutafakari juu ya hili kwaweza kusaidia mama aliye peke yake ashinde hisia za kujikirihi ziwezazo kumpata nyakati fulani. Ahisipo amevunjika moyo, aweza kumwegemea Yehova na kumfikia katika sala. Aweza pia kuomba sana msaada wa Mungu katika kulea mtoto wake.—Linganisha Waamuzi 13:8.
Yehova huandaa utegemezo kupitia kutaniko la Kikristo pia. Ingawa Mashahidi wa Yehova hawakubalii ukosefu wa adili, wao huwapa ufikirio wale ambao kwa kutubu hufanya mabadiliko katika maisha zao ili kumpendeza Mungu. (Warumi 15:7; Wakolosai 1:10) Watu fulani katika kutaniko huenda wakasukumwa kutafuta njia za busara za kutoa usaidizi fulani wenye kutumika kwa mzazi aliye peke yake. (Linganisha Kumbukumbu la Torati 24:17-20; Yakobo 1:27.) Angalau kabisa, wao waweza kuandaa urafiki na usikizi uhitajiwapo. (Mithali 17:17) Ingawa wale wazazi walitenda dhambi nzito, mtoto hana lawama. Kwa hiyo kutaniko laweza kusaidia ikiwa mama aonyesha mtazamo ufaao.
Ni afadhali zaidi kama nini kutovunja sheria za Mungu pale mwanzoni! Lakini wakosaji ambao wametubu juu ya mwendo wao mpotovu, na wametenda kulingana na toba yao, waweza kuwa na uhakikisho wa kwamba Yehova atawasaidia washughulikie hali yao vizuri iwezekanavyo.
[Maelezo ya Chini]
a Baadhi ya majina yamebadilishwa.
b Makala hii haielekezwi kwa majeruhi waliotendwa ngono ya kiukoo au unajisi, ingawa baadhi ya mambo yaliyo humu yaweza kuthibitika kuwa yenye msaada kwa hao.
c Ona “Vijana Huuliza . . . Mimba za Utineja—Msichana Apaswa Kufanya Nini?” katika toleo letu la Oktoba 8, 1990.
d Ona “Nani Apewe Mtoto?” katika toleo letu la Oktoba 22, 1988 (Kiingereza).
e Baadhi wametumia kwa faida programu za serikali zifundishazo stadi za kupata kazi. Huenda hata kukawa na programu zitoleazo watu kazi ya kutunza kitoto kichanga palepale mama alipo huku yeye akiendelea kuhudhuria masomo.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Mama asiyeolewa huhitaji msaada na utegemezo