Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 10/8 kur. 26-28
  • Mimba za Utineja—Msichana Apaswa Kufanya Nini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mimba za Utineja—Msichana Apaswa Kufanya Nini?
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ‘Je! Tufunge Ndoa?’
  • Utoaji Mimba—Maoni ya Biblia
  • ‘Siwezi Kumfanyia Yaliyo Bora Kabisa’
  • Je, Utoaji-Mimba—Ndio Suluhisho?
    Amkeni!—1995
  • Akina Mama Wasioolewa Waweza Kushughulikiaje Hali Yao Vizuri Iwezekanavyo?
    Amkeni!—1994
  • Akina Baba Wanaotoroka Wajibu—Je, Kweli Waweza Kutoroka?
    Amkeni!—2000
  • Kukabili Magumu ya Kuwa Mama Mchanga
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 10/8 kur. 26-28

Vijana Wauliza . . .

Mimba za Utineja—Msichana Apaswa Kufanya Nini?

Mimba za utineja na utoaji mimba ni matatizo yenye kuenea katika tufe lote. Na ingawa walio wengi wa wasomaji wetu ni vijana Wakristo ambao kwa hekima hujiepusha na ngono kabla ya ndoa, Amkeni! husomwa pia na mamilioni ya watu mmoja mmoja wa hali zote za maisha. Kwa hiyo mazungumzo yanayofuata yamekusudiwa kusaidia kijana yeyote anayekabili utatanisho wa kuwa mzazi asiyefunga ndoa, na wakati ule ule kukazia matokeo yenye msiba ambayo hutokana na ngono kabla ya ndoa.

“NILIKUWA na miaka 15 na mwenye mimba,” akasema Ann. “Sikujua la kufanya—kutoa mimba, kupeleka mtoto huyo akawe wa kulelewa na mtu mwingine, au vipi.” Ann alikuwa mmoja tu wa wasichana matineja zaidi ya milioni moja katika United States walioshika mimba mwaka huo.

Ingawa katika visa vichache vyenye msiba msichana hushika mimba kwa sababu ya kulalwa kinguvu, mimba za utineja kwa kawaida huwa ni tokeo la ushiriki wa nia katika ngono kabla ya ndoa.a Vyovyote vile, mimba hukabilisha msichana asiyeolewa machaguo kadhaa yenye maumivu makali: Je! afunge ndoa? Je! apeleke mtoto huyo akawe wa kulelewa na mtu mwingine? Je! jibu ni kutoa mimba? Yakubalika kwamba huhitajiwa watu wawili kutunga mtoto, na kwa haki zote baba ya mtoto huyo apaswa kuchukua furushi lake la daraka. (Ona sanduku.) Lakini mara nyingi sana, msichana (labda kwa msaada wa wazazi wake) ndiye huachwa afanye machaguo hayo magumu. Na uamuzi afanyao utakuwa na tokeo la kudumu juu ya hali ya kimwili, ya kihisia-moyo, na ya kiroho, yake na ya mtoto anayebeba.

‘Je! Tufunge Ndoa?’

Wengi wangeweza kuhisi kwamba utatuzi ulio bora kabisa ungekuwa kufunga ndoa na baba ya mtoto huyo. Ingawaje, kufanya hivyo kungeondolea msichana na familia yao aibu mbele ya watu, na kungeruhusu mtoto huyo alelewe na wazazi wawili. Lakini ndoa si dawa ya kuponya matatizo yote. Kwanza, ni toba ya kimungu tu iwezayo kurekebisha kosa hilo machoni pa Mungu.b (Isaya 1:16, 18) Tena, kuharakisha kuingia katika ndoa kungeweza kwa kweli kuongezea matatizo ya msichana. Kwa kuwa mvulana na msichana wangali katika “uzuri wa ujana,” huenda wakawa hawana kabisa ukomavu wa kihisia-moyo ambao wahitajiwa ili kufanikisha ndoa. (1 Wakorintho 7:36) Yaelekea kwamba mvulana huyo si Mkristo wa kweli na hivyo hafai kuwa mwenzi wa ndoa.—1 Wakorintho 7:39.

Dakt. Arthur Elster aonelea zaidi hivi: “Mara nyingi uzazi usiokomaa husababisha mababa hawa waache shule, na hivyo huwaweka katika hali ya kutoweza sana kupata kazi.” Magumu ya kiuchumi yanayofuata yaweza kuharibu ndoa. Kwa kweli, uchunguzi fulani-fulani wadai kwamba kuna kiasi cha talaka za kuanzia asilimia 50 hadi 75 miongoni mwa ndoa ambazo hutokezwa ghafula na mimba kabla ya ndoa!

Ndoa ni hatua nzito na haipasi kukimbiliwa. (Waebrania 13:4) Baada ya kufikiria jambo hilo, huenda wahusika wote wakaafikiana kwamba halingekuwa hekima kufunga ndoa, kwamba ingekuwa afadhali msichana alee mtoto huyo nyumbani kwa usaidizi wa familia yao badala ya kumlea katika ndoa yenye matatizo chungu nzima.

Utoaji Mimba—Maoni ya Biblia

Msichana mmoja mchanga alisema: ‘Mimi nataka kufanya mengi sana maishani mwangu, na mtoto mchanga hangekuwa na mahali pa kumfaa humo.’ Hivyo utoaji mimba ndilo chaguo la wasichana karibu nusu milioni kila mwaka katika United States pekee. Lakini je! yafaa au hata ni haki kutoa mimba ya uhai wa mtoto kwa sababu yeye ‘hana mahali pa kumfaa’ katika mipango ya kibinafsi?

Angalia isemayo Biblia kwenye Kutoka 21:22, 23 kuhusu uhai wa mtoto ambaye hajazaliwa: “Watu waume wakiteta pamoja, wakamwumiza mwanamke mwenye mimba hata akaharibu mimba, tena yasiwe madhara zaidi; sharti atatozwa mali kama atakavyomwandikia mumewe huyo mwanamke . . . Lakini kwamba pana madhara zaidi [“yenye msiba wa kifo,” NW, kwa mama au kwa mtoto ambaye hajazaliwa], ndipo utatoza uhai kwa uhai.” Ndiyo, kuua mtoto aliyekuwa hajazaliwa kulionwa kuwa uuaji!

Ni kweli kuwa madaktari fulani hudai kwamba mtoto ambaye hajazaliwa ni kijusi tu, au tishu ya kijusi—si mtu. Lakini Mungu husema vingine. Yeye huona kiinitete kuwa mtu mwenye upambanufu wa pekee, binadamu hai! (Zaburi 139:16) Je! mtu angeweza kutoa mimba ya uhai usiozaliwa na abaki katika upendeleo wa Mungu, “anayewapa wote uzima”?—Matendo 17:25.

Kitabu Growing Into Love hutoa hoja nyingine dhidi ya utoaji mimba: “Ingawa matokeo ya kuchukua mimba husahilishwa [hupunguziwa uzito] kwa kutoa mimba, jambo ambalo hutokea wakati wa kukomesha mimba huwa la kufadhaisha na kuhangaisha sana. . . . Tineja . . . huenda akadhani kwamba kijusi ndivyo kilivyo hasa—kijusi tu . . . Lakini hakuna kiasi chochote cha maelezo ya kisheria yawezayo kumfanya yeye asahau, katika kina kirefu cha ndani yake mwenyewe, kwamba kijusi alichokichukua mimba kilikuwa na uwezekano wa kupata maisha.”

Kijana mmoja jina lake Linda alipata jambo hilo kuwa kweli. Kwa kuhofu kwamba kupata mtoto mchanga kungeleta aibu juu ya familia yake, alitoa mimba. Ingawa hivyo, baada ya upasuaji huo yeye akumbuka hivi: “Nilianza kutetemeka vibaya sana nikashindwa kudhibiti hali. Nami nikaanza kulia, na kwa ghafula nikazinduka na kuelewa kabisa, kuona nilikuwa nimefanya nini hasa. Nilikuwa nimeua uhai wa mtoto wangu aliyekuwa hajazaliwa, binadamu mwingine!” Sasa Linda ana maoni gani juu ya utoaji mimba? “Lilikuwa ndilo kosa baya kabisa la maisha yangu yote.”

‘Siwezi Kumfanyia Yaliyo Bora Kabisa’

Mama fulani wasioolewa huchagua kupeleka mtoto wao akawe wa kulelewa na mtu mwingine. Mara nyingi wao huhisi kama Heather, msichana aliyenukuliwa katika gazeti Seventeen, aliyesema hivi: “Nyakati fulani mimi hutatizika vya kutosha kushughulikia mambo yangu mwenyewe, sembuse kushughulikia mtoto mdogo. Mimi huhangaikia sana watoto, nami ni kipenzi cha watoto wadogo, lakini nilijua kwamba singeweza kumfanyia mtoto huyo yaliyo bora kabisa.”

Ni kweli kwamba kupeleka mtoto akawe wa kulelewa na mtu mwingine ni bora kuliko kukomesha uhai wake kwa kutoa mimba. Na yakiriwa kwamba, tazamio la msichana mchanga asiye na ujuzi kulea mtoto akiwa peke yake laweza kuonekana kuwa lenye kulemea mno. Kama vile mama mmoja asiyeolewa alivyoiambia Amkeni!: “Mtu hujitwalia daraka kubwa, tena kubwa ambalo ni la upweke na lenye majaribu na ambalo hutaka kujidhabihu sana.” Ingawa hivyo, kumbuka kwamba Mungu huchukua mzazi kuwa mwenye daraka la ‘kuwatunza walio wake.’ (1 Timotheo 5:8) Katika hali zilizo nyingi, ingekuwa bora kabisa msichana kujilelea mtoto yeye mwenyewe.

Kwa hiyo Ann, aliyetajwa mwanzoni, alifanya chaguo la hekima—ingawa si rahisi kamwe. “Niliamua kukaa na mtoto,” ndivyo asema. “Wazazi wangu walinisaidia na bado hunisaidia.” Yakubalika kwamba kuwa mama mseja ni jambo gumu. Lakini si jambo lisilowezekana, na mama wengi wachanga wamekuwa wazazi hodari. Ndivyo ilivyo hasa ikiwa mama huyo asiyeolewa aazimia kwa sala kulea mtoto wake “katika nidhamu na rekebisho la akilini la Yehova.”c (Waefeso 6:4, NW) Huenda wazazi wa kimalezi wakaweza kuandaa vitu bora vya kimwili. Lakini je! wataandaa mwelekezo wa kiroho ambao mtoto huhitaji ili akue akawe mwenye kumpenda Mungu wa kweli, Yehova?—Kumbukumbu 6:4-8.

Kumbuka, pia, kwamba ingawa mzazi mseja huenda asiweze kumpa mtoto wake vitu bora kabisa vya kimwili, aweza kumpa kitu ambacho umaana wacho wazidi hivyo vingine kwa mbali: upendo. “Chakula cha mboga penye mapendano; ni bora kuliko ng’ombe aliyenona [“nyama iliyo laini kabisa,” Today’s English Version] pamoja na kuchukiana.”—Mithali 15:17.

Bila shaka, mteseko huo wa bure waweza kuzuiwa mtu akiepuka dhambi ya uasherati pale mwanzoni.d Lakini ikiwa msichana amekosea katika jambo hilo, hahitaji kukata shauri kwamba maisha yake yamefikia mwisho. Kwa kutenda kwa hekima, aweza kuepuka kuongezea kosa lake na afanye hali yake iwe bora kwa kadiri awezavyo. Kwa kweli, yeye aweza kupata msaada na tegemezo la Mungu mwenyewe, ambaye ‘huwasamehe kabisa’ wale wageukao kutoka mwendo wenye makosa.—Isaya 55:7.

[Maelezo ya Chini]

a Ukosefu wa adili katika ngono hauvumiliwi miongoni mwa Mashahidi wa Yehova, kama vile haukuvumiliwa miongoni mwa Wakristo katika karne ya kwanza. (1 Wakorintho 5:11-13) Hata hivyo, wakosaji waweza kupata usaidizi wa wazee wa kundi wenye upendo. (Yakobo 5:14, 15) Kwa kutubu juu ya mwenendo wao wenye kosa, watu hao waweza kuwa na shangwe ya kupata msamaha wa Mungu na kundi la Kikristo pia.

b Chini ya Sheria ya Kimusa, Mungu alitaka mwanamume aliyekuwa ametongoza bikira amwoe. (Kutoka 22:16, 17; Kumbukumbu 22:28, 29) Lakini sheria hiyo ilitumikia mahitaji ya watu wa Mungu chini ya hali za siku na enzi hizo. Na hata ilipokuwa hivyo, haikuwa moja kwa moja kwamba sasa ndoa itafanyika, kwa kuwa baba angeweza kuikataza.—Ona jarida letu andamani Mnara wa Mlinzi, Novemba 15, 1989, “Maswali Kutoka kwa Wasomaji.”

c Mashahidi wa Yehova wamesaidia familia nyingi zianzishe programu ya maagizo ya ukawaida ya Biblia. Uwasiliano waweza kufanywa pamoja nao kwa kuandikia wachapishaji wa gazeti hili.

d Ona sura ya 24 ya kitabu Questions Young People Ask—Answers That Work, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Mimba za Utineja—Matokeo kwa Wavulana

Kwa kusukumwa na hofu—au kutojali mambo kwa sababu ya ubinafsi—wavulana fulani ambao wamekuwa baba mtoto bila kufunga ndoa hujaribu kuepa madaraka yao kabisa kabisa. Alisema hivi mvulana mmoja ambaye msichana rafiki yake alishika mimba: “Mimi nilimwambia tu, ‘Baki salama.’”

Uzuri ni kwamba, wavulana walio wengi huonekana kuwa wakitaka angalau kuhusika kwa kadiri fulani na watoto wao. Ionekanapo kuwa haifai kufunga ndoa (kama iwavyo mara nyingi), wengi hujitolea kusaidia kifedha. Baadhi yao hata hujitolea kushiriki katika kule kutunza mtoto siku baada ya siku. Lakini mara nyingi jitihada hizo huthibitika kuwa za muda mfupi, zikivurugwa na uwezo haba wa mvulana kuchuma pesa za kutosha na ukosefu wake mkubwa wa subira na ustadi ambao wahitajiwa ili kutimiza madai ya kitoto kidogo.

Pia, nyakati fulani wazazi wa msichana hupinga vikali kumwacha mvulana awe na mishughuliko yoyote zaidi na binti yao, wakihofu kwamba hiyo ingeweza kutokeza mwenendo mbaya zaidi wa kingono—au ndoa isiyo ya ukomavu. Huenda wakamnyima ushiriki wowote katika maamuzi yapasayo kufanywa kuhusu mtoto huyo, labda hiyo ikimlazimisha asimame kando akiwa hoi huku ile mimba ikitolewa au mtoto akipelekwa akawe wa kulelewa na mtu mwingine, hiyo ikimaliza nafasi yoyote ya mvulana kuweza wakati wowote kushiriki katika maisha ya mtoto ambaye yeye amekuwa baba yake. Kwa upande mwingine, huenda kwa kweli mvulana akaruhusiwa kusitawisha ufungano kwa mtoto wake—ndipo tu kifungo hicho kije kukatizwa bila huruma wakati msichana afungapo ndoa kisha fungu la ubaba lichukuliwe na mwanamume mwingine.

Basi, pasipo shaka akina baba wasiofunga ndoa hulipa bei kubwa kwa mwenendo wao wa kutojali madaraka. Baba mmoja asiyefunga ndoa mwenye umri wa miaka 16 asema hivi: “Kuna hisia nyingi mno ambazo huwezi kamwe kushughulika nazo. Ni kama kwamba wasali ili urudie hali uliyokuwa nayo hapo mbele, lakini huwezi kwa vyovyote.”—Gazeti “’Teen,” Novemba 1984.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki