Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 10/22 kur. 26-27
  • Kinanda cha Mianzi—Ajabu ya Kimuziki ya Filipino

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kinanda cha Mianzi—Ajabu ya Kimuziki ya Filipino
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kukijenga Kinanda
  • Kuokoka Shida Kubwa
  • Kurudishwa
  • Nzumari za Nyasi za Visiwa vya Solomon
    Amkeni!—2002
  • Sauti za Ndege Waimbaji
    Je, Ni Kazi ya Ubuni?
  • Je, Unajua Tofauti?
    Amkeni!—2002
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2011
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 10/22 kur. 26-27

Kinanda cha Mianzi—Ajabu ya Kimuziki ya Filipino

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA FILIPINO

VINANDA vimekuwako kwa namna moja au nyingine kwa miaka zaidi ya 2,000. Mbinu za kuvitengeneza zimekuwa za namna-namna, lakini vinanda vyote vina safu za virija vilivyo sehemu ya mtambo wa kuvumisha sauti. Kwa jumla virija hivi huwa vimefanywa kwa mbao na metali. Hata hivyo, kinanda tutakacho kukueleza juu yacho kina virija vilivyofanyizwa kwa mianzi hasa. Jumla ya 832 kati ya virija vyacho 953 vya kuvumisha sauti ni mianzi. Vile vingine ni metali. Kwa kuongezea, kuna virija fulani vya kutia mapambo tu.

Kinanda cha mianzi hufanya kazi namna gani? Kanuni ni ileile ya vinanda vingine vya virija. Virija vya namna mbili hutumiwa, na upepo hupepewa ndani kufanyiza mivumo ya kimuziki. Virija-mpulizo—vyenye matundu ya nusu-duara karibu na sehemu zao za kuungana na mitambo yenye vibonyezo vya kinanda—hutoa sauti sawasawa na filimbi. Virija vya matete—vyenye kifaa cha ndani cha kutetemesha sauti—hutokeza mvumo kama klarineti au saksofoni. Kwa kuwa virija vilivyo vingi ni vya mianzi, kinanda hiki huweza kutoa mivumo bora ya sauti.

Kukijenga Kinanda

Ujenzi wa kinanda hiki cha mianzi ulianzwa katika 1816 na mishonari Mhispania, Diego Cera. Kwa nini mianzi ilitumiwa? Kwa kufikiria kwamba eneo hilo lina umaskini likilinganishwa na mengine, labda sababu moja ilikuwa uhitaji wa kutumia vifaa visivyo vya gharama kubwa. Zaidi ya hilo, bila shaka mtengeneza-kinanda hicho alitamani kutumia vifaa vizuri vya kienyeji.

Katika 1816, mianzi ilikatwa kisha ikafukiwa chini ya mchanga wa ufuo wa bahari kwa karibu mwaka mmoja. Zile zilizodumu baada ya kuachiwa hali hiyo ya kuingiliwa na wadudu na hali mbaya za hewa zilionwa kuwa na ubora wa kudumu na kutumiwa kuunda kinanda. Muda wa miaka kadhaa iliyofuata, zile sehemu mbalimbali za kinanda ziliunganishwa. Kiwiliwili cha kinanda hicho kilipomalizwa katika 1821, kilitangazwa kuwa “kilicho bora zaidi na cha aina yacho ya kwanza nchini.”

Kuokoka Shida Kubwa

Maisha ya kinanda cha mianzi hayakuwa rahisi. Mwaka 1829 uliona matetemeko ya ardhi katika mji wa Las Piñas ambako ndiko kwenye kinanda hicho. Paa ya nyumba kilimokuwa iliharibiwa, na yaelekea kinanda hicho kiliachwa wazi kwenye hali za hewa kwa kitambo fulani. Katika 1863 tetemeko la ardhi lenye nguvu zisizo za kawaida lilisababisha kuharibika zaidi kwa kinanda hicho. Virija fulani vilibadilishwa, lakini wadudu wakaviumbua kwa kipindi fulani. Katika 1880 tetemeko jingine la ardhi lenye msiba mkubwa lililiharibu vibaya jengo kilimokuwa kinanda hicho, na kimbunga kikapiga kabla ya jengo hilo kurekebishwa kikamili. Kufikia wakati huo vipande mbalimbali vya kinanda hicho vilitawanywa-tawanywa.

Marekebisho fulani yalijaribiwa muda wa miaka hiyo, lakini jaribio moja la jinsi hiyo likatokeza uharibifu wa daima. Mrekebishaji mmoja alikata kwa msumeno visehemu vya virija hivyo vya mianzi ili aingize vali fulani za kurekebishia sauti. Hii ilibadili daima kiwango cha sauti ya ala hiyo. Na, zijapofanywa jitihada za marekebisho, kinanda hicho chaendelea kuharibika.

Pia kinanda hicho kiliendelea kuwako baada ya vita. Las Piñas ilikuwa tamasha ya vita vidogo kati ya Wafilipino na Wahispania katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1890, na kati ya Wafilipino na Wamarekani wakati wa ile Vita ya Wafilipino na Wamarekani. Hata hivyo, rekodi za kuanzia 1911 hadi 1913 zaonyesha kwamba wageni walikuja kuona kinanda hicho.

Miaka 1941 hadi 1945 ilileta vita ya ulimwengu ya pili Ufilipino. Wakati Wajapani walipokaa katika nchi hiyo, kinanda hicho kilipewa uangalifu na Marquess Y. Tokugawa, mtu wa ukoo wa Maliki Hirohito. Alipanga kuwe na marekebisho nusunusu, lakini baada ya hapo ni machache sana yaliyofanywa kwa miaka mingi.

Halafu, katika miaka ya 1970, watu walisisitiza sana kirudishwe katika hali ya zamani. Kati ya mamia ya virija vya mianzi, 45 havikuwapo, na 304 havikuwa vikifanya kazi. Kiota cha ndege kilipatikana ndani ya kimoja. Je, lolote lingeweza kufanywa kufanya kinanda hicho kirudie kiwango cha kuweza kufanya kazi?

Kurudishwa

Mradi wa kurudishwa ulianzishwa katika Machi 1973, huku shirika la kigeni lenye sifa likikabidhiwa kazi hiyo. Virija hivyo vilisafirishwa Japani, na sehemu ile nyingine ya kinanda hicho ilisafirishwa Ujerumani. Huko, chumba maalumu kilijengwa kwa kuiga halihewa ya Ufilipino. Kazi ya kukirudisha katika hali yacho ya zamani ilianzia katika chumba hiki.

Mradi ulikuwa kufanya kikaribie kufanana kwa kadiri iwezekanavyo na ule muundo wa awali. Mwishowe, marekebisho yalimalizwa. Virija vilivyorekebishwa katika Japani vilipelekwa kwa ndege Ujerumani. Kinanda kamili kiliunganishwa upya na kujaribiwa. Halafu, katika Februari 18, 1975, kikafurahisha masikio ya wasikilizaji Wajerumani katika tamasha ya muda wa saa moja.

Upesi baada ya hapo kinanda hicho kiliingizwa katika masanduku 12, kisha chote hicho kikiwa na kilo 5,626 kikasafirishwa kurudishwa Ufilipino kwa hisani ya ndege moja ya Ubelgiji. Kilipewa mapokezi makubwa katika Las Piñas, mji ambamo kingepewa makao. Watu elfu 30 walitazama gwaride lililo kamili kwa magari ya ubebaji yenye violezo vya matukio ya historia ya ala hiyo.

Kufikia Mei 9, 1975, kinanda hicho cha mianzi kikawa tayari kwa onyesho lacho la mzinduo. Mpiga-kinanda Mjerumani alionyeshwa pamoja na wanamuziki Wafilipino huku kinanda hicho cha mianzi kikijulishwa upya kwa Wafilipino.

Je, wewe huthamini kipawa cha muziki ambacho Muumba wetu alitupa? Je, ungependa kusikia kitu tofauti kidogo? Ukija kupata fursa ya kukisikia kinanda cha mianzi katika Las Piñas, bila shaka utafurahia ajabu hii ya kimuziki ya Kifilipino.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki