Wakristo Waikabili Tena Mahakama Kuu ya Yerusalemu
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA ISRAELI
YESU alisimama mbele ya Sanhedrini, mahakama kuu zaidi katika Yerusalemu, akifanyiwa kesi kuhusu uhai wake. Ajapopatwa na msongo huu, aliwakilisha Ufalme wa Mungu bila hofu. (Mathayo 26:57-68) Mnamo majuma machache baada ya kujaribiwa kwa Yesu, wafuasi wake wa karibu zaidi walisimama mbele ya mahakama kuu hiihii. Hapo walitoa ushahidi wa nguvu nyingi kwa ajili ya Ufalme wa Mungu na Mfalme wao mwekwa rasmi.—Matendo 4:5-21.
Siku kadhaa baadaye, mitume walipoburutwa tena mbele ya Sanhedrini, kulikuwako badiliko lisilotarajiwa. Kujapokuwa na msongo mwingi sana wa marika, Gamalieli, mmojapo washirika wenye kustahiwa zaidi wa mahakama hiyo, alisema kijasiri kwa niaba ya wanafunzi wa Yesu. Kutokana na mjiingizo huu wa kushangaza, mitume waliwekwa huru.—Matendo 5:27-42.
Mionekano hii mbele ya mahakama ilitimiza maneno ya Yesu kwenye Mathayo 10:16-18: “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu . . . Watawapeleka mabarazani . . . mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.” Ingawa wafuasi wa Yesu walieleweka kimakosa mara nyingi, walikuja kujulikana vema kotekote katika Israeli. Maelfu ya Wayahudi wa karne ya kwanza walikubali ujumbe wa Yesu. (Matendo 4:4; 6:7) Yote haya yalitokana na kuhubiri kwa bidii kwa wanafunzi wa Kiyahudi wa Yesu, kutia na kuonekana-onekana kwao bila hofu mbele ya mahakama.
Katika Israeli leo, ni watu wachache kwa kulinganisha wajuao Mashahidi wa Yehova, ambao idadi yao kwa sasa ni ndogo kuliko 500 katika taifa la watu karibu milioni 5. Lakini katika 1993, si kwamba tu kesi ya Shahidi kijana mmoja ilileta uangalifu mkubwa kwenye utendaji wao bali pia ilikazia uhusiano wa kihistoria usio na kifani kati ya upendeleo usiofaa na mnyanyaso ambao wote Wayahudi na Mashahidi wa Yehova wamepatwa nao.
Ubishano Ulianzaje?
Ariel Feldman, mhamiaji Mrusi Myahudi wa miaka 17 katika Israeli, anayeishi katika Haifa, alikuwa mwanafunzi mwenye msimamo ulioheshimika kimasomo na alipendwa sana na walimu na pia na wanafunzi wenzake.
Kutokana na mazungumzo yasiyotazamiwa barabarani wakati wa ile Vita ya Ghuba ya Ajemi, Ariel na familia yake walianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Ariel alichunguza na kulinganisha kikamilifu mafundisho ya kidini ya Kiyahudi na maelezo ya Biblia yaliyotolewa kwake na Mashahidi wa Yehova. Akiwa mwenye akili ya kuchukua mambo kwa uzito, Ariel alifanya maendeleo ya kasi katika funzo lake la Biblia na alikuwa mshiriki wa kwanza wa familia yake kubatizwa kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova.
Yote haya hayakumtokezea ugumu wowote katika mafunzo yake ya shule. Hata hivyo, katika mwaka uliotangulia kuhitimu masomo yake ya juu, shule yake iliamua kuanzisha programu ya majaribio ya kutayarisha wanafunzi kwa utumishi wa kijeshi. Askari walitoa mafunzo, na programu ilitia ndani kuzoea vikao na mbinu za mapambano. Kwa kuhisi kwamba kushiriki kimatendo katika mtaala huu kungevunja dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia na msimamo wake wa kutokuwamo akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, Ariel alifanya jitihada za usababu wa kiasi kueleza msimamo wake kwa mkuu wa shule. (Isaya 2:2-4) Alieleza kwa staha kwamba alikuwa tayari kushiriki katika utendaji mwingine wowote wa shule katika kipindi hicho lakini kwamba hangeweza kutenda dhidi ya imani zake.
Ingawa hapo kwanza mkuu wake wa shule alikuwa ameonyesha uelewevu fulani kumwelekea, mwanamke huyo aliamua kwamba ombi lake lilizidi kiasi ambacho angeweza kuruhusu. Alimpa mkataa: Ama ashiriki kimatendo katika hayo mazoezi ya kutangulia kuingia jeshini ama afukuzwe shuleni. Ariel hangeweza kuvunja dhamiri yake. Siku ya Januari 31, 1993, miezi michache tu kabla ya mitihani yake ya mwisho, alifukuzwa rasmi shuleni bila kupewa chaguo lolote.
Utetezi Kutoka Chanzo Kisichotarajiwa
Ariel alitafuta msaada kwa Shirika la Haki za Wananchi katika Israeli. Walikuwa tayari kufuatia kesi yake, wakimtolea usaidizi wa kisheria bila malipo. Serikali ya Kiyahudi ya Israeli ya ki-siku-hizi ni demokrasi. Ingawa lile julisho rasmi la uhuru wa Israeli halina katiba ya kuhakikisha kabisa haki za watu mmoja-mmoja, hilo hutekeleza uhuru wa dini na uhuru wa dhamiri. Kulikuwa hakuna kanuni ya kisheria katika Israeli inayohusisha kufukuzwa shuleni kwa sababu za imani ya kidini.
Magazeti yalianza kupendezwa na kisa hicho. Akifuata ushauri wa kisheria, Ariel hakuruhusu waandishi wa habari kufanya mahoji, akipendelea kesi yake ihukumiwe katika chumba cha mahakama badala ya katika “mahakama” ya maoni ya umma. Hata hivyo, mkuu wa shule alifanya haraka kutetea vitendo vyake kuwa vyenye haki katika hoji moja. Katika gazeti Hadashot la Februari 9, 1993, si kwamba tu alieleza maoni yake kwamba msimamo wa kidini wa mwanafunzi huyo ulikuwa wenye kuudhi Serikali ya Israeli na wazalendo wote bali pia alitumia fursa hiyo kusema kijasiri dhidi ya Mashahidi wa Yehova wakiwa tengenezo, akisema: “Utendaji wao huficha mambo ya kichinichini, ni mchafu kabisa, ni wa kisirisiri. Wao hufanya kama pweza mkubwa mwenye kunyoosha madole yake kujaribu kunyaka walio dhaifu.”
Waisraeli wengi wangeweza kuona kwamba maoni ya mkuu huyo yalikuwa na mwelekeo wa upendeleo usiofaa. Tom Segev, mwanajarida-mwanahistoria Mwisraeli ambaye amefanya utafiti mwingi juu ya lile Teketezo la Umati, ndiye hasa aliyehangaishwa zaidi na mahoji hayo. Yalimkumbusha mtazamo ulioonyeshwa na watu fulani katika Ujerumani ya Nazi, ambao, kwa kuchochewa na mashtaka bandia dhidi ya Wayahudi, walitokeza wazi upendeleo wao katika mojapo matendo makubwa ya uhalifu ulio mbaya zaidi katika historia ya wanadamu. Maoni ya Segev yalikuwa kwamba hatari kubwa zaidi kwa Serikali ya Israeli ilikuwa, si katika msimamo wa kudhamiria wa yule mwanafunzi kijana, bali katika kielelezo cha kutovumilia maoni ya wengine kilichoonyeshwa na mkuu wa shule. Mwanamume huyo alisukumwa kuandika makala akitetea haki za Mashahidi wa Yehova. (Ona sanduku, ukurasa 15.)
Kufuatia makala ya Segev, wengine walisema kwa ujasiri pia. Mkaaji mmoja wa Yerusalemu, ambaye alikuwa amefungwa katika kambi moja wakati wa Vita ya Ulimwengu 2 kwa sababu ya kuwa Myahudi alimwandikia mhariri barua akiukumbuka mwenendo mwema wa Mashahidi wa Yehova waliokuwa katika kambi ileile kwa sababu ya kukataa kwao kutumikia jeshi katika jeshi la Ujerumani.
Kwa kuwa yule mwanafunzi Shahidi kijana hakutaka kukubali mahoji, waandishi wa habari waligeukia washirika wengine wa kutaniko. Ingawa hawakueleza kihususa kisa cha Ariel kabla hakijapelekwa mahakamani, walifurahi kutoa habari juu ya imani za Mashahidi wa Yehova na utendaji wao katika Israeli. Hii iliongoza kwenye uandikaji wa makala zenye upendelevu katika magazeti ya Israeli na pia hoji moja la redio pamoja na mmoja wa wazee wenyeji. Wengi walisikia juu ya Mashahidi wa Yehova kwa mara ya kwanza kutokana na utangazaji huu usio wa kujiombea.
Ile Siku Katika Ile Mahakama ya Yerusalemu
Tawi la Haifa la Shirika la Haki za Wananchi katika Israeli lilijaribu-jaribu kusababu na yule mkuu, Baraza la Elimu, na Wizara ya Elimu katika Yerusalemu. Hata hivyo, jitihada zote hizi hazikupata maitikio ya kuridhisha. Siku ya Machi 11, 1993, ombi rasmi lilitokezwa kwa niaba ya Ariel Feldman kwenye Mahakama Kuu Zaidi katika Yerusalemu, mahakama iliyo kuu zaidi katika Israeli ya ki-siku-hizi.
Machi 15, 1993, iliwekwa kuwa tarehe ya usikizi wa kwanza wa kesi. Wanasheria kutoka lile Shirika la Haki za Wananchi katika Israeli waliwakilisha kesi ya Ariel dhidi ya Baraza la Elimu, mkuu wa shule, na manispaa ya jiji la Haifa. Mahakimu Waisraeli watatu wa Mahakama Kuu Zaidi waliketi kwenye usikizi wa kwanza wa kesi.
Wakili wa Serikali alitokeza suala hilo kuwa moja ambalo lingedhoofisha mamlaka ya shule ikiwa mwanafunzi huyo angeruhusiwa “kuamrisha” ni masomo yapi angeyashiriki au hangeyashiriki. Waliiomba mahakama iunge mkono uamuzi wao wa kwamba chini ya hali zozote mwanafunzi huyo asiruhusiwe kukanyaga uwanja wa shule.
Wanasheria wa haki za wananchi walitokeza suala hilo kuwa jambo la haki za msingi za uhuru wa kuabudu na uhuru wa dhamiri uliokuwa umevunjwa na jinsi shule ilivyoshughulikia jambo hilo. Mahakimu hao walitokeza maswali kuhusu kanuni za Mashahidi wa Yehova ili waelewe sababu ya msimamo wa huyo mwanafunzi kijana. Pia walitokezewa habari nyingi katika lile ombi rasmi lililoandikwa kuhusu kesi kama hiyo ulimwenguni pote ambamo mahakama kuu zilikuwa zimeamua kwa kuwapendelea Mashahidi wa Yehova.
Katika muhtasari wao mahakimu walitaarifu kwamba pande zote mbili zilikuwa zikipigania kanuni fulani. Hata hivyo, wakati wa kupima ni upande upi ungepatwa na dhara kubwa zaidi kwa kuiacha hali ibaki vile ilivyokuwa, ilikuwa wazi kwamba ni huyo mwanafunzi. Mahakimu walionyesha mshangao kuhusu mwenendo wa yule mkuu na Baraza la Elimu, wakiwapa siku kumi za kueleza sababu ya vitendo vyao kwa maandishi. Mahakama ilitoa agizo la kipindi hicho cha kungojea ikitaka kwamba Ariel Feldman akubaliwe kurudi kwenye nyanja za shule amalizie mwaka wa shule na kwamba asizuiliwe kufanya mitihani yake ya mwisho.
Siku kadhaa kabla ya ule usikizi wa mwisho, uliopangiwa Mei 11, 1993, Baraza la Elimu lilitupa mashtaka yao dhidi ya Ariel Feldman. Kutokana na hilo, ule usikizi wa mwisho ulifutwa, yale masuala ya msingi ya kesi hayakuamuliwa kamwe na mahakama, na hakuna kanuni yoyote ya ushurutisho wa kisheria iliyowekwa. Ingawa hii yaacha mambo wazi kwa majadiliano zaidi ya kisheria, Mashahidi wa Yehova walithamini ule mtazamo wenye usababu wa kiasi ulioonyeshwa na mahakimu wa Mahakama Kuu Zaidi ya Israeli.
Masomo Yaliyofunzwa
Kuanzia siku ya Yesu hadi sasa, Mashahidi wa Yehova wamekutana na upinzani na upendeleo mbaya ambao umewaleta kwenye mahakama zilizo kuu zaidi za nchi nyingi. Kesi hizi hugeuka kuwa ‘ushahidi kwa mataifa.’ (Mathayo 10:18, NW) Hata iwapo Mashahidi wake katika bara fulani ni wachache, Yehova aweza kuhakikisha kwamba jina lake lapata kujulikana kwa mapana. Na sawa na vile ilivyokuwa katika karne ya kwanza kuhusu ule mjiingizo wa kushangaza wa Gamalieli yule mshirika mstahiwa wa Sanhedrini, Mungu leo aweza kutokeza tegemezo kwa watu wake kutoka vyanzo visivyotarajiwa.
[Sanduku katika ukurasa wa 15]
“Jambo Ajualo Mkuu wa Shule Juu ya Mashahidi wa Yehova”
(Madondoo kutoka makala ya Tom Segev katika Ha’aretz, Februari 12, 1993)
“Katika taifa lililo na kila kitu, kuna Mashahidi wa Yehova walio Waisraeli pia. Wao si wengi, na si watu wengi wamesikia juu yao, ujapokuwa uhakika wa kwamba katika Israeli, kama ilivyo katika kila nchi, wao hujitahidi kupata wafuasi wa kufuata kanuni zao, kwa kutumia neno lililoandikwa na pia kwa mdomo. Kwa njia fulani walimfikia mwanafunzi yule katika shule ya Hugim. Kwa kuwa alichagua kufuata kanuni za harakati hiyo, alikataa kushiriki katika masomo ya siha ya mwili shuleni yafanywayo kabla ya kuingia jeshini. Yule mkuu hakukubali kumwachilia asihusike katika masomo haya. Ikiwa nilimwelewa kwa usahihi, mkuu huyo amwona kijana huyo kuwa tisho kwa wakati ujao wa Dini ya Sayuni. Juma hili mkuu huyo alinieleza hivi: ‘Sisi ni shule ya Kisayuni; sisi hufundisha watoto wawe na uaminifu-mshikamanifu kwa Serikali na taifa.’ . . .
“Rina Shmueli, wa Shirika la Haki za Raia katika Haifa, alijaribu kusadikisha mkuu huyo akubali haki ya mwanafunzi huyo ya kutii dhamiri yake na kumwachilia asiwe katika mazoezi yafanywayo kabla ya kuingia jeshini; hili lingaliweza kuwa somo linalofaa sana la kuvumilia maoni ya wengine na la demokrasi. Lakini mkuu huyo wa kike alishikilia msimamo wake. Ana maoni ya kwamba sisi tunashughulika na dhehebu hatari lipatalo washiriki walo kwa njia ya ushawishi. . . .
“Hii ilinikumbusha jambo fulani lisilo jema sana. Kwa hiyo nikapigia mkuu huyo simu nikamwuliza alilolijua hasa juu ya Mashahidi wa Yehova. Akasema kwamba hakujua mengi lakini kwamba alikuwa amesikia kwamba wao ni watendaji katika nchi nyinginezo pia, naye mwenyewe alikutana nao katika Kanada na Ujerumani. Nikamwuliza kama alijua waliyowatenda katika Ujerumani. ‘Sijui, wala sitaki kujua,’ mkuu huyo akajibu.
“Labda Shule ya Sekondari ya Hugim ina maktaba, na labda katika maktaba hiyo wana The Encyclopedia of the Holocaust, iliyohaririwa na Israel Gutman. Ikiwa hawana nakala, yawapasa kununua moja. Chini ya kichwa ‘Wanafunzi wa Biblia Wenye Bidii,’ mkuu atapata kwamba Wanazi walipeleka Mashahidi wa Yehova kwenye kambi za mateso.”