Kwa Nini Kuna Mahakama ya Kimataifa Ulaya?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UHOLANZI
WAKATI mwenye gereji moja katika sehemu ya kaskazini ya Uholanzi aliponyimwa kibali cha kuuza gesi-oevu, lililomaanisha pia kwamba hakuruhusiwa kubadili mitambo ya magari itumie gesi-oevu, alipiga vita vya kisheria kwa muda mrefu katika mahakama mbalimbali ili ageuze vizuizi vilivyokuwa vimewekwa na serikali. Kwa wakati huo, akafilisika.
Akihisi kuwa alikuwa amenyimwa haki na mahakama za Uholanzi, alikata rufani kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu katika Strasbourg. Katika 1985 Mahakama ya Ulaya iliamua kwa kumpendelea. Huyo mwenye gereji aliona uamuzi huo wa mahakama kuwa ushindi mkubwa wa kiadili kwa kuwa, kama alivyosema, ‘ilithibitisha kwamba kwa muda wote huo nilikuwa na haki.’
Yeye ni mmoja wa raia wengi katika Ulaya ambao kwa miongo iliyopita wamekata rufani kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Mahakama hii iko tayari kusikia si malalamishi ya watu mmoja-mmoja katika Ulaya tu bali pia malalamishi ya nchi kadhaa dhidi ya nchi nyingine zihisipo haki za msingi za kibinadamu hazikuheshimiwa. Ongezeko katika idadi ya kesi zinazofikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa huonyesha ile tamaa ya raia na baadhi ya serikali ya kupata haki.
Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu
Katika 1950 serikali kadhaa za Ulaya, zilizokuwa zimeunganishwa katika lile Baraza la Ulaya zilikutana Roma, zikaamua kufanya mkataba ambao ungehakikishia raia zazo na wageni katika maeneo wanayomiliki kisheria haki na uhuru fulani. Baadaye haki nyingine zikaongezwa, na wakati huohuo idadi yenye kuongezeka ya serikali zikajiunga na Mkataba wa Ulaya zikitarajia kupata ulinzi wa haki za kibinadamu na uhuru wa msingi. Baadhi ya haki hizi zinahusu ulinzi wa uhai na kuzuia kuteseka, na nyingine zinahusika na maisha ya familia pamoja na uhuru wa kidini, wa usemi, wa maoni, wa kukusanyika na kushirikiana. Wale ambao haki zao zinavunjwa wanaweza kutoa malalamishi yao dhidi ya serikali kwa katibu-mkuu wa Baraza la Ulaya.
Tangu kuanzishwa kwa mahakama hiyo, malalamishi zaidi ya 20,000 yametolewa. Mahakama hiyo huamuaje ni kesi zipi itakazosikiza? Kwanza, juhudi za kupatanisha hufanywa. Hilo lishindwapo na lalamishi laonekana kuwa lenye uzito, linapelekwa mbele ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu katika Strasbourg. Ni kama asilimia 5 tu ya malalamishi yanayofika kwenye mahakama hiyo. Kufikia mwishoni mwa 1995, mahakama hiyo ilikuwa imefikia maamuzi 554. Ingawa uamuzi wa mahakama katika kesi ya lalamishi la mtu mmoja hushurutisha serikali inayohusika, katika hali ambayo lalamishi linatolewa na serikali moja au serikali kadhaa si rahisi. Katika kisa hicho, uwezekano uliopo ni kwamba serikali ambayo imehukumiwa itachagua mwendo utakaoifaidi kisiasa badala ya kukubaliana na madai ya mkataba huo. Ingawa Mahakama ya Haki ya Kimataifa katika Hague hushughulikia ubishi mbalimbali kati ya mataifa, lakini ile Mahakama ya Ulaya hutoa uamuzi hata katika kesi kati ya raia na mataifa.
Ushindi Mbalimbali Wenye Kupendelea Uhuru wa Ibada Katika Ulaya
Katika 1993 Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilifikia maamuzi mawili yenye umaana kwa kupendelea uhuru wa ibada. Kesi ya kwanza ilihusisha mkazi wa Ugiriki, Minos Kokkinakis. Akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alikuwa amekamatwa zaidi ya mara 60 tangu 1938, akalazimishwa kwenda mbele ya mahakama ya Ugiriki mara 18, naye alikuwa amefungwa zaidi ya miaka sita.
Katika Mei 25, 1993, Mahakama ya Ulaya iliamua kwamba serikali ya Ugiriki ilikuwa imevunja uhuru wa kidini wa Minos Kokkinakis aliyekuwa wakati huo mwenye umri wa miaka 84 na kumlipa ridhaa ya dola 14,400 kwa ajili ya hasara alizopata. Mahakama hiyo ilikataa madai ya serikali ya Ugiriki ya kwamba Kokkinakis na Mashahidi wa Yehova kwa ujumla walitumia mbinu za kulazimisha watu walipokuwa wakizungumza na wengine juu ya dini yao.—Kwa habari zaidi, ona Mnara wa Mlinzi la Septemba 1, 1993, kurasa 27-31.
Katika kesi ya pili, Mahakama ya Ulaya iliamua kwa kumpendelea Ingrid Hoffmann wa Austria. Kwa kuwa alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova baada ya kuolewa, alinyimwa haki ya kuwalea watoto wake wawili, kufuatia talaka yake. Mbeleni mahakama za chini zilikuwa zimempa mgawo wa kuwalea, lakini Mahakama Kuu ikampa mumewe aliyekuwa Mkatoliki mgawo huo. Mahakama hiyo ilifanya uamuzi huo kwa msingi wa sheria ya Austria isemayo kwamba watoto lazima walelewe katika dini ya Katoliki ikiwa wazazi walikuwa Wakatoliki wakati wa kuoana isipokuwa wote wawili wanakubali kubadilisha dini yao. Aliyekuwa mume wake alisisitiza kwamba kwa kuwa Ingrid alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, hangeweza kuwalea watoto katika njia ya kawaida iliyo timamu. Katika Juni 23, 1993, Mahakama ya Ulaya iliamua kwamba Austria ilikuwa imefanya ubaguzi dhidi ya Bi. Hoffmann kwa msingi wa dini yake nao walikuwa wamevunja haki yake ya kuilea familia yake. Alilipwa ridhaa kwa hasara alizopata.—Kwa habari zaidi, ona Amkeni! la Oktoba 8, 1993, ukurasa 15.
Maamuzi haya yanavutia watu wote wanaopenda uhuru wa dini na usemi. Rufani zinazokatwa kwenye mahakama za kimataifa zaweza kuchangia kulindwa kwa haki za msingi za raia. Ni vyema pia kutambua mipaka ya mashirika ya kisheria. Licha ya makusudio mema, hayawezi kamwe kuhakikisha kuwepo kwa amani yenye kudumu na kuheshimiwa kikamili kwa haki za kibinadamu.