Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 3/22 kur. 14-16
  • Mashahidi wa Yehova Watetewa Katika Ugiriki

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mashahidi wa Yehova Watetewa Katika Ugiriki
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uhuru wa Dini, na Haki za Kibinadamu
  • Mashahidi wa Yehova Hawawezi Kukomeshwa
  • Uhuru wa Kidini Wategemezwa
  • Si Mzaha Tu
  • Kwa Nini Kuna Mahakama ya Kimataifa Ulaya?
    Amkeni!—1996
  • Ushindi Katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Kulinda Kisheria Habari Njema
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Mahakama ya Ulaya Yasahihisha Ukiukwaji wa Sheria
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 3/22 kur. 14-16

Mashahidi wa Yehova Watetewa Katika Ugiriki

NA MLETA-HABARI WA AMKENI!

KASISI wa Othodoksi katika kijiji cha Gazi katika Krete alisema hivi katika mojawapo ya mahubiri yake: “Mashahidi wa Yehova wana jumba humu kijijini mwetu. Nataka mniunge mkono katika kuwaondosha.” Jioni moja siku chache baadaye, madirisha ya Jumba la Ufalme yalivunjwa-vunjwa na jumba lilifyatuliwa risasi na watu wasiojulikana. Basi suala la uhuru wa kidini likazuka tena Ugiriki.

Visa hivyo vilifanya wanne kati ya Mashahidi wa huko, Kyriakos Baxevanis, Vassilis Hatzakis, Kostas Makridakis, na Titos Manoussakis, kupeleka ombi kwa Waziri wa Elimu na Masuala ya Kidini ili wapewe kibali cha kufanya mikutano ya kidini. Wao walitumaini kwamba kwa kupata kibali hatimaye watapata ulinzi wa polisi. Kumbe mambo hayangekuwa rahisi hivyo.

Kasisi alipeleka barua kwa makao makuu ya polisi wa usalama katika Heraklion, akiwaambia wenye mamlaka kwamba Mashahidi wa Yehova wana Jumba la Ufalme katika parokia yake na akaomba wawekewe vikwazo na mikutano yao ipigwe marufuku. Hilo likafanya polisi wapeleleze na kufanya mahoji. Hatimaye, kiongozi wa mashtaka akaanzisha kesi ya jinai dhidi ya Mashahidi, kesi hiyo ikapelekwa mahakamani.

Oktoba 6, 1987, Mahakama ya Jinai ya Heraklion iliwaachilia huru hao washtakiwa wanne, ikisema kwamba “hawajafanya tendo ambalo wameshtakiwa kuwa walitenda, kwa sababu washiriki wa dini wana uhuru wa kuendesha mikutano . . . , bila masharti ya kuwa na kibali.” Hata hivyo, kiongozi wa mashtaka akaomba rufani siku mbili baadaye, na kesi hiyo ikapelekwa mahakama ya juu. Februari 15, 1990, mahakama hii iliwahukumu Mashahidi hao kifungo cha miezi miwili na kuwatoza faini ya dola 100 hivi. Washtakiwa hao nao wakaomba rufani kwa Mahakama Kuu ya Ugiriki.

Machi 19, 1991, Mahakama Kuu ilifutilia mbali rufani hiyo na kushikilia hukumu iliyokuwa imetolewa. Zaidi ya miaka miwili baadaye, Septemba 20, 1993, wakati uamuzi wa Mahakama Kuu ulipotangazwa, Jumba la Ufalme lilifungwa na polisi. Kama ilivyofunuliwa na hati za polisi, Kanisa Othodoksi la Krete lilichochea tendo hilo.

Hali hii ilitukia kwa sababu sheria fulani, zilizotungwa katika 1938 ili kuzuia uhuru wa kidini, zingali zinatumika katika Ugiriki. Hizo zasema kwamba mtu yeyote akitaka kuendesha mahali pa ibada, ni lazima apate kibali cha Wizara ya Elimu na Masuala ya Kidini na pia cha askofu wa mahali hapo wa Kanisa Othodoksi. Kwa miongo kadhaa, sheria hizo za kikale zimewasababishia Mashahidi wa Yehova matatizo mengi.

Uhuru wa Dini, na Haki za Kibinadamu

Walipojua kwamba Mahakama Kuu imeshikilia hukumu waliyopewa, hao Mashahidi wanne wakapeleka maombi kwa Tume ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, katika Strasbourg, Ufaransa, Agosti 7, 1991. Hao walidai kwamba hukumu waliyopewa ilikiuka Ibara ya 9 ya Mkataba wa Ulaya, ambayo inalinda uhuru wa mawazo, dhamiri, na dini, na vilevile uhuru wa kufuata dini yako ukiwa peke yako au katika jumuiya pamoja na wengine na katika mahali pa umma au faraghani.

Mei 25, 1995, washiriki 25 wa Tume hiyo waliamua kwa kauli moja kwamba katika kesi hiyo Ugiriki ilikuwa imekiuka Ibara ya 9 ya Mkataba wa Ulaya. Walisema kwamba hukumu iliyotolewa haipatani na uhuru wa kidini na kwamba hukumu hiyo haifai katika jamii ya kidemokrasi. Uamuzi wa uhalali wa kesi hiyo pia ulisema: “Wenye maombi . . . ni washiriki wa dini ambayo desturi zayo za ibada na matendo yayo yanajulikana kote na kuruhusiwa katika nchi nyingi za Ulaya.” Hatimaye, Tume hiyo ikapeleka kesi hiyo isikizwe na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.

Mashahidi wa Yehova Hawawezi Kukomeshwa

Kesi hiyo ilipangiwa kusikilizwa Mei 20, 1996. Kulikuwa na zaidi ya watu 200 mahakamani, kutia ndani wanafunzi na maprofesa kutoka chuo kikuu cha sehemu hiyo, waandishi wa habari, na Mashahidi wa Yehova kadhaa kutoka Ugiriki, Ujerumani, Ubelgiji, na Ufaransa.

Bw. Phédon Vegleris, profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Athens aliye pia wakili wa Mashahidi, alisisitiza kwamba sera iliyotumiwa na hukumu zilizotolewa na wenye mamlaka wa Ugiriki hazikukiuka tu Mkataba wa Ulaya bali pia zilikiuka Katiba ya Ugiriki. “Kwa hiyo ni sheria ya kitaifa na jinsi inavyotumiwa ndiyo imepelekwa Mahakamani.”

Wakili wa serikali ya Ugiriki alikuwa hakimu wa Kamati ya Serikali, ambaye, badala ya kuzungumzia mambo ya hakika, alirejezea msimamo uliochukuliwa na Kanisa Othodoksi katika Ugiriki, kuhusu uhusiano walo wa karibu na Serikali na watu, na madai ya uhitaji wa kudhibiti dini nyinginezo. Isitoshe, akasema kwamba tangu 1960 na kuendelea mbele, Mashahidi wa Yehova wamefanikiwa kuongezeka sana. Yaani, udhibiti wa Othodoksi ulikuwa umepingwa kwa mafanikio!

Uhuru wa Kidini Wategemezwa

Hukumu ingetolewa Septemba 26. Kukawa na wasiwasi wa yatakayotokea, hasa miongoni mwa Mashahidi wa Yehova. Msimamizi wa Kikao, Bw. Rudolf Bernhardt, akasoma uamuzi: Mahakama, iliyoshirikisha mahakimu tisa, iliamua kwa kauli moja kwamba Ugiriki ilikuwa imekiuka Ibara ya 9 ya Mkataba wa Ulaya. Pia iliamuru Mashahidi hao walipwe ridhaa ya dola karibu 17,000 za gharama zao. Jambo kuu zaidi, uamuzi huo ulitia ndani hoja kuu zenye kutetea uhuru wa kidini.

Mahakama ilisema kwamba sheria ya Ugiriki inaruhusu “wenye mamlaka za kisiasa, utawala na za kanisa kuingilia sana uhuru wa kidini.” Iliongezea kwamba utaratibu wa kupata kibali ulitumiwa na Serikali ili “kuweka vikwazo vigumu, vyenye kukandamiza juu ya kufuata itikadi za dini fulani ambazo si za kiothodoksi, hasa Mashahidi wa Yehova.” Hizo mbinu kali ambazo zimetumiwa na Kanisa Othodoksi kwa miongo mingi zilifunuliwa na mahakama hii ya kimataifa.

Mahakama hiyo ilikazia kwamba “haki ya kuchagua dini kama ambavyo imehakikishwa chini ya Mkataba haiipi Serikali haki yoyote ya kuamua kama itikadi za kidini au njia zinazotumiwa kuonyesha itikadi hizo ni halali.” Pia ilisema kwamba “Mashahidi wa Yehova wapatana na ufafanuzi wa ‘dini inayojulikana’ kwa mujibu wa sheria ya Kigiriki . . . Isitoshe, jambo hilo lilikiriwa na Serikali yenyewe.”

Si Mzaha Tu

Katika siku chache zilizofuata, mengi kati ya magazeti mashuhuri ya Ugiriki yalichapisha kesi hiyo. Katika Septemba 29, 1996, toleo la Jumapili la Kathimerini lilisema hivi: “Hata Serikali ya Ugiriki ijaribu kadiri gani kuiona kuwa ‘mzaha tu,’ ‘karipio kali ililopokea’ kutoka kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu katika Strasbourg ni jambo la hakika, uhakika ambao kwa kufaa umerekodiwa kimataifa. Mahakama hiyo ilikumbusha Ugiriki juu ya Ibara ya 9 ya Mkataba wa Haki za Kibinadamu, nayo ilishutumu kwa kauli moja sheria ya Ugiriki.”

Gazeti la kila siku la Athens Ethnos liliandika katika Septemba 28, 1996, kwamba Mahakama ya Ulaya “ilishutumu Ugiriki, ikiiamuru ilipe ridhaa wananchi wayo ambao wametukia kuteseka kwa sababu ya kuwa Mashahidi wa Yehova.”

Mmoja wa wakili wa Mashahidi hao, Bw. Panos Bitsaxis, alihojiwa katika kipindi kimoja cha redio, naye alisema: “Twaishi katika mwaka wa 1996, tukikaribia karne ya 21, na bila shaka hakupaswi kuwa na ubaguzi, mnyanyaso, au kuingiliwa na wenye mamlaka kwa habari ya kudhihirisha haki ya kimsingi ya uhuru wa kidini. . . . Hii ni fursa nzuri kwa serikali kuchunguza upya sera yayo na kukomesha ubaguzi huu wa kishenzi, ambao haufai hata kidogo katika siku hizi za kisasa.”

Uamuzi wa kesi ya Manoussakis na Wengine dhidi ya Ugiriki wazusha tumaini la kwamba Serikali ya Ugiriki itarekebisha sheria yayo kwa kuambatana na hukumu ya Mahakama ya Ulaya, ili Mashahidi wa Yehova katika Ugiriki waweze kufurahia uhuru wa kidini bila kuingiliwa na wenye mamlaka, polisi, au kanisa. Isitoshe, hii ni hukumu ya pili iliyotolewa na Mahakama ya Ulaya dhidi ya mfumo wa sheria wa Ugiriki kwa masuala yanayohusu uhuru wa kidini.a

Imejulikana kote kwamba Mashahidi wa Yehova hutii “mamlaka zilizo kubwa” katika mambo yote ambayo hayapingani na Neno la Mungu. (Waroma 13:1, 7) Hao hawatishi kamwe utengamano wa umma. Kinyume cha hilo, vichapo vyao na huduma yao ya peupe hutia moyo kila mtu kuwa mwananchi mwenye kutii sheria na kuishi maisha yenye amani. Dini yao ni nyoofu na madhubuti, na washiriki wao wamechangia sana hali-njema ya ujirani wao. Azimio lao la kutegemeza viwango vya juu vya maadili vya Biblia na upendo wao kwa jirani yao, kama ionyeshwavyo katika kazi yao ya kufundisha watu Biblia, imekuwa na athari nzuri katika nchi zaidi ya 200 ambazo wamo.

Inatumainiwa kwamba maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Ulaya yatasaidia katika kuleta uhuru zaidi wa kidini kwa Mashahidi wa Yehova na dini nyinginezo ndogo-ndogo katika Ugiriki.

[Maelezo ya Chini]

a Uamuzi wa kwanza, uliotolewa katika 1993, ulikuwa kesi ya Kokkinakis dhidi ya Ugiriki.—Ona Mnara wa Mlinzi, Septemba 1, 1993, ukurasa 27.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Jumba la Ufalme la awali lililofungwa na polisi Septemba 20, 1993

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, Strasbourg

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mashahidi waliohusika: T. Manoussakis, V. Hatzakis, K. Makridakis, K. Baxevanis

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki