Mahakama ya Ulaya Yasahihisha Ukiukwaji wa Sheria
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI
UTUMISHI wa kijeshi ni lazima katika Ugiriki. Katika kipindi chochote kile cha wakati, Mashahidi wa Yehova wapatao 300 wamo gerezani kwa sababu ya kukataa kufanya utumishi wa kijeshi. Shirika la Amnesty International lawaona kuwa wafungwa kwa sababu ya dhamiri na mara kadhaa limesihi serikali za Ugiriki zenye kufuatana kuwaachilia huru na kutunga sheria ambayo ingewaruhusu kufanya utumishi wa kiraia ambao si adhabu.
Katika mwaka wa 1988, sheria mpya ya bunge ihusuyo utumishi wa kijeshi ilitungwa. Kati ya mambo mengine, hii iliweka masharti kwamba “wafuatao wameruhusiwa wasitumikie katika utumishi wa kijeshi: . . . Makuruta ambao ni wahudumu wa kidini, watawa au watawa-wakufunzi wa dini inayotambuliwa, ikiwa wanataka.” Wahudumu wa Kanisa Othodoksi la Kigiriki sikuzote huruhusiwa kwa urahisi na mara moja, bila kukabili tatizo lolote au kuvunjiwa kwa namna yoyote haki zao za msingi za kibinadamu. Je, hilo pia lingetumika kwa wahudumu wa dini ndogo? Upesi kesi moja ikaandaa jibu.
Kufungwa Gerezani Kinyume cha Sheria
Kulingana na sheria hii, mwishoni mwa mwaka wa 1989 na mwanzoni mwa mwaka wa 1990, Dimitrios Tsirlis na Timotheos Kouloumpas, ambao ni wahudumu waliowekwa rasmi wa Kutaniko la Kikristo la Central la Mashahidi wa Yehova katika Ugiriki, waliwasilisha maombi yao katika ofisi zilizowahusu za uandikishaji wa askari ili waruhusiwe wasijiandikishe katika utumishi wa kijeshi. Pamoja na fomu zao za maombi, waliwasilisha hati zinazothibitisha kwamba wao walikuwa wahudumu wa kidini. Kama ilivyotarajiwa, maombi hayo yalikataliwa kwa sababu zisizo na ukweli kwamba Mashahidi wa Yehova si “dini inayojulikana.”
Ndugu Tsirlis na Kouloumpas waliripoti katika vituo walivyotakiwa vya mafunzo ya kijeshi na kukamatwa, wakashtakiwa kwa kukosa utii, na kuwekwa kizuizini. Wakati huohuo, Makao Makuu ya Jeshi yalikataa rufani zao dhidi ya uamuzi wa ofisi za uandikishaji wa askari. Wenye mamlaka wa kijeshi walisema kwamba Sinodi Takatifu ya Kanisa Othodoksi la Kigiriki ilikuwa imewaarifu kwamba Mashahidi wa Yehova si dini inayotambuliwa! Hili lilipingana na maamuzi mengi ya mahakama za kiraia ambazo zilikuwa zimesema kwamba kwa kweli Mashahidi wa Yehova ni dini inayojulikana.
Mahakama za kijeshi nazo zikawapata Tsirlis na Kouloumpas kuwa na hatia ya kukosa utii na kuwahukumu kifungo cha miaka minne gerezani. Ndugu hao wawili walikata rufani ya maamuzi haya kwa Mahakama ya Kijeshi ya Rufani, ambayo iliahirisha kusikiliza kwa rufani mara tatu kwa sababu mbalimbali. Hata hivyo, ilikataa kila mara kutoa amri ya kuruhusu wakata-rufani kutolewa gerezani, ingawa sheria za Ugiriki zinatoa ruhusa ya jambo hili.
Wakati huohuo, katika kesi nyinginezo, Mahakama Kuu Zaidi ya Usimamizi ilibatilisha maamuzi ya Makao Makuu ya Jeshi, kwa msingi wa kwamba Mashahidi wa Yehova kwelikweli ni dini yenye kujulikana!
Katika kipindi cha miezi 15 ambacho Tsirlis na Kouloumpas walilazimika kukaa katika Gereza la Kijeshi la Avlona, walikabili matendo yasiyo ya kibinadamu kabisa na ya kushusha sana pamoja na Mashahidi wengine waliotiwa gerezani. Ripoti moja ya wakati huo ilisema kuhusu “hali mbaya sana za gereza ambazo [wafungwa Mashahidi wa Yehova] wanakaa, ikitaja nyama zilizooza na mikia ya panya, ambayo mara nyingi huandaliwa pamoja na chakula, kukatizwa kwa saa za kutembelewa kulingana na maoni ya Usimamizi, ukosefu wa nafasi kwa sababu ya kujaa kupita kiasi kwa wafungwa na kutendwa kubaya kwingi zaidi kulikotolewa kwa wafungwa kama hao walio wakataaji wa kudhamiria.”
Hatimaye, Mahakama ya Rufani ya Kijeshi iliwaondolea hatia Ndugu Tsirlis na Kouloumpas lakini wakati huohuo iliamua kwamba Serikali haikuwa na wajibu wa kuwalipa fidia kwa kuwekwa kwao kizuizini kwa sababu “kuwekwa kwao kizuizini kulitokana na uzembe mzito kwa upande wa wakata-rufani.” Hili lilitokeza maswali halali miongoni mwa wanasheria: Ni nani aliyekuwa na uzembe mzito? Mashahidi hao au mahakama za kijeshi?
Mara moja ndugu hao waliachiliwa kutoka gerezani na hatimaye waliondolewa jeshini kwa msingi wa kwamba wao walikuwa wahudumu wa kidini. Walipoachiliwa, shirika la Amnesty International lilitangaza kwamba lilifurahia kuachiliwa kwa Dimitrios Tsirlis na Timotheos Kouloumpas na lilieleza matumaini ya kwamba kwa wakati ujao, wahudumu wa Mashahidi wa Yehova wangeruhusiwa wasishiriki katika utumishi wa kijeshi kulingana na ruhusa itolewayo na sheria ya Kigiriki. Lakini, baada ya muda mfupi, matumaini haya yangetupiliwa mbali.
Ndani na Nje ya Magereza
Mhudumu mwingine wa kidini wa Mashahidi wa Yehova aliyewekwa rasmi alilazimika kupitia masaibu yaliyo tofauti kidogo kwa sababu hiyohiyo. Katika Septemba 11, 1991 Anastasios Georgiadis alipeleka maombi katika njia hiyohiyo ili aruhusiwe asitumikie katika utumishi wa kijeshi. Siku sita baadaye ofisi ya uandikishaji wa askari ilimwarifu kwamba maombi yake yalikuwa yamekataliwa, kwa mara nyingine tena kwa sababu Sinodi Takatifu ya Kanisa Othodoksi la Kigiriki haikubali kuwa Mashahidi wa Yehova ni dini inayojulikana. Na jambo hili lilitokea ingawa maamuzi ya waziwazi ya Mahakama Kuu Zaidi ya Usimamizi juu ya kesi za Tsirlis na Kouloumpas!
Jibu la maandishi kutoka Makao Makuu ya Jeshi lilisema hivi: “Usimamizi ulifikia uamuzi wa kuhukumu kuhusu maombi ya [Georgiadis], kwa kutegemea maoni ya wataalamu yaliyotolewa na Sinodi Takatifu ya Kanisa la Ugiriki, ambayo haioni Mashahidi wa Yehova kuwa dini yenye kujulikana.”—Italiki ni zetu.
Januari 20, Georgiadis alikwenda kwenye Kambi ya Mazoezi ya Nafplion na mara moja aliwekwa katika seli ya adhabu ya hiyo kambi. Baadaye alihamishwa hadi Gereza la Kijeshi la Avlona.
Katika Machi 16, 1992, Mahakama ya Kijeshi ya Athens ilimwondolea hatia Georgiadis. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mahakama ya kijeshi katika Ugiriki kutambua kwamba kwa kweli Mashahidi wa Yehova ni dini ijulikanayo. Mkurugenzi wa Gereza la Kijeshi la Avlona alimwachilia huru lakini akamwamuru mara aripoti tena kwa ajili ya kazi katika Aprili 4, katika kituo cha uandikishaji wa askari cha Nafplion. Katika siku hiyo, Georgiadis alikataa tena kujiandikisha na kwa mara nyingine alishtakiwa kwa kukosa utii, akiwekwa kizuizini kwa mara ya pili, na kufikishwa mahakamani.
Katika Mei 8, 1992, Mahakama ya Kijeshi ya Athens ilimwondolea hatia ya mashtaka ya hiyo kesi mpya ya jinai lakini iliamua kwamba hakuna fidia astahiliyo kwa kuwekwa kizuizini. Georgiadis alifunguliwa mara hiyo kutoka Gereza la Kijeshi la Avlona lakini aliamriwa aripoti kwa mara ya tatu kwa ajili ya utumishi wa kijeshi katika kituo cha uandikishaji wa askari cha Nafplion, katika Mei 22, 1992! Alikataa tena kujiandikisha na kwa mara ya tatu alishtakiwa kwa makosa ya kukosa utii na aliwekwa kizuizini.
Katika Julai 7, 1992, Mahakama Kuu Zaidi ya Usimamizi ilibatilisha uamuzi wa Septemba 1991, kwa msingi wa kwamba Mashahidi wa Yehova kwa kweli ni dini inayojulikana. Hatimaye katika Julai 27, 1992, Georgiadis alifunguliwa kutoka Gereza la Kijeshi la Thessalonica. Katika Septemba 10, 1992, Mahakama ya Kijeshi ya Thessalonica ilimwondolea hatia lakini ilishikilia kwamba Georgiadis hakustahili kupata fidia kwa sababu kuwekwa kwake kizuizini tena kulisemwa kuwa ‘kwa sababu ya uzembe wake mzito.’
Itikio Iliyoenea
Likitoa maoni kuhusu kesi ya Georgiadis, Bunge la Ulaya lilitangaza hivi: “Hii ni hali ya ubaguzi dhidi ya wahudumu wa dini ya Mashahidi wa Yehova kwa habari ya usawa mbele ya sheria na kufurahia haki ya kutendewa sawa.”
Katika Februari 1992, shirika la Amnesty International lilisema kwamba “linaamini kwamba [Anastasios Georgiadis] ametiwa gerezani kwa sababu tu ya msingi wa matendo ya ubaguzi kwa upande wa wenye mamlaka wa kijeshi dhidi ya wahudumu wa Mashahidi wa Yehova na linatoa mwito wa kuachiliwa kwake mara moja na bila masharti yoyote akiwa mfungwa wa dhamiri.”
Hata mwendesha-mashtaka wa kijeshi wa moja ya kesi za Georgiadis alilazimika kusema hivi: “Kiwango cha maendeleo ya kitamaduni ya jamii kinadhihirishwa kwa njia ambayo inashughulika na hali fulani zihusuzo raia zake. Ikiwa sisi hapa katika Ugiriki twatamani maendeleo yetu ya kitamaduni yawe sawa na viwango vya Ulaya, ikiwa twataka kuendelea, basi ni lazima tujipatanishe na kanuni za kimataifa na kuacha ubaguzi. Sehemu ambayo hili liko dhahiri zaidi ni kuhusu haki za raia mmoja-mmoja. Lakini, mambo yanayoendelea hasa na mbinu za wasimamizi zaonyesha wazi ubaguzi na kutostahimili kidini kunakodumu dhidi ya dini ndogondogo. Kesi hii inayoendelea inafedhehesha.”
Ian White, aliye mbunge wa Bunge la Ulaya, kutoka Bristol, Uingereza, aliandika hivi: “Wazo la kwamba Mashahidi wa Yehova si ‘dini inayojulikana’ lingechekesha wengi katika wilaya hii. Kwa hakika, ingawa wako wachache kwa kulinganishwa, Mashahidi wanajulikana sana katika Nchi hii na kwa mara nyingi huwafikia watu mlango hadi mlango.” Kukiwa na Mashahidi zaidi ya 26,000 wakihubiri katika Ugiriki, hawawezi kamwe kuwa ‘dini isiyojulikana’!
Kikundi cha wabunge kumi wa Bunge la Ulaya waliandika kuonyesha ghadhabu zao kuhusu kesi ya Georgiadis, wakisema kwamba walikuwa “wameshangazwa na kusikitishwa sana” juu ya uvunjaji kama huo wa haki za kibinadamu katika Ugiriki.
Kukata Rufani kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu
Baada ya kuondolewa hatia na kufunguliwa kutoka gerezani, wahasiriwa wote watatu wa ubaguzi huu wa kidini walihisi kimaadili kukata rufani kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Msingi wa rufani hii ulikuwa kuwekwa kizuizini kwao kulikokuwa kinyume cha sheria, ambako kwenyewe hakukuwa halali, na mateso ya kiakili na ya kimwili waliyopata, hali kadhalika matokeo ya kiadili na ya kijamii yaliyohusika kutokana na kunyimwa-nyimwa uhuru wao kwa kipindi kirefu sana cha wakati. Kwa sababu hizi walifuatilia kiasi cha haki na kinachostahili cha fidia.
Tume ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilifikia mkataa kwa pamoja kwamba katika kesi za Tsirlis na Kouloumpas, walivunjiwa haki zao za uhuru na usalama wakiwa watu, kwamba kuwekwa kwao kizuizini hakukuwa halali, kwamba walikuwa na haki ya kupata fidia, na kwamba hawakupata haki ya kusikilizwa vizuri na mahakama katika kesi yao. Mkataa kama huo ulifikiwa na Tume hiyo katika kesi ya Georgiadis.
Udhalimu Wasahihishwa
Kesi ilipangwa kusikilizwa Januari 21, 1997. Wengi walikuwapo mahakamani, kutia ndani wanafunzi kutoka chuo kikuu cha mahali hapo, waandishi wa habari, na Mashahidi wa Yehova kadhaa kutoka Ugiriki, Ujerumani, Ubelgiji, na Ufaransa.
Bw. Panos Bitsaxis, wakili wa Mashahidi, alizungumza juu ya “ukaidi wa daima na mtazamo wenye kudumu wa wenye mamlaka wa Ugiriki kutotambua kuwepo kwa dini moja ndogo,” yaani Mashahidi wa Yehova. Alishutumu mazoea ya wenye mamlaka wa Ugiriki ya kutegemeza maoni yao rasmi juu ya Mashahidi juu ya maoni ya wapinzani wao wakuu—Kanisa Othodoksi la Kigiriki! Aliendelea: “Hali hii itaruhusiwa kuendelea kwa kadiri gani? . . . Na hadi lini?” Alisema juu ya “kukataa kutambua jamii fulani ya kidini, kukataa ambako kwaonekana kuwa upuuzi, uonapo kwamba huja moja kwa moja, kwa wazi, na bila kusababu, dhidi ya sheria, dhidi ya makumi ya maamuzi ya Mahakama Kuu Zaidi ya Usimamizi.”
Mwakilishi wa serikali ya Ugiriki alithibitisha huo mtazamo wenye upendeleo wa wenye mamlaka wa Ugiriki kwa kudai hivi: “Haipaswi kusahauliwa kwamba kihalisi watu wote wa Ugiriki wamekuwa sehemu ya Kanisa Othodoksi kwa karne kadhaa. Tokeo moja la kawaida ni kwamba muundo wa Kanisa hilo na hadhi ya wahudumu wake na majukumu yao katika Kanisa yako wazi kabisa. . . . Hadhi za wahudumu kutoka Kanisa la Mashahidi wa Yehova si wazi sana.” Ni hali iliyoje ya kukubali kwa wazi matendo ya ubaguzi dhidi ya dini ndogondogo katika Ugiriki!
Uhuru wa Kidini Wategemezwa
Hukumu ilitolewa Mei 29. Msimamizi wa Mahakama, Bw. Rolv Ryssdal, alisoma kwa sauti uamuzi huo. Mahakama, ikiwa imeundwa na majaji tisa, kwa kauli moja imeona kwamba Ugiriki ilikuwa imevunja Ibara ya 5 na ya 6 ya Mkataba wa Ulaya. Pia iliwapa wakata-rufani dola za Marekani 72,000 kwa fidia na gharama. Jambo la maana zaidi kuliko yote, uamuzi huo ulitia ndani mabishano mengi ya maana yakipendelea uhuru wa kidini.
Mahakama ilisema kwamba “wenye mamlaka wa kijeshi walipuuza vibaya sana” ukweli wa kwamba Mashahidi wa Yehova wanatambuliwa kuwa “dini inayojulikana” katika Ugiriki, kulingana na maamuzi ya Mahakama Kuu Zaidi ya Usimamizi. Pia ilitoa maelezo haya: “Kudumu kukataa kwa wenye mamlaka waliohusika kutambua Mashahidi wa Yehova kuwa ‘dini inayojulikana’ na kudharau haki za walalamikaji kwa uhuru waliotaka kulikuwa ubaguzi kwa kulinganishwa na njia ambayo wahudumu wa Kanisa Othodoksi la Kigiriki hupata ruhusa.”
Kesi hiyo ilitangazwa sana na vyombo vya habari vya Ugiriki. Gazeti la Athens News lilitangaza hivi: ‘Mahakama ya U[laya] yailaumu vikali Ugiriki kuhusu madai ya Yehova.’ Uamuzi wa kesi ya Tsirlis & Kouloumpas and Georgiadis v. Greece ulitoa matumaini kwamba Serikali ya Ugiriki itapatanisha sheria zake na Uamuzi wa Mahakama ya Ulaya, ili Mashahidi wa Yehova katika Ugiriki waweze kufurahia uhuru wa kidini bila kuingiliwa na usimamizi, jeshi au kanisa. Zaidi ya hayo, hii ni hukumu nyingine tena iliyotolewa na Mahakama ya Ulaya dhidi ya mahakama za Ugiriki juu ya masuala yahusuyo uhuru wa kidini.a
Mashahidi wa Yehova huthamini sana uhuru wao, nao hujitahidi kuutumia katika kumtumikia Mungu na kuwasaidia jirani zao. Wahudumu wa kidini watatu walio Mashahidi walipeleka kesi zao hadi Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, si kwa sababu ya kupata faida zozote za kimwili, lakini kwa sababu tu za kimaadili. Hivyo, wote watatu wameamua kwamba fidia waliyopata itatumika tu kwa ajili ya kuendeleza kazi ya kielimu ya Mashahidi wa Yehova.
[Maelezo ya Chini]
a Uamuzi wa kwanza, uliotolewa mwaka wa 1993, ulikuwa wa kesi ya Kokkinakis v. Greece; wa pili, uliotolewa katika mwaka wa 1996, ulihusu kesi ya Manoussakis and Others v. Greece.—Ona Mnara wa Mlinzi, Septemba 1, 1993, ukurasa wa 27-31; Amkeni!, Machi 22, 1997, ukurasa wa 14-16.
[Picha katika ukurasa wa 20]
Esther na Dimitrios Tsirlis
[Picha katika ukurasa wa 21]
Timotheos na Nafsika Kouloumpas
[Picha katika ukurasa wa 22]
Anastasios na Koula Georgiadis