Je, Ufanisi wa Vitu vya Kimwili Hutoa Uhakikisho Kamili wa Furaha?
“KATI ya karibu wanafunzi 50 katika shule yetu, ni 1 au 2 tu waliovaa viatu,” akumbuka Poching mwenye miaka 45, aliyekulia kusini mwa Taiwan katika miaka ya 1950. “Hatungeweza kuvinunua. Hata hivyo, hatukujifikiria kuwa maskini kamwe. Tulikuwa na vyote tulivyovihitaji.”
Hiyo ilikuwa yapata miaka 40 iliyopita. Tangu wakati huo, maisha yamebadilika sana kwa Poching na wale wakaaji wengine milioni 20 wa kisiwa hicho kwa njia ya kutazamisha. Kama vile kitabu Facts and Figures—The Republic of China on Taiwan kielezavyo, “Taiwan [ili]geuzwa kutoka kuwa jamii ya kilimo ikawa jamii ya viwanda yenye kuvuvumuka.” Kufikia mwishoni mwa miaka ya 1970, Taiwan ilionwa kuwa “jamii thabiti, yenye ufanisi.”
Kwa kweli, ithibati ya ufanisi yaonekana kila mahali katika Taiwan. Kuanzia majengo-tata ya ofisi za ghorofa zilizo kiuka-mamboleo ambazo zimevuvumuka kote kisiwani hadi zile barabara kuu zilizosongamana magari ghali yaliyoingizwa nchini kutoka ugenini, ufanisi wa vitu vya kimwili wa Taiwan huliliwa ngoa na mataifa mengine yanayositawi. China Post, gazeti kuu la lugha ya Kiingereza la Taiwan, huona fahari kwamba leo “watu wa Taiwan hufurahia kiwango cha maisha cha juu kupita yote katika historia ya Kichina.”
‘Wingi wa Matatizo Yaliyo Miiba’
Je, ufanisi wote huu wa kimwili umewaletea watu furaha na uradhi wa kweli? Ingawa hakuna shaka kwamba watu wa Taiwan wana mengi ya kujivunia, kuna upande mwingine wa kisa hiki cha mafanikio. China Post laendelea kuonyesha: “Pamoja na kadiri kubwa hii ya utajiri umekuja wingi wa matatizo tata yaliyo miiba.” Ufanisi wa vitu vya kimwili wa Taiwan haukuja bila gharama.
Kuhusu hayo “matatizo tata yaliyo miiba” yanayosumbua kisiwa hiki kilichokuwa bila uhalifu kwa kulinganishwa na mahali penginepo, China Post lasema hivi: “Katika miaka ya majuzi uhalifu na fujo zimeongezeka ajabu katika jamii yetu yenye utajiri, zikitokeza tisho linaloongezeka kwa maisha na mali za raia wote wanaofuata sheria.” Katika makala moja yenye kichwa “Utajiri Wafanya Taiwan Iwe Bara la Uchu,” Post lashutumu matatizo ya “mikahawa na mabaa yenye vidosho” na ya nyumba haramu za umalaya zinazoongezeka ajabu zikiendeshwa kwa kisingizio cha kuwa vyumba vya vinyozi. Unyakuzi na utoroshi wenye madhumuni ya kupata fidia umekuwa tatizo jingine. Ripoti moja yasema juu ya kutoroshwa kwa watoto kuwa “biashara mpya inayositawi sana ya Taiwan.” Wengi hugeukia kufanya vitendo hivyo vya uhalifu kama njia ya kulipa madeni ya kucheza kamari au hasara nyingine za kifedha.
Watoto si watendwa uhalifu wasio na hatia tu. Wao wanazidi kuhusika katika vitendo vya uhalifu. Ripoti zaonyesha kwamba katika 1989 pekee, hesabu ya vitendo vya uhalifu vilivyofanywa na watoto viliruka vikawa asilimia 30. Wengine hufuatilia kisababishi cha ongezeko hili na kupata ni mvunjiko wa familia, na takwimu zaelekea kuunga hili mkono. Kwa kielelezo, kuanzia 1977 hadi 1987, idadi ya wenzi Wataiwan waliooana ilipungua, lakini hesabu ya talaka ilikuwa zaidi ya maradufu. Kwa kuwa utamaduni wa Kichina kwa mapokeo hukazia umaana wa kuwa na familia katika jamii thabiti, si ajabu kwamba wengi wanahangaika sana juu ya hali hizo zinazozidi kuwa mbaya.
Shina la Tatizo Hilo
Maelezo mbalimbali yametolewa kwa kujitahidi kuielewa sababu ya mzoroto wa utaratibu wa kijamii katikati ya jamii yenye ufanisi. Kwa kupunguza kidogo uzito wa mambo, watu fulani husema kwamba hiyo ni gharama ya mafanikio tu. Lakini kulaumu mafanikio au ufanisi ni kama kulaumu chakula kwa ulafi. Si walaji wote walio walafi, wala si kila mfanisi aliye mfuatiaji wa vitu vya kimwili wala mhalifu. Sivyo, ufanisi wa vitu vya kimwili wenyewe hausababishi uhalifu na fujo ya kijamii.
Tahariri moja katika China Post ilionyesha kisababishi kimoja kilicho kichangiaji kikuu. Ilisema hivi: “Sisi, muda wa miongo ya miaka iliyopita, tuliweka mkazo mwingi mno juu ya usitawi wa vitu vya kimwili. Hili ndilo limesababisha mzoroto wa thamani za viwango vya kiadili na vya kiroho katika jamii yetu leo.” (Italiki ni zetu.) Ndiyo, kukazia kupita kiasi ufuatiaji wa vitu vya kimwili huongoza kwenye roho ya ufuatiaji wa vitu vya kimwili na pupa. Hukuza kujifikiria tu. Roho ya namna hiyo hasa ndiyo huongoza kwenye mvunjiko wa familia na ongezeko kubwa la masaibu ya kijamii. Lile ambalo Biblia ilisema miaka 2,000 iliyopita bado ni kweli leo: “Shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha [wala si fedha yenyewe iliyo shina la hayo].”—1 Timotheo 6:10.
Tatizo la Ulimwenguni Pote
Katika utafutaji wa amani na utulivu—na usalama—maelfu ya watu wamehama Taiwan kwenda nchi nyinginezo. Lakini matatizo yanayopata Taiwan si ya Taiwan pekee. Yametapakaa ulimwenguni pote.
Miaka kadhaa iliyopita uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba kaunti iliyo tajiri zaidi katika California, Marekani, ndiyo iliyokuwa na hesabu ya juu zaidi ya talaka nchini. Karibu asilimia 90 ya mishughulikano yote ya mali halisi katika maeneo fulani ya kaunti hiyo ilitokana na ndoa zilizovunjika. Visa vya kujiua viliripotiwa kuwa mara mbili kuliko vile vya wastani wa kitaifa. Hesabu ya waraibu wa alkoholi ilikuwa mojapo zilizo juu zaidi nchini, na ilisemwa kwamba katika kaunti hiyo kuna madaktari na matabibu wengi wa akili kwa kila mtu kuliko walivyo kwingineko katika Marekani.
Yesu Kristo alionyesha wazi kweli moja ya msingi aliposema: “Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” (Mathayo 4:4) Mali za vitu vya kimwili, hata ziwe nyingi kadiri gani, haziwezi kutosheleza kila uhitaji wa mtu, wala haziwezi kutoa uhakikisho kamili wa furaha. Kwa kinyume, mara nyingi ni kama vile msemo mmoja wa Kichina utamkavyo: “Mtu awapo ameshiba na kupashwa joto, fikira zake hugeukia mambo ya kupita kiasi na tamaa za kimwili.” Hii ni kama ionyeshwavyo na linalotendeka katika Taiwan na kwingineko—ufanisi wa vitu vya kimwili pekee hutokea mara nyingi kuwa utangulizi wa uozo wa kiadili na kijamii na matatizo yaambatanayo nao.
Basi, ni nini kihitajiwacho ili ufanisi wa vitu vya kimwili uweze kuwa sehemu ya furaha halisi na inayodumu? Ili kupata jibu, tafadhali soma makala inayofuata.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Mtu awapo ameshiba na kupashwa joto, fikira zake hugeukia mambo ya kupita kiasi na tamaa za kimwili.”—Msemo wa Kichina
[Picha katika ukurasa wa 5]
Utajiri wa vitu vya kimwili uligeuza miji midogo ikawa majiji yenye kuvuma kwa pirikapirika, yakiwaka kwa taa za neoni