Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 1/22 kur. 16-17
  • Megapodi na Mayai Yake ya Kuvuruga

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Megapodi na Mayai Yake ya Kuvuruga
  • Amkeni!—1995
  • Habari Zinazolingana
  • Nyuki Wangu Waliangua Vifaranga!
    Amkeni!—1998
  • Kiota cha Ndege Anayeitwa Mallee
    Je, Ni Kazi ya Ubuni?
  • Maajabu ya Yai la Mbuni
    Amkeni!—2002
Amkeni!—1995
g95 1/22 kur. 16-17

Megapodi na Mayai Yake ya Kuvuruga

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA VISIWA VYA SOLOMON

KARIBU mwendo wa saa mbili kwa mtumbwi kutoka Honiara, mji mkuu wa Visiwa vya Solomon katika Guadalcanal, kipo kisiwa cha Savo, kijulikanacho sana kwa volkeno yacho tendaji na ndege megapodi, ajulikanaye pia kuwa kuku wa Australia wa vichakani. Nyakati fulani wenyeji hutumia miamba yenye moto na mivuke yenye joto ichachatayo kutoka kwenye mianya ya ardhi ili kupika chakula chao na kuupasha joto ugavi wao wa maji. Ndege megapodi hutumia kwa akili mali ya asili hii.

Ingawa kwa kulinganishwa yeye ni mdogo kuliko kuku wa kawaida, ndege megapodi ana sura kama hiyo, akiwa na mwili mzito, mabawa mafupi ya mviringo na nyayo kubwa zenye nguvu, zenye vidole vinne. Mdomo wake ni mfupi na umejikunja kidogo kuelekea chini. Mruko wa megapodi ni wa kasi lakini wa muda mfupi.

Ndege megapodi (maana yake “miguu mikubwa”) ni wa jamii ileile ya ndege kama kuku wa kawaida—kikundi cha Galliforme. Yeye ni ndege mwotamiaji afukiaye mayai yake katika marundo ya majani yanayooza ili ayaangue katika joto lenye udumifu wa digrii 32 Selsiasi. Katika kisiwa hiki megapodi wana kiotamio tofauti. Ni nini kingeweza kuwa bora kuliko ule mchanga uliopashwa joto kwa njia ya volkeno katika fuo za Savo?

Hektari za ufuo tambarare, uliolala sawia zimezungushiwa na wenyeji ukuta wa majani imara ya mitende kwa uangalifu. Hizi ndizo “nyanja” za megapodi. Humo ndani, eneo lafanana na bustani ya mitunda iliyopandwa kwa uangalifu. Miti midogo imepangwa kwa safu zenye utaratibu, yaonekana ili kuandaa mazingira yenye uhakikishio mwingi zaidi kwa ndege hao wanaozuru. Katika eneo zima hili, mchanga uliotiwa matundu na mibonyeo midogo ya karibu kipenyo cha sentimeta 60, hiyo ikiwa ni ithibati ya ziara za wakati wa macheo na machweo za ndege-mwitu hawa wa ajabu wajao kuchimba tundu jembamba la kufikia kina cha sentimeta 90 ili kutaga na kufukia mayai yao humo.

Nayo ni mayai yaliyoje! Yana wastani wa urefu wa sentimeta tisa na karibu kipenyo cha sentimeta sita, ukubwa wa kustaajabisha kwa ndege mdogo jinsi hiyo. Yaanguliwapo, yule kifaranga mwenye manyoya kamili hufukua njia ili atokee kwenye uso wa ardhi na kujikimbiza akiwa peke yake. Katika muda wa saa 24 aweza kuruka.

Kila siku wanavijiji huteremka kwenye “nyanja” hizo kuyafukua mayai, ambayo yaonekana kuwa sehemu kubwa ya chakula kikuu cha wanakisiwa hao. Inastaajabisha jinsi wao watayarishavyo mayai yao mepesi, ya mkaango teketeke wa kuvurugwa. Yale mayai ya megapodi hualishwa kwa ustadi yafunguke juu ya uti wa kisehemu cha shina la mwanzi kijani kisha humiminwa ndani ya ushimo wa shina hilo. Shina hilo la mwanzi, ambalo sasa huwa limejaa yai, hulazwa kwa mlalo wa digrii 45 katika kuni zinazowaka za ule moto wa kupikia. Upesi mayai hayo yanatokota-tokota na kuchanganyika na utomvu-tomvu utokao katika ule mwanzi wa kijani wenye joto jingi. Yawapo tayari, ule mwanzi hupasuliwa ukafunguka, na hapo mtu hula mayai ya mkaango wa kuvuruga yaliyoumbika kama soseji yakiwa na ladha nzuri isiyo na kifani. Njoo kwenye Visiwa vya Solomon, uyaonje wakati fulani!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki