Vijana Huuliza...
Naweza Kuboreshaje Jumla ya Mavazi Yangu?
ROBERT ana hangaiko kubwa! Lazima ahudhurie arusi ya dada yake na hana kabisa kitu cha kuvaa. Si kwamba Robert “yu uchi” kama isemavyo Biblia. (Yakobo 2:15) Lakini mavazi ya kila siku ya Robert hayatafaa pindi rasmi hii.
Ingawa hivyo, Angela kijana ana matukio matatu ya kijamii ya kuhudhuria, kila moja likitaka mtindo tofauti wa mavazi. Lakini, tofauti na Robert, msichana huyo hana shida kubwa ya kupata vazi lifaalo. Si kwamba Angela ni tajiri. Ni kwamba tu yeye amejiongezea jumla ya mavazi ya msingi yamwezeshayo kuvalia vema katika hali za namna mbalimbali.
Makala moja katika gazeti Woman’s Day ilisema hivi: “Mavazi ni ya maana. Yaweza kusaidia sana kukufanya uhisi vizuri sana juu yako mwenyewe.” Uvaacho kina matokeo makubwa pia juu ya jinsi wengine wakuonavyo na kukutendea. Basi, Biblia ina sababu nzuri ya kutuhimiza tujipambe kwa “mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri na moyo wa kiasi.” (1 Timotheo 2:9) Ikiwa wewe ni Mkristo, kuwa na jumla ifaayo ya mavazi kwapasa kuwe jambo la maana kwako.
Ingawa hivyo, ingeweza kuwa kwamba ujapokuwa na kabati iliyojaa mavazi kemkem, nyakati fulani wahisi kwamba huna cha kuvaa? Tatizo ni nini, nawe waweza kurekebishaje mambo?
Gharama Kubwa ya Fashoni
Mara nyingi tatizo si fedha bali ni tokeo la kufanywa mtumwa wa mitindo na fashoni za ulimwengu zinazobadilika daima. Kitabu Youthtrends chasema kwamba “ulimwengu wa biashara watambua jinsi vijana watakavyotumia fedha nyingi kwa nguo zenye vibandiko vya sifa.” Kwa kuongozwa na pupa ya fedha, shughuli ya kuuza nguo hutumia matangazo ya magazeti na televisheni yanasayo fikira ili kushawishi vijana watumie fedha—wazitumie, na kuzitumia! Kwa kutiliwa nguvu na msongo wa marika, mbinu hiyo hufanya kazi. Aomboleza mwalimu mmoja: “Kila mtu anatumia kiasi kikubwa kununua nguo na watoto wale wasioweza kufanya hivyo . . . wanafanya kazi baada ya shule ili tu wanunue madangarizi yenye mishono bora.”
Kuwa mtumwa wa fashoni hugharimu fedha na huenda kukakuacha bila fedha nyingi za kutumia kununua mavazi zaidi yafaayo ambayo wayahitaji kikweli. Hivyo Warumi 12:2 hutoa ushauri mwema lisemapo hivi: “Msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu.” Ni kweli, si rahisi sikuzote kutokeza kuwa tofauti. Charlene mwenye miaka 16 akubali hivi: “Watoto shuleni hukutazama kiajabu usipovaa kama wao.” Hata hivyo, uachapo wengine wakuamuru-amuru juu ya upaswalo kufanya, wapata kuwa mtumwa wao. (Linganisha Warumi 6:16.) Mwanamke kijana jina lake Johanna akubali hivi: “Mimi huudhika kwa sababu nahisi kama kwamba sikuzote navaa ili nipendeze mtu mwingine.”
Je, hili ni jambo la hekima sikuzote? Chukua, kwa kielelezo, ile mitindo ya genge la barabarani, hipu-hopu, na “granji” (uzembe). Wengi huvaa mitindo hii kwa sababu yapendwa na wengi. Hata hivyo, mitindo hiyo huonyesha wazi hasira na uasi. Je, kuivaa kungeweza kuwapa wengine wazo lisilofaa juu yako? (Yohana 15:19; linganisha 2 Wakorintho 6:4.) Isitoshe, kuwa na sura ya mwanagenge kungeweza kufanya uuawe. Kwa hiyo shule fulani za Marekani zimepiga marufuku kuvaa mitindo ya magenge. Somo? Si jambo la akili kuacha marika wako wakuchagulie jumla yako ya mavazi, seuze maisha yako. Badala ya kuhangaikia yatakayowapendeza, ‘fuliza kuhakikisha ni nini lililo lenye kukubalika kwa Bwana’!—Waefeso 5:10, New World Translation.
Kufikiria Mahitaji Yako
Ukiisha kuacha kufuata ushokoa wa mitindo na fashoni, waweza kuanza kuongezea jumla ya mavazi yatimizayo mahitaji yako halisi. Kwa kielelezo, wakati wako mwingi hutumiwa shuleni. Ikiwa shule yako hutaka yunifomu au hufuata sheria kali za mavazi, machaguo yako yatakuwa na mipaka. Lakini katika shule nyingi hiari huruhusiwa, na ni kawaida kuwa na sura ya kikawaida tu.
Katika hali kama hiyo, huenda lisiwe jambo la hekima kujifanya utokeze wazi kwa kujishaua kwa jaketi na tai au rinda la kimapambo. Ungetaka kuonekana kikawaida tu bila kuonekana wa kimitindo wala wa kizembe. Msichana tineja jina lake Millie alifanya hivyo. Akiwa shuleni aliepuka mivao ya fashoni za kupita kiasi. Ikiwa hali yako iko hivyo, huenda wewe vilevile ukahitaji suruali kadhaa, shati, au blauzi za kikawaida tu kati ya jumla ya mavazi yako. Ikiwa fedha ni adimu, huenda ikatosha kuwa na vichache tu vya vitu hivi.—Linganisha Luka 10:42.
Kuweka mavazi yako ya shuleni yakiwa mengi kiasi huenda kukakuachia fedha za kutosha kutimiza mahitaji mengine. Kwa kielelezo, je, una kazi ya nje au kazi za nyumbani za kufanya? Basi wahitaji mavazi fulani ya kudumu, yaliyo madhubuti. Mavazi yafaayo yaweza kuhitajiwa pia yakahitajiwa kwa michezo na starehe nyinginezo. Ingawa huenda ikawa ni desturi kuvaa makaptura, mablauzi, na masnika ya mishono bora, utapata kwamba mavazi fulani yasiyo ghali sana yaweza kufaa jinsi hiyohiyo.
Ikiwa wewe ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, utataka pia kufikiria kwamba una uhitaji wa mavazi yafaayo kwenda kwenye mikutano ya Kikristo, kwa kuwa nguo za kikawaida hazifai kwa ibada. Katika mabara ambako mavazi ya mtindo wa Magharibi huvaliwa, wanaume vijana kwa kawaida huvaa suruali za pindi rasmi, shati ya pindi rasmi, tai, na jaketi. Kwa kawaida wanawake vijana huvaa vazi refu au rinda na blauzi. Mavao kama hayo huvaliwa pia katika kazi ya kuhubiri mlango kwa mlango. Wingi uwezao kununua wa mavazi hayo utategemea uwezo wako wa kifedha. Uzuri ni kwamba, si lazima nguo zako ziwe maridhawa wala za karibuni zaidi katika fashoni. Zapasa kuwa nadhifu na safi.
Yesu Kristo alihudhuria arusi, na huenda wewe ukaombwa uhudhurie matukio fulani ya kijamii. (Yohana 2:1, 2) Ikiwa ni desturi kuvalia rasmi kwa ajili ya matukio kama hayo, basi ni jambo la akili kuwa na mavazi fulani yafaayo. “Mimi nimekuwa katika hali ambazo sikuwa nimevalia kwa ajili ya pindi ile, na hiyo haikufurahisha,” akubali wazi Johanna. Kuwa na angalau vazi moja la uvalio rasmi kwaweza pia kukuepusha na msongo na gharama ya ununuzi wa dakika ya mwisho.
Kufanya Orodha ya Yaliyopo
Wewe ungeweza kufanya ule ambao mwandikaji Jean Patton auita ukaguzi wa kabati la mavazi. (Color to Color) Pekua-pekua nguo zako, kutia na vitu vilivyowekwa akibani. Huenda ukagundua mavazi uliyokuwa umeyasahau. Wakati huohuo, waweza kuondolea mbali vitu ambavyo vimeacha kukutosha au usivyovihitaji tena.
Halafu, fanya orodha ya vilivyopo, labda ukivipanga kwa aina za mavazi makuu (koti, suti, mavazi marefu, bleza, jaketi za michezo), mavazi maambatani (mablauzi, sweta, shati za mavazi marefu), na mavazi ya nyongeza (skavu, mishipi, glavu, kofia, viatu, vikoba vya mkononi, tai). Orodha ya jinsi hiyo husaidia kukazia ni vitu gani huenda ukavihitaji ili kukamilisha jumla ya mavazi yako.
Ununuzi Wenye Akili
Katika mabara fulani ni anasa kununua nguo mpya. Vijana hujikakamua kutunza nguo zozote walizo nazo na kuziweka zikiwa nadhifu na safi kiasi. Ingawa hivyo, namna gani ikiwa una uwezo wa kununua nguo fulani zilizo mpya? Katika kitabu chake Working Wardrobe, Janet Wallach ataarifu kwamba “mwanamke aweza kuokoa wakati na fedha ikiwa amenunua nguo zake kwa mpango na kusudi.” Ndivyo ilivyo kwa wanaume vijana pia. Yaelekea kwamba wewe una fedha kidogo, kwa hiyo wahitaji kuhesabu gharama ya chochote ununuacho. (Linganisha Luka 14:28.) Huenda hiyo ikamaanisha kupunguza orodha ya manunuo yako, ukishikamana na vitu vyenye umaana wa kwanza. Kawaida nzuri ni kutumia fedha zilizo nyingi kwa mavazi utakayovaa zaidi.
The Better Business Bureau A to Z Buying Guide hutoa ushauri huu: “Ongeza wingi wa mavazi yako kwa kutegemea kikundi kimoja cha rangi fulani ya msingi, kama vile samawati na kijivu au kahawia na nyeusi. Chagua nguo kuu zikiwa za rangi hizo, na uache rangi za kukamilishia hizo nyingine ziwe za shati, mablauzi, na mavazi ya nyongeza.” Nguo zenye rangi za kati zitabaki zikiwa za kimtindo kwa muda mrefu zaidi. Kwa kushikamana na rangi za msingi, waweza kujaribia na kufanyiza kwa urahisi zaidi mavao mapya.
Mithali 14:15 husema hivi: “Mwenye busara huangalia sana aendavyo,” na kuwa na mpango halisi wa manunuo yako kwaweza kukusaidia uepuke ununuzi wa kushtukia ulio na gharama nyingi. “Sikuzote mimi huenda dukani nikiwa na orodha yangu ya ununuzi,” asema mwanamke mmoja kijana. Kumbuka, pia, kwamba hatimaye, kuna faida za kufuatia ubora, si wingi. Vazi bora laweza kudumu kwa miaka mingi. “Mimi ningali na sweta nilizovaa nikiwa tineja,” asema mwanamke kijana mmoja. Hata hivyo, jina la muundo si lazima liwe uhakikisho kamili wa ubora, ambao huamuliwa vizuri zaidi kwa kulichunguza vazi lenyewe kwa makini.a
Uwe mwangalifu kutokimbilia kufuata mitindo. Vazi sanifu la kike au suti ya mwanamume itadumu na mtindo ufaao karibu sikuzote. Mitindo ya kufuata maelekeo huacha upesi kupendwa na walio wengi. Katika kitabu chake Conservative Chic, Amelia Fatt asema hivi: “Nguo za kukawia kufuata mitindo ni rahisi zaidi kuongezewa vitu vingine, ni rahisi zaidi kuongezewa mavazi mengine mwaka ujao, ni akiba nzuri zaidi.”
Usisahau kwamba wazazi wako wana miaka ya uzoefu katika kununua nguo. Baadhi ya mapendezi yenu huenda yakawa yameachana kwa kizazi kimoja, lakini huenda mkakubaliana zaidi ya vile ufikirivyo katika mambo yale ya msingi. “Mama yangu alisaidia mimi na dada yangu kusitawisha mapendezi mazuri katika mavazi,” akumbuka Angela. Baada ya muda na saburi, wewe pia huenda ukaweza kuongezea jumla ya mavazi yafaayo, yenye kutimiza mahitaji yako. Labda hutalazimika tena kusema, ‘Sina cha kuvaa!’
[Maelezo ya Chini]
a Ona “Vijana Huuliza . . . Ni Nini Siri ya Kuchagua Nguo Zifaazo?” katika toleo letu la Mei 8, 1990.
[Picha katika ukurasa wa 19]
Kwanza fanya orodha ya mavazi uliyo nayo tayari