Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 2/8 kur. 4-6
  • Watoto Watekwapo na Watu Wasiojulikana

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Watoto Watekwapo na Watu Wasiojulikana
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ono Lenye Kuogofya
  • Je, Jamii Inashiriki Lawama Hiyo?
  • Mlinde Mtoto Wako Ili Asiathiriwe na Ponografia
    Msaada kwa Ajili ya Familia
  • Kunyanyasa Watoto Kingono—Tatizo la Ulimwenguni Pote
    Amkeni!—1997
  • Ponografia—Je, Ina Madhara?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Madhara Yanayosababishwa na Ponografia
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 2/8 kur. 4-6

Watoto Watekwapo na Watu Wasiojulikana

“TAFADHALI TUSAIDIENI KUTAFUTA MSICHANA HUYO. TAFADHALI, TAFADHALI SAIDIENI SARA!”

Kilio hiki chenye huzuni nyingi kutoka kwa wazazi wawili walioumia vibaya sana kilionyeshwa katika televisheni kotekote Marekani katika jitihada ya kumwokoa binti yao mwenye umri wa miaka 12, Sara Ann Wood. Alikuwa ametoroshwa majuma matatu mapema alipokuwa akiendesha baiskeli kwenye barabara ya mashambani kuelekea alikokuwa akiishi.

KIKUNDI kikubwa cha kumtafuta kilimsaka mbugani, nyanjani, na kwenye maziwa yaliyo karibu karibu kikitafuta dalili za msichana aliyepotea. Karibu wakati huohuo, Tina Piirainen, mzazi mwingine mwenye huzuni nyingi katika jimbo jirani, alitokea kwenye televisheni akisihi kwa ajili ya binti yake aliyekuwa amepotea. Akiwa ameshawishiwa kando-kando ya kijia chenye miti mingi, Holly mwenye umri wa miaka kumi alitokomea kwa muda usiopata saa moja. Baadaye mwili wake ulipatikana katika uwanja fulani.

Maisha kwa wazazi wa mtoto aliyepotea ni uguo lenye kuumiza. Kila siku wao hushindana na kutokuwa na hakika kama mtoto wao yu hai, labda akiwa ameumizwa kimwili au kutendwa vibaya kingono, au mfu, kama kilivyokuwa kisa cha kijana Ashley. Ashley aliandamana na familia yake ili kumtazama kakaye akishindana katika mchezo wa soka. Akiwa amechoka kutazama msichana huyo, alitembea kwenye uwanja wa michezo—naye akatokomea. Baadaye, mwili wa Ashley ulipatikana katika uwanja ulio karibu. Alikuwa amenyongwa.

Ono Lenye Kuogofya

Kila mwaka, katika Marekani, kati ya familia 200 na 300 hupatwa na ono lenye kuogofya la mtoto kutoroshwa kisha labda kukosa kumwona kamwe akiwa hai tena. Ingawa idadi zaonekana ndogo kwa kulinganisha na uhalifu mwingine wenye jeuri unaotendwa, hofu na tisho zisambaazo katika jumuiya nzima-nzima huathiri maelfu ya watu. Kwa mshtuko, wao huuliza, ‘Msiba kama huo wawezaje kutukia hapa? Je, mtoto wangu ndiye atakayefuata?’

Katika Marekani, idadi ya kesi zinazoripotiwa kila mwaka za watoto waliotekwa nyara ni kati ya 3,200 na 4,600. Theluthi mbili au zaidi za hizi hutendwa vibaya kingono. Ernest E. Allen, msimamizi wa Kitovu cha Kitaifa cha Watoto Waliopotea na Kutumiwa Vibaya, aliandika hivi: “Sababu iliyo kuu ni ngono, ikifuatiwa na kusudi la kuua kikusudi.” Pia, kulingana na Idara ya Hukumu, utekaji-nyara mwingine zaidi ya 110,000 hujaribiwa kila mwaka na waendesha-magari, sana sana na wanaume, wakijaribu kushawishi mtoto kuingia ndani ya gari lao. Mabara mengine pia yanapatwa na ongezeko la jeuri dhidi ya watoto.

Je, Jamii Inashiriki Lawama Hiyo?

Kuhusu uuaji wa watoto, mtafiti Mwaustralia aonyesha kwamba “si tukio la hivi hivi tu.” Katika kitabu chake Murder of the Innocents—Child-Killers and Their Victims, Paul Wilson hutaarifu kwamba “wote wawili muuaji na muuliwa hunaswa katika mfumo mbaya ambao jamii yenyewe imeubuni.”

Huenda ikashangaza kufikiri kwamba jamii yaweza kuwa yenye daraka la, au kwa kiasi yaweza kuwa imechangia, msiba huu, kwani watu walio wengi hupata unyanyasaji na uuaji wa watoto kuwa tendo lenye kukirihisha. Hata hivyo, jamii zilizoendelea kiviwanda, na hata nyingi za zile ambazo hazijaendelea sana, zimekolezwa na filamu, maonyesho ya televisheni, na kusoma vichapo vinavyotukuza ngono na jeuri.

Sasa kuna filamu za kiponografia zaidi na zaidi zinazoonyesha watoto na hata watu wazima wakiwa wamevalia kiasi cha kufanana na watoto. Hizi huonyesha ngono na jeuri dhahiri inayohusisha watoto. Wilson aandika zaidi katika kitabu chake kwamba kunavyo vichwa vya filamu kama vile Death of a Young One, Lingering Torture, na Dismembering for Beginners (Kifo cha Aliye Mchanga, Kutesa-Tesa Polepole, na Kufunza Wapya Kukata-Kata Viungo). Je, jeuri na ponografia zina athari ya kadiri gani? Ni biashara ya dola mabilioni mengi!

Jeuri inayoongezeka na ponografia zina matokeo makubwa sana kwa maisha ya wale wanaowatumia vibaya watoto. Mhukumiwa mkosaji kingono aliyeua wavulana watano alikiri hivi: “Mimi ni mgoni-jinsia-moja wa watoto, niliyehukumiwa kwa mauaji ya kikusudi, na ponografia ilichangia kuanguka kwangu.” Profesa Berit As, wa Chuo Kikuu cha Oslo, aeleza athari ya ponografia ya watoto: “Tulifanya kosa kubwa mwishoni mwa miaka ya 1960. Tuliamini kwamba ponografia ingeweza kubadili uhalifu wa kingono kwa kuandaa kijia cha kuondolea wahalifu wa kingono, na tukaondoa kizuizi hicho. Sasa twajua tulikosea: ponografia kama hiyo huhalalisha uhalifu wa kingono. Huongoza mkosaji kufikiri, ‘Ikiwa naweza kutazama hii, ni lazima iwe ni sawa kuifanya.’”

Tamaa fulani ya mtu mzima izidipo kutekenywa ndivyo anavyokuwa mraibu wa ponografia. Kama tokeo, watu fulani wako radhi kutumia ama nguvu ama jeuri ili kuwapata watoto kwa matumizi yao mabaya, kutia ndani kuwalala kinguvu na kuwaua kikusudi.

Kuna sababu nyingine za utekwaji-nyara wa watoto. Katika mabara fulani hili limeongezeka kwa sababu ya hali mbaya za kiuchumi. Wakiwa wameshawishwa na fedha nyingi za fidia zinazolipwa na familia tajiri, watoroshaji huwalenga watoto. Kila mwaka vitoto vingi huibwa na kuuzwa kwa vigenge vya kuhodhi ambavyo huvisafirisha nje ya nchi.

Ni nani hufanyiza sehemu iliyo kubwa ya watoto wanaopotea? Ni nini huwapata? Makala mbili zifuatazo zitachunguza jambo hili.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Mamilioni ya Malaya Watoto

Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu watoto milioni kumi, hasa katika nchi zinazositawi, wamelazimika kuingilia umalaya, wengi wao wakiwa ni waliokuwa wametoroshwa. Kazi hii mbovu imeongezeka katika Afrika, Asia, na Amerika ya Latini sambamba na lile ongezeko katika utalii wa kigeni. Katika maeneo fulani, kati ya mamilioni ya watalii, hasa kutoka mabara yenye utajiri, karibu theluthi mbili ni “watalii wa ngono.” Lakini kuna siku ya kutozwa hesabu, kwa kuwa uhalifu wa mwanadamu ‘u utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu,’ Yehova Mungu.—Waebrania 4:13.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Ni ono lenye kuogofya mtoto atekwapo nyara

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki