Kunyanyasa Watoto Kingono—Tatizo la Ulimwenguni Pote
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA SWEDEN
Jamii ya kibinadamu inakumbwa na namna ya kutenda watoto vibaya ambayo ina mweneo na asili ambayo haikujulikana sana hadi miaka ya majuzi. Ili kuona ni nini kiwezacho kufanywa kuhusu hilo, wawakilishi wa mataifa 130 walikutana Stockholm, Sweden, kwenye Mkutano wa kwanza Ulimwenguni Dhidi ya Kunyanyasa Watoto Kingono kwa Faida za Kibiashara. Mleta-habari wa Amkeni! katika Sweden alikuwapo pia.
MAGDALEN alipokuwa na umri wa miaka 14, alishawishiwa kufanya kazi ya kusimamia baa katika Manila, Filipino. Kwa hakika, kazi yake ilihusisha kuwapeleka wateja wa kiume katika chumba kidogo na kuvua nguo kwa ajili ya unyanyasaji wao wa kingono—wastani wa wanaume 15 kwa usiku mmoja na 30 siku za Jumamosi. Nyakati fulani, aliposema kwamba hangeweza kuvumilia zaidi, meneja wake alikuwa akimlazimisha kuendelea. Mara nyingi siku yake ya kazi ilikwisha saa kumi alfajiri, akihisi mchovu, akiwa ameshuka moyo, na mwenye huzuni.
Sareoun alikuwa mvulana mchanga yatima aliyekuwa akiishi barabarani katika Phnom Penh, Cambodia. Alikuwa na kaswende, na ilijulikana kwamba alikuwa ‘akitembea’ na watu kutoka nchi za nje. Alipewa makao madogo ya kuishi katika pagoda, ambapo alikuwa atunzwe na mtu aliyekuwa hapo awali mtawa wa kiume. Hata hivyo, mwanamume huyu, alimtenda vibaya kingono mvulana huyo na kumpelekea watu kutoka nchi za nje ili wafanye naye ngono. Makao ya kuishi ya Sareoun katika hiyo pagoda yalipobomolewa, alianza kuishi na shangazi yake lakini bado alilazimishwa kwenda kufanya kazi barabarani.
Hivyo ni vielelezo viwili tu vya tatizo baya sana lililoshughulikiwa kwenye Mkutano wa Ulimwenguni Dhidi ya Kunyanyasa Watoto Kingono kwa Faida za Kibiashara mwishoni mwa mwaka jana. Zoea hili limeenea kadiri gani? Mamia ya maelfu ya watoto wanashiriki—kwa hakika, wengine husema mamilioni. Mjumbe mmoja alieleza kifupi tatizo hilo: “Watoto wananunuliwa na kuuzwa kama bidhaa za kingono na za kibiashara. Wanaingizwa isivyo halali kuvuka mipaka kama bidhaa zisizo halali, wakizuiwa madanguroni na kulazimishwa kukubali idadi kubwa ya wanyanyasaji wa kingono.”
Katika taarifa yake ya ufunguzi kwa kikusanyiko hicho, waziri mkuu wa Sweden, Göran Persson, aliuita unyanyasaji huu kuwa “uhalifu mkatili kupita wote, na wa kiwango cha kuchukiza.” Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa alisema kwamba huo “ni shambulizi kwa watoto linalokuja kwa njia nyingi . . . , ni baya kabisa na ni uvunjaji wa haki za kibinadamu wenye kuchukiza kuliko wote unaowazika.” Maelezo mengi kama hayo ya hasira kuelekea kunyanyasa watoto kingono yalitolewa kutoka jukwaani kotekote katika mkutano huo wakati mweneo, asili, visababishi, na matokeo ya unyanyasaji huo yalipofikiriwa.
“Mweneo wao hupita mipaka ya kitaifa, kishindo chao kutoka kizazi kimoja hadi kingine,” hati moja ikasema. Nyingine ilitaarifu hivi: “Yaaminika kwamba watoto wakadiriwao kuwa milioni moja huingia katika biashara isiyo halali yenye kuchuma mabilioni ya dola kila mwaka.” Kukiwa na tokeo gani? “Hisi ya watoto hao ya adhama, utambulisho na kujiheshimu huharibiwa na uwezo wao wa kutumaini humalizwa nguvu. Afya yao ya kimwili na kihisia-moyo huwekwa hatarini, haki zao huvunjwa na wakati wao ujao huhatarishwa.”
Baadhi ya Visababishi
Ni nini baadhi ya visababishi vya tatizo hili lenye kuongezeka sana? Ilitaarifiwa kwamba watoto “wanalazimishwa na hali kuingia katika ukahaba, kufanya hivyo kukiwa njia ya kusalimika barabarani, kukisaidia kutegemeza familia zao, au kulipia mavazi na bidhaa. Wengine wanashawishiwa na wonyesho wa daima wa watu wanaofurahia bidhaa za kibiashara.” Na wengine hutekwa nyara na kulazimishwa kuingia katika ukahaba. Kuzorota kwa haraka kwa maadili kila mahali, na vilevile hisi ya kawaida ya kutokuwa na tumaini, vilitajwa kuwa miongoni mwa visababishi.
Wasichana wengi na wavulana hujihusisha katika kazi ya ngono kwa sababu ya kutendwa vibaya katika familia—jeuri na ngono ya maharimu nyumbani huwafanya waende barabarani. Huko, wamo hatarini mwa kutendwa vibaya na wanaovutiwa na watoto kingono na wengine, hata, yaonekana na polisi fulani. Ripoti moja kuhusu tatizo hilo yenye kichwa Kids for Hire hueleza kuhusu Katia mwenye umri wa miaka sita, katika Brazili. Aliposhikwa na polisi, polisi huyo alimlazimisha afanye vitendo visivyo na adabu akamtisha kuua familia yake ikiwa angemwambia mkuu wake. Kesho yake alirudi tena na wanaume wengine tano, wote wakitaka awafanyie huduma hizo za kingono.
The Children’s Ombudsman, shirika la Sweden, liliwaambia wajumbe hivi: “Wakati ambapo uchunguzi umefanywa juu ya kile kisababishacho ukahaba wa watoto, hakuna shaka kwamba utalii [wa ngono] ndio mmojawapo visababishi vikuu.” Ripoti moja ilisema: “Kuongezeka kunakotazamisha kwa ukahaba wa watoto kwa miaka kumi iliyopita kunasababishwa moja kwa moja na biashara ya utalii. Ukahaba wa watoto ndio kivutio cha watalii kilicho kipya zaidi kinachoandaliwa na nchi zinazoendelea.” “Watalii wa ngono” kutoka, Ulaya, Marekani, Japani, na kwingineko hufanyiza uhitaji mkubwa wa makahaba watoto ulimwenguni pote. Shirika moja la ndege la Ulaya lilitumia mchoro wa katuni ulio wazi wa mtoto akiwa katika kikao cha kingono ili kuendeleza utalii wa ngono. Mashirika ya kupanga safari hupanga utalii wa ngono kwa maelfu kila mwaka.
Pia katika orodha hiyo ndefu ya visababishi kuna uendelezaji wa kimataifa wa biashara ya ngono ya watoto ambao hufanywa kupitia tekinolojia mpya. Mfumo wa Internet, pamoja na tekinolojia nyinginezo za kompyuta, huripotiwa kuwa chanzo pekee kilicho kikubwa kuliko vyote vya ponografia. Vifaa vya vidio vya bei ya chini pia vimerahisisha utokezaji wa ponografia ya watoto.
Wanyanyasaji Hao Ni Nani?
Watu wazima wengi ambao hutumia watoto vibaya kingono ni wanaovutiwa na watoto kingono. Mtu wa aina hiyo huvutiwa kingono na watoto kwa njia iliyopotoka. Kulingana na Children’s Ombudsman la Sweden, “wao si lazima wawe ni watu wenye kuzeeka, waliovalia makoti ya mvua kizembe au watu wajeuri wenye kiburi cha kiume. Mtu wa kawaida mwenye kuvutiwa isivyofaa na watoto kingono ni mwanamume aliyesoma vyema wa umri wa makamo, mara nyingi akifanya kazi pamoja na watoto akiwa mwalimu, daktari, mfanyakazi wa umma au kasisi.”
Kikundi hicho cha Sweden kilitokeza kielelezo cha Rosario, msichana Mfilipino mwenye umri wa miaka 12 ambaye alitumiwa vibaya kingono na mtalii wa kingono, daktari kutoka Austria. Kutendwa kwake vibaya kulimfanya afe.
Carol Bellamy, mkurugenzi mkuu wa UNICEF (Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa) huko Geneva, alitaarifu yafuatayo kuhusu msichana huyo Mfilipino mwenye umri wa miaka 12: “Mara nyingi ni watu wazima walewale ambao wameamaniwa na utunzaji na ulinzi wa watoto ambao huruhusu na kutenda zoea hili lisilostahimilika. Kuna walimu, wataalamu wa afya, maofisa wa polisi, wanasiasa, na makasisi ambao hutumia umashuhuri wao na mamlaka kunyanyasa watoto kingono.”
Dini Yahusika
Mjumbe kutoka Kanisa Katoliki la Kiroma kwenye mkutano huo wa Stockholm alitangaza kwamba unyanyasaji wa watoto ndio “uhalifu mwovu kupita wowote wenye kuchukiza” na “tokeo la upotoshaji mkubwa na mvunjiko wa maadili.” Hata hivyo Kanisa Katoliki limeathiriwa vibaya sana na mazoea hayo miongoni mwa makasisi walo lenyewe.
Katika toleo la Agosti 16, 1993 la Newsweek, makala yenye kichwa “Makasisi na Utendaji Vibaya” iliripoti juu ya “kashfa mbaya sana ya kikasisi katika historia ya kisasa ya Kanisa Katoliki la Marekani.” Hiyo ilitaarifu: “Ingawa madai yamezushwa dhidi ya makasisi wakadiriwao kuwa 400 tangu 1982, wanakanisa wengine hutaja kutokana na tarakimu zilizopo kwamba makasisi wapatao 2,500 wametenda watoto au matineja vibaya kingono. . . . Zaidi ya fedha, kashfa hiyo imegharimu kanisa aibu mbaya sana—na kiasi fulani cha mamlaka yalo ya maadili.” Dini nyinginezo kotekote ulimwenguni ziko katika hali hiyohiyo.
Ray Wyre, mshauri wa kitalaamu wa uhalifu wa kingono kutoka Uingereza, aliuambia mkutano wa Stockholm kuhusu wavulana wawili ambao walikuwa wametendwa vibaya kingono kwa ukatili na kasisi. Mmoja wa wavulana hao sasa huendesha shirika la wahasiriwa wa kutendwa vibaya kingono na makasisi, na yule mwingine mwenyewe ni mtendaji-vibaya.
Mettanando Bhikkhu, msomi Mbuddha kutoka Thailand, aliripoti kwamba “mazoea fulani ya Kibuddha hushiriki lawama kwa ajili ya utendaji vibaya watoto kingono wa kibiashara katika Thailand kwa hali kadhaa. Katika vijiji vyenyeji katika Thailand, watawa wa kiume nyakati fulani wamenufaika kutokana na fedha zilizorudishwa kwa jumuiya hiyo na watoto ambao wamekuwa wakilazimishwa kuingia katika ukahaba.”
Ni Nini Kiwezacho Kufanywa?
Dakt. Julia O’Connell Davidson, wa Chuo Kikuu cha Leicester katika Uingereza, alialika mkutano huo utoe mwito wa ushindani kwa ujiteteaji wa wanyanyasaji wa mwenendo wao. Watendaji vibaya mara nyingi hukazia ulegevu wa kingono na ukosefu wa adili wa mtoto, wakisababu kwamba tayari mtoto huyo si safi kiadili na ameharibika. Wanyanyasaji wengine hutumia dai lililopotoka na lisilo la kweli kwamba hakuna dhara litatokezwa na vitendo vyao na kwamba mtoto ananufaika.
Kikundi chenye kushughulikia utalii wa kingono kilipendekeza kwamba pambano lifanywe kupitia elimu katika utaratibu wa masomo shuleni. Kwa kuongezea, habari dhidi ya unyanyasaji wa kingono wa watoto zapaswa kufikia wasafiri kotekote safarini—kabla ya kuondoka, wakati wa safari, na mwishoni mwa safari.
Kuhusu tekinolojia mpya za mawasiliano, kikundi kimoja kilidokeza kwamba mataifa yaandae miongozo ya kuondosha habari yoyote ambayo hunyanyasa watoto. Kuanzishwa kwa shirika moja la kimataifa la kuratibu utendaji katika uwanja huu kulifikiriwa. Kikundi kingine kilipendekeza kwamba ponografia ya kuendelezwa kwenye kompyuta na kumiliki ponografia ya watoto kwa ujumla kufanywe kuwa makosa ya jinai katika nchi zote, kukiwa na adhabu iliyotolewa kisheria.
Wazazi waweza kufanya nini? Kikundi chenye kushughulikia daraka la vyombo vya habari kilidokeza kwamba wazazi wachukue daraka la kulinda watoto wao. Hilo lilitaarifu hivi: “Wazazi hawawezi tu kuongoza watoto wao wanapoendelea kukua huku wakitumia vyombo vya habari lakini wapaswa kuandaa habari ya ziada, maelezo na unamna-namna wa vyanzo vya habari ili kusawazisha athari yenye msukumo ya vyombo vya habari na kumsaidia mtoto kukua katika uelewevu.”
Programu moja ya Kisweden ikiripoti kuhusu mkutano huo ilikazia uhitaji wa wazazi kuwatazama watoto wao vyema na kuwatahadharisha juu ya hatari. Hata hivyo, hiyo ilishauri hivi: “Usiwaonye watoto tu dhidi ya ‘wanaume wazee wapotovu kingono,’ kwa sababu . . . kwa kufanya hivyo watoto watafikiri kwamba wapaswa kujihadhari na wanaume wazee-wazee, waliovalia kizembe, ilhali mtu afanyaye uhalifu huo aweza sana kuwa amevalia yunifomu au suti nzuri. Hivyo, waonye dhidi ya wageni wanaoonyesha upendezi usio wa kawaida.” Bila shaka watoto wapaswa pia kuonywa kuhusu—na kuhimizwa kuripoti kwa wenye mamlaka—mtu yeyote anayewajia kwa njia ya utongozi, kutia ndani watu wanaowajua.
Suluhisho Pekee
Kile ambacho mkutano wa Stockholm haukuweza kudokeza ni jinsi ya kushinda visababishi vya unyanyasaji watoto kingono. Visababishi hivi hutia ndani maadili yanayozorota kwa haraka kotekote; ongezeko la ubinafsi na kutamani vitu vya kimwili; ongezeko la ukosefu wa staha kwa sheria zilizoundwa ili zilinde watu kutokana na ukosefu wa haki; ongezeko la kupuuza hali-njema, hadhi, na uhai wa wengine; kuvunjika kwa haraka sana kwa mpango wa familia; umaskini ulioenea sana kwa sababu ya idadi yenye kupita kiasi ya watu, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, watu kumiminika majijini, na uhamaji; ongezeko la ubaguzi wa kijamii dhidi ya wageni na wakimbizi; utokezaji unaoongezeka daima wa dawa za kulevya pamoja na ulanguzi; na maoni ya kidini, mazoea na desturi zilizopotoka.
Ingawa unyanyasaji watoto kingono ni habari yenye kushtua, ubaya huo haushangazi wasomaji waangalifu wa Biblia. Kwa nini? Kwa sababu sasa tunaishi katika kipindi ambacho Biblia hukiita “siku za mwisho” na, kulingana na Neno la Mungu, “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo” zipo. (2 Timotheo 3:1-5, 13) Kwa hiyo ishangaze kwamba maadili yameendelea kuwa mabaya hata zaidi?
Hata hivyo, Biblia hutaja suluhisho pekee la matatizo makubwa ya ulimwengu—usafishaji kamili utakaofanywa na Mungu Mweza Yote. Karibuni yeye atadhihirisha uwezo wake na kuondoa duniani wote ambao hawafuati kanuni na sheria zake adilifu: “Maana wanyofu watakaa katika nchi, na wakamilifu watadumu ndani yake. Bali waovu watatengwa na nchi, nao wafanyao hila watang’olewa.”—Mithali 2:21, 22; 2 Wathesalonike 1:6-9.
Wale ‘watakaong’olewa’ watatia ndani wote wafanyao watoto kuwa makahaba na watu wafisadi ambao hutumia vibaya watoto. Neno la Mungu hutaarifu: “Wala waasherati . . . wala wazinzi . . . wala wanaume walalao pamoja na wanaume [au wavulana] hawatarithi ufalme wa Mungu.” (1 Wakorintho 6:9, 10) Hilo huongeza kwamba “wale wenye kuchukiza sana katika uchafu wao . . . na waasherati” watakabidhiwa kwa “kifo cha pili”—uharibifu wa milele.—Ufunuo 21:8.
Mungu atasafisha dunia na kuleta mfumo mpya kabisa wa mambo na wenye haki, “mbingu mpya na dunia mpya.” (2 Petro 3:13) Kisha, katika ulimwengu huo mpya atakaoufanyiza, watu wafisadi waliopotoka hawatatumia vibaya tena kamwe wale wasio na hatia. Na wasio na hatia hawatahofu tena kamwe kutumiwa vibaya, kwa kuwa “hapana mtu atakayewatia hofu.”—Mika 4:4.
[Blabu katika ukurasa wa 12]
“Namna ya uhalifu mkatili kupita wote na wa kiwango cha kuchukiza.”—Waziri mkuu wa Sweden
[Blabu katika ukurasa wa 13]
“Kila juma, wanaume milioni 10 hadi milioni 12 huzuru makahaba wachanga.”—The Economist, London
[Blabu katika ukurasa wa 14]
Utalii wa ngono ndio kisababishi kikuu cha unyanyasaji watoto katika nchi zinazoendelea
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Utalii wa Ngono—Kwa Nini Upo?
(Baadhi ya sababu zinazofanya watalii wajihusishe katika ngono na watoto)
(1) Kwa kuwa mtalii hajulikani na wenyeji anahisi akiwa amewekwa huru na vizuizi vya kijamii vya kwao
(2) Kwa sababu ya kutofahamu sana au kutofahamu kabisa lugha ya wenyeji, watalii waweza kuongozwa vibaya kwa urahisi kufikiri kwamba kulipa ili kufanya ngono na watoto hukubalika kwa kawaida au ni njia ya kuwasaidia watoto kutoka kwenye umaskini
(3) Mitazamo ya ubaguzi wa kijamii hufanya wageni wanyanyase wale ambao huwaona kuwa wa hali ya chini
(4) Watalii hujihisi wakiwa matajiri wanapoona kwamba huduma za kingono ni za bei rahisi katika nchi zinazoendelea
[Sanduku katika ukurasa wa 15]
Mweneo wa Ulimwenguni Pote wa Tatizo Hilo
(Yafuatayo ni makadirio ya wataalamu kadhaa wa serikali na mashirika mengineyo)
Brazili: Kuna angalau makahaba watoto 250,000
Kanada: Maelfu ya wasichana matineja wanafanywa kuwa makahaba na vikundi vilivyopangwa vya kikahaba
China: Kuna watoto waliofanywa kuwa makahaba kuanzia 200,000 hadi 500,000. Katika miaka ya hivi majuzi wasichana Wachina 5,000 hivi wamekuwa wakishawishiwa kuvuka mipaka na kuuzwa Myanmar wakiwa makahaba
Kolombia: Idadi ya watoto wanyanyaswao kingono kwenye mitaa ya Bogotá imeongezeka mara tano katika miaka saba ambayo imepita
Ulaya Mashariki: Watoto wazururao barabarani 100,000. Wengi hupelekwa kwenye madanguro katika Ulaya Magharibi
India: Watoto 400,000 wanashiriki katika biashara ya ngono
Msumbiji: Mashirika ya kutoa misaada yalishutumu vikosi vya UM vya kudumisha amani kwa kunyanyasa watoto kingono
Myanmar: Wasichana na wanawake 10,000 hupelekwa kwenye madanguro katika Thailand kila mwaka
Filipino: Watoto 40,000 wanashiriki
Sri Lanka: Watoto 10,000 kati ya miaka 6 hadi 14 wanatumikishwa katika madanguro na 5,000 wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 18 wanafanya kazi kwa kujitegemea katika makao ya watalii ya waenda-likizo
Taiwan: Watoto 30,000 wanashiriki
Thailand: Watoto 300,000 wanashiriki
Marekani: Vyanzo rasmi husema juu ya zaidi ya watoto 100,000 wanaoshiriki