Nahodha James Cook—Mvinjari Hodari wa Pasifiki
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA
MBALI na Uingereza, Australia, New Zealand, Hawaii, na visiwa vya Pasifiki, jina Nahodha James Cook, huenda hata lisijulikane na watu wengi. Ingawa, katika nchi zilizoorodheshwa hapo juu, karibu kila mtoto wa shule amjua Nahodha Cook—sawa na vile watoto wa Waamerika wajifunzavyo juu ya Christopher Columbus.
Hata hivyo, bila shaka ni katika Australia—kontinenti ya kisiwa cha Pasifiki Kusini—na katika New Zealand kwamba baharia huyo mvinjari ajulikana vizuri zaidi, kwani jina Nahodha Cook laweza kuonekana kila mahali. Kwa kuongezea, maneno ya kwanza ya ule wimbo “Kweza Haiba ya Australia,” ambao katika 1974 ulikuja kuwa wimbo wa taifa, kihalisi huimba sifa za nahodha huyo hodari.
Yule Mwanamume James Cook
James Cook alikuwa mvulana wa mashambani, aliyezaliwa katika Yorkshire, Uingereza, katika Oktoba 1728. Ingawa maisha yake ya mapema hayajulikani sana, kwa wazi alipokea elimu kiasi fulani katika shule ya kijiji ambayo ingalipo ya Ayton. Baadaye alizoezwa kuuza vyakula katika bandari ya uvuvi ya Staithes. Kutoka hapo, hewa ya baharini ikiwa puani mwake, alibadili kazi-maisha yake kuwa biashara ya makaa-mawe na akajifunza kuendesha merikebu, akifanya kazi karibu na fuo zenye pepo za Bahari ya Kaskazini.
Mitumbwi ya makaa-mawe haikuwa ndiyo matayarisho pekee Cook alikuwa nayo kwa ajili ya safari za baharini za baadaye. Akiwa bado ufuoni, aliendeleza mafunzo yake ya hisibati na hatimaye alijiandikisha katika Jeshi la Wanamaji wa Uingereza katika 1755. Hata ingawa alifanya utumishi fulani wa uanamaji, alikuja kujulikana vizuri zaidi kwa ramani na chati zake za Newfoundland, Nova Scotia, na Labrador.
Mandhari ya Ulimwengu ya 1769
Uingereza ilipata ukwezi katika 1763 ikiwa milki ya ulimwengu yenye nguvu zaidi kiukoloni na kibiashara. Baada ya miaka 200 ya vita vya hapa na pale, ilikuwa imeshinda Hispania, Uholanzi, na Ufaransa. Wa mwisho kati ya maadui hao, Ufaransa, iliramba vumbi kwelikweli. Hiki kilikuwa kipindi chenye kutazamisha. Mafanikio ya kisayansi kwa kasi yakishinda ushirikina na kueneza kiu kwa ajili ya ujuzi. Mbinu za kuabiri baharini pia zilikuwa zimefanyiwa maendeleo sana. Jeshi la Wanamaji wa Uingereza na vikoa vya wanasayansi kwa uharaka walikuwa wakitafuta utumishi wa wanasayansi mabaharia ili kuongoza safari katika Pasifiki. James Cook ndiye aliyechaguliwa kwa ajili ya kazi hii ngumu.
Safari za Cook Zaanza
Maagizo Cook aliyoyapokea kwa ajili ya safari yake ya kwanza, 1768-1771, yalikuwa “kufanya Uvumbuzi wa Nchi zisizojulikana kwa wakati huu, na Kupata Ujuzi fulani wa Maeneo ya mbali ambayo hata ingawa awali yalivumbuliwa bado hayajavinjariwa kikamili.” Zaidi ya hayo maagizo yake yalitaarifu kwamba “kuna sababu ya kuwazia kwamba Kontinenti au Bara lenye ukubwa, huenda lipatikane kuelekea Kusini” na kwamba yeye alikuwa “aendelee kuelekea kusini ili kufanya uvumbuzi wa Kontinenti hiyo.” Ingawaje, jukumu la kwanza, lilikuwa kuchungulia mwendo wa Zuhura ivukapo uso wa Jua katika matumaini ya kukadiria kihususa umbali uliopo kati ya Dunia na Jua. Hilo lilikuwa lifanyiwe Tahiti.
Urefu wa safari ya kwanza ulikuwa miaka mitatu kasoro siku 43. Cook alikuwa ametekeleza maagizo yake, na hata zaidi. Ilikuwa ni wakati wa safari hii ya kwanza kwamba alitia nanga katika Ghuba ya Botany jambo linalojulikana sana, kilometa chache tu kusini mwa Bandari ya Sydney yenye umaridadi, ambayo haikuvumbuliwa hadi baadaye. Alikuwa pia amekamilisha safari ya kuzunguka visiwa vyote viwili vya New Zealand na alikuwa Mwanaulaya wa kwanza kuchora ramani ya pwani ya mashariki ya Australia. Bila shaka, hakuvumbua ile kontinenti kubwa ya kusini iliyowaziwa.
Safari ya Pili Yenye Mafanikio
Katika uabiri wake wa pili, 1772-1775, Cook aliagizwa kuchukua zile merikebu mbili Resolution na Adventure kwenye safari ya kuabiri kuzunguka ulimwengu iliyothibitika kuwa yenye mafanikio tena, wakati huu katika Antaktiki, kutia ndani pitapita kadhaa kuvuka utupu wa Pasifiki Kusini. Lakini miezi ya halijoto yenye kuganda na pepo zenye kung’ang’anaza kwa baridi zilimsaidia kusadiki kwamba hakukuwa na kontinenti kusini yenye kufichika. Kikundi chake kilichokuwa kichovu kilifurahi kujikwanyua kutoka kwa bahari zenye theluji na kurudi Tahiti.
Safari ya pili ya Cook ilikuwa yenye mafanikio yasiyo na kifani na ilifikiriwa na kurekodiwa kuwa tukio lililo la maana zaidi katika historia. Alan Moorehead katika kitabu chake The Fatal Impact ataarifu hivi: “Mnamo Julai 1775 walitia nanga kwenye Plymouth. Walikuwa wamekuwa baharini kwa miaka mitatu na siku kumi na nane. Walikuwa wameabiri kwa zaidi ya maili 60,000 baharini—mara tatu uzingo wa dunia—na Cook alikuwa amepoteza wanakikundi wanne tu . . . Safari yake ilimwidhinisha kuwa mmojapo baharia mkubwa kupita wote wa wakati wote.”
Safari ya Tatu Yaleta Msiba
Uabiri wa tatu ulikuwa wa kuvumbua pwani ya Kanada ya Pasifiki na kutafuta Mlango-Bahari wa Kaskazini-Magharibi uliounganisha Pasifiki na Atlantiki kupitia Bahari-Kuu ya Aktiki. Hii ilithibitika kuwa safari ya mwisho ya Nahodha Cook. Alitweka kutoka Uingereza katika Julai 12, 1776, kwenye Resolution, akichukua pia ile meli Discovery iliyorekebishwa upya. Januari 18, 1778, alifikia vile viitwavyo leo Visiwa vya Hawaii, ambapo yeye pamoja na wanaume wake walilakiwa kwa ukarimu. Waliandaa maandalizi upya katika visiwa hivyo murua, kisha wakatumia kiangazi cha kaskazini cha mwaka huo katika kujitahidi kutafuta njia ya baharini kuvuka Atlantiki. Ndipo wakarudi Hawaii katika kipupwe.
Wanahistoria hawajaamua kuhusu kilichosababisha lililoonekana kuwa badiliko kwa upande wa hulka ya Cook. Kuna mashaka kuhusu matendo yake kwa Wahawaii aliporudi. Baadhi yao hudokeza kwamba alianza kuwadhulumu kwa ukatili. Wengine hushuku kama alikiuka mfumo wao wa ibada. Lolote liwalo kweli, ni hapa kwamba alifia katika Februari 14, 1779.
Alikufaje? Wakiwa njiani kuelekea Ghuba ya Kealakekua Januari 17, wavinjari walikuwa wamesalimiwa na Wahawaii 10,000. Wanakisiwa walikuwa wakisherehekea sherehe ya makahiki kwa mungu wao Lono, mungu wa bara. Yaonekana kwamba Cook aliwakilishwa na mungu Lono, naye na wanaume wake walionyeshwa fadhili na ukarimu usio wa kawaida mara nyingine tena. Majuma matatu baadaye, Februari 4, waling’oa nanga na kuabiri baharini. Baada ya siku nne tu, walipambana na dhoruba mbaya sana, na Resolution ikapoteza mlingoti mmoja. Cook alirudi Hawaii.
Kwa mshangao wa Cook, wakati huu ukaribishaji haukuwa wa kirafiki. Wengine huamini kwamba Wahawaii huenda kufikia pale walikuwa wamefikiria kila kitu kwa makini na kufikia mkataa kwamba walidhulumiwa na Cook pamoja na watu wake. Wengine hudokeza kwamba kurudi kwa Cook hakukupatana na kuwa kwake “mungu.” Hata sababu iwe ni gani, wanaume wa Cook waliokuwa wamefumaniwa kwa kusikitisha waliitikia kwa ukali. Hilo liliongoza kwa wizi wa mashua moja kutoka Discovery. Cook alidhubutu kuokoa chombo hicho kwa kujaribu kumchukua chifu, Kalaniopu’u, kama mateka. Mkabiliano ulifuata, na Cook alidungwa kwa kisu na kisha kupigwa hadi akafa ufuoni.
Jarida la mwanakikundi cha Resolution, mwanafunzi wa ubaharia George Gilbert, afafanua kwa undani dakika za mwisho za maisha ya Cook. “Nahodha Cook alikuwa amefika tu kwenye ufuo wa maji na kuzipungia mashua zikome kupiga risasi, wakati mmoja wa Machifu aliyejasiria kuliko wale wengine alipomrukia na kumdunga kisu mgongoni katikati ya mabega kwa Jambia ya Chuma. Mwingine katika wakati Huohuo alimfyatua kichwani kwa rungu ambapo alianguka ndani ya maji; mara walimrukia na Kumweka majini kwa dakika chache, kisha wakamvua miambani na kumpigisha kichwa kwenye mawe mara kadhaa; hivi hakuna shaka bali kwamba alikata pumzi haraka.”
Utu Uliobadilika Wazuka
Kwa wazi kigezo cha tabia cha Cook kilianza kubadilika kwenye safari ya tatu, na tena hakuonyesha utimamu na udhibiti aliokuwa nao katika safari zake mbili za awali katika Bahari za Kusini. Kwenye safari ya tatu, alikuwa amecharaza asilimia 37 ya wanaume wake, karibu maradufu kuliko safari ya kwanza. Wakati huu jinsi alivyowatendea wanakisiwa wa Polynesi ilikuwa pia kinyama. Kwa kielelezo, kwa kukusudia aliagiza uchomaji wa nyumba na kuharibu kwa mashua kwenye kisiwa cha Eimeo katika Tahiti kwa sababu ya wizi wa mbuzi mjamzito. Hata alikuwa ameingilia kuwakata masikio wanakisiwa waliopatikana wakiiba. Je, alikuwa mgonjwa au mchovu au mkatili tu?
Urithi wa Safari
Profesa Bernard Smith katika kitabu chake Captain James Cook and His Times adokeza kwamba “Cook alikuwa si mvumbuzi wa mabara mapya katika njia yoyote ile ya kimsingi ya neno hilo.” Hili huenda likawa kweli, kwani mengi ya maeneo yaliyoonekana na Cook tayari yalikuwa na watu. Hata hivyo, Grenfell Price ataarifu hivi: “Mchango wake uliotokeza kwa ujuzi wa kijiografia ulikuwa kukamilishwa kwa ramani ya Pasifiki kwa uvumbuaji wa ufuo mrefu wa mashariki ya Australia, kuchorwa kwa New Zealand, kuchunguzwa kwa sehemu zilizo ndefu za pwani ya Amerika Kaskazini; kuvumbuliwa kwa visiwa vilivyo vipya kabisa, kama vile Hawaii na New Caledonia; na uvumbuaji upya na usahihishaji wa mahali vilipo vikundi vingine vya visiwa. Kwa wazi Cook atokeza kuwa baharia aliyevumbua . . . kontinenti ya Antaktiki, akiwa angali katika Aktiki alithibitisha uvumbuzi wa Mlango-Bahari wa Bering.” Chati na ramani za Cook zilikuwa zenye manufaa muda mrefu baada ya uyoyomeaji wake kwenye peo za macho za Pasifiki.
Ingawa kwa kusikitisha, yaliyofuata baada ya uabiri wa Cook, yalikuwa vichafuzi vya magonjwa ya kupitishwa kingono, jeuri ya silaha za kutupa risasi, kufyekwa kwa wanyama wa pori wa Antaktiki, na kudhulumu Wanavisiwa vya Pasifiki. Kuhusu mavumbuo ya Cook ya Antaktiki, Alan Moorehead aliandika hivi: “Mara nyingine tena lilikuwa daraka la Cook kuleta msiba baada ya safari zake. Alikuwa amepata kile huenda kilikuwa kikundi kikubwa cha wanyama wa pori kilichokuwako ulimwenguni, na alikuwa mtu wa kwanza kujulisha ulimwengu kuwapo kwacho. . . . Ujiingizi wa Cook katika Tahiti na Australia ulikuwa na madhara ya kutosha kwa wenyeji: kwa wanyama wa Antaktiki lilikuwa teketezo kubwa.”
Kufuatia ripoti na chati kamili za Cook, wawindaji na mashua za kuvua nyangumi zilivamia kuua. Moorehead aendelea hivi: “Uuaji uliendelea hadi kulipokuwa hakuna chochote kilichoachwa kuuawa, hakuna chochote ambacho kingeliweza kuuliwa kwa urahisi na kwa faida.”
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kifo cha kijeuri cha Cook katika Hawaii
Uvumbuzi wake wa Ghuba ya Botany, Australia
[Hisani]
Michoro: Kwa hisani ya Australian International Public Affairs
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]
Mchoro na John Weber/Dictionary of American Portraits/Dover.Nyuma: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck