Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 4/8 kur. 26-27
  • Kutano la Usiku Katika Tanzania

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutano la Usiku Katika Tanzania
  • Amkeni!—1995
  • Habari Zinazolingana
  • Kutembelea Bonde la Ngorongoro
    Amkeni!—2005
  • Chui—Paka Mwenye Usiri
    Amkeni!—1995
  • Chui wa Ajabu wa Theluji
    Amkeni!—2002
  • Kundi Kubwa Lahama
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 4/8 kur. 26-27

Kutano la Usiku Katika Tanzania

BAADA ya mkusanyiko wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova katika Kenya, tulianza kwa furaha safari yetu ya kibinafsi kuingia Tanzania.

Mahali petu pa kwanza kutua palikuwa Mbuga ya Kitaifa ya Ziwa Manyara. Tulishangaa kuona wanyama wa mbuga wa aina nyingi—kima, swala pala, nyati, punda milia, na zaidi. Wazia ukitazama kiziwa kilichotapakaa viboko. Ukitazama twiga akila upande ule mwingine, simba katika nyasi zilizo mbali, na kundi la nyumbu ng’ambo ya hapo.

Baada ya kufika Kreta ya Ngorongoro, tulikodi mwongoza-watalii na gari ambalo magurudumu yalo yote manne hudhibitiwa na usukani kwa ajili ya kisafari cha siku moja kuingia katika kaldera (kreta ya volkeno iliyoporomoka). Mwendo wenye mitikiso ulituchukua yapata meta 600 kutoka kwenye mzingo hadi kwenye sakafu ya kreta. Jinsi ilivyokuwa mandhari yenye kupendeza! Wanyama wa mbuga walikuwa wameenea kwenye uwanda mkubwa mno. Makundi ya nyumbu yalisonga kana kwamba yalikuwa katika hali ya kuhama. Punda milia, kongoni, na swala tomi na swala granti walijaa tele. Katika mahali pamoja tuliposimama, simba alipumzika katika kivuli cha gari letu, bila kuwa na habari kwamba tulikuwa tukimtazama moja kwa moja tukiwa juu yake. Baadaye tulisimama ili kumtazama kifaru kwa umbali na tembo wa mbugani kwa ukaribu akila kwenye miti. Tulipokuwa tukirudi kuelekea mzingoni, tulikumbuka wanyama wengi sana wenye kuvutia. Je, tulikuwa tumekosa yeyote?

Ndiyo, chui wa Afrika. Lakini tumaini la kuona mmoja mbugani ni karibu sana na kuwa fantasia. Mpigaji picha Erwin Bauer alionelea hivi: “Watalii hufuatia chui kwa idili kupita kiasi na kwa bidii, angalau kwa sehemu sababu ikiwa kwamba wanyama hao ni vigumu mno kuwapata, mbali na kuwapiga picha. Wengi wa wasafiri katika safari zao hawapati kuona kamwe hata mmoja. Katika safari zangu 15, nimeona jumla ya chui wanane, kukiwa na mmoja tu aliyekuwa karibu kiasi cha kupiga picha.”—International Wildlife.

Kufikia usiku tulikuwa na suala jingine lililotusumbua. Mipango ya kupata makao katika loji ilikuwa imefutwa, hivyo ilitulazimu kutafuta mahali pa kulala. Hali hii ilifanya tupitie barabara ya mchanga katika kiza. Ghafula sisi wawili tuliokuwa kwenye viti vya mbele tulishtushwa. Kitu chenye rangi ya hudhurungi yenye madoa-doa kilipita mbele ya miali ya taa zetu za mbele. Tulisimama mara moja na kutweta kwa mshangao!

Hapo mbele yetu tu kulikuwa na chui aliyekomaa! Ikiwa wale waliokuwa wamekaa viti vya nyuma walikosa kuona, hilo lilikwisha kwa dakika moja. Chui huyo alikimbia kando ya barabara upande wa kulia—na kubaki tuli. ‘Nifanye nini?’ yaonekana alikuwa akiwaza pale katika taa na akionwa nasi sote. ‘Nishambulie, au nigeuzie mgongo wangu “adui” asiyejulikana na kujaribu kukimbia ndani ya kichaka?’

Adrian, mmoja wa waandamani wetu, ndiye aliyekuwa karibu zaidi, meta moja tu kutoka kiumbe hiki chenye kuvutia kilichokazika kwa nishati na tayari kuruka. “Haraka, nipe kimweko,” alinong’ona huku akishika kamera yake otomatiki. Watu waliokuwa nyuma yake walinong’ona, “Usifanye kelele.” Kamera ilitayarishwa haraka na picha kupigwa, lakini ilielekea kutotokea vizuri kwa kuwa mmweko ulikuwa tu ndani ya gari. Betri za kamera zilipokuwa zikijirudisha katika hali ya kawaida ili kamera ianze kazi tena, Adrian kwa uangalifu alishusha dirisha lake. Chui sasa alikuwa umbali wa urefu wa mkono, ncha ya mkia wake ikitetema, macho yake yaking’aa.

Mara tu tulipopiga picha ya pili, alifanya chaguo lake. Chui huyo mwenye fahari aliruka ndani ya kichaka na kupotelea humo. Msisimuko ulioje ndani ya gari letu! Lilikuwa ono lisilopaswa kusahauliwa, ono ambalo waongoza-watalii walitueleza baadaye kuwa lisilo la kawaida kabisa. Wakati picha hiyo ya pili ilipotokea vizuri sana, ilichochea akili zetu juu ya kutano hilo la usiku lenye kusisimua katika Tanzania.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki