Chui—Paka Mwenye Usiri
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA
UA lilikuwa likitua. Siku yetu ilikuwa imetumika kutazama na kupiga picha wanyama wa mbuga wenye kutazamisha katika Mbuga ya Wanyama ya Masai Mara ya Kenya. Kabla ya kwenda kupumzika usiku katika loji ya mahema, tulikuwa tujionee tamasha nyingine yenye kusisimua. Matayarisho yalifanywa wakati mmoja wa wafanyakazi wa loji alipotembea polepole kuvuka daraja la kamba juu ya Mto Talek, kipande kikubwa cha nyama ya mbuzi kikiwa kimening’inia juu ya bega lake. Alifunga nyama hiyo katika tawi-panda juu ya mti wa mshita.
Zile rangi za maondokeo ya nuru ya jioni ya kitropiki zilipokuwa zikiishia gizani, chui mkubwa wa kiume alipanda juu ya mti kwa ukimya na kuanza kuvutavuta na kuirarua nyama ile. Aliangazwa kwa taa kutoka kwenye varanda ya kutazamia. Hata hivyo, akiazimia kufurahia mlo wake, chui huyo alitupuuza tulipokuwa tukimtazama kwa kicho na mshangao. Tulielezwa baadaye kwamba ziara yake kwenye mti huo uliochambishwa ilikuwa kawaida ya kila usiku, ambayo aliifuata kwa miaka sita. Kwa hiyo usiku uliofuata tuliandaliwa burudiko la tamasha ileile!
Tungeweza kuthamini kikweli kwa nini chui ameelezwa kuwa “mkamilifu zaidi wa paka wote wakubwa, mwenye kuvutia katika sura na mwenye madaha katika miendo yake.” Akiwa na uzito wa kilogramu 60 au zaidi, chui ni mmoja wa wanyama wenye misuli yenye nguvu sana, akiwa kwa wastani na kimo cha zaidi ya sentimeta 60 mabegani na urefu wa sentimeta 200 kutoka puani hadi ncha ya mkia. Kutazama madoa-doa meusi ya namna ya pekee yaliyopangwa kama shada juu ya ngozi yake ya rangi ya hudhurungi, twakumbushwa juu ya swali lililoulizwa wakati mmoja na nabii Yeremia: “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake?”—Yeremia 13:23.
Yenye kustaajabisha zaidi ni macho yake yenye kung’aa yaliyo ya kijani. Yana utando wa chembe za pekee—ile sehemu yenye kurudisha nuru ya kiwambo mboni katika macho ya wanyama fulani—inayompa mwono wa usiku usio wa kawaida. Chui aweza kuona akiwa na sehemu ya sita tu ya kiwango cha nuru kinachohitajika na macho ya kibinadamu. Utando huu wa chembe, unaorudisha nuru nje kupitia retina, hufanyiza lile tokeo la kung’aa wakati nuru ielekezwapo kwenye macho yake usiku.
Ikiwa ungemtazama chui akipumzika mchana, ungeona kwamba ahema kana kwamba alikuwa kwenye upeo wa uchovu. Hata hivyo, kupumua kwake kwa haraka mno ni sehemu ya mfumo ufaao wa utiaji baridi. Kwa kuhema kwake hadi mara 150 kwa dakika, unyevu waweza kuvukiza kutoka ulimi wake, mdomo, na vipitio vya pua.
Wakiwa wenye kubadilikana zaidi kati ya paka wakubwa, chui waweza kupatikana jangwani na misituni; milimani na katika usawa wa bahari; katika nchi za namna mbalimbali kama vile China, India, na Kenya. Kujapokuwa kujiingiliza kwa binadamu katika sehemu kubwa ya makao ya chui, wanasayansi wanakadiria kwamba kuna karibu chui wapatao milioni moja katika Afrika na Asia pekee. Ingawa hivyo, kwa karne nyingi chui waliepuka machunguo ya kindani ya kisayansi. Fikiria kwa kielelezo, chui wa Sinai. Hadi hivi majuzi alipogunduliwa tena katika jangwa la Yudea, chui huyo kwa muda mrefu alikuwa amefikiriwa kuwa alitoweka!
Paka Mpweke
Chui huepukaje kuonwa na binadamu? Yeye hufanya hivyo kimsingi kwa kuwa hayawani wa usiku—na zaidi ya hilo, ni mwenye kunyatanyata mno na mwenye usiri. Katika sehemu ambazo mwanadamu anatoa tisho, chui ni mnyamavu mwenye tahadhari. Ni wakati anapokasirishwa tu atakapotoa ngurumo na mivumo kama ya simba. Chini ya hali za kawaida, sauti yake haiwi yenye kutisha sana: sauti kali na yenye kuparuza—inayolingana sana na ile sauti ya msumeno ukikata mbao. Kulingana na kitabu Animals of East Africa, kilichoandikwa na C. T. Astley Maberly, husikika kama “Grant-ha! Grant-ha! Grant-ha! Grant-ha!—kwa kawaida ikiishia kwa sauti kali yenye kutweta.” Katika kujipatanisha na kupenda kwake usiri, chui pia hutoa namna mbalimbali za sauti ndogo, nyingi zazo ambazo binadamu hawawezi kusikia.
Zaidi ya hayo, tofauti na simba mwenye kupenda kukaa pamoja na wengine, chui si paka mwenye kushirikiana na wengine. Ingawaje jozi za chui huonekana pindi kwa pindi, chui ni wawindaji wapweke. Ili kupunguza makabiliano yasiyotazamiwa au ya kihasama, chui huweka mipaka ya eneo la kibinafsi ambalo huenda likawa na mweneo wa kilometa 25 hadi 65 za mraba. Yeye hunyunyiza mnyeso kutoka tezi za kipekee ili kuonyesha mipaka ya sehemu ya utendaji wake. Harufu ya kipekee kutoka mnyeso huo inayoweka alama ya eneo lake huenda ikajulisha chui wengine kuhusu jinsia, umri, hali ya kingono, na yawezekana hata utambulisho wa ni nani “mwenye eneo.”
Uwindaji hufanywa kwa unyatunyatu wake ujulikanao sana. Katika nyakati za Biblia alijulikana kuvizia karibu na miji, akiwa tayari kurukia ghafula wanyama wa kufugwa kwa wepesi wa kiajabu. (Yeremia 5:6; Hosea 13:7; Habakuki 1:8) Ili kulinda windo lake kutokana na wala-mizoga, kama vile fisi na mbweha, chui huweka mawindo yake makubwa katika panda ya mti zapata meta 9 hadi 12 juu ya ardhi. Lakini yeye hufauluje kuburuta mzoga wa paa au mtoto wa twiga mwenye urefu wa meta 1.5 hadi mahali pa juu namna hiyo? Hii siyo siri anayofunua chui kwa urahisi. Lakini watazamaji wenye saburi hudai kuwa hilo huwezekana kwa kani za kimwili. Chui hupendelea kula wakiwa starehe, miili ikining’inia kilegevu kwenye matawi ya mti, na katika usiri kamili, wakiwa wamefunikwa kwa matawi na majani.
Asipotishwa, chui huwa mwenye haya na mtulivu na ataepuka ukabiliano na mwanadamu. Hivyo ingawa chui wengine wamepoteza hofu yao ya binadamu na wamekuja kuwa wala-watu, wengi si tisho kwa binadamu. Hata hivyo, akiumizwa au kukabiliwa bila njia ya kutokea chui haonyeshi hofu hata iwe adui yake ni nani. “Chui aliyekasirika,” aandika Jonathan Scott katika The Leopard’s Tale, “ndiye umbo hasa la ukali, . . . akiwa na uwezo wa kuweka nishati zake zote katika mashambulizi ya karibu yenye kasi ya umeme.”
Mama wa Chui
Haishangazi basi, kwamba chui hulea watoto wao katika usiri wa kadiri. Watoto waliozaliwa karibuni hufichwa, mara nyingi pangoni, kwa miezi miwili ya kwanza ya uhai. Ingawa baba hachukui sehemu yoyote katika kulea watoto, mama hufanyiza kifungo cha karibu pamoja nao kwa kuwalisha na kuwasafisha na kuwaweka katika hali ya ujoto. Hatimaye, mama anaweza kuhamisha mkumbo mmoja wa watoto wawili au watatu hadi kwenye makao mapya, akiwabeba katika mdomo wake ikiwa ni wadogo sana au kwa kuwaita tu wamfuate ikiwa ni wakubwa.
Mama wa chui pia hujaribu kuwaficha watoto wake kutokana na maadui kama vile mbega. Lakini iwapo mbega wanashambulia watoto wake, yeye atawashambulia, akijihatarisha ili kuwapa watoto wake nafasi ya kukimbilia usalama. Yeye pia hujihatarisha sana ili kulisha watoto wake. Paka huyo ambaye kwa ukawaida huwa mwenye utulivu aweza kutembea katikati ya kundi la tembo wenye kupiga milio ili kuletea watoto wake wenye njaa nyama.
Kwa kupendeza, chui wachanga hawadhihirishi roho yao ya kujitegemea kwa kipindi fulani. Watoto huachishwa kunyonya yapata miezi sita hivi lakini hawaui windo lao wenyewe hadi wanapokuwa na umri wa mwaka mmoja. Dume hawawi wapweke waliokomaa hadi wanapokuwa na miaka miwili na nusu. Watoto wa kike wanaweza kuendelea kushiriki eneo la makao ya mama yao wakiwa wakubwa.
Chui—Hatimaye Mwenye Amani?
Lakini vipaka hivyo vyenye kujikunyata hukua wakawa wauaji. Hivyo basi huenda ikaonekana vigumu kuamini kwamba maneno ya nabii Isaya yatakuja kuwa kweli wakati wowote: “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui pamoja na mwana-mbuzi.”—Isaya 11:6.
Jitihada za hivi majuzi za kufuga chui zimekuwa na mafanikio machache tu. Sieuwke Bisleti van der Laan na mume wake walilea mkumbo wa watoto wa chui katika shamba lao la Afrika. Watoto hao walifurahia “uhuru kamili” na mara nyingi walilishwa kwa mkono. Lakini hawakufugwa kikweli hata kidogo. Sieuwke Bisleti aandika hivi: “Mara tu chui akuapo kikamili, yeye hujiendea kivyake. Simba atakupenda nyakati zote na kukutii; chui atakutambua nyakati zote lakini hujichagulia mwenyewe jinsi atakavyotenda wakati wowote.”
Hatimaye ilionekana kuwa hatari kuruhusu watoto waliokua kuendelea kuzurura huru kwenye shamba hilo. Uamuzi ulifanywa kuwarudisha mbugani. Je, kulelewa miongoni mwa binadamu wenye urafiki kuliharibu mtazamo au tabia ya chui hao wachanga? Sivyo hata kidogo. Katika kipindi cha siku tatu baada ya kuachwa kwao, chui dume alionekana ameketi kando ya kuro aliyekuwa ameua.
Hata hivyo, mafanikio hayo machache katika kufuga chui hayabatilishi maneno ya unabii wa Isaya juu ya amani kati ya chui na mbuzi. Tukio hili la ajabu litatokea, si kwa jitihada za binadamu, bali kupitia mwingilio wa kimungu. Ingawa hivyo, utawala wa Mungu utafanya mengi zaidi ya kuleta amani kwa jamii ya wanyama. “Dunia itajawa na kumjua BWANA,” akatabiri Isaya. (Isaya 11:1-9) Hata wanadamu wataacha tabia za unyama ambazo zimesababisha vita na migawanyiko. Wakati uleule, mtazamo wa mwanadamu kuelekea ulimwengu wa wanyama utabadilika pia. Hakuna mnyama yeyote atakayekuwa jeruhi wa machinjo yasiyozuiwa. Wala mwanadamu hataharibu makao yao au kuhatarisha kuwapo kwao, kwa kuwa Yehova atakuwa ‘ameharibu hao waiharibuo nchi.’—Ufunuo 11:18.