Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 9/8 kur. 5-9
  • Je! Binadamu na Mnyama Waweza Kuishi kwa Amani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je! Binadamu na Mnyama Waweza Kuishi kwa Amani?
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kumfuga Simba Mkali
  • “Hali Zilizo Tofauti na Kanuni Hiyo”
  • Namna Gani Juu ya Chui?
  • Tembo wa Kiafrika
  • Chui—Paka Mwenye Usiri
    Amkeni!—1995
  • Simba—“Paka” Wenye Manyoya na Wenye Fahari wa Afrika
    Amkeni!—1999
  • Vipingamizi vya Amani Kati ya Binadamu na Mnyama
    Amkeni!—1991
  • Chui wa Ajabu wa Theluji
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 9/8 kur. 5-9

Je! Binadamu na Mnyama Waweza Kuishi kwa Amani?

“Nilijihisi kama nilikuwa kwenye mlango wa paradiso; binadamu na mnyama wakiwa katika upatano wa kutumainiana.” Hivyo ndivyo Joy Adamson alivyoeleza mandhari moja kando ya Mto Ura wa Kenya alipokuwa akitazama aina ya ndege na wanyama wakija kunywa maji. Sehemu yenye kupendeza ya mandhari hiyo ilikuwa ni yule mnyama aliyeketi kwa amani kando yake—simba jike aliyekua kabisa!

Je, kulikuwa na jambo lisilo la kawaida kuhusu huyo simba jike hususa, Elsa, ambaye mamilioni walikuja kumfahamu kupitia kitabu Born Free, cha Joy Adamson? Sivyo, yeye alikuwa simba jike wa kikawaida. Tofauti ilikuwa kwamba alikuwa amejifunza kuishi kwa amani na wanadamu.

Baadaye, wakati filamu Born Free ilipofanyizwa, idadi fulani ya simba wa kike waliofugwa walitumiwa kama kiolezo cha Elsa. Mmoja aliitwa Mara. Kwanza alikuwa na shuku, halafu akawa mwenye kujidaia sana haki zake, bila kuruhusu rafiki zake wapya wa kibinadamu waondoke bila yeye. Ili kumtuliza, George Adamson, mume wa Joy, alihamisha hema lake likaegemea kizimba cha Mara. Mwishowe alihamisha hema lake ndani kabisa ya kizimba! “Kwa miezi mitatu iliyofuata,” akaandika katika kitabu chake Bwana Game, “yeye alilala kwa ukawaida ndani ya [hema langu], mara nyingi akiwa amejinyosha sakafuni kando ya kitanda changu na wakati mwingine juu yacho. . . . Hakunipa kamwe sababu ya kuhangaikia usalama wangu binafsi.”

“Mmoja wa michezo yetu iliyokuwa ya kupendeza zaidi,” akaandika Bw. Adamson, “ulikuwa mimi kulala nikiwa nimejitandaza kabisa juu ya ardhi nikiwa nimefichwa na kishungi cha nyasi. Mara angeninyemelea kwa usiri mkubwa, tumbo likiwa chini karibu na ardhi katika njia ya kawaida ya simba halafu kungekuwa na mtimko wa mwisho wa mbio kama umeme na angeanguka juu yangu. Kila mara alidhibiti kucha zake zenye kutisha na hakuniumiza kamwe.”

Simba mwingine wa kike aliyecheza sehemu ya Elsa alikuwa anaitwa Girl (Msichana). Wakati filamu hiyo ilipokamilika, Girl alirudishwa kwenye pori, ambapo akiwa na simba mwingine alizaa watoto wawili. Rafiki wawili wa Adamson waligundua pango lake. Adamson aliandika: “Akiwa na imani ya kutokeza sana na tabia njema, Girl aliwaruhusu wanaume wawili hao, waliokuwa wakijasiria sana hatari, kukaribia kufikia futi chache kutoka mahali alipozalia . . . Tabia ya Girl ilikuwa ya kutokeza sana kwa vile [mmoja wa wanaume hao] alikuwa kwa ulinganifu ni mgeni zaidi kwake.” Kwa habari ya Adamson, Girl hata alimruhusu kugusa watoto wake, hali simba wengine walifukuzwa.

Kumfuga Simba Mkali

Tabia zinatofautiana kutoka simba mmoja hadi mwingine. Wakati Joy Adamson alipokuwa akimtunza Elsa, kusini zaidi katika Rhodesia ya Kaskazini (sasa Zambia), mlinzi mmoja wa wanyama Norman Carr, alikuwa akifanya vivyo hivyo na wana wawili wa simba. Mmoja wa wana hao, Big Boy (Mvulana Mkubwa), alikuwa mwenye urafiki sana. Yule mwingine, Little Boy (Mvulana Mdogo), alielekea kuwa mwenye kununanuna. Kuhusu huyu wa mwisho, Carr aliandika yafuatayo katika kitabu chake Return to the Wild:

“Wakati Little Boy yuko katika hali hizo za moyo, ninachutama kando yake hali akiningurumia, nikiwa mbali tu na miguu yake ambayo anaweza kuitumia kwa mtupo wa kucha zilizonyoshwa za inchi mbili zilizo kama wembe. Kwa subira ninajaribu kumtuliza kwa kuongea naye kwa njia ya wororo ninapokaribia karibu zaidi na zaidi; na hatimaye ninapomgusa bado ananguruma lakini bila kujikakamua sana. Ninapoweka mkono wangu kwenye mabega yake yenye nywele nyingi na kumkumbatia kifuani, atatulia kwa wazi kama kwamba misuli yake yote imeondolewa hewa. . . . Anaweka kichwa chake kwenye paja langu, akinikaribisha nimpapase.”

Katika utangulizi wa kitabu cha Carr, Kabaila wa Dalhousie, aliyekuwa gavana-mkuu wa nchi hiyo, aeleza kituko alichoshuhudia wakati simba hao walipokuwa wenye umri zaidi ya miaka miwili wakizurura bila kuangaliwa katika pori karibu na kambi ya Carr. Carr alipiga ubinja, na hivi ndivyo Kabaila huyo alivyoeleza itikio: “Walikuja wakiruka sana baada ya ubinja huo kutoka kwa bwana wao wakajisugua vichwa vyao vikubwa kwa kumwegemea yeye, wakati ule ule wakitoa salamu yao ya mngurumo wa furaha lakini wenye kuogofya. Hakika shauku yao kumwelekea haikuwa imepungua.”

Simba wana hofu ya asili kwa binadamu na kwa kawaida hutafuta kumwepuka. Mwitikio huo wa asili unaopatikana miongoni mwa simba na wanyama wengine unaelezwa kwa usahihi katika Biblia. (Mwanzo 9:2) Bila huo binadamu angekuwa mawindo rahisi. Hata hivyo, wanyama fulani hupata kuwa wala-watu.

“Hali Zilizo Tofauti na Kanuni Hiyo”

Mtaalamu wa habari hiyo, Roger Caras, aeleza: “Miongoni mwa karibu kila aina ya mapaka wakubwa inaonekana ikiwamo idadi fulani ya wanyama mmoja mmoja wasio wa kawaida wanaowinda binadamu kama chakula chao. Wao wana hali zilizo tofauti na kanuni hiyo . . . Binadamu kwa kawaida aweza kuishi kwa amani kwa kadiri kubwa pamoja na [mapaka wakubwa].”

Wanyama wengi huonekana kama hawamtambui mtu aliyeketi ndani ya gari. Katika njia hii binadamu aweza kupiga picha za karibu sana za simba. “Lakini,” chaonya kitabu Maberly’s Mammals of Southern Africa, “hatari ya kiasi kikubwa inakaribishwa iwapo unafungua mlango wako, au unajaribu kutoka nje karibu na simba, kwa sababu wanatambua kuwapo kwa binadamu, na kwa kutokea kwa ghafula unaongeza mshtuko wao wa hofu ambao kwa urahisi unaweza kuanzisha shambulizi kwa shauri la kujikinga. . . . Kuna kadiri ndogo zaidi ya hatari unapokutana kihalisi uso kwa uso na simba katika kichaka kuliko kutokea kwa ghafula nje ya gari lako mbele yake!”

Namna Gani Juu ya Chui?

Chui wanaogeuka kuwa wala-watu huwa na hali zilizo tofauti ya kanuni hiyo pia. Jonathan Scott anaeleza katika kitabu chake The Leopard’s Tale: “Bila kuchokozwa na akiwa katika afya njema, chui ni kiumbe mwenye haya, na mpole anayeonyesha hofu ya mwanadamu kwa kadiri kubwa. Akikaribiwa kwa kawaida anatoroka kuelekea maficho yaliyo karibu zaidi.”

Scott alitumia miezi katika Hifadhi ya Wanyama ya Masai Mara katika Kenya akichunguza mienendo ya chui fulani wa kike. Chui huyo alizoea polepole kuwapo kwa gari la Scott, na katika pindi moja watoto wa mnyama huyo, walioitwa Dark (Cheusi) na Light (Cheupe), walikaribia lile gari na kulikagua. Scott anaamini kwamba nyuma ya ule ukatili uonekanao kwa nje-nje pana uwezekano wa tabia ya urafiki mchangamfu.

Wengine wameona upande mchangamfu wa tabia ya chui. Kwa mfano, Joy Adamson alilea mtoto yatima wa chui ambaye alimwita Penny. Baada ya kuachiliwa porini, Penny na chui mwingine walizaa kikundi cha watoto. Wakati marafiki zake wa kibinadamu walipokuwa karibu, Penny alijitokeza na kuwaomba waje waone watoto wake. Kwenye pango, Adamson akiwa ameketi kando ya huyo mama chui mwenye kujionea fahari, alieleza juu ya mandhari hiyo yenye kupendeza: “Yeye aliramba mikono yetu huku watoto wake wakikunjamana kati ya miguu yake ya mbele, wote wakiwa wenye furaha sana. Itikadi ya kawaida ni kwamba chui ndio wanyama hatari zaidi kati ya wanyama wote wa Afrika, na chui wa kike walio na watoto hasa wakiwa wakali sana.” Lakini Adamson alisema kwamba ono lake na Penny laweza kuthibitisha kwamba “nyingi za itikadi zilizokubaliwa si za kweli.”

Chui mwingine wa kike aliye wa “hali njema” anayeitwa Harriet, alimtolea Arjan Singh wa India kaskazini ono lenye kutokeza hata zaidi. Singh alimkuza Harriet kutoka uchanga na kumzoeza hivi kwamba angeweza kujitafutia riziki katika msitu uliokuwa kando ya shamba lake. Kama sehemu ya mazoezi, Singh wakati mwingine angemhimiza chui huyo aweze kumshambulia. “Nilipochutama na kumshawishi anifukuze,” anaeleza katika kitabu chake Prince of Cats, “angenijia moja kwa moja . . . , lakini aliponirukia, alihakikisha kabisa alienda juu, akitua juu ya kichwa changu na kuteleza mgongoni mwangu, bila kuacha mkwaruzo hata mmoja kwenye mabega yangu yaliyo wazi.”

Njia ya kucheza ya chui huyo pamoja na Eelie mbwa wa Singh ilikuwa ya kutokeza pia. Singh anataja kwamba “filamu [moja] huonyesha [chui huyo] ameketi kitako na kutupa ngumu hali mbwa anamshambulia—lakini hajaribu kumgonga mshambulizi huyo kumwangusha. Mafumba yake makubwa yapita upande mmoja wa shingo ya Eelie, juu ya kichwa chake na kuteremka chini upande ule mwingine yakiwa mororo sana.”

Uhusiano huu wa kirafiki kati ya binadamu, mbwa, na chui uliendelea baada ya Harriet kutoka nyumbani kufuatia maisha katika pori iliyokuwa karibu. “Ikiwa mtu fulani asema kwamba chui si wa kuaminiwa,” anamalizia Singh, “nahitaji tu kufikiria safari nyingi ambazo Harriet alikuja kwenye [shamba langu] katikati ya usiku na kuniamsha kwa wororo ili kubadilisha salamu nilipokuwa nikilala nje.”

Hatimaye, Harriet na chui mwingine waliambatana wakiwa wenzi wakazaa watoto wawili. Pango lake lilipohatirishwa na furiko, chui huyo alibeba watoto wake kwa mdomo akawaleta mmoja baada ya mwingine katika himaya ya nyumba ya Singh. Furiko lilipopungua, Harriet alipanda ndani ya mashua ndogo ya Singh, akimhimiza amvushe tena na tena kwenye mto alipokuwa akichukua watoto wake mmoja baada ya mwingine kwenye pango jipya la msituni.

Tembo wa Kiafrika

Imesemwa kwamba tembo wa Kiafrika ni mkatili mno asiweze kufugwa. Watu wengi, hata hivyo, wamethibitisha ukweli kuwa mwingine. Mfano mmoja ni uhusiano wa kupendeza kati ya tembo watatu wa Kiafrika na Mwamerika aitwaye Randall Moore. Tembo hao walikuwa sehemu ya kikundi cha vitoto vilivyokamatwa katika Mbuga ya Kitaifa ya Kruger ya Wanyama Afrika Kusini na kusafirishwa kwa meli hadi United States. Baada ya muda walizoezwa kwa kitendo cha sarakasi na wakafanya vema. Mwenyeji wao alipokufa, Moore alipewa tembo watatu hao akawarudisha Afrika.

Tembo wale wawili wa kike, walioitwa Owalla na Durga, walianzishwa kukaa kwenye Hifadhi ya Pilanesberg ya Bophuthatswana katika 1982. Katika wakati huo, mbuga hiyo ilikuwa na hesabu ya tembo wachanga yatima waliokuwa katika hali mbaya na walihitaji kuelekezwa na tembo wazima wa kike. Je, tembo Owalla na Durga waliozoezwa katika sarakasi wangeweza kuchukua daraka hilo?

Baada ya mwaka mmoja, Moore alipokea ripoti kwamba tembo zake walikuwa wamewachukua wale mayatima 14 wawe wana wao wa kimalezi na kwamba vitoto zaidi yatima vingewekwa kwenye hifadhi hiyo. Baada ya kutokuwapo kwa miaka minne, Moore alirudi ili ajionee mwenyewe. Akitarajia kuwatafuta sana katika Milima ya Pilanesberg, alishangaa, baada ya kuwasili, kumwona Owalla na Durga wakiwa kati ya kikundi kikubwa. “Nia yangu ya kwanza, isiyo na ufundi,” akaandika katika Back to Africa, “ilikuwa kuwakimbilia, kuwakumbatia na kuwasifu sana, sana. Nilibadili hamu hiyo kwa mfikio wa fikira timamu zaidi.”

Kwanza, ilikuwa lazima Owalla na Durga wawe na uhakika kwamba mwenye kuwa hapo ni rafiki yao wa zamani. Kwa mikonga yao walikagua mkono wake ulionyoshwa. “Owalla,” aandika Moore, “alisimama akinizidi kimo kama kwamba anangojea amri inayofuata. Kikundi kile kingine kilisimama zizima kikituzunguka. Nami nikafanya walivyotaka. ‘Owalla . . . Inua mkonga JUU na MGUU!’ Mara hiyo Owalla akainua mguu wake wa mbele juu na kukunja mkonga wake kuelekea angani kwa njia ya kupiga saluti [salamu] maridadi ya zile siku za zamani za miigizo ya sarakasi. Ni nani aliyekuwa wa kwanza kusema kwamba tembo hasahau kamwe?”

Miaka mitatu baadaye, katika Oktoba 1989, kumbukumbu la Owalla lilijaribiwa tena. Wakati huu Moore aliamua kujaribu jambo ambalo hakuwa amefanya tangu kuwaanzisha tembo wale katika mbuga hiyo miaka saba kabla ya hapo. Owalla alitii amri yake ya kujinyosha chini na akamruhusu apande mgongo wake. Watazamaji wa televisheni katika Afrika Kusini walisisimuka kumwona akienda juu yake kati ya tembo 30 wa porini. “Nilifanya hivyo,” Moore akaeleza katika hoji moja pamoja na Amkeni!, “si kama tendo la kujifanyia jina bali kwa sababu nilikuwa mdadisi kujua ufungamano na uelewano ambao wawezekana kufanywa pamoja na tembo.” Wale yatima wa Pilanesberg walisitawi chini ya utunzaji wa Owalla na Durga.

Ni kweli, nyakati za kuwapo kwa urafiki kati ya binadamu na mnyama wa mwitu leo hazitukii kwa kawaida; zinahitaji kusitawishwa kwa uangalifu. Ungekuwa upumbavu hatari kwa mtu wa wastani kujasiria kutembea porini na kujaribu kuwakaribia simba, chui, na tembo. Lakini ingawa urafiki huo kati ya wanyama wa mwitu na binadamu ni duni sana leo, namna gani wakati ujao? Je, hiyo itakuwa ndiyo kawaida?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Simba Waweza Kufugwa!

“NJOO unipige picha kadhaa pamoja na simba wangu,” akasema Jack Seale, mkurugenzi wa Mbuga ya Hartebeespoortdam ya Nyoka na Wanyama katika Afrika Kusini. Kwa wasiwasi, nilimfuata hadi kwenye kizimba cha simba, nikitumaini kuwa angeniruhusu nichukue picha hizo nikiwa nje ya ua wa ulinzi.

Kizimba hicho kilikuwa safi, kikiwa na kivuli kingi kutokana na miti iliyozunguka. Simba tisa wenye afya walimtambua mzoezi wao mara moja alipoingia katika kizimba hicho akiwa na msaidizi. Simba hao walinguruma kwa urafiki na kutembeatembea kwa kusisimuka.

“Njoo ndani,” Jack akasema. Nikajifanya sikusikia. “Njoo ndani,” akarudia kwa sauti kubwa zaidi. Wao walikuwa na vijiti tu ili kujikinga na simba hao! Moyo wangu ulipiga haraka huku nikipambana na woga, mwishowe nikapanda ndani. Upesi nikaanza kupiga picha wakati Jack alipokuwa akikumbatia baadhi ya watunzwa wake. Nilihisi pumziko lililoje sote tulipokuwa nje tukiwa salama! Lakini singalihitaji kuhofu.

“Sababu inayotufanya twende ndani tukiwa na vijiti,” Jack akaeleza baadaye, “ni kwamba simba ni wenye shauku na huumauma mtu kwa upendo. Sisi tunawanyoshea vijiti vyetu ili wavitafune badala ya mikono yetu.” Jack na kikundi chake cha simba walikuwa wamerudi wakati huo tu kutoka Mbuga ya Kitaifa ya Etosha katika Namibia. Kwa nini alikuwa amewapeleka mbali hivyo porini? Yeye alieleza:

“Walitumiwa katika filamu yenye kueleza jinsi wanasayansi wanafanya utafiti ili kudhibiti ongezeko la idadi ya simba katika pori ya Namibia. Lakini simba wangu wanapendelea maisha ambayo wamezoea hapa. Katika Namibia, upesi baada ya kuliona lori langu dogo, walilijia. Hakukuwa na ugumu wa kuwafanya warudi nyumbani.”—Imechangwa.

[Hisani]

Courtesy Hartebeespoortdam Snake and Animal Park

[Picha katika ukurasa wa 9]

Randall Moore, pamoja na watunzwa wake katika kichaka cha Afrika

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki