Vipingamizi vya Amani Kati ya Binadamu na Mnyama
Picha zilizo kama ile iliyo kwenye jalada la mbele la gazeti hili hupendeza watoto. Watu wazima pia mara nyingi huvutiwa na mandhari kama hiyo.
Kwa nini wanadamu huitikia hivyo? Je, amani ya kweli kati ya binadamu na mnyama hata yule mkali zaidi ni ndoto ya kitoto tu? Au itakuja kuwa jambo halisi?
Binadamu Ni Kipingamizi
Kipingamizi kikubwa cha amani kama hiyo ni binadamu mwenyewe. Mithali ya kale husema: “Mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.” (Mhubiri 8:9) Na historia ya binadamu ya kumletea hasara mwenzake inaonyeshwa na anavyotendea wanyama.
Kwa mfano, wanyama wengi wa mwitu walikamatwa na kuwekwa kwenye nyanja za michezo za Roma ya kale ili wapigane. Katika 106 W.K. mmaliki Trajan wa Roma anaripotiwa kwamba alitayarisha michezo ambayo katika hiyo wapiganaji 10,000 wa nyanja za maonyesho, na wanyama 11,000 walikufa ili kutosheleza tamaa ya damu ya watazamaji wakatili.
Ni kweli kwamba aina hiyo ya kitumbuizo si mtindo wa leo. Lakini orodha inayoongezeka ya aina ya wanyama wasiopatikana tena na walio katika hatari ya kumalizika inashuhudia kwamba kitu fulani hakiko sawa kuhusiana na jinsi binadamu anavyotendea viumbe wa mwitu. Huku idadi ya watu ikizidi kukua, makao ya wanyama wa mwitu yanazidi kupungua. Na kwa sababu ya pupa ya kibinadamu, kuna uhitaji mwingi wa ngozi za wanyama, pembe, na pembe za ndovu zinazotoka nchi za nje. Wataalamu fulani wanahofu kwamba namna pekee za wanyama walio wakubwa mwishowe zitafungiwa tu kwenye hifadhi za wanyama.
Wala-Watu
Kipingamizi kingine cha amani huenda kikawa ni wanyama wenyewe. Katika Afrika na Esia, si jambo lisilo la kawaida kusoma ripoti za wanyama ambao wameshambulia na kuua binadamu. The Guinness Book of Animal Facts and Feats chasema kwamba washiriki wa jamii ya paka “labda ndio visababishi vya vifo karibu 1,000 kila mwaka.” Katika India pekee, simba-milia huua watu zaidi ya 50 kila mwaka. Baadhi ya chui pia katika nchi hiyo wamekuwa wala-watu.
Katika kitabu chake Dangerous to Man, Roger Caras anaeleza kwamba chui wakati mwingine hugeuka kuwa mla watu baada ya kula maiti za wanadamu wakati wa mitokeo ya magonjwa ya kuambukiza. Magonjwa ya kuambukiza kama hayo, yeye aeleza, mara nyingi ‘yamefuatwa na miezi ya kuogofya wakati chui walipopendelea ladha mpya ya nyama ya kibinadamu na kuanza kuua.’
Lakini Caras aonelea kwamba magonjwa ya kuambukizwa siyo tu kisababishi cha mashambulizi yote ya chui. Kisababishi kingine ni msisimuko wa mnyama huyo, hasa anapokuwa karibu na watoto.
Wakati wa miaka ya 1918-26, chui mmoja katika India aliua wanadamu 125, kama inavyoripotiwa na Kanali J. Corbett katika kitabu chake The Man-Eating Leopard of Rudraprayag. Miongo ya miaka baadaye, chui wala-watu waliua angalau watu 82 katika wilaya ya Bhagalpur.
Mtunzaji mmoja wa wanyama wa mwitu katika Tanganyika (sasa sehemu ya Tanzania) alieleza jinsi alivyotumia miezi mitano katika 1950 akijaribu bila kufanikiwa kupiga risasi chui mmoja mla-watu ambaye alitisha watu katika kijiji cha Ruponda. Hatimaye, baada ya kuua watoto 18, chui huyo alinaswa na mwanakijiji Mwafrika mmoja. Chui mwingine aliua wanawake na watoto 26 katika kijiji cha Masaguru.
Halafu kuna simba wa Afrika. Anapogeukia kula wanadamu, mara nyingi wajeruhiwa wanakuwa ni wanaume wazima. “Katika miaka yangu 23 nikiwa katika Idara ya Wanyama wa Mwitu,” aandika C. Ionides katika kitabu chake Mambas and Man-Eaters, “Nilipiga risasi simba zaidi ya 40, wengi wao wakiwa wala-watu, na wale wengine ama wakielekea kuwa wala-watu au wavamia-mifugo.” Kulingana na Ionides, simba huwa tisho kwa binadamu wakati binadamu apunguzapo sana mawindo yao ya kawaida.
Amani ya Duniani Pote Yatabiriwa
Ingawa kuna vizuizi kama hivyo kwa amani kati ya wanadamu na wanyama wa mwitu, Biblia husema: “Kila aina ya wanyama, . . . vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu.”—Yakobo 3:7.
Biblia hutabiri katika Ezekieli 34:25: “Nami [Mungu] nitafanya agano la amani nao, nami nitawakomesha wanyama wakali kati yao; nao watakaa salama jangwani, na kulala misituni.”
Je, utabiri huo wa Biblia ni ndoto tu isiyo halisi? Kabla ya kukataa wazo la amani ya duniani pote kati ya mwanadamu na mnyama, fikiria maelekezo fulani yanayoonyesha ukweli wa yale Biblia husema. Mifano yenye kustaajabisha ya amani kati ya binadamu wenye kujali na wanyama wanaoelekea kuwa hatari imeonyeshwa.