Kivunjavunja—Mwenye Sikio Moja
Karne nyingi zilizopita, hekaya za Kigiriki zilifafanua Zimwi lenye kuogopesha, majitu yenye jicho moja yaliyoishi katika bara la mbali. Madubwana hawa walioumbuka walikuwa tu katika taswira nyingi za wanadamu.
Hata hivyo, majuzi wanasayansi wamevumbua bila kutazamia kundi la viumbe wenye sikio moja—hawajafichika. Hao ni vivunjavunja.
Kwa nini siri hiyo ya kivunjavunja sasa tu ndiyo imejulikana? Wanasayansi tangu zamani walifikiria kwamba kivunjavunja lazima awe kiziwi, kwani hatoi sauti yoyote ama kuitikia sauti kama wadudu wengine. Kufanya mambo yawe yenye kutatanisha zaidi, sikio la kivunjavunja haliko katika kichwa chayo, mahali ungetazamia liweko. Gazeti Natural History laeleza kwamba sikio “limeingia kwa ndani, karibu urefu wa milimeta moja,” kwenye sehemu ya chini ya mwili wa kivunjavunja.
Je, haitatizi sana kuwa na sikio moja tu katika mahali hapo pasipotazamiwa? Naam, sisi binadamu hutumia masikio yetu mawili kutambulisha mahali sauti inatoka. Yaonekana kivunjavunja aweza kuendelea bila uwezo huo. Usikiaji wacho umebuniwa ili kukionya hali zihatarishazo uhai zitokeapo. Kivunjavunja huwa na sona fulani iliyo ndani ya kuhisi hali.
Sikio la kivunjavunja hujibadili kulingana na udukiziwimbi katika sauti kiukani, hasa sauti azifanyazo popo anapowinda wadudu kama vile kivunjavunja. Natural History laripoti kwamba wanasayansi wamemwona kivunjavunja akichukua hatua ya haraka ya kutoroka popo amkabilipo, kwa sababu ya usikiaji mwepesi wa kiuka sauti wa kivunjavunja. Lakini kivunjavunja huepaje popo, ambaye aweza kuruka kwa kasi mara tatu au nne kupita windo layo?
Kivunjavunja anapopata kionyo cha hatari cha kiuka sauti—kwa kawaida popo anapokuwa mnamo meta 10—kufumba na kufumbua, kivunjavunja huruka kwa mwendo wa kasi mno. Yaonekana, hufanya hivyo kwa kutua na kwenda chini kimakusudi, mbinu ya kujikinga ifananayo na ile itumiwayo na marubani wa kivita wa kisasa. Kwa kweli, Natural History lilieleza kwamba kivunjavunja “hutoa funzo la hali ya juu katika mikakati ya mikabiliano ya angani.”
Kivunjavunja alijifunzaje ‘mkakati wa mkabiliano wa hali ya juu wa angani’? Ni nani aliyebuni kifaa chayo cha kusikia kiuka sauti? Kwa hakika, jibu la kiakili ni lile lililoandaliwa na mzee wa ukoo Ayubu: “Katika hawa wote ni yupi asiyejua, kwamba ni mkono wa BWANA uliofanya haya?”—Ayubu 12:9.