Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 5/8 kur. 22-24
  • Lile Pigano la Marathoni—Mtwezo wa Serikali Kubwa ya Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Lile Pigano la Marathoni—Mtwezo wa Serikali Kubwa ya Ulimwengu
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Serikali Kubwa ya Ulimwengu Yasaiwa
  • Masuala ya Mbinu za Pigano
  • Jenerali Miltiades—Mwanambinu ya Pigano
  • Umaana wa Pigano Hilo
  • Vita ya Plataea—“Dubu” Ashindwa
    Amkeni!—1999
  • Ushinde Wenye Kuhuzunisha wa Shasta
    Amkeni!—1999
  • Historia Mashuhuri ya Athens na Magumu Yake ya Wakati Ujao
    Amkeni!—2000
  • Umedi-Uajemi—Ile Serikali Kubwa ya Nne ya Ulimwengu Katika Historia ya Biblia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 5/8 kur. 22-24

Lile Pigano la Marathoni—Mtwezo wa Serikali Kubwa ya Ulimwengu

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI

MGENI wa kisasa anapotelemka vilima kuzunguka eneo la Uwanda wa Marathoni, kilometa 40 kaskazini-mashariki mwa Athene, Ugiriki, yeye huhisi mara hiyo akipatwa na amani na utulivu kamili wa mahali hapo. Ni vigumu mtu kuwazia kwamba mahali hapa palitumika kuwa jukwaa kwa ajili ya moja la mapigano yajulikanayo zaidi ya historia, pigano ambalo kwa mafanikio lilizuia maendeleo ya serikali kubwa ya ulimwengu ya Kimesopotamia kuwa Ulaya yenyewe. The World Book Encyclopedia huliita “moja la mapigano muhimu zaidi katika historia ya ustaarabu wa Magharibi.” Na mwanahistoria Will Durant hulifafanua kuwa “mojapo ushindi wa ajabu mno wa historia.”

Serikali Kubwa ya Ulimwengu Yasaiwa

Unabii wa Biblia wa kitabu cha Danieli hufafanua kwa njia dhahiri sana utawala, mpanuko, na mfuatano wa serikali kubwa za ulimwengu. Akizungumza kwa njia ya mfano lakini kwa kufaa kuhusu serikali kubwa ya ulimwengu ya Umedi-Uajemi, Danieli aliandika hivi: “Tazama, mnyama mwingine, wa pili, kama dubu. . . . Wakamwambia huyo hivi, Inuka, ule nyama tele.”—Danieli 7:5.

Hili lilithibitika kuwa kweli. Wakati wa kilele cha serikali ya Umedi-Uajemi, karibu nusu ya pili ya karne ya sita K.W.K., majeshi yayo yaliyoonekana kutoweza kushindwa chini ya uongozi wa Sairasi na Dario I yalikwenda haraka kuelekea magharibi kuvuka Lidia. Yote mawili Thrasi na Makedonia, yaliyo kaskazini mwa Ugiriki, yalitiishwa kwa nguvu. Hili lilimaanisha kwamba karibu nusu ya ulimwengu wenye kusema Kigiriki tayari ilikuwa imeangukia mikononi mwa Wamedi, kwa kuwa kwa kuteka Lidia, Wamedi walikuwa pia wamemiliki miji ya Kigiriki ya Pwani ya Kiionia ambayo ilikuwa imekuwa katika milki ya Kilidia.

Kuelekea kilio kwa ajili ya msaada kilichokuwa kikitoka kwa majiji ya Kigiriki ya Kiionia yaliyokuwa yameviziwa, ni majiji yajitawalayo ya Athene na Eretria tu yaliyoitikia. Hili halikuzuia majeshi ya kivita ya Umedi yaliyopangwa kuingia haraka na kuvunjavunja Waionia wenye kuasi hadi ujitiisho. Na zaidi, Dario aliamua kwamba angehitaji kuadhibu majiji yajitawalayo ya Kigiriki kwa sababu ya kusaidia waasi wa Ionia.

Wakati Athene, Sparta, na Eretria kwa dharau yalipokataa kutosheleza matakwa ya Umedi majeshi ya kivita yenye nguvu ya askari wapanda farasi wa Umedi na askari wapiga miguu walisafiri melini kwenda Ugiriki katika majira ya kiangazi cha 490 K.W.K. Kufikia Agosti Wamedi walikuwa tayari kupambana na Athene na eneo layo, Attica.

Masuala ya Mbinu za Pigano

Wamedi walishukia Marathoni halafu wakavuka uwanda wenye mabwawa wa pwani ya mashariki mwa Attica, ambayo ilikuwa kilometa 42 tu kutoka Athene. Matazamio yalikuwa machache sana kwa Waathene, ambao waliweza tu kukusanya askari wapiga miguu 9,000 tu, kuongezea wengine 1,000 kutoka Uwanda wa Juu, bila utegemezo wowote kutoka ama askari wapanda farasi ama wapiga upinde.a Ingawa waliomba Sparta msaada, vilio vyao havikutolewa uangalifu—Wasparta walikuwa na shughuli nyingi za sherehe za kidini zilizomheshimu Apollo. Hivyo, wakiwa na rasilimali chache za kivita, Waathene walilazimika kupigana na Wamedi wakiwa peke yao.

Majenerali kumi mbalimbali walitenda wakiwa halmashauri ili kuamua, kwa kura za wengi, mambo ya mbinu za pigano. Sasa walihitaji kuamua kati ya mambo mawili yaliyohitaji uamuzi wakati huo. Kwanza, je, waweke majeshi yao ya kivita katika Athene ili kulinda jiji, au wakutane na Wamedi uwanjani? Wakiweka akilini kwamba jiji la Athene halikuwa na kuta zenye nguvu na zenye kukinga ili kulitetea, kusanyiko hilo lilipiga kura kwa ujumla kupigana na Wamedi katika Marathoni.

Pili, je, washambulie licha ya mambo kuwa dhidi yao—la msingi likiwa idadi kubwa ya Wamedi—au yawapasa wasimame na kungojea, huku wakitarajia kwamba Wasparta wangekuja karibuni vya kutosha ili kuwasaidia wakinze kwa mafanikio mashambulio yenye kutisha ya Wamedi?

Jenerali Miltiades—Mwanambinu ya Pigano

Mtu mmoja wa maana sana aliyejitokeza kutenda kuwa kiongozi alikuwa jenerali Mgiriki Miltiades. Alikuwa kiongozi wa jeshi aliye mzoefu na mwenye ubuni, mzee-wa-kazi aliyekuwa amepigania upande wa jeshi la Wamedi wakati wa kampeni za mapema katika kaskazini. Kwa hivyo, alimjua adui vyema zaidi. Alikuwa na ujuzi mwema si tu wa mfanyizo wa jeshi la Wamedi bali pia silaha zao na, la maana zaidi, mbinu zao za pigano. Kwa kuongezea, wakati wa siku za kabla ya pigano hilo, yeye kwa hekima alichunguza kwa ukaribu zaidi mazingira ya uwanja wa pigano.

Miltiades alitambua pia kwamba tendo la mara moja lilihitajiwa, kwani miongoni mwa demokrasia mpya ya Kiathene iliyoanzishwa, kulikuwa na vikundi vilivyounga mkono Wamedi ambavyo vingefurahia kushindwa kwa Athene. Usiku wa kabla ya pigano, mwasi fulani Mmedi aliingia katika kambi ya Wagiriki na habari za kwamba askari wapanda farasi Wamedi walikuwa wamejiondoa kwa muda. Kulingana na nadharia moja askari wapanda farasi Wamedi walikuwa wamepanda meli zao kwa ajili ya shambulio liwezekanalo juu ya Athene kutoka pwani ya mashariki ya Attica ili kwamba wateke jiji mara tu baada ya ushindi wenye uhakika katika Marathoni. Kwa sababu iwayo yote, hili liliondoa hatari mbaya zaidi iliyokabili askari wapiga miguu Waathene.

Kulipokuwa kukipambazuka, kikosi kilichosongamana cha askari Wagiriki kilishambulia. (Ona sanduku, ukurasa 24.) Wamedi waliopigwa na butaa walirudi nyuma lakini mara wakashambulia kwa kuitikia na kupenya hadi katikati mwa mahali pa kinga ya pigano ya Wagiriki. Kwa njia hiyo, Wamedi bila kujua waliangukia mtego uliowekwa vizuri wa Miltiades! Alikuwa ameacha kimakusudi katikati mwa Wagiriki kukiwa dhaifu ili kuimarisha sehemu za kando zikiwa na mistari iliyoongezwa ya wanaume. Mara, majeshi waliokuwa sehemu za kando kwa ghafula wakazingira, na kuwashambulia Wamedi kwa jeuri na kuwaua kwa idadi kubwa mno hadi wachache waliofaulu kuokoka mashambulizi hayo wakatorokea kwenye meli zao. Tokeo lilikuwa machinjo makubwa mno. Wajeruhiwa Wamedi walifikia yapata wanaume 6,400, ilhali Waathene walipoteza 192 tu wa wanaume wao.

Kulingana na hekaya, habari za ushindi wa Wagiriki zilipelekwa haraka Athene na mjumbe. Pokeo fulani lisilo la kweli husema jina lake lilikuwa Pheidippides, lakini kwa kweli, Pheidippides alikimbia kutoka Athene hadi Sparta kabla ya vita ili kutafuta msaada. Hekaya yasema, Mgiriki mwingine mchanga alikimbia kilometa 42 kutoka Marathoni hadi Athene na alipofika akapaaza sauti, “Shangilieni, tumeshinda!” halafu akaanguka na kufa. Hii yasemekana ndiyo marathoni ya kwanza—hivyo chanzo cha neno hilo—ambalo liliweka mwanzo wa mbio ndefu za miguu za kisasa kama tuzijuavyo.

Ingawaje baadhi ya meli za Wamedi zilichomwa, nyingi mno za meli 600 zilifaulu kusafiri kuzunguka Rasi ya Colonna, iliyo kwenye ncha ya kusini mwa Attica, na kufika Athene. Hata hivyo, jeshi lenye ushindi la Kiathene lilifika huko kwanza na kukutana nao tena. Wamedi walilazimika kuondoka. Waathene walikuwa wamepata ushindi dhidi ya miwezekano yote!

Athene ilifurikwa na shangwe, hasa kwa sababu ya ushindi uliokuwa umepatikana bila msaada wowote kutoka kwa Wasparta.

Umaana wa Pigano Hilo

Kumbukumbu za marumaru na shaba katika Marathoni na Delphi zilifanyia ukumbusho wa daima ushindi wa Kiathene. Kulingana na mwanahistoria Pausanias, miaka 650 baadaye wasafiri bado waliamini kwamba wangeweza kusikia kelele za wanaume waliokuwa wakipigana walipokuwa wakivuka uwanja huo wa pigano.

Kwa nini pigano la Marathoni lilikuwa la maana kutokana na maoni ya Biblia? Lilikuwa ishara, muda mrefu mbele, ya ukuu wa hatimaye wa “beberu” wa Kigiriki wa unabii wa Danieli juu ya ‘kondoo mume mwenye pembe mbili’ wa Umedi-Uajemi.b—Danieli 8:5-8.

Mtu anapotazama Kaburi la Marathoni, ambalo bado lasimama kwenye eneo la pigano, anakumbushwa juu ya idadi ya juu ya kifo na miteseko ambayo wanadamu wamelipia katika tamaa isiyokwisha kwa ajili utafutaji wa uwezo na utawala. Kurasa zenye damu za historia, nyanja za mapigano zilizo kimya, na makaburi mapweke yamejaa “wanaume wakubwa,” “mashujaa,” na “wenye kushindwa,” wote wakiwa majeruhi wa siasa za ulimwengu na mg’ang’ano ili kupata uwezo. Hata hivyo, wakati uko karibu sana ambapo ming’ang’ano yote ya uwezo wa kisiasa itakwisha, kwa kuwa Mungu ametabiri: “Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.” Danieli 2:44.

[Maelezo ya Chini]

a Tarakimu za pigano la Marathoni yaonekana zina ubishanio. Will Durant adai kwamba Wagiriki “walikuwa na wanaume elfu ishirini, Wamedi yaelekea walikuwa na elfu mia moja.”

b Kwa habari zaidi juu ya kutimizwa kwa unabii wa Danieli, ona “Your Will Be Done on Earth,” kurasa 190-201, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Hopliti na Kikosi Kilichosongamana—Njia ya Kushinda

Kikitoa maelezo juu ya visababishi viwili vikuu katika ushindi wa Waathene, kitabu A Soaring Spirit chasema: “Hopliti, kama wanaume wa kijeshi wapiga miguu Wagiriki walivyoitwa, walikuwa na dirii yenye nguvu zaidi ya wenzao Wamedi, ngao ngumu zaidi na mikuki mirefu zaidi. Lakini la maana zaidi, walipigana kwa wepesi wa kimashine katika vikosi vilivyosongamana kwa kuendelea hadi safu 12 ndani, wanajeshi katika kila safu wakisongamana pamoja karibu zaidi hivi kwamba ngao zao zilitokeza ukuta wenye kuendelea. Wakikabili tazamio kama hilo, Wamedi walijua kwa nini kikosi kilichosongamana kilikuwa chombo cha pigano kilichohofiwa kuliko vyote vilivyojulikana kwa ulimwengu wa kale.”

[Credite Line]

The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck

[Picha katika ukurasa wa 23]

Uwanda wa Marathoni. Picha ndogo: Kaburi la Ukumbusho kwa Waathene 192 waliokufa katika pigano hilo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki