Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 4/8 kur. 25-27
  • Ushinde Wenye Kuhuzunisha wa Shasta

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ushinde Wenye Kuhuzunisha wa Shasta
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Shasta—Mshindi Mwenye Kuazimia
  • Thermopylae—Ukanda wa Nchi Ulio Ghali
  • Ephialtes, Ogofyo
  • Salamisi—“Kuta za Mbao” Zafanya Kazi
  • Ushinde Wenye Kuhuzunisha
  • Vita ya Plataea—“Dubu” Ashindwa
    Amkeni!—1999
  • Lile Pigano la Marathoni—Mtwezo wa Serikali Kubwa ya Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • Je, Wajua?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Umedi-Uajemi—Ile Serikali Kubwa ya Nne ya Ulimwengu Katika Historia ya Biblia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
Amkeni!—1999
g99 4/8 kur. 25-27

Ushinde Wenye Kuhuzunisha wa Shasta

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI

MSAFIRI asiyetambua historia ya mahali hapo huvutiwa sana na chemchemi za maji moto zinazorusha gesi za salfa. Huenda akashangaa kujua kwamba uwanda wa pwani—katika eneo hili linaloitwa Thermopylae, linalomaanisha “Gesi Zenye Joto”—wakati mmoja ulikuwa ukanda wa nchi ambao karibu haungevukika. Lakini huenda akavutiwa hata zaidi anapotambua kwamba anaweza kupata uthibitisho wa kutosha kuhusu usahihi usio na kifani wa unabii wa Biblia hapa, na vilevile kuelekea upande wa kusini kwenye kisiwa cha Salamisi.

Kwa kweli, kwa kuchunguza mambo yaliyopita na kwa kufikiria utimizo wake, mambo mengi kuhusu unabii fulani katika kitabu cha Biblia cha Danieli ambao husimulia juu ya maeneo haya unashangaza kikweli. Hutoa ithibati yenye kusadikisha kwamba Biblia ni Neno la Mungu. Katika Danieli sura ya 11, tunapata mfano wa kuvutia. Danieli alipewa habari za unabii “katika mwaka wa kwanza wa Dario, Mmedi,” yapata mwaka wa 538 K.W.K. (Danieli 11:1) Lakini utimizo wa yale yaliyofunuliwa wakati huo ulidumu kwa kipindi cha karne nyingi.

Danieli 11:2 kilitoa unabii huu kuhusu mfalme fulani Mwajemi: “Tazama, watasimama wafalme watatu katika Uajemi; naye mfalme wa nne atakuwa tajiri kuliko hao wote; naye atakapopata nguvu kwa utajiri wake, atawachochea wote juu ya ufalme wa Uyunani [“Ugiriki,” NW].”

Aliyemfuata Koreshi wa Pili, Cambyses wa Pili, na Dario wa Kwanza, ‘mfalme wa nne’ kwa kweli alikuwa Shasta wa Kwanza, ambaye yaelekea alikuwa Ahasuero anayetajwa katika kitabu cha Biblia cha Esta. Je, kweli ‘alichochea wote juu ya ufalme wa Uyunani,’ na tokeo lilikuwa nini?

Shasta—Mshindi Mwenye Kuazimia

Shasta alihitaji kukabiliana na matokeo ya kushindwa kwa vikosi vya kijeshi vya baba yake, Dario, huko Marathoni.a Hivyo, Shasta alitumia miaka ya kwanza katika utawala wake kukandamiza maasi katika milki yake na pia “kupata nguvu kwa utajiri wake.”

Hata hivyo, Shasta aliendelea kukumbuka ushindi wa Ugiriki, aliohimizwa autwae na watumishi wa nyumba ya mfalme wenye kutaka makuu. Hivyo, kuanzia mwaka wa 484 K.W.K., alitumia muda wa miaka mitatu kukusanya, kutoka wilaya na mikoa iliyokuwa chini ya utawala wa Waajemi, jeshi lililoripotiwa kuwa mojawapo ya jeshi kuu kupita yote lililopata kuonekana duniani. Kulingana na mwanahistoria Mgiriki Herodoto, jeshi lililounganishwa la Shasta la nchi kavu na la wanamaji lilijumlika kuwa idadi yenye kushangaza ya wapiganaji 2,641,610. b

Wakati huohuo, Wagiriki walianza kujitayarisha kwa njia yao wenyewe. Wajapokuwa mabaharia, walikuwa na jeshi dhaifu la wanamaji. Lakini sasa, kwa kuitikia tisho la shambulizi la Waajemi na jibu la mizimuni kutoka Delphi lililowaagiza wajitetee kwa “kuta za mbao,” Athene lilianza kukusanya jeshi la wapiganaji la wanamaji.

Machimbo ya serikali ya Laurium yalikuwa eneo ambapo fedha nyingi iligunduliwa, na mwanasiasa mashuhuri wa Athene Themistocles, alilisihi Bunge litumie faida iliyopatikana kutoka kwa fedha hizo kujenga kundi la manchani 200. Baada ya kushindwa kuamua mara ya kwanza, Sparta aliongoza kuanzishwa kwa Ushirika wa Kiyunani, uliofanyizwa na majimbo huru ya Ugiriki yenye majiji yapatayo 30.

Wakati uleule, Shasta alikuwa akielekeza jeshi lake lenye uchokozi na uharibifu hadi Ulaya—jambo ambalo halikuwa kazi rahisi. Chakula kiliandaliwa na majiji yaliyokuwa kandokando ya barabara, kwa gharama ya talanta 400 za dhahabu kwa siku kwa mlo mmoja tu wa kulisha jeshi lote. Miezi iliyotangulia, maofisa walikuwa wametumwa kimbele kutayarisha nafaka, ng’ombe, na kuku kwa ajili ya chakula cha mfalme. Ni Shasta peke yake aliyelala ndani ya hema, wanajeshi waliosalia walilala nje.

Kwanza jeshi hilo kubwa lilihitaji kuvuka Hellespont (sasa inaitwa Dardanelles), mlangobahari mwembamba unaotenganisha Asia na Ulaya. Baada ya madaraja mawili ya mashua kuporomoka wakati wa dhoruba, Shasta—akiwa na hasira kali zenye kichaa—aliamuru maji ya Hellespont yachapwe mijeledi 300, yatiwe alama na kufungwa pingu. Pia aliamuru wahandisi wakatwe vichwa. Madaraja mengine mawili yalipojengwa juu ya Hellespont, jeshi hilo lilichukua muda wa majuma mawili kuvuka.

Thermopylae—Ukanda wa Nchi Ulio Ghali

Karibu katikati ya mwaka wa 480 K.W.K., jeshi la kifalme la Uajemi, likiandamana na kundi la meli lilisafiri kuelekea upande wa chini wa pwani ya Thessaly. Hatimaye majeshi ya muungano ya Ugiriki yaliamua kujitetea huko Thermopylae, ukanda wa nchi ulio mwembamba ambapo wakati huo milima ya bara ilikuwa kwenye mteremko wa meta 15 kutoka ufuoni.c

Waajemi wangehitaji kupitia katika ukanda huu mwembamba hivi kwamba kikosi cha askari-jeshi madhubuti kingewasimamisha. Jeshi la askari Wagiriki 7,000 lililotangulia chini ya Mfalme Leonidas wa Sparta walishika doria kwenye milangobahari karibu na Thermopylae. Wakati huohuo, jeshi la wanamaji la Ugiriki, likiwa na meli za kivita 270, lilijificha mbali na ufuo huko Artemisium, likitumia udanganyi na ustadi kushinda kundi la meli la Uajemi.

Shasta alifika Thermopylae mapema mwezi wa Agosti, akiwa na uhakika kwamba jeshi lake kubwa lingewashinda kabisa Wagiriki. Wagiriki walipokataa kujisalimisha, alituma Waamedi na Wasisiani kuwaondoa; lakini majeshi haya yalishindwa vibaya sana, na Wanamgambo (kikosi cha wanajeshi wa majaribio), ambao Shasta alikuwa amewatuma chini ya gavana wa jimbo la Hydarnes, hawakufanikiwa.

Ephialtes, Ogofyo

Wakati tu ilipoonekana kwamba Waajemi walikuwa wamezuiwa, Ephialtes (Neno la Kigiriki linalomaanisha “ogofyo”), mkulima wa Thesalinia mwenye kutamani sana faida, alijitolea kuwaongoza juu ya milima, hadi upande wa nyuma wa jeshi la Wagiriki. Asubuhi iliyofuata Waajemi walikuwa wakizingira ili kuwashambulia Wagiriki kutoka upande wa nyuma. Wasparta, wakitambua kwamba wanaelekea kuangamizwa, walijitetea wenyewe kwa kiruu; huku wengi wa washambuliaji wao, wakiwa wamesukumwa hadi kwenye mstari wa mbele wa jeshi la adui na maamiri wao wenyewe, walikanyagwa hadi wakafa au wakatupwa baharini. Hatimaye, mfalme Leonidas na wote waliokuwa pamoja naye, wanaume wapatao 1,000, waliuawa. Hydarnes alifikia kikosi cha askari-jeshi wa Sparta waliokuwa mbali zaidi.

Jeshi la Waajemi pamoja na mabaki ya kikundi cha meli za Waajemi walianza kuwinda nyumba ya Waathene. Shasta alisafiri kuelekea Attica, akiteka nyara na kuchoma kadiri alivyosonga. Waathene walihamishwa kwenye kisiwa cha karibu cha Salamisi. Kikundi cha meli za Ugiriki kilitia nanga kati ya Athene na Salamisi. Ilichukua muda wa majuma mawili kuangusha akropoli ya Athene. Watetezi wote waliuawa, na patakatifu pote pakavunjwa-vunjwa kabisa, pakachomwa na kuporwa.

Salamisi—“Kuta za Mbao” Zafanya Kazi

Tayari meli za kivita za Wagiriki zilikuwa zimekutana na kundi la meli za Waajemi katika mapambano kadhaa makali lakini yasiyo ya kukata maneno karibu na Thermopylae. Kisha, huku jeshi la nchi kavu likirudi nyuma, kundi la meli za Ugiriki lilikuwa limejiondoa kuelekea kusini. Sasa lilijipanga kwenye ghuba ya Salamisi, mahali ambapo Themistocles alikuwa ameanza kufanya mpango wa pigano.

Alijua kwamba meli za kivita 300 za Wafoinike zilizokuwa tegemeo kuu la jeshi la wanamaji la Waajemi zilikuwa kubwa zaidi lakini zenye kuelekezwa kwa haraka kuliko manchani madhubuti zaidi za Wagiriki. Kundi la meli za Waajemi lilikuwa na manowari zipatazo 1,200, kwa kulinganishwa na meli 380 za jeshi la Wagiriki. Na mabaharia wa Ugiriki hawakuwa na uzoefu kama wale mabaharia waliokuwa kwenye meli za kivita za Waajemi. Lakini mlangobahari kati ya Salamisi na pwani ya Attica ulikuwa mwembamba, kuwezesha tu meli 50 zisafiri sambamba. Ikiwa Wagiriki wangeweza kuwashawishi Waajemi waingie kwenye mtaro huu wa asili, Waajemi hawangenufaika na idadi kubwa ya meli za kivita na uwezo wa kuzielekeza kwa urahisi. Inadaiwa kwamba Themistocles aliharakisha ushindi huo kwa kupeleka ujumbe wa udanganyifu kwa Shasta akimwambia ashambulie kabla kikundi cha Wagiriki hakijapata fursa ya kutoroka.

Ikatukia hivyo. Kundi la meli za Waajemi, kila meli ikiwa imepangwa tayari kwa vita pamoja na safu za wapiga makasia na jeshi lenye kupigana la wabeba mikuki na wapiga mishale, walizingira ncha ya Attica na kuabiri kuelekea mlangobahari huo. Shasta, akiwa na uhakika wa kupata ushindi, alikuwa ameweka kiti chake cha ufalme juu ya mlima mahali ambapo angeweza kutazama pigano akiwa amestarehe.

Ushinde Wenye Kuhuzunisha

Kulikuwa na mvurugo mkubwa Waajemi walipokuwa wakisongamana kwenye mwingilio mwembamba. Kwa ghafula, mlio wa tarumbeta ulisikika kutoka juu ya kisiwa cha Salamisi, na meli za Ugiriki zikasonga mbele kwa safu zilizopangwa kwa utaratibu. Manchani zilivunja-vunja kabisa meli za Waajemi, huku zikiponda viunzi vyao na kuzisukuma zigongane. Mashujaa Wagiriki waliruka kwenye meli za adui zilizoharibiwa, huku wakiwa wamebeba panga.

Mchanga uliokuwa kwenye kingo za Attica ulijaa takataka za mbao zilizokuwa zimevunjwa-vunjwa na miili iliyokuwa imekatwa-katwa. Baada ya msiba huu mkuu, Shasta alikutanisha meli zake zilizokuwa zimebakia na kuondoka kwenda nyumbani. Kampeni yake ya mwaka huo ilikuwa imemalizika. Lakini chini ya uongozi wa shemejiye Mardonius aliacha huko jeshi la kadri hadi kumalizika kwa majira ya baridi kali.

Kwa wanafunzi wa Biblia wenye bidii, kushindwa kwa Salamisi kulikuwa ishara, iliyokuwa imetolewa muda mrefu kabla ya hapo, ya uwezo mkubwa wa baadaye wa “beberu” wa Ugiriki dhidi ya ‘kondoo mume mwenye pembe mbili’ wa Umedi na Uajemi kama ilivyosimuliwa katika unabii wa Danieli. (Danieli 8: 5-8) La maana zaidi, unabii wa Biblia unawahakikishia watumishi wa Mungu kwamba mng’ang’ano wa kibinadamu wenye ubatili wa kutaka kutawala hatimaye utakomeshwa na utawala wa Mfalme Yesu Kristo.—Isaya 9:6; Danieli 2:44.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa habari zaidi, ona “Lile Pigano la Marathoni—Mtwezo wa Serikali Kubwa ya Ulimwengu,” katika toleo la Amkeni! la Mei 8, 1995.

b Kama ilivyo na mapigano mengi ya kale, idadi ya askari-jeshi wa Uajemi inabishaniwa. Mwanahistoria Will Durant ananukuu kadirio la Herodoto, ilhali vitabu vingine vya marejezo hutaja idadi ya wanaume kati ya 250,000 na 400,000.

c Rundo la matope limebadili pwani hiyo, hivi kwamba leo ni uwanda mpana, wa kinamasi ulio na upana wa kati ya kilometa 2.4 hadi 4.8.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

Manchani—Meli Hatari

Kitu kilichofanya Waathene huko Aegea wawe na uwezo zaidi kuliko wengine katika jeshi la wanamaji katika karne ya tano K.W.K. kilikuwa manchani, chombo chembamba kilichosafiri kwa kutumia matanga hadi mwisho wa safari yake lakini kiliendeshwa kwa makasia wakati wa mapigano ya baharini. Kila manchani ilibeba kikundi kidogo cha askari. Lakini mradi wao haukuwa hasa kupanda meli za adui, badala yake ulikuwa kumaliza uwezo wao kwa kutumia ncha ya chuma ya manchani iliyoendeshwa hadi kwenye shabaha yake na wapiga makasia 170.

[Hisani]

Hellenic Maritime Museum/Photo: P. Stolis

[Ramani katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

JESHI LA MAPIGANO LA SHASTA

HELLESPONT

THESSALY

ARTEMISIUM

THERMOPYLAE

ATTICA

ATHENE

MARATHONI

LAURIUM

SALAMISI

SPARTA

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki