Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 6/8 kur. 4-6
  • Mamilioni Wawa Watumwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mamilioni Wawa Watumwa
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ile Njia ya Pembetatu
  • Mpito wa Kati
  • Kuwasili Katika Amerika
  • Kazi na Mjeledi
  • Kuuzwa Utumwani
    Amkeni!—1995
  • Tatizo la Kidini Wakati Brazili Ilipokuwa Koloni
    Amkeni!—2002
  • Kutembea Kwenye Njia ya Watumwa
    Amkeni!—2011
  • Pambano la Muda Mrefu Dhidi ya Utumwa
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 6/8 kur. 4-6

Mamilioni Wawa Watumwa

KUFIKIA wakati Olaudah Equiano alizaliwa, meli kutoka Ulaya zilikuwa zimebeba watumwa wa Kiafrika kuvuka Bahari Kuu ya Atlantiki kwa karne mbili na nusu. Lakini utumwa ulikuwa wa kale kuliko wakati huo. Kutumikisha binadamu, kwa kawaida kama tokeo la vita, kulikuwa kumezoewa kotekote ulimwenguni tangu nyakati za kale.

Katika Afrika pia, utumwa ulinawiri muda mrefu kabla ya meli kutoka Ulaya kuwasili. Yataarifu The New Encyclopædia Britannica: “Watumwa walihodhiwa katika Afrika yenye watu weusi kwa wakati wote wa historia iliyoandikwa. . . . Utumwa ulizoewa kila mahali hata kabla ya mwanzo wa Uislamu, na watumwa weusi waliopelekwa nje ya Afrika waliuzwa kotekote katika ulimwengu wa Kiislamu.”

Kile kilichofanya biashara ya watumwa ya kuvuka Atlantiki kuwa tofauti kilikuwa kiasi chayo na kipindi cha muda. Kulingana na makadirio bora zaidi, idadi ya watumwa iliyovuka Bahari Kuu ya Atlantiki kutoka karne ya 16 hadi 19 ilikuwa kati ya milioni 10 na milioni 12.

Ile Njia ya Pembetatu

Mara baada ya safari ya Christopher Columbus katika 1492, Wanaulaya wakoloni walianzisha kazi ya kuchimba madini na mashamba makubwa ya miwa katika Amerika. Kuongezea kuwatumikisha wenyeji, Wanaulaya walianza kuingiza watumwa kutoka Afrika.a Kusafirisha watumwa kuvuka Atlantiki kulianza kama manyunyu mnamo katikati ya miaka ya 1500, lakini kufikia siku ya Equiano, katikati ya miaka ya 1700, kulikuwa kumekuwa furiko—karibu mateka 60,000 kila mwaka.

Meli kutoka Ulaya kwa ujumla zilifuata njia ya pembetatu. Kwanza zilisafiri kusini kutoka Ulaya hadi Afrika. Kisha ziliabiri mpito wa kati (muunganisho wa kati kwenye pembetatu) kuelekea Amerika. Mwishowe ziliabiri kurudi Ulaya.

Kwenye kila ncha ya pembetatu, manahodha walifanya biashara. Meli ziling’oa nanga kutoka kwa bandari za Ulaya zikiwa zimesheheni bidhaa—vitambaa, chuma, bunduki, na alkoholi. Walipofika mwambao wa magharibi wa Afrika, manahodha walibadilisha bidhaa hizi kwa ugavi wa watumwa kutoka kwa mawakala Waafrika. Watumwa walijazana kwenye meli mbalimbali, ambazo kisha ziling’oa nanga kuelekea Amerika. Katika Amerika, manahodha waliuza watumwa na kisha kusheheneza bidhaa zilizotokezwa na kazi ya watumwa—miwa, mvinyo wa miwa, sukari-guru, tumbaku, mchele, na kuanzia miaka ya 1780 pamba. Kisha meli hizo ziliabiri kurudi Ulaya, mkondo wa mwisho wa safari.

Kwa wafanyabiashara wa Ulaya na wa Afrika, pamoja na wakoloni katika Amerika, biashara katika kile walichokiita bidhaa iliyo hai ilimaanisha faida, njia ya kufanyiza fedha. Kwa wale walioshikwa utumwani—waume na wake, akina baba na mama, wana na mabinti—biashara hiyo ilimaanisha unyama na ogofyo.

Watumwa walitoka wapi? Baadhi yao walitoroshwa, kama vile Olaudah Equiano, lakini walio wengi walishikwa mateka katika vita vilivyopiganwa kati ya makabila ya Kiafrika. Wagavi walikuwa Waafrika. Mwanahistoria Philip Curtin, mtaalamu katika biashara ya watumwa, aandika hivi: “Wanaulaya mara walijua kwamba Afrika ilikuwa hatari mno kwa afya yao kufanya uvamizi wa moja kwa moja iwezekanavyo. Kushika watumwa kukaja kuwa kazi iliyofanywa na Waafrika peke yao . . . Ugavi ulioongezwa upya kwenye chanzo cha biashara ya utumwa sanasana ulikuwa mateka wa vita.”

Mpito wa Kati

Safari ya kuelekea Amerika ilikuwa ono lenye kuogofya. Wakitembezwa kwenye mwambao wakiwa wamewekwa mikatale kwa makundi, Waafrika walidhoofika, nyakati nyingine kwa miezi kadhaa, katika mangome ya mawe ama kwenye vijiji vidogo vya mbao. Kufikia wakati meli za watumwa zilipong’oa nanga kuelekea Amerika, mateka mara nyingi walikuwa tayari katika afya mbaya kutokana na kutendewa vibaya kulikowafika. Lakini hali yao ingekuwa mbaya zaidi.

Baada ya kuburutwa ndani ya meli, kuvuliwa mavazi, na kuchunguzwa na daktari ama nahodha wa meli, wanaume walifungwa miguu na kupelekwa chini ya sitaha. Mabwana wa meli waliwajaza watumwa wengi wawezavyo ndani ya shehena ili kuongeza faida yao. Wanawake na watoto walipewa uhuru zaidi wa kutembea, ingawa hili pia liliwafanya watendewe vibaya kingono na wanameli.

Hali ya hewa shehenani ilikuwa chafu, yenye uvundo. Equiano aeleza alivyoona hivi: “Ile hali ya ufungano ya mahali penyewe na lile joto la tabia-anga, kuongezea idadi kubwa ya watu melini, ambayo ilisongamana hivi kwamba kila mmoja hakuwa na nafasi ya kujigeuza, karibu itusonge pumzi. Hili lilitokeza kutokwa na jasho jingi, hivi kwamba hewa ilikuwa isiyofaa kwa ajili ya upumuaji kutokana na unamna wa harufu zenye kukirihisha, nayo ilisababisha ugonjwa miongoni mwa watumwa, ambapo wengi wao walikufa . . . Nyende za wanawake na miguno ya wafao vilifanya mandhari yote ya ogofyo kuwa isiyowazika.” Mateka waliwabidika kuvumilia hali kama hizo mwendo wote wa kuvuka bahari, ambao ulichukua karibu miezi miwili, nyakati nyingine muda mrefu zaidi.

Katika hali zenye kudhoofisha zisizo za kisiha, maradhi yalinawiri. Magonjwa ya kusambazwa ya kuhara damu na tetewanga yalikuwa ya kawaida. Kiwango cha kifo kilikuwa juu. Rekodi hudokeza kwamba hadi miaka ya 1750, 1 katika Waafrika 5 waliokuwa ndani ya meli alikufa. Wale waliokufa walitupwa baharini.

Kuwasili Katika Amerika

Meli za watumwa zilipokaribia Amerika, wanameli waliwatayarisha Waafrika kwa ajili ya uuzaji. Waliwafungua watumwa kutoka kwa minyororo yao, waliwalisha ili wanenepe, na kuwapaka mafuta ili kuwafanya waonekane wenye afya na kuyabadili majeraha na vidonda.

Kwa kawaida manahodha waliwauza watumwa kwa mnada, lakini nyakati nyingine walipanga “kamari” fulani ambayo iliwataka wanunuzi walipe bei fulani isiyo ya kujadiliana kabla ya kuwanunua. Equiano aandika hivi: “Mara ishara ilipotolewa, (kama vile kupigwa kwa ngoma) wanunuzi walikimbia wote kwa wakati mmoja kwenye kizimba walichozuiliwa watumwa, na kufanya uchaguzi wa tita walilolipenda mno. Makelele na mayowe ambayo yaliandamana na utendaji huo na ule uchu ulioonekana katika nyuso za wanunuzi ulichangia sana kuongezea hofu ya Waafrika walioshtuka.”

Equiano aongezea hivi: “Kwa namna hii, bila ubinadamu, ndivyo watu wa ukoo na marafiki waliachana, wengi wao bila kuonana tena kamwe.” Kwa familia ambazo kwa njia fulani ziliweza kukaa pamoja kupitia ogofyo hilo la maishani la miezi iliyokuwa imepita, hili hasa lilikuwa pigo lenye huzuni sana.

Kazi na Mjeledi

Watumwa wa Kiafrika walifanya kazi kwenye mashamba makubwa ili kutokeza kahawa, mpunga, tumbaku, pamba, na hasa miwa. Wengine walisulubu kwenye utendaji wa kuchimba madini. Wengine walifanya kazi wakiwa maseremala, wafua vyuma, watengeneza saa, wafuabunduki, na mabaharia. Bado wengine walikuwa wafanyakazi wa nyumbani—watumishi, wakunga, mafundi wa nguo, na wapishi. Watumwa walifyeka mashamba, walitengeneza barabara na majengo, na kuchimba mitaro ya kupitishia maji.

Hata hivyo, licha ya kazi waliyoifanya, watumwa walionekana kuwa mali, na kulingana na sheria bwana alikuwa na haki kamili juu ya mali yake. Hata hivyo, utumwa haukuendelea kwa sababu tu ya ukataaji wa haki na uhuru. Uliendelea kwa mjeledi. Mamlaka ya wenye watumwa na wasimamizi wao yalitegemea uwezo wa kusababisha maumivu. Na walisababisha maumivu mengi.

Ili kutohimiza uasi na kuwasimamia watumwa wao, wenye watumwa walitumia adhabu za kimwili zenye kushusha hata kwa makosa madogo. Equiano aandika hivi: “Lilikuwa jambo la kawaida [katika West Indies] kwa watumwa kuwekwa alama ya herufi za kwanza za jina la bwana wao kwa kuchoma, na furushi zito la vyambo vya chuma vikining’inia shingoni mwao. Katika pindi za kawaida waliwekewa mizigo mizito ya minyororo, na mara kwa mara vifaa vya kutesa viliongezewa. Kifunika mdomo cha chuma, msumari wa skrubu wa kuchonga kidole, n.k. . . . nyakati fulani vilitumiwa kwa sababu ya kosa dogo. Nimeona mtu mweusi mmoja akipigwa mpaka baadhi ya mifupa yake kuvunjwa kwa sababu ya kuacha chungu kuchemka mpaka kumwagika.”

Nyakati nyingine watumwa waliamua kuasi. Ingawaje, mwingi wa uasi wao haukufaulu na waliadhibiwa kwa unyama usio na huruma.

[Maelezo ya Chini]

a Mataifa ya Ulaya yaliyohusika moja kwa moja katika biashara ya watumwa ya kuvuka Atlantiki yalikuwa Denmark, Hispania, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, na Ureno.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Waliokufa walitupwa baharini

[Hisani]

Culver Pictures

[Picha katika ukurasa wa 5]

Watumwa wengi iwezekanavyo walijazwa shehenani

[Hisani]

Schomburg Center for Research in Black Culture / The New York Public Library / Astor, Lenox and Tilden Foundations

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki