Uchunguzi wa “Damu Yenye Dosari” ya Kanada
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kanada
MAJERUHI wa damu isiyo safi katika Kanada wanakufa kutokana na UKIMWI kwa idadi zenye kuongezeka. Kwa nini kuwe na ongezeko hilo? Zaidi ya Wakanada elfu moja waliambukizwa virusi ya UKIMWI kutokana na “damu yenye dosari” na vifanyizwa vya damu katika miaka ya 1980. Hakika hizi zenye kusumbua zilifanya serikali ya majimbo kuanzisha Tume ya Kuchunguza Mfumo wa Damu katika Kanada. Uchunguzi wa umma ungefikia mkataa juu ya usalama wa mfumo wa damu ya Kanada.
Mmojapo wa mahakimu wa nchi wa cheo cha juu waliostahiwa sana aliteuliwa awe kamishna wa uchunguzi huo. Tume hiyo inasikiza malalamishi kotekote Kanada. Usikizi ulianza katika Toronto katika Februari 14, 1994, na Mheshimiwa Bw. Hakimu Horace Krever wa Mahakama ya Rufani ya Ontario aliombwa kutoa ripoti ya uchunguzi wake kwa kipindi kilichowekwa na kupendekeza sehemu za kufanyia maendeleo.
Mama aliyefiwa ambaye mwanaye alikufa kwa UKIMWI kutokana na damu isiyo safi alimsihi hakimu hivi: “Walimchukua mwanangu na nilichopata peke yake kilikuwa uchunguzi huu. Tafadhali ufanye uwe wenye maana.” Alihangaikia sana kuona kwamba uchunguzi ulio kamili ungefanywa ili kwamba hatua zihitajiwazo zingechukuliwa ili kuepuka hatari zinazoshirikishwa na utiaji-damu mishipani. Hakuwa ndiye mama pekee aliyepoteza mwana katika kifo kutokana na damu yenye dosari. Tume hiyo ilisikia ushuhuda wenye kutetemesha kuhusu msiba huu ambao ulivunja-vunja uhai wa Wakanada wengi.
Vichwa vikuu katika Globe and Mail ya Toronto vimeripoti hivi: “Hasira, Machozi Majeruhi Waelezapo Kuhusu Ogofyo la Damu”; “Uchunguzi wa Damu Wasikia Ushuhuda Wenye Kuogofya”; “Kupuuza kwa MD (Madaktari wa Kitiba) Kwaelezwa kwa Kina”; na “Maofisa Waliamua Hatari za UKIMWI Kuwa Ndogo, Tume ya Damu Iliambiwa.”
Majeruhi walioambukizwa HIV kutokana na damu walisema hawakuonywa kuhusu hatari zayo. Katika visa kadhaa hawakujua kama walitiwa damu mishipani hadi walipojua walikuwa na virusi ya UKIMWI.
Tineja mmoja mwenye UKIMWI alipata HIV kutokana na kutiwa damu mishipani wakati wa upasuaji wa moyo alipokuwa na umri wa miaka mitatu. Mwanamume fulani aliyethibitishwa kitiba kuwa na virusi ya HIV mwenye kutotungama kwa damu kudogo alitumia vifanyizwa vya damu kabla ya 1984 wakati alipocheza hoki. Angebadili mtindo-maisha wake angelijua hatari zao. Mama mmoja alitiwa damu yenye HIV katika 1985, na sasa yeye, mumeye, na binti yao mwenye umri wa miaka minne wote wameambukizwa.
Kumekuwa na masimulizi yenye kutetemesha ya watu walioambukizwa kutokana na sehemu moja ama mbili za damu. “Ili kuboresha tu sura yake,” akasema mwanamke mmoja mwenye uchungu wa kutiwa damu ambako kulimwambukiza mume wake HIV. Sasa hata yeye ana virusi hiyo.
Kadiri mashahidi wengi walivyotoa ushahidi, uangalifu ulielekezwa kwa msiba mwingine wa kadiri kubwa—mchochota wa ini kutokana na damu. Kulingana na The Globe and Mail, yakadiriwa kwamba “Wakanada wengi kufikia 1,000 wanakufa kila mwaka kwa mchochota wa ini C.” Gazeti hilo laongezea kwamba “kufikia nusu yao huenda wakawa waliambukizwa maradhi hayo kutokana na utiaji-damu mishipani.”
Mwanamume mmoja alieleza jinsi alivyoambukizwa mchochota wa ini C kutokana na kutiwa damu wakati wa upasuaji wa mgongo katika 1961. Baada ya upasuaji wake, akawa mchangaji wa kawaida wa damu. Aligundua katika 1993 kwamba alikuwa na mchochota wa ini. “Na vipi kuhusu watu waliopokea damu niliyochanga miaka hiyo yote wakati nilipokuwa sijui nilikuwa na maradhi haya?” akauliza uchunguzi huo.
Hakimu Krever alisikiliza kwa makini Wakanada zaidi ya mia moja ambao maisha yao yalikuwa yamevunjwa-vunjwa na HIV na misiba mingine itokanayo na damu yenye dosari. Wataalamu wa kitiba wamethibitisha kwamba haiwezekani kufanya ugavi wa damu kuwa salama kabisa kutokana na mpitisho wa maradhi na hatari nyinginezo. Wamekubali hatari nzito na matumizi mabaya yanayoshirikishwa na damu. Dakt. J. Brian McSheffrey, mkurugenzi wa kitiba wa huduma ya kimkoa ya utiaji damu, alithibitisha kwamba yeye huvuta uangalifu kwa tatizo hilo kwa kusema katika mihadhara hivi: “Ukiwa daktari ikiwa unapendekeza utiaji damu, ama umeshindwa katika kuchunguza ugonjwa kwa usahihi ama umeshindwa kitiba.”
Kumekuwa na mashtaka ya hila za kisiasa na ubishi miongoni mwa wale ambao kamati ya serikali iliwaita “wanahisa wakubwa” katika mfumo wa damu wa Kanada wenye dola milioni 250 kwa mwaka. Msalaba Mwekundu na mashirika ya serikali yameshambuliwa sana. Hakuna yeyote anayeonekana kuwa na daraka la mfumo wa damu wa kitaifa ulio tata.
Utofautiano Unaotamanika
Kinyume na uthibitisho wenye kuvunja moyo, ripoti yenye kufurahisha ilitolewa kwa Hakimu Krever Mei 25, 1994, katika Regina, Saskatchewan. William J. Hall, mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 75 aliye na kutotungama kwa damu kuliko kubaya sana alisimulia jinsi kwa kufanikiwa aliiweza hali yake kwa kutumia vibadala visivyofanyizwa kwa damu. Naye hakuwa na UKIMWI. Akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, Bw. Hall ameepuka damu na vifanyizo vyayo kwa sababu ya dhamiri yake ya kidini.—Ona sanduku kwenye ukurasa 22.
Mengi yangali yatasemwa. Serikali imeongeza muda wa uchunguzi huo hadi mwishoni mwa 1995. Tume hiyo ingeweza kuwa na wakati wa kuchunguza matibabu yenye matokeo yasiyotumia damu yanayotumiwa katika maelfu ya visa vya watu wazima na watoto ambao ni Mashahidi wa Yehova. Vibadala hivi vyatumika kwa wagonjwa wengineo pia.
Madaktari wanaotumia vibadala kama hivyo wana uthibitisho kamili ambao wangeweza kushiriki pamoja na tume hiyo. Dakt. Mark Boyd wa Chuo Kikuu cha McGill aliambia The Medical Post katika 1993 hivi: “Kwa hakika tunapaswa kuwa wenye shukrani kwa Mashahidi wa Yehova kwa sababu wametuonyesha jinsi ya kufanikiwa bila utiaji-damu mishipani.” Tume fulani ya kirais ya Marekani ilionelea hivi katika 1988: “Hatua ya kuzuia iliyo hakika kuhusu ugavi wa damu ni kutotumia damu ya mgonjwa mmoja kwa wengineo, iwezekanapo.” Kwa kutii sheria ya Mungu ya ‘kujiepusha . . . na damu,’ Mashahidi wa Yehova wamebarikiwa na “hatua ya kuzuia iliyo hakika” dhidi ya damu yenye dosari na hatari nyingine za utiaji-damu mishipani.—Matendo 15:20, 29.
Elimu Yahitajika
Kwa kusikitisha, majeruhi walio wengi wa utiaji-damu mishipani wenye dosari hawakuarifiwa kuhusu vibadala ambavyo vingeweza kuzuia misiba yao. Wagonjwa hawakupatiwa uchaguzi wa haki ya kuarifiwa—kukubali hatari za damu ama kutumia vibadala vilivyo salama zaidi.
Uthibitisho mbele ya tume ulifunua uhitaji wa kuelimisha madaktari na umma kuhusu vibadala vya utiaji-damu mishipani. Tume ya serikali ya hali ya juu kama hiyo ingeweza kuwa na matokeo makubwa katika Kanada. Mapendekezo ya Hakimu Krever yangeweza kuanzisha mabadiliko yanayohitajiwa katika mitazamo na elimu katika dawa za Kanada kuhusu mazoea ya kutia damu. Uchunguzi wa Tume ya Uchunguzi utakuwa wenye faida kwa wote wanaotaka kuepuka hatari ziambatanazo na utiaji-damu mishipani.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
KUTOTUNGAMA KWA DAMU KWAWEZWA BILA DAMU
William J. Hall wa Nipawin, Saskatchewan, aliambia tume jinsi na kwa nini yeye humudu kutotungama kwa damu kuliko kubaya bila vifanyizwa vya damu. Hapa kuna dondoo kutoka kwa nakala ya ushahidi wake kwa mahakama:
◻ “Wazazi wangu walifahamu kwamba nilikuwa na kutotungama kwa damu nilipofura kutoka kidole hadi kiuno wakati mmoja, na madaktari wakapata kwamba ni kutotungama kwa damu. . . . Ningekisia nilikuwa yapata umri wa mwaka mmoja.”
◻ “Sijapata kamwe kutiwa damu ama vifanyizwa vya damu vya aina yoyote. . . . Ni kinyume cha itikadi zangu za kidini kutumia damu kwa sababu nahisi ni takatifu.”
◻ Kuhusu ndugu yake ambaye pia alikuwa na kutotungama kwa damu: “Yeye hakuwa na imani [dini] kama niliyo nayo, hivyo alitiwa damu mishipani naye akafa kutokana na mchochota wa ini.”
◻ Kuhusu kidonda cha mbuti katika 1962: “Daktari alisema kwamba, ikiwa singetumia damu, ningekufa. . . . Nilitibiwa vizuri [bila damu] hospitalini.” Kule kutokwa kwa damu kulidhibitiwa.
◻ Kuhusu upasuaji katika 1971 wa kuunga kiuno kilichovunjika: “Ilikuwa oparesheni yenye umakini bila damu. . . . Oparesheni yenyewe ilifanikiwa.” Majaribio ya tena na tena kwa wakati huo yalipata kwamba Factor 8 (damu yenye virusi) haikuwako katika damu yake.
◻ Jinsi huimudu: “Mtindo wa maisha . . . , kuwa na umakini.” Yeye hutia ndani mlo, pumziko, mazoezi, na matibabu yenye umakini ya vivimbe, michubuko, na maumio.
◻ “Mimi huamini katika kutulia na kutafakari juu ya mambo mazuri ambayo Mungu ametupa na husahau kuhusu mafadhaiko yetu. Hili huonekana kusaidia sana.”
William Hall ana umri wa miaka 76 na ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova.
[Picha katika ukurasa wa 20]
Hakimu Horace Krever, mkuu wa tume hiyo
[Hisani]
CANPRESS PHOTO SERVICE (RYAN REMIROZ)
[Picha katika ukurasa wa 21]
William na Margaret Hall waliendesha gari kwa kilometa 370 ili kutokea mbele ya Tume ya Uchunguzi