Je, Umeona Thilasini?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA
‘ATI nimeona nini?’ huenda ukauliza. ‘Hata sijui thilasini ni nini.’
Kwa kweli, “thilasini” ni ufupisho wa jina kamili la kizuolojia “Thylacinus cynocephalus” na ni jina la mnyama mwenye kuvutia kutoka Australia, simbamarara wa Kitasmania au mbwa-mwitu wa Kitasmania.
“Thylacinus cynocephalus” kihalisi humaanisha “mbwa aliye na pochi mwenye kichwa cha mbwa-mwitu,” lakini huyu mnyama alipewa majina mbalimbali yaliyo sahili zaidi na masetla Wanaulaya wa mapema wa Tasmania, jimbo dogo la kisiwa la Australia. Majina kama vile pundamilia-komba, fisi, pundamilia aliye mbwa-mwitu, komba aliye na kichwa cha mbwa yalikuwa ya kawaida. Wenyeji wa Australia, ambao walikuwa katika Tasmania muda mrefu kabla ya mtu mweupe kufika yapata miaka 200 iliyopita, walimwita thilasini kwa jina korina.
Simbamarara wa Kitasmania sasa afikiriwa kuwa aliyetoweka, lakini vielezo vilivyojalizwa vyaweza kupatikana katika majumba ya kuhifadhi vitu vya kale. Thilasini wa mwisho ajulikanaye alikufa 1936 katika hifadhi ya wanyama katika Hobart, jiji kuu la Tasmania. Hata hivyo, kuna wale wanaodai kuna thilasini wanaoishi wakijificha kwenye nyika ya Tasmania, na ripoti za kuonekana kwa thilasini zaendelea.
Ingawa si wa familia ya simbamarara, jina simbamarara wa Kitasmania labda lilizuka kwa sababu huyo mnyama ana milia na kwamba pia ni mla-nyama. Milia yenye kutofautisha, ya hudhurungi nzito, karibu na nyeusi huteremka ikivuka mgongo wake na kuteremka kwenye mkia wake ulio mrefu na thabiti. Uhakika mwingine zaidi na wenye kuvutia ni kwamba thilasini ni mnyamapochi—yaani, jike huwa na pochi. Wachanga huzaliwa wakiwa wadogo mno, wasiokomaa, na wasioona lakini hupata njia ya kwenda kwenye pochi ya mama yao, ambapo hunyonyeshwa hadi wanapokua wakubwa na wenye nguvu za kutosha ili kuondoka. Mzaliwa-karibuni aliye mdogo mno hukaa katika pochi ya mama thilasini kwa yapata miezi mitatu kabla ya kutoka nje. Ingawa hivyo, mara tu awapo nje ya pochi, thilasini mdogo huanza kumfuata mama katika utafutaji wake wa chakula.
Inadaiwa kwamba thilasini ndiye mnyamapochi mla-nyama mkubwa zaidi ya wote ajulikanaye katika nyakati za majuzi. Tofauti na wanyamapochi kama vile kangaruu, thilasini wa kike ana pochi ifunukayo kuelekea upande wa nyuma. Thilasini huyo wa kike anaweza kubeba na kunyonyesha wachanga wanne kwa wakati mmoja.
Alienea Kadiri Gani?
Ingawa michoro ya miambani ya Wenyeji wa Australia, mabaki ya vitu vya kale, na vielezo vilivyokaushwa vya thilasini vimepatikana katika sehemu nyingi za Australia, makao ya asili hasa ya thilasini yaonekana yalikuwa Tasmania. Hata huko huenda hawakuwa wengi. Binadamu ndio hasa wamekuwa wenye kulaumika kwa ajili ya kutoweka kwake. Simbamarara wa Kitasmania mwenyewe alikuwa mwindaji, na bado hakuweza kujilinda kwa matokeo dhidi ya wawindaji wajanja na wenye pupa ambao masetla weupe walithibitika kuwa. Akiwa mdadisi na kwa ujumla asiyehofu mwanadamu, thilasini alikuwa windo rahisi kwa bunduki na mtego.
Wakulima wengi walidai kwamba simbamarara wa Kitasmania alikuwa muuaji wa kondoo, kwa hiyo thawabu zenye kushawishi zilitolewa na kampuni kubwa za kufuga kondoo na vilevile na serikali ya Tasmania. Vielezi vilivyo hai ambavyo vilikuwa vimenaswa vilichukuliwa mara moja na hifadhi za wanyama za ng’ambo. Ingawa idadi ya thilasini bila shaka iliathiriwa na ugonjwa mbaya usiojulikana ulioangamiza wengi wa wanyama wa mbugani wa Tasmania miaka mingi iliyopita, ufyekaji wa idadi kubwa zaidi ya thilasini ulifanywa na mwanadamu zaidi ya njia nyingineyo yote.
Njia za Kipekee za Kuwinda
Thilasini kwa kawaida aliwinda akiwa peke yake lakini nyakati fulani kwa jozi. Njia yake ilikuwa kulenga shabaha mnyama fulani, kama vile kangaruu mdogo, halafu kumkimbiza tu, kumfukuza hadi achoke. Mara tu windo linapopunguza mwendo, likiwa limechoka, thilasini angelirukia na kuliua kwa taya zake zenye nguvu. Sehemu nyingine ya kipekee ya mnyama huyu asiye wa kawaida ilikuwa achamo la taya zake, lililokuwa digrii 120 zenye kustaajabisha!
Zoea lao la kula sehemu fulani tu za mzoga—kwa kawaida viungo vya ndani—lilifanya wengine wawaone kuwa wauaji wenye kuharibu. Lakini ili kusawazisha huu uonekanao kuwa uharabu, mnyamapochi mwingine mdogo zaidi, aitwaye ibilisi wa Kitasmania (ambaye bado yuko) angefuata huyo simbamarara na mara moja kula mabaki—mifupa, manyoya, na kila kitu.
Kwa wazi thilasini hakuwa tisho kwa mwanadamu. Hakuna uthibitisho kwamba waliwinda binadamu. Mzee mmoja wa kale akumbuka kwamba jioni moja, miaka mingi iliyopita, alikuwa ameketi mbele ya moto, akisoma, wakati ambapo kupitia miale ya moto, kwa ghafula aliona simbamarara wa Kitasmania amejikunyata chini akinyemelea, na kusonga pole pole kwa kutia hofu kumwelekea. Akihofia shambulizi, alichukua bunduki yake kimya-kimya, akalenga shabaha kwa uangalifu kupitia miale ya moto, na kufyatua. Huyo thilasini alifanya kitwangomba cha nyuma kisicho na madaha lakini kwa wazi hakuumizwa vibaya, kwani aliruka juu na kupotelea gizani. Halafu mtu alienda kuchunguza kama kulikuwa na damu yoyote, ili kuona kiasi alichomuumiza huyo simbamarara. Mbele tu ya moto alikuta komba mkubwa risasi ikiwa ndani yake. Komba huyo ndiye thilasini alikuwa akimnyemelea!
Vipi Kuhusu Kuonekana Kulikoripotiwa?
Kumekuwa na ripoti nyingi za kuonekana kwa thilasini tangu yule wa mwisho katika uhamisho alipokufa 1936, lakini kufikia wakati huu uthibitisho mchache umetolewa ili kusadikisha wanazuolojia kwamba kuna thilasini walio hai bado. Yaonekana kwamba picha halisi tu au kushika thilasini aliye hai ndiko kutasadikisha maofisa kwamba thilasini bado wako.
Watu wengi wazee zaidi wanaoishi katika sehemu za mashambani za Tasmania wanasema hawangeripoti simbamarara wa Kitasmania ikiwa wangeona mmoja. Wanahangaika kuhusu jambo hakika la kwamba mapema maishani mwao, binadamu wengine walikuwa na lawama la kutoweka kuliko wazi kwa mnyama huyu wa kipekee. Ikiwa thilasini wowote wako bado, watu kama hao wanataka waachwe bila kusumbuliwa.
Kwa hiyo ikiwa wangeulizwa, “Je, umeona thilasini karibuni?” jibu lao—la kweli au lisilo la kweli—lingekuwa, “La!”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
Tom MacHugh/Photo Researchers