Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 5/8 kur. 24-25
  • Tasmania—Kisiwa Kidogo, Simulizi la Kipekee

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tasmania—Kisiwa Kidogo, Simulizi la Kipekee
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tasmania Yawa “Jela ya Milki”
  • Jamii ya Watu Yatoweka
  • Tofauti Zinazoonekana za Tasmania
  • Upande Mtulivu wa Kisiwa Hicho
  • Kutoka Kuwa Bara la Mnyanyaso Hadi Kuwa Paradiso ya Kiroho
  • Je, Umeona Thilasini?
    Amkeni!—1995
  • Kipindi Kibaya Sana kwa Wafungwa Huko Australia
    Amkeni!—2002
  • Viumbe wa Ajabu Katika Pori la Tasmania
    Amkeni!—2012
  • Kupiga Moyo Konde Kulinisaidia Nifanikiwe
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 5/8 kur. 24-25

Tasmania—Kisiwa Kidogo, Simulizi la Kipekee

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

“BARA hili likiwa bara la kwanza kukutana nalo katika Bahari ya Kusini, na kwa kuwa halijulikani na taifa lolote la Ulaya, tumelipatia jina la Anthoony van Diemenslandt, kwa heshima ya Mheshimiwa [wetu] Gavana-Mkuu.” Haya ni maneno ya Abel Tasman Mholanzi katika Novemba 25, 1642, siku ambayo aliona kisiwa cha Tasmania, jimbo la pili kwa kuwa la zamani katika Australia.a Tasman hakuona watu, lakini aliona moshi wa mioto ya mbali na mikato kwenye miti iliyoachana kwa meta 1.5 katika miti iliyokuwa karibu. Wale waliofanyiza hiyo mikato, akaandika, ama walikuwa na njia isiyo ya kawaida ya kuparamia miti au walikuwa majitu! Kwa hakika, mikato hiyo ilikuwa ya kusaidia kuparamia.

Baadaye, Bara la Van Diemen lilitoweka kutoka kwa njia za safari za wavumbuzi wa bahari kwa miaka 130, hadi Mfaransa Marion du Fresne na Mwingereza Tobias Furneaux walipozuru. Nahodha James Cook aliwasili katika 1777 na, kama Du Fresne, alikutana na watu waliopatikana kwenye kisiwa hicho tu, Wenyeji wa Australia. Hata hivyo, ziara yake ilikuwa mwanzo wa msiba: “Mataifa fulani yalimwona [Cook] kuwa mtu ambaye alifungua njia ya ustaarabu na dini,” asema John West katika The History of Tasmania, “[lakini] kwa jamii hii ya [Wenyeji wa Australia] yeye alikuwa mtangulizi wa kifo.” Ni nini kilichoongoza kwenye matokeo hayo yenye kuhuzunisha?

Tasmania Yawa “Jela ya Milki”

Ufukuzo, au kuhamishwa, kulikuwa fimbo ya adhabu ya Uingereza, na Tasmania pakaja kuwa mahali pa kutumikia adhabu pa Uingereza. Tangu 1803 hadi 1852, wanaume, wanawake, na hata watoto 67,500 hivi—baadhi yao wakiwa wachanga wenye umri wa miaka saba—walifukuzwa kutoka Uingereza waende Tasmania kwa uhalifu mbalimbali kuanzia kuiba vitabu vya sala hadi ubakaji. Hata hivyo, washtakiwa wengi, walifanya kazi kwa masetla au katika miradi ya serikali. “Wasiozidi asilimia 10 . . . hata hawakuona makao ya kutumikia adhabu,” yasema The Australian Encyclopaedia, “na wengi ambao waliona walikuwa huko kwa vipindi vifupi tu.” Port Arthur, kwenye Peninsula ya Tasman, ilikuwa mahali pakuu pa makao ya kutumikia adhabu, lakini washtakiwa sugu walipelekwa Bandari ya Macquarie, iliyozingirwa ikiwa “pahali palipowekwa kando kwa desturi ya utesaji.” Kiingilio chembamba cha bandari hiyo kilipata jina lenye kutisha Lango la Helo.

Katika kitabu This Is Australia, Dakt. Rudolph Brasch aeleza sehemu nyingine muhimu ya koloni hii changa—hali yayo ya kiroho, au ukosefu wayo wa hali ya kiroho. Yeye aandika: “Tangu mwanzo dini katika Australia [kutia ndani Tasmania, bila shaka] iliachwa na kupuuzwa na, kwa sehemu kubwa, ilitumiwa na kutumiwa vibaya na viongozi wa taifa kwa ajili ya faida yao wenyewe. Koloni hiyo ilianzishwa bila sala na ibada ya kwanza kwenye nchi ya Australia yaonekana ilikuwa jambo lililofikiriwa baadaye.” Ingawa Wasafiri wa Amerika Kaskazini walijenga makanisa, “wakazi wa mapema wa Australia,” chasema kitabu The History of Tasmania, “walichoma kanisa lao la kwanza ili kuepuka uchovu wa kuhudhuria.”

Maadili haya yaliyopotoka yalipotoshwa hata zaidi na wingi wa mvinyo. Kwa raia na vilevile mwanajeshi, mvinyo ulikuwa “njia hakika kuelekea utajiri,” asema mwanahistoria John West.

Hata hivyo, nyakati fulani chakula kilikuwa haba. Wakati wa vipindi hivi wafungwa waliowekwa huru na masetla walitumia bunduki kuwinda wanyama walewale ambao Wenyeji wa Australia waliwafuatia kwa mikuki. Kwa kueleweka, mikazo ikazidi. Sasa ongeza katika mchanganyiko huo uwezao kutokeza jeuri madharau ya kijamii ya wazungu, wingi wa mvinyo, na tofauti zisizoweza kupatanishwa za kitamaduni. Wanaulaya wanaweka mipaka na kutengeneza uzio; Wenyeji wa Australia wanawinda na kukusanya wakizunguka huku na huku. Kilichohitajika tu ni kichocheo.

Jamii ya Watu Yatoweka

Kichocheo hicho kilikuja katika Mei 1804. Kikundi cha watu kilichoongozwa na Luteni Moore kilifyatua bunduki zao, bila kuchokozwa, kuelekea kikundi kikubwa cha kuwinda cha Wenyeji wa Australia wanaume, wanawake, na watoto—kikiua na kujeruhi wengi. “Vita vya Weusi”—mikuki na mawe dhidi ya risasi—vilikuwa vimeanza.

Wanaulaya wengi walichukizwa na machinjo hayo ya Wenyeji wa Australia. Gavana Sir George Arthur alihuzunishwa sana hivi kwamba alieleza utayari wake wa kufanya lolote lililohitajiwa ili ‘kulipia majeraha ambayo serikali bila kukusudia ililetea Wenyeji hao wa Australia.’ Hivyo, akaanzisha programu ya “kukusanya” na “kuwastaarabisha.” Katika kampeni iliyoitwa “Mpaka wa Weusi,” wanajeshi, masetla, na wafungwa wapatao 2,000 waliingia vichakani katika jitihada ya kuwashika Wenyeji hao wa Australia na kuwapa makao mapya katika mahali salama. Lakini utendaji huo ulikosa kufaulu kwa njia yenye kufedhehesha; wazungu hao walishika mwanamke na mvulana tu. Kisha George A. Robinson, Mmethodisti mashuhuri, aliongoza mfikio wa kirafiki zaidi, ambao ulikuwa na matokeo. Wenyeji hao wa Australia walimtumaini na kukubali toleo lake la kuhamia mahali papya kwenye Kisiwa Flinders, kaskazini ya Tasmania.

Katika kitabu chake A History of Australia, Marjorie Barnard asema juu ya matimizo ya Robinson: “Kwa uhalisi, ingawa huenda hakujua hili mwenyewe, upatanishaji wake ulikuwa kama usaliti wa Yudasi. Wenyeji hao maskini walitengwa kwenye Kisiwa Flinders katika Mlangobahari wa Bass na Robinson akiwa mlinzi wao. Walidhoofika na kufa.” Badala ya kuendelea kuuawa kwa bunduki, waliuawa na mtindo-maisha na ulaji wa wazungu. Kitabu kimoja chasema kwamba “Mwenyeji kamili wa mwisho wa Australia wa Tasmania alikuwa Fanny Cochrane Smith, ambaye alikufa katika Hobart mwaka 1905.” Wataalamu wana maoni tofauti kuhusu hilo. Wengine humtaja Truganini, mwanamke aliyekufa katika Hobart katika 1876, wengine mwanamke aliyekufa kwenye Kisiwa Kangaroo katika 1888. Wazao wa mchanganyiko wa wazungu na Wenyeji wa Australia wa Tasmania bado wako hai na katika hali nzuri leo. Kukiongezwa kwenye orodha inayoendelea ya matendo mabaya yanayofanywa na wanadamu, kutoweka huku kwa Wenyeji kamili wa Australia kumeitwa kwa kufaa “msiba mkuu zaidi wa Jimbo la Tasmania.” Isitoshe, huko hukazia kweli ya Biblia kwamba “mwanadamu amemtawala mwanadamu kwa hasara yake.”—Mhubiri 8:9 (UV chapa ya 1989).

Tofauti Zinazoonekana za Tasmania

Leo, isipokuwa uzuru majumba ya kuhifadhi vitu vya kale, maktaba, au magofu ya magereza, hutajua masaibu ya mwanzoni ya kisiwa hiki chenye kuvutia. Tasmania ina umbali kusini ya ikweta sawa na umbali ambao Rome, Sapporo, na Boston zilivyo kaskazini. Na sawa na historia yayo, jiografia yayo inatofautiana sana, hata ingawa hakuna mahali kwenye kisiwa hiki ambapo pana umbali uzidio kilometa 115 kutoka baharini.

Kati ya eneo la jumla la Tasmania, asilimia 44 ni msitu na asilimia 21 ni hifadhi ya kitaifa. Huu ni ulinganifu usio wa kawaida! Kulingana na The Little Tassie Fact Book, “eneo la urithi wa ulimwengu wa Tasmania Magharibi ni moja ya maeneo ya nyika yasiyoharibiwa yenye tabia nchi ya kiasi zaidi ulimwenguni.” Maziwa yenye kujazwa na mvua na theluji, mito, na maporomoko ya maji—yaliyojaa samaki aina ya tirauti—hulisha misitu ya miti aina ya pencil pines, eucalyptus, myrtle, blackwood, sassafras, leatherwood, celery-topped pines, na Huon pines, kutaja michache tu. Si ajabu kwamba mwono unaopatikana kwenye nyanda za juu za magharibi ya kati na vilele vyayo vyenye theluji huvutia wapenda maumbile ya asili na kuwafanya warudi tena na tena.

Lakini kulinda “Urithi wa Ulimwengu” hakukuja bila upinzani. Na watu wanaopendezwa na mazingira bado wanapinga uchimbaji wa migodi, utengenezaji wa karatasi, na mapendezi ya nishati ya umeme itokanayo na maji. Mandhari ya nchi yenye kufanana na uso wa mwezi ya Queenstown, mji wa uchimbaji migodi, ni kikumbusha kikali cha matokeo ya utumiaji usio na ufikirio wa maliasili.

Wanyama wa huko wameteseka pia—hasa thilasini, au simbamarara wa Tasmania, mnyamapochi wa hudhurungi afananaye na mbwa. Milia myeusi kuvuka mgongo na tako lake ilimpa jina simbamarara. Kwa kuhuzunisha, mlanyama huyo asiye na mafuta na mwenye haya aliwinda kuku na kondoo. Kukiwa na zawadi ya fedha kwa yeyote ambaye angeua thilasini, mnyama huyo alitoweka kufikia 1936.

Mnyamapochi mwingine wa kipekee wa Tasmania, shetanimwitu wa Tasmania, bado yupo. Akitumia taya zake zenye nguvu na meno, mlanyamafu huyu aliyejenga kimsuli na mwenye uzani wa kilo 6 hadi 8 aweza kula mwili wote wa kangaroo mfu, fuvu na kila kitu.

Tasmania yajulikana sana pia kwa ndege wayo aina ya shearwater mwenye mkia mfupi, au muttonbird. Baada ya kuanza kuhama kutoka Bahari ya Tasmania na kuzunguka Pasifiki, ndege huyo hurudi kila mwaka kwenye shimo lilelile—tendo la ajabu ambalo ni sifa kwa Mbuni na Muumba wake.

Karibu na mahali pake pa uzazi pa usiku huishi ndege mwingine—yule ambaye “hupuruka” chini ya maji—ngwini mwenye kupendeza mwenye uzani wa kilo moja aliye na mdoni mdogo. Ngwini huyo mdogo kuliko wote ndiye pia mwenye kelele kupita wote! Maonyesho yake hutofautiana kwa wingi, kukiwa na utendaji wa sauti na mwili nyakati fulani ukiwa mwingi mno. Wanapohisi mahaba, jozi ya ndege hao hucheza wimbo wa wawili ili kuhakikishiana ushikamano. Ingawa hivyo, kwa kusikitisha, wengi wanauawa na nyavu za wavuvi, mmwagiko wa oili, na vitu vya plastiki wanavyokula wakifikiri ni chakula, au na mbwa na paka waliogeuka kuwa wa mwituni.

Upande Mtulivu wa Kisiwa Hicho

Tazama kaskazini au mashariki ukiwa ukingoni mwa uwanda wa juu wa kati nawe utaona sehemu yenye kupendeza ya Tasmania, ikiwa na mashamba yayo yaliyolimwa, yenye rangi ya hudhurungi ya kijivu, mito na hori zenye kupinda-pinda, barabara pana zenye miti kandokando, na malisho ya kijani kibichi yaliyotapakawa na kondoo na ng’ombe. Karibu na mji wa kaskazini Lilydale, wakati wa Januari, mashamba ya maua aina ya lavender yakiwa yamechanua kabisa huongezea mandhari hii ya mashambani inayofanana na usanii wa mozeiki wa rangi nyekundu nyangavu yenye manukato yavutiayo.

Lililovuka Mto Derwent, si mbali sana na mashamba ya matofaa ambayo yalipatia Tasmania jina Kisiwa cha Matofaa, ni jiji kuu Hobart, lenye idadi ya watu 182,000 hivi. Juu yalo kuna Mlima Wellington ulio mkubwa na wenye huzuni, ambao una kimo cha meta 1,270. Katika siku isiyo na mawingu, mlima huu ambao mara nyingi hufunikwa na theluji huandaa mwono wa juu wa jiji lililoko chini. Kwa kweli Hobart limebadilika na kufanya maendeleo mengi tangu 1803, wakati Luteni John Bowen na kikundi chake cha watu 49, kutia ndani wafungwa 35, kiliposhuka kutoka melini katika Risdon Cove. Ndiyo, merikebu za zamani hazipo tena, lakini mara moja kwa mwaka mashindano ya mashua ya kutoka Sydney hadi Hobart hukumbusha watu usafiri wa baharini wa hapo awali huku mashua za tanga za pembetatu na zenye kuundwa kwa mbio huenda kwa mwendo wa kasi zikipita umati wa watu wenye kushangilia, moja kwa moja hadi katikati mwa Hobart.

Kutoka Kuwa Bara la Mnyanyaso Hadi Kuwa Paradiso ya Kiroho

Geoffrey Butterworth, mmoja wa wajumbe 2,447 kwenye “Hofu ya Kimungu” Mkusanyiko wa Wilaya wa Mashahidi wa Yehova wa 1994 katika Launceston, akumbuka: “Nakumbuka wakati hakukuwa na zaidi ya Mashahidi 40 katika Tasmania yote.” Sasa kuna makutaniko 26 na Majumba ya Ufalme 23.

“Lakini hali hazikuwa nzuri sana sikuzote,” aongeza Geoff. “Kwa kielelezo, huko nyuma katika 1938, Tom Kitto, Rod McVilly, nami, sote tukiwa tumevalia vibao mbele na nyuma, tulikuwa tukitangaza hotuba ya Biblia ya hadharani ‘Yakabilini Mambo ya Hakika.’ Ulikuwa ufichuaji wenye kuchoma dini isiyo ya kweli ambao ungesambazwa kutoka London kupitia mfumo wa redio. Nilipoungana na wenzangu, walikuwa wakidhulumiwa na kikundi cha vijana. Na polisi walikuwa wakitazama tu! Nilikimbia kuwasaidia lakini muda si muda nikapigwa. Lakini mwanamume mmoja alinivuta kwa nyuma ya shati langu na kuniondoa. Badala ya kunipiga, mwanamume huyo alisema kwa sauti kuu nzito: ‘Waacheni!’ Kisha, akaniambia kimya-kimya: ‘Najua jinsi ilivyo kunyanyaswa, rafiki, mimi natoka Ireland.’”

Yehova alibariki mapainia hao wa mapema, kwa kuwa leo habari njema za Ufalme wa Mungu zimefika sehemu zote za kisiwa hiki chenye watu 452,000. Wazao wengi wa wafungwa na Wenyeji wa Australia hutazamia kwa hamu kukaribisha kwenye dunia iliyosafishwa—watu weusi na weupe—waliokufa isivyo haki katika siku hizo za mapema zenye ukatili, kwa kuwa Biblia huahidi “ufufuo wa waadilifu na wasio waadilifu.” (Matendo 24:15) Badiliko hili litakuwa kamili sana hivi kwamba “mambo ya kwanza [hata] hayatakumbukwa.”—Isaya 65:17.

[Maelezo ya Chini]

a Jina Tasmania lilikubaliwa rasmi Novemba 26, 1855. Jimbo la kale zaidi ni New South Wales.

[Picha/ katika ukurasa wa 25]

Juu: Mlima Cradle na Ziwa Dove

Juu kulia: Shetanimwitu wa Tasmania

Chini kulia: Msitu wa mvua katika Tasmania ya Kusini-magharibi

Australia

TASMANIA

[Hisani]

Shetani mwitu wa Tasmania na ramani ya Tasmania: Department of Tourism, Sport and Recreation - Tasmania; Ramani ya Australia: Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki