Ulimwengu Ulikuwaje Miaka 50 Iliyopita?
JE, WEWE una umri wa kutosha kukumbuka vile ulimwengu ulivyokuwa katika 1945? Ulikuwa ndio tu unaanza kupata nafuu kutokana na Vita ya Ulimwengu 2 iliyoanza katika 1939 wakati Uingereza na Ufaransa zilitangaza vita dhidi ya Ujerumani kwa sababu ya uvamizi wa Nazi katika Poland. Ikiwa wewe ni mchanga sana kukumbuka hilo, je wakumbuka ile vita katika Korea iliyozuka katika 1950? Ama ile vita katika Vietnam ambayo ilidumu kutoka miaka ya 1950 hadi 1975? Ama ile vita katika Kuwait iliyochochewa na Iraki katika 1990?
Je, haikushangazi kwamba tunapopitia historia tangu Vita ya Ulimwengu 2, ni lazima tukumbuke vita vingi zaidi ambavyo vimesababisha maafa na mateseko kwa mamilioni ya watu na ambavyo vimeangamiza uhai wa mamilioni mengine? Ni matokeo gani Vita ya Ulimwengu 2 iliachia watu wakati huo?
Matokeo ya Vita ya Ulimwengu 2
Watu wapatao milioni 50 waliuawa katika Vita ya Ulimwengu 2, na kufikia 1945, mamilioni ya wakimbizi walikuwa wakimangamanga kuvuka Ulaya wakijaribu kurudi nyumbani mwao katika majiji na miji iliyoharibiwa kwa mabomu ili kujenga upya maisha yao yaliyoharibiwa kabisa. Mamia ya maelfu ya wanawake na wasichana, hasa katika Urusi na Ujerumani, walikuwa wakijaribu kupata nafuu kutokana na lile umizo la kulalwa kinguvu na majeshi yenye kuvamia. Kupimiwa chakula kulienea karibu Ulaya nzima—chakula na mavazi vilikuwa haba mno. Mamia ya maelfu ya askari-jeshi walioondolewa jeshini walikuwa wakitafuta kazi. Mamilioni ya wajane na mayatima waliomboleza kwa sababu ya kupoteza waume na wazazi wao.
Wayahudi bado walijaribu kutafakari uhalisi wa lile Teketezo la Umati ambalo liliangamiza mamilioni ya Wayahudi wenzao na ule uwezekano wa kutokeza vizazi vya wakati ujao. Mamilioni ya watu—kutoka Amerika, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Urusi, na mataifa mengine mengi—walikufa katika vita hiyo. Umati mkubwa wa kizazi chenye uwezo mwingi ulipotezwa ili kufaidi masilahi ya kisiasa na kibiashara ya serikali za ulimwengu pamoja na watawala wazo.
Nchi nyingi zilifikwa vibaya mno na Vita ya Ulimwengu 2 hivi kwamba jambo zilizohitaji kutanguliza lilikuwa kupata nafuu kiuchumi. Upungufu wa chakula ulibaki ukiwa umeenea katika Ulaya kwa miaka kadhaa baada ya vita. Hispania, ingawa haikuwamo kirasmi wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, ilikuwa imeathiriwa sana na vita vyayo vya wenyewe kwa wenyewe (1936-1939) na vikwazo vya kibiashara—vitabu vya kuweka vipimo vya chakula bado vilitumiwa hadi Juni 1952.
Katika Mashariki ya Mbali, kumbukumbu za ukatili wa Wajapani zilikuwa bado akilini mwa majeruhi katika Burma, China, na Filipino, na nchi nyinginezo za Mashariki. Ingawa taifa mshindi, Marekani ilipoteza wanajeshi wapatao 300,000, karibu nusu ya hasara hizi zikitokea katika vita vya kanda ya Pasifiki. Katika Japani, umaskini, kifua kikuu, na milolongo mirefu ili kupata chakula cha kupimiwa zilikuwa kawaida ya maisha ya watu.
Wito wa Churchill wa Kutenda
Katika hotuba yake ya ushindi aliyotolea watu wa Uingereza Mei 13, 1945, kwenye umalizio wa Vita ya Ulimwengu 2 katika Ulaya, Waziri Mkuu Winston Churchill alitaarifu hivi: “Natamani ningeweza kuwaambia nyinyi jioni hii kwamba kujisulubu kwetu kwote na matatizo yetu yalikwisha. . . . Ni lazima niwaonye . . . kwamba kuna mengi bado ya kufanya, na kwamba ni lazima mwe tayari kwa ajili ya jitihada zaidi za kiakili na kimwili na ujitoaji zaidi wa harakati kubwa za kijeshi.” Akiwa na mwono mbele zaidi, akitazamia mweneo wa Ukomunisti, yeye alisema hivi: “Katika bara la Ulaya ni lazima bado tuhakikishe kwamba . . . yale maneno ‘uhuru’, ‘demokrasi’, na ‘kuweka huru’ hayatavurugwa kutoka kwa maana yao halisi kama tuyaelewavyo.” Kisha akatamka wito wa ushindani: “Songeni mbele, bila kuyumba-yumba, mkiwa imara, bila kushindwa, mpaka kazi yote ifanywe na ulimwengu wote uwe salama na safi.”—Italiki ni zetu.
Nusu-Karne ya Migongano na Vifo
Katika hotuba fulani katika 1992, Katibu-Mkuu wa UM Boutros Boutros-Ghali alikubali kwamba “tangu kubuniwa kwa Umoja wa Mataifa katika 1945, zaidi ya migongano mikubwa 100 ulimwenguni pote imeua watu wapatao milioni 20.” Likionyesha hata idadi ya vifo ya juu zaidi, gazeti la World Watch lilitaarifu hivi: “Hii imekuwa karne iliyo na amani kidogo sana katika historia.” Chanzo hichohicho kilinukuu mtafiti mmoja akisema kwamba “watu zaidi wameuawa na vita mbalimbali katika karne hii kuliko historia yote ya awali ya binadamu ikijumlishwa. Vifo milioni 23 vya hivyo vimetokezwa tangu Vita ya Ulimwengu 2.”
Hata hivyo, The Washington Post, liliripoti kadirio jingine pia: “Tangu mwisho wa Vita ya Ulimwengu 2, karibu vita 160 vimepigwa tufeni pote, vikitokeza vifo zaidi ya milioni 7 vitani na vifo vya raia kufikia milioni 30. Kwa kuongezea, kumekuwa na waliotiwa majeraha, waliolalwa kinguvu na wale waliofanywa kuwa wakimbizi.” Hakuna mojapo ya tarakimu hizi inayotia ndani mamilioni ya majeruhi wa uhalifu wenye jeuri duniani pote wakati wa miaka 50 iliyopita!
Sasa, katika 1995, bado tuna migongano yenye kuua ichochewayo na chuki mbaya mno ambayo huua si wanajeshi tu ambao wameweka mkataba kufia jeshini bali pia maelfu ya raia katika Afrika, Balkani, Mashariki ya Kati, na Urusi.
Basi, je, tunaweza kusema kwamba miaka 50 baada ya 1945, “kuwa ulimwengu mzima ni salama na safi”? Wanadamu wamefanya maendeleo yapi kuelekea kufanya dunia yetu kuwa mahali pafaapo na salama pa kuishi? Sisi tumejifunza nini kwa miaka 50? Je, mwanadamu amefanya maendeleo katika mambo yaliyo ya maana kwelikweli—mambo yafaayo, maadili, adabu? Makala mbili zifuatazo zitajibu maswali haya. Makala ya nne itazungumzia matazamio ya wakati ujao kwa sisi sote katika makao ya tufeni.
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Kumbukumbu za Enzi ya Baada ya Vita ya Ulimwengu 2
Mwingereza mmoja sasa aliye katika umri wa miaka ya 60 akumbuka hivi: “Huko nyuma mwishoni-mwishoni mwa miaka ya 1940, hatukuwa na televisheni nyumbani mwetu. Redio ilikuwa ndiyo kiwasilisha-habari kikuu mawazoni mwetu. Kwa kuwa nilikuwa bado shuleni, kusoma na kufanya kazi ya shuleni nyumbani kulishughulisha akili yangu. Nilikuwa nikienda kwenye sinema angalau mara moja kwa mwezi. Nilikuwa nikiendesha baiskeli kilometa kadhaa siku za Jumamosi ili kutazama timu ya kandanda niliyoipenda. Kwa kulinganishwa ni familia chache zingeweza kuwa na gari ama simu. Kama ilivyokuwa na mamilioni mengine katika Uingereza, hatukuwa na bafu ya kando. Choo kilikuwa nje, na beseni la kuogea lilikuwa jikoni, lililotumiwa kama bafu. Wakati wa vita, tulijiruzuku kwa milo iliyotengenezwa kwa vyakula vilivyokaushwa—mayai, maziwa, na viazi vya unga-unga. Matunda, kama vile machungwa na ndizi, yalikuwa ya vipindi vya kipekee. Kuwasili kwayo kwenye duka la mboga la mahali petu kulikuwa ishara ya kila mmoja kukimbia kama mwehu ili kupanga mstari kwa ugavi wao. Wanawake wengi walilazimika kufanya kazi katika viwanda vya silaha. Huko nyuma watu hawakung’amua mabadiliko makubwa ambayo yalikuwa akibani—ulimwengu wa televisheni, video, kompyuta, ulimwengu wa kompyuta, mawasiliano ya faksi, mruko wa angani, na uhandisi wa kijeni.”