Kuchungua Mafumbo ya Uhamaji
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HISPANIA
KUNA wimbo mmoja wa kale unaoeleza juu ya kurudi kwa vijumbamshale hadi kwenye Mission San Juan Capistrano ya kale katika San Juan Capistrano, California, Marekani. Yasemekana kwamba bila kukosa, Machi 19 kila mwaka, wao hurudi kwenye viota vyao huko.
Kijumbamshale wa Ulaya hufuata ratiba kama hiyo ya wakati. Msemo mmoja wa Kihispania hutabiri kwamba kufikia Machi 15 wimbo wa kijumbamshale utasikika tena.
Katika Kizio cha Kaskazini, watu wa mashambani sikuzote wamekaribisha kurudi kwa kijumbamshale, kitangulizi cha kidesturi cha msimu wa jua. Lakini watu fulani wadadisi pia walijiuliza mahali walipokuwa wakati wa kipupwe. Wengine walifikiri kwamba walikuwa katika usingizi wa kupisha majira. Wengine walidokeza kwamba walikuwa wameenda mwezini—mtu fulani alipiga hesabu kwamba ndege hao wangeweza kupuruka hadi mwezini kwa miezi miwili. Askofu mkuu Msweden wa karne ya 16 alidai kwamba vijumbamshale hukaa chini ya maji wakati wa kipupwe, wakiwa wamejikusanya pamoja chini ya maziwa na mabwawa. Maoni yake hata yalikuwa na picha iliyoonyesha mvuvi akivuta jarife lililojaa vijumbamshale. Ingawa dhana hizi zaonekana kuwa za ajabu wakati huu, ukweli ulikuja kushangaza kama hadithi yenyewe.
Katika karne hii wastadi wa ndege wametia alama maelfu ya vijumbamshale. Asilimia ndogo lakini yenye umaana ya ndege hawa waliotiwa alama walipatikana katika makao yao ya wakati wa kipupwe. Ingawa inashangaza mno, vijumbamshale kutoka Uingereza na Urusi walipatikana wakitumia wakati wa kipupwe wakiwa pamoja maelfu ya kilometa mbali na nyumbani—katika ncha ya mbali mno ya kusini-mashariki mwa Afrika. Baadhi ya wenzao wa Amerika ya Kaskazini hupuruka mbali mno kufikia Argentina au Chile. Na si vijumbamshale peke yao hufunga safari hizo kubwa sana. Mamia ya mamilioni ya ndege kutoka Kizio cha Kaskazini hutumia wakati wa kipupwe katika Kizio cha Kusini.
Wastadi wa ndege walishangazwa kugundua kwamba ndege mdogo kama vile kijumbamshale aweza kufunga safari ya kuzunguka kilometa 22,500 kabla ya kurudi kwenye kiota kilekile msimu wa jua ufuatao. Kujua walikokwenda vijumbamshale kulitokeza tu maswali yenye kutatanisha zaidi.
“Kijumbamshale, kwa Nini Wewe Huacha Kiota Chako?”
Ni nini kinachofanya ndege asafiri hadi mwisho ule mwingine wa tufe? Au, kulingana na msemo wa Kihispania, “Kijumbamshale, kwa nini wewe huacha kiota chako?” Je, ni kwa sababu ya baridi au ili kutafuta chakula? Bila shaka, uhitaji wao wa ugavi wa chakula wenye kutegemeka ndio jibu badala ya kuanza kwa halihewa yenye baridi, kwa kuwa ndege wengi wadogo ambao wana tatizo kuokoka vipupwe vyenye baridi hawahami. Lakini uhamaji wa ndege si kuzurura tu kwa kutafuta chakula. Tofauti na wahamaji wa kibinadamu, ndege huhama iwe nyakati ni mbaya au la.
Wanasayansi wamegundua kwamba ni mchana mfupi unaosababisha hamu ya kuhama. Wakati wa vuli ndege waliozuiliwa hukosa kutulia sana sana wakati mchana unapokuwa mfupi. Ndivyo ilivyo hata nuru itokezwapo na ndege hao wanapolelewa na wachunguzaji. Ndege aliyewekwa kizimbani hata hugeuka upande ambao anajua kisilika anapaswa kuelekea wakati wa uhamaji. Bila shaka, msukumo wa kuhama katika wakati hususa wa mwaka na katika upande hususa ni wa kiasili.
Ndege husafirije mbali mno kwa mafanikio? Wengi huhama kwa kuvuka bahari kuu na majangwa yasiyo na alama, nao hufanya hivyo usiku na mchana. Katika aina fulani ya ndege, ndege wadogo husafiri peke yao bila msaada wa ndege waliokomaa na wenye uzoefu. Hata hivyo wanabaki katika njia yao licha ya dhoruba au upepo wa kando.
Safari—hasa kuvuka bahari au majangwa makubwa mno—si rahisi hata kidogo. Ilimchukua mwanadamu maelfu ya miaka ili kuweza kujua sawasawa. Bila shaka, Christopher Columbus hangesafiri kamwe mbali sana kuvuka bahari bila misaada ya kusafiri baharini kama vile dira ya kisumaku au ya astrolabe.a Hata hivyo, kuelekea mwisho wa safari yake ya kwanza, ni ndege waliomwonyesha njia ya kwenda Bahamas. Kufuatia desturi ya wanamaji wa kale, yeye aligeuza mwendo wake kuelekea kusini-magharibi alipoona ndege wa bara wenye kuhama wakipuruka kuelekea upande huo.
Safari yenye mafanikio yahitaji mfumo wa kudumisha mwendo usiobadilika na pia njia ya kujua mahali ulipo. Kwa usahili, unahitaji kujua mahali ulipo kwa uwiano na mahali unakoenda na ni upande upi utaelekea ili kufika huko. Sisi binadamu hatujatayarishwa ili kushughulikia kazi hiyo bila vyombo—lakini ndege kwa wazi wako hivyo. Kwa subira, wanasayansi wamekusanya habari zinazoeleza jinsi ndege hujua upande ulio sawa wa kupuruka.
Baadhi ya Majibu
Hua wa nyumbani ndio “hufanyiwa utafiti” na wanasayansi walioazimia kuvumbua mafumbo ya usafiri wa ndege. Hua wenye ustahimilivu wamewekewa “miwani” ya kioo kisichoona vizuri ili wasione alama hususa za bara. Wengine wamewekewa vitu vya kisumaku ili kuwazuia kutumia ugasumaku wa dunia kwa ajili ya mwongozo. Wengine hata walileweshwa walipokuwa wakisafiri kuelekea kituo chao cha kuachiliwa, ili kuhakikisha kwamba hawakuwa na namna ya kujua njia. Hua hao wenye njia nyingi walishinda kila kizuizi peke yacho, ingawa kuunganishwa kwa vizuizi fulani kuliwazuia kurudi nyumbani kwa mafanikio. Kwa wazi, ndege hawategemei njia moja tu ya usafiri. Ni njia zipi nyingine wanazotumia?
Majaribio kwa kutumia jua na anga bandia la usiku yanaonyesha kwamba ndege wanaweza kusafiri kwa jua wakati wa mchana na kwa nyota wakati wa usiku. Namna gani ikiwa anga limefunikwa? Ndege wanaweza pia kuanzisha njia kwa kutumia ugasumaku wa dunia, kama kwamba walikuwa na dira ya ndani ya mwili. Ili kurudi kwenye kiota au makao yale yale, lazima waweze kukumbuka alama za bara wanazozifahamu. Isitoshe, watafiti wamepata kwamba ndege ni wepesi sana kugundua sauti na harufu kuliko binadamu—ingawa hawajui ni kwa kiwango gani uwezo huu hutumiwa kwa usafiri.
Lile Fumbo la “Ramani ya Ndege”
Ingawa utafiti wote huu umekuwa wenye msaada kuelekea kujua jinsi ndege wanaweza kupuruka katika upande maalum, tatizo lenye kusumbua bado labaki. Ni rahisi kuwa na dira yenye kutegemeka, lakini kufika nyumbani, wahitaji pia ramani—kwanza kujua mahali ulipo na kisha kutafuta njia bora zaidi ya kurudi.
Ni “ramani [zipi] za ndege” ambazo ndege hutumia? Je, wao hujuaje mahali walipo baada ya kupelekwa mahali pasipojulikana mamia ya kilometa kutoka nyumbani? Wao hupambanuaje njia bora zaidi, ilhali hawana ramani au nguzo za ishara za kuwaongoza?
Mwanabiolojia James L. Gould asema kwamba “hisi ya ramani [ya ndege] yaonekana hudumisha hali yayo ya kuwa fumbo lisiloweza kujulikana na lenye kushangaza katika tabia ya mnyama.”
Akili Itokezayo Hilo Fumbo
Jambo lililo wazi sana ni kwamba uhamaji ni tabia ya kisilika. Aina nyingi za ndege wamepangwa kiasili ili kuhama katika nyakati hususa za mwaka, na wanaanguliwa na huo uwezo na hisi zinazohitajika kusafiri kwa mafanikio. Uwezo huo wa kisilika ulitoka wapi?
Kiakili, hekima hii ya kisilika ingeweza kutoka tu kwa Muumba mwenye hekima, ambaye angeweza “kupanga” msimbo-jeni wa hao ndege. Mungu alimwuliza waziwazi mzee wa kale Ayubu hivi: “Je, mwewe hujifunza kutoka kwako jinsi ya kupuruka anaponyoosha mabawa yake kuelekea kusini?”—Ayubu 39:26, Today’s English Version.
Baada ya miaka mia moja ya utafiti mkali kuhusu uhamaji wa ndege, wanasayansi wamekuja kustahi bongo ndogo mno za ndege. Baada ya kupata njia kuu za kuhama, wanasayansi hushangaa tu na umbali wenye kustaajabisha ambao ndege husafiri. Kizazi baada ya kizazi, wakati wa msimu wa jua na wa vuli, mamilioni ya ndege wahamaji husafiri kuzunguka tufe. Husafiri kwa jua wakati wa mchana na kwa nyota wakati wa usiku. Wakati wa halihewa yenye mawingu wao hutumia ugasumaku wa dunia, na hujifunza haraka kutambua mandhari za bara wanazozifahamu. Yawezekana kwamba hata wanajifahamisha kwa harufu na mawimbi yasiyosikika na wanadamu.
Jinsi wanavyopanga ramani ya safari zao inabaki ikiwa fumbo. Twajua wanakoenda vijumbamshale wote; hatujui wanavyofika huko. Hata hivyo, tuonapo vijumbamshale wakiruka pamoja wakati wa vuli, tuwezacho tu ni kushangazwa na hekima ya Mungu aliyefanya uhamaji huu uwezekane.
[Maelezo ya Chini]
a Astrolabe ilitumika kupiga hesabu ya latitudo.
[Sanduku katika ukurasa wa 18]
Mabingwa wa Uhamaji Ulimwenguni
Umbali. Katika kiangazi cha kaskazini cha 1966, ndege aitwaye membe wa aktiki alitiwa alama katika North Wales, Uingereza. Katika Desemba wa mwaka huo huo, alionekana—kwa wakati ufaao—katika New South Wales, Australia. Alikuwa amepuruka zaidi ya kilometa 18,000 katika miezi sita. Tendo hilo yaelekea ni la kawaida kwa membe wa aktiki. Katika kipindi cha mwaka mmoja, baadhi ya ndege hawa huzunguka tufe kwa ukawaida.
Mwendo. Viluwiluwi-dhahabu wa Kiamerika labda ndio wahamaji wenye mwendo wa kasi kuliko wote. Baadhi ya ndege hawa wamevuka kilometa 3,200 za bahari inayotenganisha Hawaii na Visiwa vya Aleutian, Alaska, kwa muda wa saa 35 tu—kwa mwendo wa wastani wa kilometa 91 kwa saa!
Uvumilivu. Ndege aina ya pepeo wa Amerika Kaskazini, ambao wana uzito wa gramu 20 tu, ndio hupuruka mbali zaidi bila kutua. Kwenye safari yao kuelekea Amerika Kusini, wao hupuruka kilometa 3,700 bila kutua kuvuka bahari Atlantiki kwa siku tatu unusu tu. Mtihani huu wa uvumilivu usio wa kawaida umelinganishwa na mwanadamu kukimbia kilometa 1,900 bila kusimama kila kilometa kwa dakika nne. Huo mruko pia ni mradi wa watu wanaohangaikia kupunguza uzani wao—ndege huyo hupoteza uzani upatao nusu ya uzito wa mwili wake.
Kufuata Wakati. Zaidi ya kijumbamshale, koikoi (aliyeonyeshwa juu) pia ana sifa ya kufuata wakati. Nabii Yeremia alifafanua koikoi kuwa ndege ambaye “ajua nyakati zake zilizoamriwa” na ‘wakati wa kuja kwake.’ (Yeremia 8:7) Karibu koikoi nusu milioni hupitia Israeli kila wakati wa msimu wa jua.
Stadi za Kusafiri. Kwa ndege aina ya Manx shearwaters hakuna mahali palipo kama nyumbani. Ndege wa kike aliyetolewa kiotani mwake katika Uingereza aliachiliwa umbali wa kilometa 5,000 hivi katika Boston, Marekani. Ndege huyo alivuka Atlantiki kwa siku 12 1/2 na kufika nyumbani kabla ya kufika kwa barua yenye kupelekwa kwa ndege iliyokuwa na habari za kuachiliwa kwake. Matokeo yalikuwa yenye kushangaza hata zaidi kwa kuwa ndege hawa huwa hawavuki kamwe Atlantiki ya Kaskazini katika safari zao za uhamaji.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Koikoi hurudi kiotani mwake kwa wakati kila mwaka
[Picha katika ukurasa wa 17]
Taji wanaohama katika umbo la kawaida la V
[Habari kuhusu chanzo cha Picha Line katika ukurasa wa 15]
Picha: Caja Salamanca y Soria