Kuwatazama Ndege—Je, Kwavutia Kila Mtu?
“Maisha ya mtazamaji wa ndege yamejaa mshangao.” W. H. Hudson—The Book of a Naturalist.
KATIKA Ghuba ya Kosi, karibu na mpaka kati ya Afrika Kusini na Msumbiji, Keith, Evelyn, Jannie na kiongozi wao walitembea kwa kilometa 22 kuona ndege fulani. Huyo hakuwa ndege wa kawaida tu! Walikuwa wakitafuta aina fulani ya tai-mzoga—ndege mkubwa mwenye rangi nyeusi na nyeupe aliye na rangi nyekundu kuzunguka macho na uso mweupe. Yeye hula samaki waliokufa na machikichi.
Keith asimulia: “Baada ya kutembea kwa muda mrefu, tulirudi nyumbani tukiwa tumevunjika moyo kwa kuona tu tai-mzoga mmoja—na isitoshe tulimwona kwa umbali akipuruka. Tukapata nini tulipofika kambi yetu? Tai-mzoga watatu wakiwa wametua kwenye mchikichi juu yetu! Tukafurahia kuwatazama kwa karibu nusu saa kabla ya wao kuondoka, wakitupa wonyesho wa ajabu, mabawa yao yakiwa yamepanuliwa. Siku iyo hiyo, pia tuliona bundi-mvuvi kwa mara ya kwanza. Ndiyo, bundi avuaye samaki!”
Kwasisimua Mtu Yeyote
Ulimwenguni pote, ndege ni warembo kwa kutazama na kuvutia kuwasikia. Zile aina 9,600 za ndege, hutokeza fursa nyingi kwa mtazamaji yeyote aliye makini kuwatazama. Ni nani hasisimuliwi kuona ndege-mvumi au chopoa mwenye rangi nyangavu akipita? Ni nani asiyetua anaponaswa na nyimbo za ndege-mwigo, ndege aina ya kinega au sauti dhahiri ya mlemba au sauti kama muziki ya Australian magpie?
Kutazama ndege ni kuwatazama ndege wa mwituni. Kunaweza kuhusisha mambo mengi kulingana na jinsi utakavyo. Huenda usiwe na tamaa ya kupitia mabwawa au kupanda milima ili kuwatafuta ndege walio nadra kuonekana. Hata hivyo, watu wengi huridhika na kuburudika kwa kuwatazama ndege katika bustani yao. Wengi huweka maji na kitu cha kulisha ndege ili kuvutia ndege wa eneo lao. Kila mwaka watazamaji wa ndege huongezeka. Watu wanaozidi kuongezeka huamini kwamba kuwatazama ndege hunufaisha.
Kwa Nini Kunapendwa Sana?
Kulingana na kitabu An America Challenged, cha Steve H. Murdock, kati ya miaka ya 1990 na 2050, idadi ya watu wenye kutazama ndege inatarajiwa kuongezeka kwa kiwango cha haraka zaidi kuliko idadi ya watu wa Marekani. Gazeti New Scientist laripoti kwamba “watu wengi zaidi katika India wanaanza kupenda kuwatazama ndege.” Na Gordon Holtshausen, ambaye ni mwenyekiti wa Publications Committee of BirdLife South Africa, aamini kwamba “nchini Afrika Kusini . . . vitabu juu ya [ndege] vinauzwa zaidi ya vitabu vingine ila Biblia.”
Mara ufurahiapo kuwatazama ndege, utanaswa! Kuwatazama ndege huambukiza. Kwaweza kuwa tafrija isiyo ghali ambayo inakupeleka nje kwenye nyanja na kutahini akili yako. Kunavutia kama vile kuwinda lakini bila wewe kuua chochote. Kwa kuwa watoto na watu wazima hukuzoea kwa urahisi, kunaweza kufurahiwa na familia au pamoja na marafiki. Hata unaweza kukufurahia ukiwa peke yako. Kuwatazama ndege ni kipitisha-wakati kizuri na kunaweza kufanywa mwakani mahali popote.
Mambo ya Msingi ya Kuwatazama Ndege
Je, nyakati nyingine wewe huona ndege na kujiuliza anaitwaje? Mtu huridhika ajifunzapo majina ya ndege wakubwa kama tai, tausi, na bata-maji na vilevile kujua majina ya ndege wa kawaida tu kama vile kipasuasanda na ndege wa vichakani. Pia kuna chamchanga wenye kufanana, na vilevile pepeo na ndege wengine wenye kufanana na hao.a
Ili kuwatambulisha, utahitaji kitabu cha ndege wa nchi yenu au eneo lenu. Hicho ni kitabu kidogo chenye picha na ufafanuzi wa ndege wa kiume na wa kike wa kila aina. Vitabu bora hutia ndani pia manyoya ya ndege wachanga na manyoya yanayokuja na majira.
Ni nini pia ambacho mtazamaji mpya wa ndege ahitaji? Darubini nzuri ni muhimu kwa mtazamaji wa ndege kama vile ndoana au wavu ilivyo muhimu kwa mvuvi. Utashangaa kwa mambo mengi yaliyo katika ndege wa eneo lenu unapowaona kupitia darubini. Kwa mfano, katika Afrika kiboko hawezi kukosa kuonekana kwa sababu ya ukubwa wake. Lakini usipotumia darubini, huenda usimwone mla-kupe anayekula wadudu akiwa amening’inia kwenye mgongo wa kiboko.
Si darubini zote zimekusudiwa kuwatazama ndege, na njia bora ni kulinganisha ubora wa darubini kadhaa. Miongoni mwa watazamaji wa ndege, aina mbili za darubini zipendwazo ni 7 x 42 na 8 x 40. Tarakimu ya kwanza (7 au 8) inarejezea uwezo wa kukuza kitu, na tarakimu ya pili (42 au 40) yarejezea kipenyo cha lenzi kubwa kwa kipimo cha milimeta. Gazeti Field Guide to the Birds of North America cha National Geographic chaeleza kwamba “uwiano wa 1-5 kati ya uwezo wa kukuza vitu na ukubwa wa lenzi kwa ujumla huonekana kufaa kwa sababu ya uwezo wake wa kukusanya nuru.” Hiyo yakuwezesha kuona rangi hata wakati wa gizagiza kidogo. Hivyo, uwezo mkubwa wa kukuza si lazima uwe bora. Kile unachotaka ni kuona kwa wazi zaidi.
Tuanzie Wapi? Ujirani Wako
Mtu ajuaye ndege walio katika ujirani wake atakuwa katika hali njema zaidi ya kusafiri sehemu nyingine kuwatafuta ndege ambao si wa kawaida sana au wasioonekana sana. Je, unajua ni ndege gani walio wakazi wa daima katika eneo unaloishi? Ni ndege gani ambao hupitia hapo ambao huonekana kana kwamba hawatui, labda wakielekea kwenye ziwa au bwawa lililo karibu? Ni ndege gani wenye kuhama ambao hupitia hapo wakati wa safari zao za msimu? Katika kitabu The Birdwatcher’s Companion, Christopher Leahy aliandika: “Katika Amerika Kaskazini [uhamaji] huhusisha karibu asilimia 80 ya aina zipatazo 645 za ndege.”
Baadhi ya wahamaji hao waweza kutua karibu na kwenu ili kula na kupumzika. Wapenzi wa utazamaji wa ndege katika maeneo fulani wametambulisha zaidi ya aina 210 za ndege kwenye bustani zao! Kwapendeza na kuelimisha kuweka orodha ya tarehe ambapo wewe huona aina fulani za ndege kwa mara ya kwanza na kwa mara ya mwisho kila mwaka.
Njia za Kuwatazama Ndege
Ukiwa na darubini na kitabu cha ndege, sasa uko tayari kuchunguza ndege wasio karibu na kwenu. Orodha za ndege wanaoonekana hupatikana mara nyingi katika mbuga na hifadhi za wanyama. Orodha hizo huonyesha ni misimu gani aina fulani za ndege huonekana huko na uwezekano wa wewe kuwaona. Orodha hiyo itakuwa chombo muhimu cha kuthibitisha ndege ambao umewaona. Ikiwa ndege ambaye umetoka kumwona anaorodheshwa kuwa aliye nadra kuonekana, basi ingekuwa vizuri kumchunguza, hasa ikiwa wewe ni mgeni kwa mambo hayo. (Ona sanduku “Mwongozo wa Msingi wa Kuwatambulisha Ndege.”) Kwa upande mwingine, ikiwa ameorodheshwa kuwa anapatikana kwa wingi, basi yaelekea umemtambulisha vizuri.
Jaribu kupata ramani mapema inayoonyesha njia na mazingira ambayo utapata. Mara nyingi kuna ndege wengi mahali mazingira mawili yakutanapo. Ukitembea au ukibaki tu mahali pamoja, jaribu kujipatanisha na mazingira, halafu ungoje ndege hao waje kwako. Uwe mwenye subira.
Katika sehemu fulani kuna nambari ya simu ambayo wapenzi wa kutazama ndege waweza kupiga na kusikilizia ripoti zenye kupendeza za ndege walioonekana hivi karibuni katika eneo hilo.
Kujitayarisha Mapema Hunufaisha
Utathawabishwa ukiwa na lengo la kuwatazama ndege fulani hususa, lakini inafaa kusoma kabla ya wakati huo juu ya ndege ambao ungependa kuwaona. Kama upo Karibea, labda umeazimia kumwona detepwani wa huko, awe ni aina ya Kuba, ya Puerto Riko, au ya Jamaika. Yeye ni ndege mdogo mzito mwenye kuvutia sana aliye na manyoya ya rangi za kijani na nyekundu zenye kumetameta. Kitabu Guide to the Birds of Puerto Rico and the Virgin Islands cha Herbert Raffaele chatuambia kwamba “ni vigumu kumwona, lakini yeye husikika mara nyingi.” Wale detepwani wa Kuba wamejulikana kwa hamu yao kubwa ya kula na uharaka ambao wao huwalisha makinda yao. Baada ya kufafanua njia ya ndege huyo ya kulisha, Raffaele atoa shauri hili: “Kugonganisha mawe mawili huwavutia mara nyingi.”
Huenda ukataka kuzuru mahali pa mambo ya asili ili uweze kuona tukio fulani katika maisha ya aina fulani ya ndege, kama vile kuruka kwa njia yenye kuvutia angani kwa woodcock mapema katika masika. Au yaweza kuwa kuyu wengi ajabu katika Gibraltar au Bosporus wakijitayarisha kwenda Afrika wakati wa vuli. Au uhamaji wa ndege juu ya Israel.
Ni kweli kwamba kupanga kupata ndege fulani wa kipekee si kama kuzuru mahali fulani pa ukumbusho ambapo unajua papo pindi zote. Ndege huhama daima. Wao ni wachangamfu. Wao hutofautiana. Wao hustaajabisha. Lakini kunathawabisha kuwatafuta na kuwangoja!
Hayo yote ndiyo hufanya kuwatazama ndege kupendeze. Japo mpango wako, huenda ndege wasiwepo wakati unapoenda kuwatazama—angalau si ndege ambao unatamani kuwaona. Lakini hakuna mtu awezaye kujua mambo uwezayo kugundua huko. Jambo la hakika ni kwamba ndege hawawezi kukuvunja moyo kamwe. Uwe tu mwenye subira. Ufurahie kuwatazama! Na usisahau Muumba wao!—Mwanzo 1:20; 2:19; Ayubu 39:13-18, 27-29.
[Maelezo ya Chini]
a Ndege wamegawanywa katika sehemu nane kuu: (1) waogeleaji—bata na jamii yake, (2) ndege wa kupaa juu angani—shakwe na jamii yake, (3) ndege wa kutembea majini wenye miguu mirefu—kulasitara na korongo, (4) ndege wadogo-wadogo wa kutembea majini—kiluwiluwi na chamchanga, (5) ndege wa jamii ya kuku—kanga na kware, (6) ndege wawindaji—mwewe, tai, na bundi, (7) ndege wenye kutulia mitini, na (8) ndege wa bara wasiotulia mitini.—A Field Guide to the Birds East of the Rockies, cha Roger Tory Peterson.
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
Mwongozo wa Msingi wa Kuwatambulisha Ndege
Mara ya kwanza utazamapo ndege asiye wa kawaida, huenda likawa jambo lenye msaada kujaribu kujibu baadhi ya maswali yafuatayo:
1. Ndege huyo ana rangi za aina gani—rangi moja, milia, au madoa? 2. Ndege huyo yuko katika mazingira ya aina gani—maji, bwawa, konde la nyasi au msitu?
3. Ndege huyo anatoshanaje? Linganisha na ndege unaowafahamu—shorewanda, njiwa au mwewe.
4. Ndege huyo ana tabia zipi—hufuata-fuata wadudu, hupaa juu, hutikisa mkia, huweka mkia juu au chini, au hutembea ardhini?
5. Mdomo wake una umbo gani—mfupi na wenye ncha kali, mfupi na mzito, mrefu au umepindwa?
Kwa kutazama “alama” hizo na kurejezea kitabu cha msingi cha ndege, hata mtu asiye na ujuzi wa kuwatazama ndege aweza kutambulisha ndege wa kawaida.—Exhibit Guide, Merrill Creek Reservoir, New Jersey, Marekani.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Michoro ya ndege kwenye ukurasa wa 23-27: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 24, 25]
BATA BUKINI
Amerika Kaskazini
NDEGE-MVUMI
Amerika Kaskazini na ya Kati
KUNGURU MREMBO
Amerika Kaskazini
KASUKU
Amerika ya Kati na Kusini
TAI WA MAREKANI
Amerika Kaskazini
CARDINAL
Amerika Kaskazini na ya Kati
MWARI
Mabara na Visiwa vya Amerika
TAI
Afrika, Asia
TOUCAN
Amerika Kusini
KWARARA-MWEKUNDU
Amerika Kusini
SHAKWE
Mabara na Visiwa vya Amerika
YANGEYANGE-MKUU
Ulimwenguni pote
CHAFFINCH
Ulaya, Afrika Kaskazini
BATA-MANDARIN
China
KORONGO
Ulaya, Afrika, Asia
HEROE
Nchi za Kitropiki
TAJI
Afrika
GOULDIAN FINCH
Australia
KOOKABURRA
Australia
TAUSI
Ulimwenguni pote
MBUNI
Afrika
ROSELLA
Australia
[Hisani]
U.S. Fish and Wildlife Service, Washington, D.C./Glen Smart▸
Courtesy of Green Chimney’s Farm
Courtesy of San Diego Wild Animal Park
Ramani: The Complete Encyclopedia of Illustration/ J. G. Heck
Courtesy of San Diego Wild Animal Park