Ushindi wa Wachache Katika Bara la Usawa
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAPANI
KAMERA saba za televisheni na vilevile maripota wengi walikuwa wakimngoja mlalamishi mchanga aje mbele ya Shirika la Utangazaji Habari la Mahakama Kuu ya Osaka ambapo Kunihito Kobayashi mwenye umri wa miaka 19 na wazazi wake waliingia chumba cha mazungumzo wakiwa na tabasamu pana nyusoni mwao. Vimweko vya kamera viliwaka mara kwa mara chumbani walipokuwa wakijibu maswali ya maripota.
“Ninafurahi sana kuwa nilipata hukumu isiyopendelea kwa kesi yangu,” akasema Kunihito. “Ningependa kuona ulimwengu ambapo mtu yeyote anaweza kukubaliwa, kupandishwa darasa, na kufuzu kutoka shule yoyote ya sekondari licha ya itikadi zake za kidini.”
Mahakama Kuu ya Osaka ilikuwa imetangua uamuzi wa Mahakama ya chini ya Wilaya ya Kobe na kumpa Kunihito kile alichokuwa akitafuta, haki ya kupata elimu licha ya itikadi zake za kidini.
Lile Suala
Kile kilichokuwa kikizozaniwa katika mashtaka hayo kilikuwa kufukuzwa kutoka Chuo cha Ufundi wa Viwanda cha Manispaa ya Kobe (kiitwacho kwa kifupi Kobe Tech) kwa kutoshiriki katika mazoezi ya kendo, (utumiaji upanga wa Kijapani) kwa sababu za kidini. Kufuatia uamuzi wa mahakama ya Osaka wa kuondoa hatua ya shule ya kumnyima kupelekwa kwa darasa la juu na kumfukuza, Kunihito alionyesha kutaka kwake kuendelea na mafunzo yake katika ustadi wa umeme. Miaka mitatu ya kwanza ya chuo hiki cha miaka mitano ni sawa na miaka mitatu ya shule ya sekondari.
Kobe Tech ilikuwa imesisitiza kwamba Kunihito ashiriki katika mazoezi ya kendo yakiwa somo la elimu ya mazoezi ya mwili. Hata hivyo, kwa sababu alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, dhamiri yake iliyozoezwa Kibiblia haikumruhusu kushiriki katika mazoezi ya mbinu za karate. Kwa maripota katika mahojiano na waandishi wa habari, Kunihito alifungua Biblia yake na kueleza msimamo wake hivi: “Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu. Taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.”—Isaya 2:4.
Kwa nini, basi, mwanafunzi mchanga aliamua kugeukia sheria ili kupata uhuru wa dini na haki ya kuelimishwa? Profesa Koji Tonami wa Chuo Kikuu cha Tsukuba alionelea hivi: “Kwaweza kuwa na vizuizi visivyotazamiwa vilivyowekwa dhidi ya imani ya waamini kama tokeo la ubaridi na ukosefu wa uelewevu.” Ingawa serikali au jamii huenda isikandamize dini kimakusudi, huenda kukawa na visa ambapo dini inakandamizwa bila kujua.
Kwa nini ‘vizuizi hivyo visivyotazamiwa’ viliwekwa juu ya haki ya wachache? “Kwa sababu jamii ya Kijapani imeheshimu mfumo wa kijamii unaolazimisha wachache wajipatanishe na walio wengi,” ajibu Profesa Hitoshi Serizawa wa Chuo Kikuu cha Aoyama Gakuin. Msongo wa kujipatanisha na jamii nzima ni wenye nguvu sana katika Japani.
Si rahisi kwa wachanga kuwa katika mifumo ya shule inayotenga wale ambao wako tofauti. Hata hivyo, hilo si jambo tu la hangaikio kwa wachache wafuatao dini. Ebu tufuatie hiyo kesi tangu mwanzo wayo na kuona ni nini kilichokuwa kizozanio na jinsi uamuzi huu unavyoathiri umma.
Kutambulisha Haki za Wachache
Kabla ya 1990, Kobe Tech haikulazimisha wanafunzi wayo kuchukua kozi ya mbinu za karate. Lakini baada ya kumalizika kwa jumba la mazoezi ya mwili lililokuwa na ukumbi wa mazoezi ya mbinu za karate, hiyo shule ilianza kulazimisha mazoezi ya kendo kwa wanafunzi wayo. Katika 1990 taaluma ya shule ya elimu ya mazoezi ya mwili ilichukua msimamo mgumu mno kuelekea Mashahidi wa Yehova walioingia Kobe Tech wakiwa na umri wa miaka 16. Walipoomba kutohusishwa katika mazoezi ya kendo, mwalimu mmoja alisema hivi: “Acheni shule ikiwa hamwezi kufanya kile mnachoambiwa na shule!”
Kwa vijana Mashahidi waliosimama imara kwa itikadi yao, taraja la kupandishwa kwenye darasa lifuatalo lilikuwa dogo sana. Mwalimu mwingine alisema hivi: “Hamtapata cheti hata mkitia bidii nyingi katika michezo mingine ya [elimu ya mazoezi ya mwili].” Wanafunzi watano walishikilia itikadi yao katika mafundisho ya Biblia kwa kutochukua upanga hata ikiwa ulitengenezwa kutokana na mwanzi. Watatu kati yao walikuwa Mashahidi wa Yehova waliobatizwa, na wawili hawakuwa wamebatizwa, lakini wote walihakikisha itikadi yao katika Biblia. Walikuwa tayari kukubali utendaji wowote wa badala ambao walimu wangewataka wafanye.
Kama tokeo la msimamo wao, hawakupandishwa darasa lililofuata. Mwaka wa shule uliofuata ulipoanza katika 1991, walimu wa elimu ya mazoezi ya mwili walikusanya hao wanafunzi watano waliokataa kushiriki katika mazoezi ya kendo na wapya tisa walioshiriki itikadi ileile na kusema hivi: “Mtalazimika kupata maksi za juu isivyo kawaida mkitaka kupandishwa hadi darasa lifuatalo. Haitawezekana hata kidogo kwa yeyote wenu kupata maksi hizo.” Hao walimu waliwaeleza zaidi hivi: “Hii si elimu ya lazima. [Katika Japani, elimu ya lazima ni kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha kwanza.] Twaweza kuwaambia ‘ondokeni hapa.’”
Hao wanafunzi watano waliwasilisha malalamiko yao mahakamani dhidi ya shule katika Mahakama ya Wilaya ya Kobe wakilalamika kwamba hatua ya shule ilivunja haki zao za kikatiba za uhuru wa kuabudu na kupata elimu. Wakati huo huo, wanafunzi hao watano waliomba Mahakama ya Wilaya ya Kobe na kisha Mahakama Kuu ya Osaka isimamishe kutekelezwa kwa hatua ya kukataa kupandishwa darasa ili waendelee kupata masomo huku kesi ikiendelea kusikiwa. Hata hivyo, maombi hayo yalikataliwa na mahakama zote mbili.
Wawili kati ya hao wanafunzi watano walinyimwa tena cheti chao cha elimu ya mazoezi ya mwili kwa mwaka wa shule uliofuata na wakatishwa kufukuzwa. Kama tokeo, mmoja wao akaacha shule aliposhurutishwa na shule. Yule mwingine alikataa kukubali dokezo la shule kwamba aache. Mwanafunzi huyo, Kunihito Kobayashi, alifukuzwa shuleni.
Kanuni za shule zilitaarifu kwamba mwanafunzi ambaye alianguka darasa mara mbili alipaswa kufukuzwa mara hiyo akiwa “mmoja ambaye ni hafifu katika kujifunza bila taraja la kufuzu.” Lakini je, Kunihito alikuwa “hafifu katika kujifunza?” Hata kutia ndani elimu ya mazoezi ya mwili, ambayo, kwa sababu ya suala la kendo alianguka kwa pointi 48 kwa 100, wastani wake wa masomo yote ulikuwa pointi 90.2. Yeye ndiye aliyekuwa juu kabisa ya darasa lake la wanafunzi 42! Alikuwa mwenye mwenendo mwema na mwenye nia ya kujifunza.
Maombi yalifanywa kwa Mahakama ya Wilaya ya Kobe na kisha kwa Mahakama Kuu ya Osaka ili kusimamisha kutekelezwa kwa hatua ya kufukuzwa. Lakini mahakama zote zilikataa ombi hilo.
Uamuzi wa Mahakama ya Wilaya
Februari 22, 1993, karibu miaka miwili baada ya hao wanafunzi watano kupeleka malalamishi mahakamani, Mahakama ya Wilaya ya Kobe ilitoa uamuzi wayo kwa kupendelea shule. “Haiwezi kukataliwa kwamba uhuru wa kuabudu wa walalamishi ulizuiwa na agizo la shule la kushiriki katika mazoezi ya kendo,” akakiri hakimu msimamizi, Tadao Tsuji. Lakini akamalizia kwamba “hatua zilizochukuliwa na shule hazikuasi katiba.”
Wanafunzi mara moja wakakata rufani kwa Mahakama Kuu ya Osaka. Hata hivyo, uamuzi wa mahakama ya wilaya, ulisumbua watu wengi wenye akili yenye kufikiri. Mtu mmoja alijieleza katika safu ya wasomaji ya gazeti la habari Mainichi Shimbun na kusema hivi: “Uamuzi wakati huu ulitegemea hukumu kwamba ‘kuvumilia kutoshiriki katika masomo ya kendo kwa misingi ya kidini huvunja kutokuwamo kwa kidini.’ Hata hivyo, kutokuwamo humaanisha kutounga mkono sehemu yoyote katika pande mbili zinazozozana. Na inapokuja kwa kutokuwamo kwa kidini, suala ni kulinda imani ya wachache dhidi ya walio wengi. Kwa hivyo, uamuzi huu yaelekea wakataa uhuru wa dini, na mahakama yenyewe imevunja kutokuwamo kwa kidini.”
Wengi waliamshwa na wakaguswa moyo kutoa maoni yao. Dakt. Takeshi Kobayashi, profesa wa Katiba kwenye Chuo Kikuu cha Nanzan, alipeleka maoni yake juu ya kesi hii kwa Mahakama Kuu ya Osaka na kusema hivi: “Kesi hii inayobishaniwa kwa wazi inauliza mahakama za nchi yetu jinsi zitakavyoshughulikia tatizo la kulinda haki za wachache. . . . Hicho chuo, chini ya kisetiri cha utengano wa dini na Serikali na vilevile msimamo wa kutokuwamo wa elimu ya umma, kilikataa waziwazi kuvumilia msimamo wa kidini wa wachache kwa msingi wa maoni ya kawaida ya walio wengi. Uamuzi wa mahakama ya chini ulisifu vitendo kama hivyo kuwa vyenye kufuata sheria na vya kikatiba. Hata hivyo, hata ikiwa itikadi za wachache huenda zisieleweke kutokana na maoni ya kile kinachokubaliwa kwa kawaida kuwa cha kidini, ikiwa itikadi hizo ni zenye unyofu, lazima zistahiwe. Mahakama hasa yapaswa kuhukumu kwa utambuzi wa kuwa mteteaji mkuu wa wachache.”
Mtaalamu mwingine wa sheria, Profesa Tetsuo Shimomura wa Chuo Kikuu cha Tsukuba, alisema hivi: “Kinachoshangaza katika kesi hii ni maelekeo yaliyoko yaliyotia mizizi sana na yaliyo ya kikatili kwa upande wa shule.” Alisema katika mahoji ya televisheni kwamba inaonyesha kupungukiwa kwa upande wa waelimishaji kufukuza mwanafunzi bila kumpa hatua zozote za badala na inafunua ukosefu wa ufikirio kwa hali-njema ya wanafunzi.
Februari 22, 1994, Shirika la Wanasheria la Kobe lilifanya pendekezo rasmi kwa mwalimu mkuu wa Kobe Tech kumrudisha Kunihito. Lilitangaza kwamba hatua ya shule ya kumnyima Kunihito kupandishwa darasa na kumfukuza ilikuwa kuvunja uhuru wake wa kuabudu na haki yake ya kupata elimu.
Uamuzi Usiopendelea
Usikizi wa rufani ulipokuwa ukiendelea, wale walalamishi wanne kando na Kunihito waliamua kuachana na kesi yao. Hii ilikuwa kwa sababu walikuwa wamepandishwa darasa lililofuata na mmoja alikuwa amelazimishwa kuacha. Hili lilifanya hoja ya kubishaniwa juu ya namna shule ilivyoshughulika na Kunihito ielekezewe fikira.
Hata hivyo, wale wanne waliokuwa wanadarasa wenzi wa Kunihito, walimpa utegemezo wa kihisia kwa kujaribu kuwapo kila wakati wa usikizi wa kesi. Kwa kuweka akiba machumo yake madogo mno kutokana na kazi yake ya nusu wakati, yule mwanafunzi aliyelazimishwa kuacha shule alichanga jumla ya yen 100,000 ili kumsaidia Kunihito kupambana na pigano hilo la kisheria.
Desemba 22, 1994, Kunihito pamoja na wale wanafunzi wengine walingojea maneno ya Hakimu Mkuu Reisuke Shimada wa Mahakama Kuu ya Osaka.
“Uamuzi wa mwanzoni umeondolewa,” akaamua Hakimu Shimada.
Hakimu Shimada, katika uamuzi wake ulio wa maana sana, aliamua kwamba sababu ya Kunihito ya kukataa mazoezi ya kendo ilikuwa nyofu. Hakimu huyo alitaarifu kwamba ikiwa taasisi ya kielimu iliyo wazi kwa umma, Kobe Tech ina wajibu wa kutoa ufikirio wa kielimu kwa wanafunzi wayo. Yeye pia alitaarifu kwamba ubaya aliofanyiwa Kunihito kwa kukataa kufanya mazoezi ya kendo ulikuwa mkubwa sana na kwamba hatua ya kumfukuza ilikuwa hasa kumpokonya fursa yote ya kupata elimu.
Hakimu Shimada aliamua kwamba shule ilihitajika kuandaa hatua za badala. Kuandaa hatua hizo za badala, yeye alisema, si kuunga mkono au kusaidia dini ya mkata-rufani kamwe, wala hilo halikandamizi wanafunzi wengine. “Hakuna uthibitisho kwa upande wa Washtakiwa [shule] kwamba walifikiria kwa uzito hatua za badala,” hakimu huyo akataarifu. “Badala yake, . . . Washtakiwa walidumisha kwa shingo ngumu sera ya kutovumilia ukataaji wa mazoezi ya kendo na hata hawakuanza kufikiria kuandaa hatua za badala.”
Jinsi Uamuzi Huo Unavyokuathiri
Kwa nini upendezwe na ushindi huu wa kijana aliye wa kikundi cha wachache? Katika kitabu chake The Court and the Constitution, aliyekuwa wakili wa mashtaka wa pekee wa kesi za kashifa Archibald Cox aliuliza swali kama hilo, kuhusu Mashahidi wa Yehova katika suala la kusalimu bendera katika Marekani: “Kwa nini tuhangaikie uhuru wa kiroho wa wachache hao wadogo mno?”
Katika kujibu swali hili, Cox alisema hivi: “Sehemu ya jibu hutegemea kanuni ya hadhi ya mtu mmoja-mmoja ambayo juu yayo jamii yetu hukaa, hadhi ya wote wanaojipatanisha na wasiojipatanisha. Sehemu nyingine hutegemea utambuzi wa kwamba ikiwa Serikali yaweza kunyamazisha usemi wa Mashahidi wa Yehova. . . , usemi wetu huenda ukafuata kunyamazishwa.”
Profesa Takeshi Hirano wa Chuo Kikuu cha Ryukoku alikubaliana na Cox na kusema hili kuhusu kesi ya kendo: “Watu wanaofikiri huona kwamba wanawiwa uhuru wa kuabudu ambao watu wanafurahia sasa Marekani na Mashahidi wa Yehova ambao walipigania haki zao katika kesi nyingi za mahakamani. Katika nchi yetu [Japani] pia, inatumainiwa kwamba uhuru wa kuabudu utaanzishwa na kuendelezwa kupitia kesi kama hii.”
Mashahidi wa Yehova wamefanya wawezavyo katika kutetea itikadi zao kisheria, na wamechangia sana kuanzishwa kwa haki za msingi za kibinadamu katika karne ya 20. Katika nchi nyingi Mashahidi wa Yehova waliongoza vita vya kisheria wakitetea haki za wagonjwa za kutoa ruhusa ya tiba, haki za watu za kuamua jinsi ya kuonyesha staha kwa bendera ya taifa, na haki za mtu mmoja-mmoja za kueleza wengine itikadi zake za kidini. Ushindi katika Mahakama Kuu ya Osaka ni mwongezo wenye umaana katika rekodi ya kuchangia kwa Mashahidi wa Yehova kuanzishwa kwa haki za wachache.
Kustahi Wengine Walio na Viwango Tofauti
Kwa kuongezea manufaa ya kutetea haki za kibinadamu, lile suala la kuvumilia itikadi za wachache lina uhusiano na uhai wako katika njia nyingine. Profesa Kaname Saruya wa Chuo Kikuu cha Wanawake cha Komazawa alirejezea kesi hii na kusema hivi: “Uhuru wa dini unaotambuliwa na katiba ulipuuzwa kwa sababu tu ya [huyo mwanafunzi] kuwa tofauti na wengine. Kukataliwa kwa kile kilicho tofauti kumeenea sana katika Japani.”
Katika jamii ya leo msongo wa kuharibu kilicho tofauti, au kilicho tofauti na mwenendo wa kawaida, ni wenye nguvu sana. Uchokozi, ambao umeenea sana katika Japani na vilevile katika nchi nyinginezo, ni kielelezo cha huu mwelekeo wa kutenga kilicho tofauti na jamii. Akitoa maelezo kuhusu tatizo la wachokozi wa shule, Hiroshi Yoshino, supritenda msimamizi wa Metropolitan Police ya Tokyo, alisema kwamba kulingana na uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kitaifa wa Sayansi ya Polisi, sehemu yenye kushangaza ya sababu za kuchokoza wengine, kutoka kwa upande wa wenye kuchokoza wengine, ilihusisha tofauti za kiutu kati yao na waliowachokoza. Yeye alimalizia hivi: “Nafikiri jambo la maana lililofichika chini sana katika jamii ya Kijapani, lile la kukataa kile kisicho cha kawaida, au kile kilicho tofauti kimwili au kiakili, sasa lajitokeza.”
Mwelekeo wa kutenga kilicho tofauti na jamii unaonekana kila mahali, si tu katika Japani. Lakini uwezo wa kuvumilia viwango tofauti ndio ufunguo wa kuishi pamoja kwa amani. Kuhusiana na hili makala katika Asahi Shimbun ilitaarifu kwamba maamuzi ya Mahakama Kuu ya Kobe na Mahakama Kuu ya Osaka “yalitokeza tofauti iliyo wazi sana.” “Maamuzi hayo mawili,” likasema hilo gazeti la habari, “yaonekana kufananisha njia mbili za kufikiri,” moja ya ukatili wa usimamiaji na ile nyingine ya kuvumilia viwango tofauti.
Je, uko tayari kuvumilia viwango tofauti? Je, una nia ya kuangalia ukweli wa msimamo wa wengine? Kwa kupendeza, Archibald Cox, aliyetajwa mapema katika makala hii, aliongeza sababu nyingine ya hangaiko kuhusu wachache: “Sehemu iko katika utambuzi kwamba wachache wasio wa kawaida huenda wakagundua ukweli—ukweli uliowekwa kando au uliopotea milele kwa kukandamizwa.”
Kwa wazi, Kobe Tech haipendezwi na ukweli kwamba huenda walikandamiza, wala hawajaonyesha maoni ya kuvumilia. Badala yake, wamekata rufani kesi hiyo kwa Mahakama Kuu ya Japani. Mahakama Kuu itaamuaje kesi hiyo? Lazima tungojee tuone.
[Picha katika ukurasa wa 14]
Kunihito (katikati) na wale walalamishi wanne wa mbeleni