UKIMWI-Wanatiba Chukueni Tahadhari!
“WAFANYAKAZI wa kutunza afya wako katika hatari ya kupata HIV kutoka kwa wagonjwa walioambukizwa.” Onyo hili, kutoka Koleji ya Matibabu ya Afrika Kusini, limenukuliwa katika South African Medical Journal. Limetolewa baada ya vifo kadhaa vya wataalamu wa kitiba ambao wamekufa kutokana na maambukizo ya UKIMWI ya kiaksidenti.
Miongozo iliyokusudiwa kulinda wafanyakazi wa kutunza afya sasa yachukuliwa kwa uzito. Yafuatayo ni baadhi ya mambo makuu ya sera ya hiyo taarifa ya koleji kwa wafanyakazi wa kitiba ambao, katika harakati za kazi zao, huenda wakabili mtu mwenye HIV:
Katika hali isiyo ya dharura, iwapo mgonjwa atakataa kuchunguzwa UKIMWI katika damu, mfanyakazi wa kutunza afya ana idhini ya “kuachisha utunzi wa kitaaluma . . . baada ya kuzungumza na mgonjwa kikamilifu.” Onyo limetolewa kwamba katika hali ya dharura, wagonjwa wote wapaswa “kutibiwa kana kwamba ni wenye HIV.”
Katika nyongeza ya hiyo barua, orodha ndefu ya hatua za kutahadhari kimbele zimeorodheshwa. Kwa kielelezo, kuvaa glovu za mpira “unapogusa damu ama umajimaji wa mwili, kiwamboute, ama sehemu yoyote iliyochubuka ya ngozi . . . , unaposhika vifaa ama sehemu zenye damu ama umajimaji wa mwili . . . , unapofanya taratibu ambazo katika hizo mikono itaelekea kugusa damu.” Wafanyakazi wa kutunza afya pia wameshauriwa “kuvaa visetiri vya uso na macho ili kujilinda wakati wa taratibu zielekeazo kutokeza kutonatona kwa damu ama umajimaji wa mwili.”
Nusu nzima ya sehemu moja ya hilo jarida imetengwa ili kutoa maonyo kwa wafanyakazi wa kutunza afya dhidi ya kubeba sindano zikiwa wazi ama kuacha vifaa vikali vilivyotumika vikiwa ovyo-ovyo. Hata kule “kupitisha vifaa vyenye ukali moja kwa moja kati ya wafanyakazi katika chumba cha upasuaji” wakati wa upasuaji mbalimbali wapaswa kuepukwa. Zaidi ya hilo, yashauriwa kwamba “violezo vyote vya damu ama umajimaji wa mwili vyapaswa kuwekwa katika viwekeo thabiti visivyovuja” na kwamba hivi vyapaswa kupelekwa tu katika “mfuko wa plastiki ama kiwekeo kisichopenyezea maji.”
Iwapo mfanyakazi wa kutunza afya atapatwa na hiyo virusi ama kupitia kifaa chenye makali kilichochafuliwa na damu kikisababisha jeraha ama kupitia damu inapogusa sehemu iliyochubuka, hatua ya haraka yahitajiwa. Hiyo barua yasema hivi: “Mfanyakazi wa kutunza afya apaswa kuchunguzwa HIV mara anapopatwa, na tena baada ya majuma 6, majuma 12 na miezi 6. Wakati wa kipindi hicho hatua maalumu za tahadhari zapaswa kuchukuliwa ili kuzuia kupitisha kingono kwa mwenzi wake.”
Hatua hizi zaonyesha mwelekeo wenye kukua kwa upande wa wafanyakazi wa kitiba walioeleweshwa kuelekea tahadhari kubwa katika utumiaji na ushughulikiaji wa damu.