Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/8 kur. 4-7
  • Ukimwi—Jinsi ya Kupigana Nao

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ukimwi—Jinsi ya Kupigana Nao
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Siri za Kuuzuia
  • Wakati wa Kupimwa
  • Elimu Yaweza Kusaidia Jinsi Gani?
  • Unaweza Kuchagua Matibabu Gani?
  • Je, Chanjo Ndilo Suluhisho?
  • Mafanikio Katika Pambano Dhidi ya UKIMWI
    Amkeni!—2004
  • UKIMWI Waenea Katika Afrika
    Amkeni!—2002
  • Dawa ya UKIMWI Yahitajiwa Upesi!
    Amkeni!—2004
  • Naweza Kuepukaje Kupata UKIMWI?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/8 kur. 4-7

Ukimwi—Jinsi ya Kupigana Nao

KUFIKIA wakati huu UKIMWI hauna tiba, na sayansi ya kitiba haielekei kupata tiba moja hivi karibuni. Ingawa matibabu mapya huzuia maendeleo ya haraka ya maradhi haya, ni vizuri zaidi kuepuka kuambukizwa. Hata hivyo, kabla hatujazungumzia kuuzuia, acheni tufikirie jinsi kirusi cha UKIMWI (HIV) kinavyopitishwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine na jinsi kisivyopitishwa.

Mtu aweza kuambukizwa katika njia nne za msingi: (1) kwa kutumia sindano iliyochafuliwa, (2) kwa kufanya ngono (ya uke, ya mkundu, au ya mdomo) pamoja na mtu aliyeambukizwa, (3) kwa kutiwa damu mishipani na umajimaji wenye damu, ingawa tisho hili limepungua katika nchi zilizoendelea zaidi ambapo damu huchunguzwa kama ina HIV, na (4) mama aliyeambukizwa HIV, awezaye kumwambukiza mtoto kabla ya kumzaa au wakati wa kumzaa au anapomnyonyesha.

Kulingana na Vitovu vya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi vya Marekani (CDC), uthibitisho wa sayansi wa kisasa wasema kwamba (1) huwezi kupatwa na UKIMWI kwa njia ambayo ungeshikwa na mafua au homa, (2) huwezi kupatwa nao kwa kuketi kando ya mtu aliye na UKIMWI au kwa kugusa au kukumbatia mtu aliyeambukizwa, (3) huwezi kupatwa nao kwa kula chakula kilichotayarishwa na kuandaliwa na mtu aliyeambukizwa, na (4) huwezi kupatwa nao kwa kutumia pamoja vyoo, simu, mavazi, au vyombo kama sahani na vikombe. Isitoshe, kitovu cha CDC chasema kwamba kirusi hicho hakipitishwi na mbu au na mdudu yeyote.

Siri za Kuuzuia

Virusi vya UKIMWI hujificha katika damu ya watu walioambukizwa. Mtu aliyeambukizwa anapodungwa sindano, kiasi fulani cha damu pamoja na virusi chaweza kubaki kwenye sindano hiyo. Hivyo mtu mwingine akidungwa sindano hiyohiyo iliyo na uchafu, kirusi hicho kingeweza kupitishwa. Usiogope kamwe kumwuliza daktari au muuguzi kuhusu sindano unapokuwa na shaka. Una haki ya kujua; maisha yako yamo hatarini.

Virusi vya UKIMWI hupatikana pia katika shahawa au umajimaji unaotoka kwenye sehemu za uke za watu walioambukizwa. Hivyo, kuhusu kuuzuia, kitovu cha CDC chapendekeza: “Njia iliyo salama zaidi ya kujilinda ni kutofanya ngono. Ikiwa utafanya ngono, subiri mpaka utakapokuwa na uhusiano wa muda mrefu, wenye uaminifu kati ya wote wawili, kama vile ndoa, pamoja na mwenzi ambaye hajaambukizwa.”

Ona kwamba ili usiambukizwe, “uhusiano wa uaminifu kati ya wote wawili” wapaswa kudumishwa. Ukiwa mwaminifu na mwenzi wako akose kuwa mwaminifu, haujalindwa. Mara nyingi jambo hili hutokeza tatizo kubwa kwa wanawake wanaoishi katika jamii zinazotawaliwa na wanaume kingono na kiuchumi. Katika nchi fulani wanawake hawaruhusiwi kuzungumza juu ya ngono na wanaume, sembuse kujadiliana juu ya mazoea ya ngono yaliyo salama zaidi.

Hata hivyo, si wanawake wote wa namna hiyo wasiokuwa na mamlaka. Uchunguzi mmoja uliofanywa katika nchi moja ya Afrika Magharibi ulionyesha kwamba wanawake fulani wanaojitegemea kifedha, walifaulu kuwanyima ngono waume wao walioambukizwa bila kutendwa jeuri. Katika New Jersey, Marekani, wanawake fulani walikataa kufanya ngono ikiwa mwanamume hakutaka kuvalia kondomu. Bila shaka, ingawa kondomu za plastiki zaweza kuandaa kinga dhidi ya HIV na maradhi mengine yanayoambukizwa kingono, zapasa kutumiwa vizuri sana na wakati wote.

Wakati wa Kupimwa

Karen, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, hangeweza kufanya lolote ili kujilinda asiambukizwe. Mume wake aliambukizwa miaka kadhaa kabla ya ndoa yao, na walifunga ndoa wakati ugonjwa huo wa kuenea na kupimwa kwa ajili ya HIV ulipokuwa katika hatua za mwanzo-mwanzo. Hata hivyo, sasa, kupimwa kwa ajili ya HIV kumekuwa desturi ya kawaida katika nchi fulani. Kwa hiyo ikiwa mtu ana shaka lolote ikiwa ana HIV au la, litakuwa jambo la hekima kupimwa kabla ya kuanzisha uchumba. Karen ashauri hivi: “Chagua mwenzi wako wa ndoa kwa hekima. Chaguo baya laweza kukufanya uteseke sana na hata lifanye upoteze uhai wako.”

Kupimwa kwaweza kusaidia kulinda mwenzi asiye na hatia katika visa vya uzinzi. Kwa kuwa huenda HIV isidhihirike wakati wa kupimwa mpaka miezi sita ipite baada ya ambukizo, huenda ikawa lazima kupimwa mara nyingi. Mkianza kufanya ngono tena (hivyo ikionyesha kwamba mzinzi amesamehewa), kondomu yaweza kuandaa kinga dhidi ya ambukizo.

Elimu Yaweza Kusaidia Jinsi Gani?

Yafaa iangaliwe kwamba ingawa Biblia iliandikwa muda mrefu uliopita kabla ya UKIMWI kutokea, kuishi kwa kupatana na kanuni zake husaidia kuzuia maradhi hayo. Kwa kielelezo, Biblia hushutumu ngono nje ya ndoa, hudai uaminifu katika ndoa, na husema kwamba Wakristo wapaswa kufunga ndoa na wale tu wanaotumia kanuni za Biblia kama wao. (1 Wakorintho 7:39; Waebrania 13:4) Pia Biblia hukataza kila namna ya matumizi mabaya ya vitu vinavyouchafua mwili na matumizi ya damu, yanayouchafua mwili.—Matendo 15:20; 2 Wakorintho 7:1.

Ni jambo la hekima kujielimisha juu ya hatari zinazoweza kuhusika katika kushirikiana na watu walioambukizwa HIV. Kujifunza juu ya UKIMWI huwasaidia watu wajilinde dhidi yake.

Shirika la Kupambana na UKIMWI lasema: “Katika visa vingi UKIMWI waweza kuzuiwa. Mpaka tiba itakapopatikana elimu ndiyo ulinzi bora kwa [jumuiya] dhidi ya UKIMWI na ndiyo ulinzi wa pekee kwa wakati huu.” (Italiki ni zetu.) Ni vizuri wazazi wazungumze waziwazi kati yao na pamoja na watoto wao kuhusu UKIMWI.

Unaweza Kuchagua Matibabu Gani?

Kwa kawaida, dalili za maradhi haya mara nyingi hazionekani mpaka baada ya miaka sita hadi kumi baada ya mtu kuambukizwa HIV. Katika miaka hiyo kunakuwa na pigano kali ndani ya mwili. Kirusi kimoja-kimoja huongezeka na kuua chembe za mfumo wa kinga. Chembe za mfumo wa kinga hujipigania. Hatimaye, kwa kuwa mabilioni ya virusi vipya hutokezwa kila siku, mfumo wa kinga hushindwa kabisa.

Dawa za namna mbalimbali zimetokezwa kusaidia mfumo wa kinga, dawa zenye majina magumu zinazotambulishwa kwa herufi—AZT, DDI, na DDC. Ingawa wengine waliamini kwamba dawa hizi zingetokeza manufaa kubwa na hata kuweza kuponya, upesi matumaini hayo yaliambulia patupu. Dawa hizo hazipotezi tu uwezo wake baada ya muda lakini pia husababisha madhara hatari kwa watu fulani—kupunguka kwa chembe za damu, kasoro za kutoganda kwa damu, na kuharibiwa kwa neva za mikono na miguu.

Sasa aina mpya za dawa zimewasili: vizuia proteasi. Madaktari hutoa mchanganyiko wa dawa tatu hizi pamoja na dawa nyingine za kuzuia virusi. Majaribio yameonyesha kwamba ingawa hiyo tiba ya dawa tatu haiui virusi, hiyo huzuia, au inakaribia kuzuia virusi visiongezeke mwilini.

Tiba ya dawa tatu imetokeza maendeleo makubwa kwa afya ya wagonjwa. Hata hivyo, wataalamu wanaamini kwamba tiba hiyo hufanya kazi vizuri zaidi wakati watu walioambukizwa HIV wanapotibiwa nayo mapema, kabla dalili hazijaanza kujitokeza. Hilo lifanywapo, yawezekana kuzuia, labda kwa muda usio dhahiri, ambukizo lisizidi na kuwa UKIMWI. Kwa kuwa tiba hii ni mpya, baada ya muda itajulikana inaweza kuzuia ambukizo kwa muda mrefu kadiri gani.

Tiba hiyo ya dawa tatu ni ghali. Gharama ya wastani ya dawa za kuzuia virusi pamoja na kupimwa kwenye maabara ni dola 12,000 kwa mwaka. Mbali na gharama ya kifedha, mgonjwa anayetumia matibabu haya atahitaji kufunga safari nyingi kwenda kwenye friji, ambapo dawa hizi zapaswa kuwekwa. Kwa kawaida, mtu humeza tembe fulani mara mbili kwa siku na nyingine mara tatu kwa siku. Nyingine zapaswa kumezwa tumbo linapokuwa bila kitu, nyingine tumbo linapokuwa limejaa. Tiba huwa ngumu zaidi inapokuwa lazima dawa za ziada zitumiwe ili kupigana na maambukizo mengine mengi ambayo mgonjwa wa UKIMWI huathiriwa nayo kwa urahisi.

Madaktari wanahangaishwa sana na jambo linaloweza kutokea iwapo mtu ataacha kutumia tiba ya dawa tatu. Virusi vingeanza kuongezeka tena kwa nguvu ileile, na virusi ambavyo viliokoka tiba hiyo vyaweza kushinda nguvu dawa ambayo mtu alitumia hapo awali ili kupigana navyo. Uzao wa HIV usiotibika ungekuwa mgumu sana kutibu. Isitoshe, virusi hivi vyenye nguvu sana vingeweza kupitishwa kwa watu wengine.

Je, Chanjo Ndilo Suluhisho?

Watafiti fulani wa UKIMWI wanaamini kwamba ufunguo wa kukomesha ugonjwa wa UKIMWI unaoenea sana ni chanjo salama, yenye matokeo. Chanjo zinazofaulu dhidi ya homa ya kimanjano, surua, matubwitubwi, na surua ya Ujerumani zinatengenezwa kutokana na virusi vilivyodhoofishwa. Kwa kawaida, aina ya kirusi kilichodhoofishwa kinapoingizwa mwilini, mfumo wa kinga hautendi tu ili kukiharibu lakini pia hujenga kinga ambayo itapigana kwa mafanikio na kirusi chochote halisi kitakachouvamia mwili.

Majaribio mawili yaliyofanyiwa tumbili hivi karibuni yamedokeza kwamba tatizo la HIV ni kwamba hata kirusi kilichodhoofishwa chaweza kugeuka na kusababisha kifo. Yaani, chanjo yaweza kusababisha maradhi inayokusudiwa kuandaa ulinzi dhidi yake.

Utafutaji wa chanjo umekuwa wenye kutamausha na kubatilisha. HIV imebaki bila kudhuriwa na makumi ya michanganyiko ya majaribio ambayo kwa kweli yangeweza kuua virusi vinginevyo visivyo na nguvu zaidi. Zaidi ya hilo, HIV hubadilika, kukiifanya iwe shabaha isiyoweza kushikwa kwa urahisi. (Kufikia sasa kuna angalau familia kumi za HIV ulimwenguni pote.) Kuongezea tatizo hilo, kirusi hicho hushambulia moja kwa moja chembe za mfumo wa kinga ambazo chanjo inapaswa kukinga.

Pia uchumi huchangia fungu fulani katika utafiti. Shirika lililoko Washington la International AIDS Vaccine Initiative lilisema kwamba “mashirika ya kibinafsi hayajishughulishi.” Inasemwa kwamba hayajishughulishi kwa sababu yanahofu kwamba chanjo hizo hazingeleta faida, kwa kuwa nyingi zake zingeuzwa katika nchi ambazo hazijaendelea.

Yajapokuwa magumu, watafiti wanaendelea kuchunguza mifikio kadhaa katika utafutaji wa chanjo yenye mafanikio. Hata hivyo, kwa wakati huu huenda chanjo isitokezwe hivi karibuni. Chanjo yenye kutumainiwa itokezwapo kwenye maabara, hufuatia kazi ngumu, yenye gharama, na iwezayo kutokeza hatari ya kufanya majaribio kwa binadamu.

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

Ni Nani Wanaoambukizwa HIV?

Ulimwenguni pote, karibu watu 16,000 huambukizwa kila siku. Inasemekana kwamba zaidi ya asilimia 90 huishi katika nchi zinazositawi. Karibu 1 kati ya 10 ni mtoto aliye na umri unaopungua miaka 15. Wale wengine ni watu wazima ambao asilimia 40 ni wanawake na zaidi ya nusu wana umri wa kati ya miaka 15 na 24.—Shirika la Afya Ulimwenguni na Muungano wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhusu HIV/UKIMWI.

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Unaweza Kujuaje Ni Nani Ameambukizwa?

Huwezi kujua ikiwa mtu fulani ameambukizwa kwa kumtazama tu. Ingawa watu wenye HIV wasioonyesha dalili waweza kuonekana kuwa wenye afya, wanaweza kupitisha virusi hivyo kwa wengine. Je, waweza kuitibari uhakikishio wa mtu kwamba hajaambukizwa? Si lazima iwe hivyo. Wengi ambao wameambukizwa HIV wenyewe hawana habari. Huenda wale wanaojua wakaweka jambo hilo kuwa siri, au wadanganye. Uchunguzi uliofanywa Marekani ulifunua kwamba watu 4 kati ya 10 walioambukizwa HIV walikosa kuwaambia watu wanaofanya ngono nao kwamba wameambukizwa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Uhusiano Ulioko Kati ya HIV na UKIMWI

HIV yamaanisha “virusi ya upungufu wa kinga ya mwili,” virusi ambayo huharibu polepole sehemu za mwili za mfumo wa kinga ambazo hupigana na maradhi. UKIMWI wamaanisha “ukosefu wa kinga mwilini.” Ndiyo hatua ya mwisho yenye kutisha uhai ya ambukizo la HIV. Jina hilo lafafanua jinsi HIV imeharibu mfumo wa kinga vibaya sana, ikimfanya mgonjwa aweze kupatwa kwa urahisi na maambukizo ambayo kama sivyo mfumo wa kinga ungaliweza kushindana nayo.

[Hisani]

CDC, Atlanta, Ga.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Ni chaguo la hekima kupimwa HIV kabla ya kufikiria ndoa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki