Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 9/8 kur. 13-15
  • Naweza Kuepukaje Kupata UKIMWI?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Naweza Kuepukaje Kupata UKIMWI?
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • UKIMWI—Kutenganisha Ngano na Mambo Hakika
  • “Ngono Salama”?
  • Mibano
  • Kukataa
  • UKIMWI—Je! Nimo Hatarini?
    Amkeni!—1993
  • Ukimwi—Jinsi ya Kupigana Nao
    Amkeni!—1998
  • UKIMWI— Shida kwa Matineja
    Amkeni!—1992
  • Kusaidia Wale Walio na UKIMWI
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 9/8 kur. 13-15

Vijana Wanauliza...

Naweza Kuepukaje Kupata UKIMWI?

“JAMBO hilo hunifanya nikasirike kwamba nililiruhusu litokee,” asema Kaye. “Kwa sababu ya njia niliyochagua, nilipoteza fursa ya kufanya machaguzi ambayo ningekuwa nayo wakati ujao.” (Gazeti la Newsweek, Agosti 3, 1992) Akiwa na umri wa miaka 18, Kaye aliambukizwa virusi vya UKIMWI.

Kaye ni mmoja tu kati ya watu zaidi ya milioni moja katika United States ambao wameambukizwa virusi hatari vya HIV (Human Immunodeficiency Virus)—virusi ambavyo madaktari wasema husababisha ugonjwa wa UKIMWI unaoogopwa.a Hakuna ajuaye hasa ni vijana wangapi wanaoambukizwa, lakini vijana kwa wazi wanahangaishwa. Uchunguzi ulionyesha kwamba miongoni mwa vijana Waingereza, UKIMWI ndio unaowapa wasiwasi wao mkubwa zaidi. Kujapokuwa hangaiko hilo, Vituo vya Kudhibiti Maradhi vya U.S.. vyasema: “Wabalehe wengi wanaendelea kuripoti jinsi wanavyojiingiza katika tabia ambayo mtu anaweza kuambukizwa HIV.”

UKIMWI ni wenye kufisha sikuzote, na unasambaa ulimwenguni pote kwa kiwango kikubwa sana. Unaweza kujilindaje?

UKIMWI—Kutenganisha Ngano na Mambo Hakika

Kijitabu kilichotayarishwa na Vituo vya Kudhibiti Maradhi vya U.S. chaeleza hivi: “Ambukizo la HIV ‘halitokei tu.’ Huwezi ‘kulipati’ kama vile mafua au homa.” Kwa hiyo, kushughulika kikawaida na watu wa UKIMWI kila siku hakuonekani kuwa hatari. Si lazima uwe na wasiwasi juu ya kuambukizwa UKIMWI kutoka kwa mwanadarasa mwenzi aliyeambukizwa kwa sababu tu ya kuketi karibu naye. Kwa kuwa HIV si virusi vya kuambukizwa kupitia hewa, huhitaji kuwa na wasiwasi na mtu mwenye UKIMWI akikohoa au kupiga chafya. Kwa kweli, familia zilizo na watu wenye UKIMWI, wametumia taulo moja, vyombo vya kulia chakula, na hata miswaki bila kusambaza virusi hiyo.b

Hii ni kwa sababu virusi hivyo hatari hukaa ndani ya damu ya mtu, shahawa, au umajimaji wa uke. Katika visa vingi, basi, UKIMWI hupitishwa kwa ngono—ugoni-jinsia-moja au ugoni-jinsia-tofauti.c Wagonjwa wengi wameambukizwa pia kwa kushiriki sindano au mabomba madogo ya kutilia dawa ya sindano mara nyingi katika utumizi mbaya wa dawa za kulevya na mtu mwenye kuambukizwa HIV.d Na ijapokuwa madaktari wanadai kuwa hatari hiyo “imeondolewa kabisa” kwa uchunguzi wenye bidii, UKIMWI waweza pia kupitishwa kwa kutiwa damu mishipani.

Kwa hiyo yeyote anayejiingiza katika ngono ya kabla ya ndoa au anayetumia dawa haramu za kulevya zinazoingizwa mwilini kwa sindano yumo katika hatari kubwa ya kuambukizwa UKIMWI. Ni kweli kwamba, mwenzi wa ngono huenda asionekane kuwa mgonjwa. Lakini kijitabu Voluntary HIV Counseling and Testing: Facts, Issues, and Answers chakumbusha: “Huwezi kujua kama mtu ana ambukizo la HIV kwa kumtazama. Mtu aweza kuonekana na kuhisi kuwa na afya bora na bado awe ameambukizwa. Kwa sababu hiyo, watu wengi walio na ambukizo la HIV hawajui kuwa wameambukizwa.”

“Ngono Salama”?

Wafanyakazi na waelimishaji wengi wanahimiza utumizi wa kondomu.e Matangazo ya televisheni, vibao vya matangazo, na mafundisho ya shule yameeneza ujumbe hivi kwamba utumizi wa vifaa hivyo vya kuzuia uzazi hufanya ngono iwe “salama”—au angalau “salama zaidi.” Shule kadhaa hata zimegawia wanafunzi kondomu. Wakichochewa na matangazo hayo, vijana wengi zaidi wanazitumia.

Hata hivyo, “ngono salama” ni salama kadiri gani? Broshua iliyoandikwa na chama cha Msalaba Mwekundu cha Amerika yasema: “Kondomu zaweza kuzidisha uwezekano wa kuepuka maambukizo.” Lakini utahisi salama ikiwa tu ‘utazidisha uwezekano’ wa kuepuka ugonjwa ambao sikuzote unathibitika kuwa wenye kuua? Vituo vya Kudhibiti maradhi vya U.S. vyakubali: “Kondomu za mipira zimeonyeshwa kuwa zasaidia kuzuia ambukizo la HIV na magonjwa mengine yanayopitishwa kingono . . . Lakini hazizuii kabisa bila kasoro.” Naam, zaweza kuvunjika, kuraruka, au kutoka wakati wa ngono. Kulingana na Time, kondomu “zaweza kukosea kwa kiwango cha kati ya asilimia 10 na 15”! Je! ungehatarisha uhai wako kwa kiwango hicho cha juu hivyo? Na hata vibaya zaidi, chini ya nusu ya vijana wenye kufanya ngono wa United States wanatumia kondomu.

Shauri la Mithali 22:3 lafaa: “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; bali wajinga huendelea mbele wakaumia.” Mojapo njia za kuepuka kupata UKIMWI ni kuepukana kabisa na utumizi mbaya wa dawa za kulevya na ngono isiyo na adili. Je! ni rahisi kusema kuliko kufanya? Wengi huhisi hivyo, hasa kwa sababu ya mibano mikubwa mno ambayo vijana hukabili.

Mibano

Wakati wa “uzuri wa ujana,” tamaa za ngono zina nguvu sana. (1 Wakorintho 7:36) Sasa, kuongezea hayo, kuna uvutano wa televisheni na sinema. Kulingana na uchunguzi fulani, matineja hutazama Televisheni zaidi ya saa tano kila siku—mandhari nyingi zikionyesha ngono. Lakini katika ulimwengu wa Televisheni wa kuwaziwa, ngono haina matokeo yayo. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba katika televisheni ya U.S. “wagoni-jinsia-tofauti wasiooana hufanya ngono mara nne hata nane zaidi ya wanaume na wanawake waliooana. Vizuiaji kutunga mimba huwa havitajwi au kutumiwa kamwe, lakini wanawake mara nyingi hawapati mimba; wanaume na wanawake hawaambukizwi magonjwa yanayopitishwa kingono isipokuwa kama wao ni makahaba au wagoni-jinsi-moja.”—Kituo cha Machaguo ya Watu Wote.

Je! viwango vikubwa vya vipindi hivyo vya televisheni kweli vyaweza kuathiri mwenendo wako? Ndiyo, kulingana na kanuni ya Biblia kwenye Wagalatia 6:7, 8: “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu.” Uchunguzi mmoja wa vijana 400 uligundua kwamba “wale waliotazama kiwango kikubwa cha televisheni yenye ‘ngono’ walifanya ngono zaidi ya wale waliotazama kwa kiwango kidogo.”

Uvutano mwingine ni mbano wa marika. “Nilikuwa nikitafuta kikundi cha watu ambao ninge-faana nao, na ni vigumu kukipata,” akiri tineja mmoja anayeitwa David. “Nilijiweka kwenye hali hatari mara nyingi. . . . Nilipimwa nikaambiwa nina UKIMWI.” Vivyo hivyo, vijana wa nyakati za Biblia walipatwa na mibano ya marika mara nyingi. Namna gani shauri la Biblia? “Mwanangu,” akasema mwandikaji wa Mithali, “wenye dhambi wakikushawishi, wewe usikubali.”—Mithali 1:10.

Kukataa

Wenye kuhimiza utumizi wa “ngono salama” hutoa hoja kwamba, kutofanya ngono ni jambo lisilowezekana. Lakini mwishowe, je, kwa kweli inafaa kuendeleza ukosefu wa adili? Tineja mmoja akubali kwamba jambo hilo hutatanisha vijana, akisema: “Wao hutuambia tu tukatae ngono na ni sawa kuwa mwema na safi. Wakati uleule, wanatoa [kondomu] na kutuambia jinsi tunavyoweza kufanya ngono na kukosa kulipia matokeo yayo.”

Usitatanishwe hivyo na maadili. Biblia—hata ionekane kuwa ya kizamani—hukusihi kuepuka mwenendo ambao ungekuhatarisha kuambukizwa UKIMWI. Ukitii amri ya Biblia ya ‘kuepukana na damu,’ hutapata UKIMWI kupitia kutiwa damu mishipani. (Matendo 15:29) Tii katazo la Biblia dhidi ya utumizi wa “dawa za kulevya” na hauhitaji kuogopa kuambukizwa na sindano yenye viini inayotumiwa kutia dawa za kulevya mwilini. (Wagalatia 5:20; Ufunuo 21:8; The Kingdom Interlinear) Hasa sheria ya Biblia ya adili ya ngono itakulinda wewe. “Ikimbieni zinaa,” Biblia yaamuru. “Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.” (1 Wakorintho 6:18) Tatizo la UKIMWI hukazia hekima ya maneno hayo.

Kijana aweza ‘kuukimbiaje’ ukosefu wa adili? Kwa miaka mingi makala za “Vijana Wanauliza . . .” zimetoa madokezo kadhaa yanayofaa, kama vile kufanya uchumba katika vikundi, kuepuka hali za kuridhiana (kama vile kuwa peke yako na mtu wa jinsia tofauti katika chumba au nyumba au gari lililoegeshwa), kuiweka mipaka juu ya maonyesho ya upendo, kuepuka utumizi wa kileo (ambako kwa kawaida huzuia uamuzi mzuri), na kukataa katakata hali ikiwa yemye mahaba sana.f Katika hali yoyote ile usiache mtu akubane katika mwenendo ambao ni hatari si kimwili tu bali pia wenye kuangamiza kiroho. (Mithali 5:9-14) “Je! unataka uhai wako uhatirishwe na mtu huyo mwingine?” akauliza kijana mwanamke aitwaye Amy aliyenukuliwa katika makala ya Newsweek. Alipata HIV kutoka kwa rafiki yake mvulana kabla ya kuhitimu shule ya sekondari. Aliuliza hivi moja kwa moja: “Je! unaweza kufa kwa ajili ya mvulana au msichana huyo? Sidhani.”

[Maelezo ya Chini]

a Kwa mfano, ona zile makala za “Vijana Wanauliza . . .” katika matoleo ya Amkeni! ya Agosti 8, 1987 Kiswahili au Aprili 22, 1986; Aprili 22, 1989 Kiingereza; na Aprili 22, 1992 Kiingereza.

b Ona makala “Vijana Wanauliza . . . UKIMWI—Je! nimo Hatarini?” inayopatikana kwenye toleo la Amkeni! la Agosti 22, 1993.

c Aliyekuwa mpasuaji mkuu wa United States Dakt.  C. Everett Koop alijibu wenye kutilia shaka kwa kusema: “Visa vya kwanza vya UKIMWI viliripotiwa katika nchi hii 1981. Kufikia sasa tungekuwa tumejua kama UKIMWI hupitishwa kwa kuwa pamoja kwa kawaida kusiko kwa kingono.”

d Hili latia ndani ngono ya kinywa na ya kinyo.

e Vituo vya Kudhibiti Maradhi vya U.S.. vyatahadharisha zaidi: “Ukipanga kutobolewa masikio yako . . . , hakikisha unaenda kwa mtu mwenye ustadi anayetumia chombo kipya au kilichosafishwa vizuri. Usione haya kuuliza maswali.”

f Gazeti FDA Consumer laeleza: “Kondomu ni kifuniko kinachofunika uume wote. Hulinda dhidi ya magonjwa ya kupitishwa kingono kwa kuwa kama kizuizi, au ukuta, ili kuzuia shahawa, damu, na umajimaji wa uke usipite kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa yule mwingine.”

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kukubali mbano wa ngono kwaweza kuongoza kwenye UKIMWIy

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki