Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 3/22 kur. 12-15
  • Kusaidia Wale Walio na UKIMWI

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kusaidia Wale Walio na UKIMWI
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Upendo wa Mungu kwa Wenye Kuteseka
  • Ni Nani Wapatwao na Virusi ya UKIMWI?
  • Lijulikanalo kwa Sasa
  • Wewe Utaitikiaje?
  • Wenye UKIMWI Waweza Kusaidia Pia
  • UKIMWI— Lile Wazazi na Watoto Wanapaswa Kujua
    Amkeni!—1992
  • UKIMWI— Shida kwa Matineja
    Amkeni!—1992
  • UKIMWI—Je! Nimo Hatarini?
    Amkeni!—1993
  • UKIMWI—Matokeo Yenye Msiba Mkubwa kwa Watoto
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 3/22 kur. 12-15

Kusaidia Wale Walio na UKIMWI

“ASHIKWAPO na UKIMWI, Kasisi Akuta Milango Imefungwa” ndicho kilichokuwa kichwa cha makala moja katika The New York Times. Gazeti hilo lilisimulia hadithi ya kasisi mmoja Mbaptisti ambaye mke na watoto wake wawili waliambukizwa na virusi ya UKIMWI kutokana na damu aliyotiwa mishipani katika 1982 (watoto waliambukizwa katika tumbo la uzazi la huyo mke). Muda si muda, yeye na familia yake walivunjwa moyo wasihudhurie makanisa mbalimbali ya Kibaptisti kwa sababu ya ugonjwa wao. Alipozinduka kuona ukweli wa mambo, alikoma kujaribu kuhudhuria akaacha ukasisi wa Kibaptisti.[1]

Kuvurugika hisia kwa mwanamume huyo juu ya kushindwa kwa kanisa lake kwatokeza maswali kadhaa: Je! Mungu hujali wagonjwa, kutia na wale walio na UKIMWI? Waweza kusaidiwaje? Ni tahadhari gani zahitaji kuchukuliwa wakati wa kuandaa kitulizo cha Kikristo kwa wale walio na UKIMWI?

Upendo wa Mungu kwa Wenye Kuteseka

Biblia huonyesha kwamba Mungu Mweza Yote huonyesha hisiamwenzi ya kina kirefu kwa wale watesekao. Alipokuwa duniani, Yesu pia alionyesha huruma yenye kuhisiwa moyoni kwa wagonjwa. Na Mungu alimpa nguvu ya kuponya watu magonjwa yao yote, kama Biblia isimuliavyo: “Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya.”—Mathayo 15:30.

Bila shaka, leo Mungu hajampa yeyote duniani uwezo wa kuponya wagonjwa kimuujiza kama alivyofanya Yesu. Lakini unabii wa Biblia waonyesha kwamba karibuni, katika ulimwengu mpya wa Mungu, “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Biblia yaahidi hivi: “[Mungu] atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu.” (Ufunuo 21:4) Kwa sababu ya upendo wake mkuu kwa wanadamu, Mungu ametayarisha dawa ya daima kwa magonjwa yote, kutia na UKIMWI.

Zaburi 22:24 yasema hivi juu ya Mungu: “Hakulidharau teso la mteswa, wala hakuchukizwa nalo; wala hakumficha uso wake, bali alipomlilia akamsikia.” Upendo wa Mungu upo kwa wale wamwitao awasaidie.

Ni Nani Wapatwao na Virusi ya UKIMWI?

UKIMWI sana-sana ni ugonjwa wa mtindo-maisha fulani.[2] Kwa kukumbuka yaliyopita, watu wengi walioambukizwa hukubaliana na Zaburi 107:17, Habari Njema kwa Watu Wote, litaarifulo hivi: “Baadhi walipumbaa kwa sababu ya dhambi zao, waliteseka kwa sababu ya uovu wao.”

Wakati mtu aachapo viwango vya Biblia na kujitia katika ngono nje ya mpango wa Mungu wa ndoa, hatari ya kuambukizwa UKIMWI au kuambukiza wengine huwa halisi sana. Pia, wakati watu mmoja-mmoja washirikipo sindano ili kutia dawa za kulevya mishipani, wao waweza kupata UKIMWI na waweza kupitishia wengine hiyo virusi. Kwa kuongezea, wengi wamepata UKIMWI kwa kutiwa mishipani damu ya wachangaji walioambukizwa.

Hata hivyo, ni msiba kwamba idadi kubwa sana za watu wasio na hatia wanaambukizwa na virusi ya UKIMWI, tena kwa njia kadhaa. Kwa kielelezo, wenzi wengi wa ndoa walio waaminifu wanapatwa na UKIMWI kwa kosa lisilo lao wenyewe, kupitia kufanya ngono na mwenzi wao aliyeambukizwa. Halafu pia, asilimia kubwa ajabu ya watoto wachanga, hasa katika maeneo fulani, wanapatwa na virusi ya UKIMWI kutoka kwa akina mama walioambukizwa, hiyo ikifanya mtoto aliyezaliwa sasa hivi akiwa na UKIMWI awe mmoja wa majeruhi wenye kusikitisha zaidi. Pia, wanatiba na wengine wamepata ugonjwa huo kwa sababu ya aksidenti zilizowapata walipokuwa wakishughulika na damu iliyoambukizwa.

Vyovyote vile UKIMWI upatikanavyo na mtu fulani, Maandiko yaonyesha wazi kwamba si Mungu wa kulaumika kwa upitishaji wa ugonjwa huo wenye kuua. Ingawa leo walio wengi wa wale walioambukizwa wamejiletea wenyewe UKIMWI na wameambukiza wengine kwa mwenendo usiopatana na viwango vya Biblia, asilimia za wenye kuambukizwa hivyo zinabadilika, zikionyesha kwamba kuna idadi kubwa zaidi za wenye kuambukizwa wakiwa majeruhi wasio na hatia, kama vile watoto wachanga na wenzi wa ndoa walio waaminifu.

Shirika la Afya Ulimwenguni lataarifu kwamba wanawake ulimwenguni pote sasa wanaambukizwa na virusi ya UKIMWI karibu mara nyingi kama wanaume na kwamba kufikia mwaka 2000, mengi ya maambukizo mapya yatakuwa katika wanawake.[2A] Wafanyakazi wa afya katika Afrika wasema kwamba asilimia 80 ya visa vya UKIMWI huko “hupitishwa na ngono kati ya mtu wa kiume na wa kike, na karibu vingine vyote hupitishwa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto wakati wa ujauzito au wa kuzaliwa.”[2B]

Hata hivyo, ingawa Mungu hupinga ukiukaji wowote wa sheria zake, kutia na mivunjo ya sheria ambayo hutokeza mateso, yeye hufanya haraka kuwanyoshea mkono wa rehema wale wote watesekao hivyo. Hata wale ambao wamepata UKIMWI kwa kufanya makosa waweza kunufaika na rehema ya Mungu kwa kutubu na kukoma kutenda lililo baya.—Isaya 1:18; 1 Wakorintho 6:9-11.

Lijulikanalo kwa Sasa

UKIMWI ni tatizo la kiafya ulimwenguni pote. Ingawa wanasayansi huhakikishia watu kwamba “HIV si kiini kiwezacho kupitishwa kwa urahisi kutoka mtu hadi mtu,” hiyo haiwafariji sana mamilioni ambao tayari wana kiini hicho na wale mamilioni wengi sana watakaokipata miaka ijayo. Mambo ya hakika yaonyesha kwamba kinaenea duniani pote. [3]

Ikitoa muhtasari wa zile njia za kawaida za upitishaji, mamlaka moja yasema hivi: “Karibu maambukizo yote ya HIV hupitishwa kwa mgusano wa kingono au kwa kuwa katika hali isiyo na kinga dhidi ya kuingiwa na damu iliyoambukizwa.”[4] Ripoti moja yataarifu hivi kwa kufikiria vile wataalamu wengi wa kitiba wamekata maneno: “Ili ambukizo litukie, lazima kuwe na mwingizo wa umajimaji wa mwili (karibu sikuzote huwa ni damu au shahawa) kutoka kwa mtu aliyeambukizwa mpaka ndani ya mwili wa mtu asiyeambukizwa.”[5]

Hata hivyo, vile vifungu visemavyo “karibu maambukizo yote” na “karibu sikuzote” vyakiri uwezekano wa visa vilivyo tofauti. Kwa hiyo ingawa kadiri kubwa sana ya zile njia za kupitisha UKIMWI zajulikana leo na wale walio katika uwanja wa tiba, njia ya kupata hiyo virusi huenda ikawa haijulikani katika visa vya asilimia ndogo sana. Kwa hiyo, huenda bado kukawa na uhitaji wa tahadhari.[10,11,12]

Wewe Utaitikiaje?

Watu wapatao milioni 12 hadi milioni 14 ulimwenguni pote tayari wameambukizwa na virusi ya UKIMWI. Na makadirio yaonyesha kwamba mamilioni wengi zaidi watakuwa wameambukizwa mwishoni mwa karne hii. Hivyo, yaelekea wewe umekutana au utakutana karibuni na wale walio na ugonjwa huo.[20] Kwa kielelezo, katika jiji kubwa lolote, kukutana na watu wa jinsi hiyo hutukia kila siku kazini, katika mikahawa, majumba ya sinema, nyanja za michezo, mabasi, magari mengine ya abiria, ndege, na magari-moshi, na pia katika hekaheka nyingine za umma.

Hivyo, huenda Wakristo wakazidi kuwakuta kisha wasukumwe na moyo kuwasaidia wenye kuteswa na UKIMWI ambao wataka kujifunza Biblia, kuhudhuria mikutano ya Kikristo, na kufanya maendeleo kuelekea kujiweka wakfu kwa Mungu. Wakristo wapaswa kuitikiaje mahitaji hayo ya wenye UKIMWI? Je! kuna tahadhari ambazo zingesaidia kwa manufaa ya mtesekaji na wale walio katika kutaniko la Kikristo?

Kwa kutegemea maoni yakubaliwayo sasa, kukutana katika hekaheka za kawaida hakupitishi UKIMWI. Kwa hiyo yaonekana yafaa mtu asiwe akiogopa-ogopa kuwa karibu na watu wenye UKIMWI. Na kwa kuwa wenye UKIMWI wana mfumo wa kinga iliyodhoofika sana, sisi twapaswa kuwa waangalifu ili wao wasipatwe na maambukizo ya virusi ambayo huenda sisi tukawa nayo. Huenda miili yao ikapatwa na hasara kubwa kutokana na magonjwa hayo ya kawaida.[21]

Kwa sababu ya hali ya UKIMWI yenye kuhatarisha uhai, ni hekima kukumbuka tahadhari fulani zifaazo tunapokaribisha mwenye UKIMWI katika ushirika wetu wa kibinafsi au ule wa kutaniko la Kikristo. Kwanza, ingawa tangazo kwa watu wote halipasi kutolewa, huenda tukataka kujulisha mmoja wa wazee katika kutaniko juu ya hali hiyo ili awe tayari kumpa jibu lenye fadhili na lifaalo yeyote awezaye kuulizia jambo hilo.

Kwa kuwa virusi yaweza kupitishwa na damu ya mtu aliyeambukizwa, huenda ikafaa makutaniko kuwa na mazoea ya kufuata zile ziitwazo tahadhari kwa wote wakati wa kusafisha vyoo na vikojoleo, hasa ikiwa damu yahusika katika mkojo. “Tahadhari kwa wote” ni mtajo uliochaguliwa na wanatiba kueleza fungu la kanuni za kwamba damu yote kutoka kwa mtu yeyote huonwa kuwa chafu na iwezayo kuwa hatari na kwa hiyo hushughulikiwa kwa njia fulani hususa. [25] Kwa sababu Jumba la Ufalme ni jengo la watu wote, huenda ikawa hekima kuwa na visafishio pamoja na sanduku la vifunika-mikono (vya Lateksi au vainili) ili kuandaa utunzaji ufaao na usafishaji iwapo kutakuwa na aksidenti.[22] Mchanganyo wa maji na asilimia 10 ya dawa ya kuondoa madoa (blichi) ndio hupendekezwa kwa kawaida katika usafi wa kuondoa mikojo yenye damu.[23, 24]

Katika shughuli zetu zote na wengine, kutia na wenye UKIMWI, Wakristo huagizwa kufuata kielelezo cha Yesu. Lile sikitiko alilokuwa nalo kwa wale wenye kuteseka, na bado wenye kutamani kwa moyo mweupe kumpendeza Mungu, lastahili kuigwa nasi. (Linganisha Mathayo 9:35-38; Marko 1:40, 41.) Hata hivyo, kwa kuwa hakuna ponyo la UKIMWI kwa sasa, yafaa Mkristo achukue tahadhari zifaazo atoapo msaada wenye huruma kwa wale walio na ugonjwa huo.—Mithali 14:15.

Wenye UKIMWI Waweza Kusaidia Pia

Mwenye UKIMWI aliye na busara hung’amua kwamba wengine ni wepesi kuogopa ugonjwa huo. Kwa hiyo, kwa kustahi hisia za wale watakao kumsaidia, ingekuwa vizuri zaidi huyo mwenye UKIMWI asiwe wa kwanza kuonyesha shauku kama zile za kukumbatiana na kubusiana. Hata ikiwa kuna uwezekano kidogo tu au hakuna wowote kwamba vitendo hivyo vingeweza kupitisha huo ugonjwa, kizuio hicho kitaonyesha kwamba mwenye ugonjwa huo ana ufikirio kwa wengine, hivyo akiwafanya wao wawe na ufikirio kwake pia.a

Aking’amua kwamba watu wengi wana hofu mbalimbali juu ya mambo yasiyojulikana, mtu mwenye UKIMWI hapaswi kuwa mwepesi kuudhika ikiwa haalikwi kwenye nyumba za kibinafsi moja kwa moja au ikiwa yaonekana kwamba mzazi fulani huzuia mtoto asikaribiane naye. Na ikiwa moja la Mafunzo ya Kitabu ya Kutaniko hufanywa kwenye Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova, huenda ikawa hekima mtu mwenye UKIMWI kuchagua kuhudhuria huko, badala ya katika nyumba ya faragha, isipokuwa kama amezungumzia hali hiyo na mwenye nyumba.

Wenye UKIMWI wapaswa pia kuhangaikia wengine kwa tahadhari wakati ambapo, kwa kielelezo, wana kikohozi chenye mtoko na yajulikana kuwa wana kifua kikuu. Hapo basi wangetaka kutumia miongozo ya kijumuiya kuhusu afya kwa habari ya hali hiyo kuhusiana na taratibu za kuweka mtu peke yake.

Hali nyingine ambamo mtu asiye na hatia angeweza kuambukizwa ni kwa kufunga ndoa na mtu aliye na virusi ya UKIMWI bila kujua. Huenda tahadhari ikahitajika katika hali hizo hasa ikiwa mwenzi mmoja au wote wawili wanaokusudia kufunga ndoa walikuwa wamekuwa wakiishi maisha ya ovyoovyo au walikuwa wametumia sindano za kutumia vibaya dawa za kulevya kabla ya kupata ujuzi sahihi wa Neno la Mungu. Kwa kuwa idadi ya watu walio na ambukizo la HIV ambayo haijaonekana wazi inaongezeka, halingekuwa jambo lisilofaa mtu au wazazi wanaojali kuomba damu ya atazamiwaye kuwa mwenzi wa ndoa ichunguzwe kama ina UKIMWI kabla ya uchumba au ndoa. Kwa sababu ugonjwa huo humenya watu sana na kuwaua, mtu atazamiwaye kuweza kuwa mwenzi wa ndoa hapaswi kuudhika ikiwa aombwa kufanya hivyo.

Ikiwa uchunguzi wathibitisha kuna kitu, haingefaa mwenye ambukizo amsonge yule akusudiwaye kuwa mwenzi wa ndoa kuendeleza mafahamiano ya kirafiki au uchumba ikiwa sasa yule atazamiwaye kuwa mwenzi wa ndoa ataka kuumaliza uhusiano. Na ingekuwa hekima mtu yeyote ambaye hapo kwanza aliishi mtindo-maisha wenye hatari kubwa ya kuambukizwa, aliyeishi maisha ya ovyoovyo au aliyetumia dawa za kulevya kwa kuzidunga mishipani, ajitolee mwenyewe kuchunguzwa kabla ya kuanza uchumba. Kwa njia hiyo, kuoneana uchungu kungeweza kuepukwa.

Hivyo, kwa kuwa sisi ni Wakristo twataka kutenda kwa kusikitikia wala si kuepuka kabisa watu walio na UKIMWI, hata hivyo tutambue kwamba hisia za watu mmoja-mmoja huenda zikatofautiana juu ya habari hiyo yenye kuamsha hisia kwa urahisi. (Wagalatia 6:5) Kuhusiana na ugonjwa kama UKIMWI, kuna mambo yasiyojulikana, kwa hiyo huenda wengi wakasitasita kushughulikia masuala yahusikayo.[25A] Maoni yenye usawaziko juu ya jambo hilo yangekuwa kuendelea kukaribisha wenye UKIMWI ndani ya kutaniko la Kikristo na kuwaonyesha upendo na uchangamfu, huku pia tukifanya tahadhari za kiasi kujilinda wenyewe na familia zetu na huo ugonjwa.

[Maelezo ya Chini]

a Mtu ajuaye ana UKIMWI apaswa kufanya nini atakapo kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova na kubatizwa? Kwa kustahi hisia za wengine, huenda likawa jambo la hekima aombe ubatizo wa faragha, ingawa hakuna uthibitisho wa kudokeza kwamba UKIMWI umepitishwa katika vidimbwi vya kuogelea. Ingawa Wakristo wengi wa karne ya kwanza walibatizwa kwenye mikusanyano mikubwa ya watu wote, wengine walibatizwa katika mazingira ya faragha zaidi kwa sababu ya hali mbalimbali. (Matendo 2:38-41; 8:34-38; 9:17, 18) Njia nyingine ingekuwa kwamba yule mtaka kubatizwa mwenye UKIMWI abatizwe mwisho.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

Nilihurumia Msichana Huyo

Siku moja nikiwa katika huduma ya peupe, nilifikia msichana wa karibu miaka 20. Macho yake makubwa ya kahawia yalionekana yenye huzuni sana. Kwa kujaribu kuanzisha mazungumzo juu ya Ufalme wa Mungu, nilimtolea moja ya trakti nilizokuwa nimeshika. Bila kusitasita akachagua Faraja kwa Walioshuka Moyo. Aliitazama trakti kisha akanitazama mimi na kusema kwa sauti baridi hivi: “Dada yangu amekufa juzi kwa UKIMWI.” Kabla sijamaliza kutaja masikitiko yangu, yeye akasema: “Mimi pia ninakufa kwa UKIMWI, na nina watoto wadogo wawili.”

Nilihurumia msichana huyo, nikamsomea kutokana na Biblia juu ya wakati ujao ambao Mungu amewaahidi wanadamu. Yeye kaboboka hivi: “Kwa nini Mungu anijali mimi hali sijapata kamwe kumjali yeye?” Nikamwambia kwamba kwa kujifunza Biblia, yeye angekuja kuelewa kwamba Mungu hukaribisha kila mtu atubuye kwa moyo mweupe na kuja kuwa na tumaini katika yeye na katika dhabihu ya fidia ya Mwana wake. Yeye akajibu hivi: “Najua wewe ni nani. Wewe umetoka Jumba la Ufalme pale chini barabara hii—lakini je! mtu kama mimi angekaribishwa katika Jumba la Ufalme?” Nikamhakikishia kwamba angekaribishwa.

Alipoendelea kwenda zake, akiwa amekishika sana kitabu Biblia—Neno la Mungu au la Binadamu? na trakti yake, mimi nikawaza, ‘Natumaini ataipata faraja ambayo ni Mungu tu awezaye kuitoa.’[35]

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki