UKIMWI— Lile Wazazi na Watoto Wanapaswa Kujua
JAMBO la kusikitisha ni kwamba, shida za wabalehe wengi ambao wamepatwa na UKIMWI huongezewa na fikira isiyo na usawaziko ya watu wazima wengi wanaojua machache tu kuhusu UKIMWI. Katika visa vingi wazazi wamefanya watoto wao wawe na maoni mabaya juu ya ugonjwa huo. Hata baada ya madaktari kusema kwamba hakuna hatari, wasimamizi wa shule na waalimu wakuu wamekataa kukubali watoto walio na ambukizo la UKIMWI. Hivyo basi wazazi wengi wenye watoto walio na ambukizo la HIV wanaficha sana siri hiyo. Wanaogopa, kwa upande mwingine kwa sababu nzuri, kwamba watoto wao watakataliwa, kuumizwa, au watendwe vibaya zaidi.
Kwa mfano, mama mmoja mwenye binti aliye na UKIMWI aliogopa sana matata na majirani zake hata akamwepusha mtoto wake kucheza na watoto wao. “Hutaki watu wanaoishi karibu nawe wajue kwamba mtoto wako ana UKIMWI, kwa sababu watu watafanya mambo ya ajabu sana.” Kulingana na ripoti mbalimbali, hili si kutia chumvi. Wazazi wameepukwa na baadhi ya marafiki zao wa karibu na majirani. Marafiki wamegeukia mitaani badala ya kuonyesha kuwapo kwao na kuwasalimu. Sifa mbaya ya UKIMWI inachukiwa sana hivi kwamba watu wametoka nje ya mikahawa, kupiga kelele za matukano wakati familia yenye mtoto aliye na UKIMWI inapoingia. Akina baba wamepoteza kazi zao. Wengine wamepata vitisho vya makombora. Hata wengine nyumba zao zimechomwa moto.
Watoto wenye UKIMWI wamefanyiwa mizaha ya ukatili na wanadarasa wenzi. Mmoja aliyekuwa na UKIMWI, ambaye aliupata kupitia kutiwa damu mishipani, alilaumiwa shuleni mara nyingi kuwa mgoni wa jinsia moja. Wangemchokoza hivi: “Tunajua hasa jinsi ulivyoupata UKIMWI.” Familia iliepukwa na washirika wa kanisa. Barua za makuruhi zisizo na majina ziliwafikia. Takataka nyingi zilitupwa kwenye bustani yao. Mwingine hata alilipua bunduki kwenye dirisha la mbele.
“Huwa ni siri ya kubanwa sana,” akasema mama mmoja mwenye mtoto aliyeambukizwa UKIMWI, “na hilo ndilo linaloleta upweke sana.” The New York Times laongezea kwa kusema: “Wengi wa watoto Waamerika 1,736 walio chini ya miaka 13 wenye UKIMWI wametengwa kando na ugonjwa wao, wakalazimika kuficha hali yao kwa marafiki wenye afya au wanashule wenzi ambao labda wangewaepuka.” Na, hatimaye, kulikuwa na uchunguzi huu kutoka The Toronto Star: “Hata kijana mdogo akifa, familia nyingi zinaogopa kufichua ukweli, ambako huongeza uchungu na mtengo ambao huambatana na kupoteza mtoto yeyote.”
Unalopaswa Kujua
Ni lazima ikiriwe kwamba UKIMWI haujali watu. Unaweza kuambukiza matajiri, maskini, wachanga, wachanga sana, na wazee. Miongoni mwa watu wachanga, katika nchi nyingine, kuna maarifa yasiyotosha na ya kijuujuu ya UKIMWI. Watu wengi “hawana wazo la jinsi UKIMWI ulivyo hatari kwa matineja,” akasema mtaalamu mmoja wa New York City wa UKIMWI.
Kwa mfano, uchunguzi mmoja wa vijana katika mji mkubwa wa Kiamerika ulifunua kwamba asilimia 30 ya waliokaguliwa waliamini kwamba UKIMWI waweza kuponywa ukitibiwa mapema. Matibabu yoyote ya UKIMWI hayajapatikana. Theluthi moja hawakujua kwamba mtu hawezi kupatwa na UKIMWI kwa kumgusa tu mwenye ugonjwa huo au kwa kutumia kichana chake. Uchunguzi zaidi wa matineja 860 , wenye umri wa miaka 16 hadi 19, katika sehemu nyingine ya United States ulipata kwamba asilimia 22 hawakujua kwamba vairasi ya UKIMWI inaweza kuambukizwa kwa shahawa na asilimia 29 hawakujua kwamba ingeweza kuambukizwa kwa umajimaji unaotoka katika uke.
Wakati wa kipindi cha kuambukizwa na dalili za kwanza pamoja na wakati ambapo UKIMWI umejitokeza, wenye kuambukizwa wanaweza kuambukiza wengine vairasi ya UKIMWI. Hata hivyo, haiwezi, kuambukizwa kwa kusalimiana au kukumbatiana na aliye na UKIMWI, kwa maana vairasi hiyo hufa upesi nje ya mwili. Vilevile, vairasi hiyo haiwezi kuishi katika vikalio vya vyoo, woga ambao una wengi. Je! walimu wakuu na wakuu wa shule waliogopa kwamba wanafunzi wasio na UKIMWI wangepata ugonjwa kutokana na mfereji wa maji uliotumiwa na mwenye UKIMWI? Wataalamu wanasema kwamba woga huo si wenye sababu nzuri kwa sababu vairasi haingeweza kuwa na njia ya kuingia katika mshipa wa damu wa mtu asiyeambukizwa.
Madaktari huuliza juu ya hatari ya kutobolewa kwa masikio, kwa vile sindano hutumiwa. Wataalamu wakubali kwamba ikiwa chombo kinachotumiwa kimechafuliwa na ugonjwa huo, hii inaweza kuwa njia ya kupata vairasi ya UKIMWI. Na vipi kubusu? “Ikiwa mtu aliye na UKIMWI au ambukizo la HIV anakubusu, na una mkato wenye kuvuja damu au kidonda mdomoni au kinywani mwako, kuna uwezekano, lakini kwa kadiri kubwa haielekei kuwa hivyo,” akasema mtaalamu mmoja. Inawezekana, hata hivyo.
Njia pekee unayoweza kujua kama umeambukizwa, hata ikiwa dalili zenye kudhaniwa zatokea, ni kupitia uchunguzi kamili wa daktari na kupimwa damu.
Na, hatimaye, ikiwa wewe ni mtoto, waambie wazazi wako ukweli. Wengine wote wakukatishapo tamaa, wao wanaweza kuwa wakikaa na wewe na kukupa faraja na usaidizi unaohitaji. Uwe mwenye hekima ukatae dawa za kulevya na ngono ya kabla ya ndoa. Kufanya hivyo kwaweza kuokoa maisha yako. Vijana ambao wamepata vairasi ya UKIMWI kupitia ngono au sindano zenye maradhi hayo wamekubali kwamba walivutwa na mashirika mabaya. Kweli, maneno ya mtume Paulo yana maana sana kwao sasa. “Msidanganyike; Mazungumzo [mashirika, NW] mabaya huharibu tabia njema.”—na katika hali nyingine, yaweza kuhusisha uhai wako.—1 Wakorintho 15:33.