UKIMWI—Matokeo Yenye Msiba Mkubwa kwa Watoto
JE! UMEONA picha zao? Je! umesikia au kusoma hadithi yao? Ikiwa ndivyo, je! ilikushtua? Ungeweza kuzuia machozi au kubanwa na hisia ngumu kooni mwako? Je! moyo wako unaumia kwa ajili yao? Je! bado waweza kusikia vilio vya polepole vya wale walio karibu kufa bila kutambulika? Hata sasa, je! unaweza kufuta mandhari zenye kuhuzunisha za watoto wachanga—wawili, watatu, na wanne kitandani? Wengi wao waliachwa. Kuteseka kwao na kufa kwatokana na ugonjwa huu wenye kutisha unaokumba dunia—UKIMWI!
Ripoti na picha za televisheni kutoka nchi moja ya Ulaya katika Februari 1990 ilishtua watazamaji makumi ya mamilioni. Ulimwenguni pote, mamilioni wengi zaidi walisoma msiba huo kwenye nyusipepa na magazeti. Gazeti Time liliripoti: “Mwono huo unachukiza na kuogofya. Katika kijitanda hadi kijitanda kingine pamelala vitoto vichanga na watoto wanaoanza kutembea wakiwa na sura kama ya wazee, ngozi yao ikiwa imesinyaa, nyuso zao zilizobakia mifupa zikiwa na alama iliyo wazi ya kukaribia kifo.” “Ni baya kuliko lolote ambalo nimewahi kuona,” akaomboleza daktari mmoja. “Ni dhahiri kwamba, huu ni ugonjwa unaoambukizwa watu kupitia matendo ya kitiba.”
Jinsi gani hivyo? Tofauti na wengi wa watoto wenye UKIMWI waliozaliwa wakiwa na vairasi ya UKIMWI kutoka kwa mama zao walioambukizwa, watoto hawa hawakuzaliwa na vairasi HIV. Msiba huo ulitokea baada ya watoto hao kuzaliwa wakiwa wanyonge au kabla ya kukomaa walipotiwa damu mishipani ikiaminiwa kwamba itaweza kuimarisha wachanga hao dhaifu—tabia ambayo imetiliwa shaka na wastadi wa kitiba kwa muda mrefu. “mpeana damu mmoja mwenye vairasi HIV angeweza kuambukiza watoto 10, 12 au zaidi,” akasema daktari mmoja.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya UKIMWI,” akasema Dakt. Jacques Lebas, msimamizi wa Shirika la kutetea haki za kibinadamu liitwalo Madaktari wa Ulimwengu (Doctors of the World) “tunakabiliana na UKIMWI wa utotoni. Ni ugonjwa wenye kuenea sana.”
Kwa mfano, katika Septemba 1990, kwa mara ya kwanza Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), lilitoa ushuhuda wenye kushtusha ambao ulifunua kwamba ule ugonjwa wa UKIMWI unaoenea sana ulimwenguni umeambukiza watoto. WHO liliripoti kwamba vairasi inayosababisha Ukosefu wa Kinga Mwilini labda itaambukiza watoto milioni kumi kufikia mwaka 2000. “Wengi wao watakuwa wamepata Ukimwi na kufa kufikia mwaka 2000,” akasema Dakt. Michael Merson, mkurugenzi wa progaramu ya shirika hilo kukabiliana na UKIMWI duniani pote. Katika kipindi cha mwisho cha 1990, theluthi moja ya milioni 1.2 ya visa vyenye kuongezeka vya UKIMWI uliokomaa vyaaminiwa kutokea kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Je! ni ajabu kwamba usambaaji wa pigo la UKIMWI umeitwa mweneo wa kikumbo? Kufikia mwisho wa 1992, yapata watoto wachanga milioni nne watazaliwa kutokana na akina mama wenye ambukizo. Wanne kati ya watoto watano wanaozaliwa na vairasi hiyo hupata UKIMWI katika mwaka wao wa tano. Wakiisha kupata UKIMWI, wao hufa katika muda wa mwaka mmoja au miwili, Dakt. Merson aliambia mjadala wa habari wa Geneva.
Wastadi wakadiria kwamba kutakuwa na visa vya UKIMWI 150,000 katika wanawake Waafrika peke yake katika 1992 na pia visa 130,000 katika watoto Waafrika. Katika United States, kufikia sasa watoto wachanga 20,000 huenda wamezaliwa kutokana na wanawake wenye vairasi HIV, likaripoti WHO. Evening Post la Wellington, New Zealand, liliripoti katika toleo la Julai 12, 1989, kwamba vijana 140,000 wa Brazili wanakadiriwa kuwa na vairasi hiyo. Lakini wenye kufuatilia sana jambo hilo wanahofu kwamba huenda kadirio hilo likawa la chini,” gazeti hilo likaripoti. “Mimi naamini kwamba kikundi hiki, ikiwa hakitapewa matibabu ya kipekee, kitakuwa kombora la atomi lililoachiliwa jijini,” akasema mkurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Masilahi ya Watoto. “Ni taabu kubwa kwelikweli,” akaomboleza mwanasaikolojia mmoja Mbrazili.
Matatizo Yaongezeka
Je! yeyote aweza kukosa hisia-moyo kwa jambo baya la wenye kuumizwa wasio na hatia wanaoteseka kutokana na pigo hili lenye kuumiza? Fikiria, kwa mfano, ripoti hii: “Angalau watoto 50 wameuawa katika Afrika ya kati—wengine na wazazi wao wenyewe—kwa sababu walikuwa na Ukimwi, kulingana na shirika la Msalaba Mwekundu la Norwei.” Watoto wengine wa Afrika wenye UKIMWI wanatengwa nyumbani mwao na familia zao zenye kukata tamaa ili kuondolea fungamanisho lolote pamoja na ugonjwa wenye kufedhehesha kuliko ukoma, likaripoti Sunday Star, gazeti la Johannesburg, Afrika Kusini. “Katika maeneo mengine, wenye Ukimwi pomoja na familia zao huzuiwa kwenye visima vya maji na makanisani,” likasema gazeti hilo.
Tarakimu zaidi zenye kuhofisha haziachi nafasi ya kukaa bila kujali. Ripoti za ulimwenguni pote zalaumu mweneo wa kikumbo cha UKIMWI kuwa ndicho kisababishi cha moja kwa moja cha msiba mwingine. Mamilioni ya watoto ambao hawajaambukizwa vairasi ya UKIMWI watakuwa mayatima kwenye miaka ya 1990. Kwa nini? Wazazi wao watakufa kwa UKIMWI. Shirika la WHO lakadiria kwamba kutakuwako na mayatima wenye UKIMWI milioni tano ulimwenguni pote kufikia 1992. “Ni gharika inayoanza kutokea. Na ikiwa hatutakuwa na busara ya kufanya mipango ya kuwatunza, itatubidi tufungue makao makubwa ya mayatima,” akasema mtaalamu mmoja wa utunzaji watoto.
“Ni uchungu usioweza kuwaziwa,” akasema mfanyakazi wa kijamii, akifafanua juu ya familia moja ya New York. “Mama ameambukizwa, baba ameambukizwa, mtoto ni mgonjwa, wazazi na mtoto watakufa, na wataacha mvulana wa miaka 10 ambaye atakuwa bila familia yoyote.”
Na, hatimaye, kuna uchunguzi wa makini wa Dakt. Ernest Drucker wa koleji ya madawa ya Albert Einstein katika New York. “Baada ya kifo cha mzazi, mara nyingi watoto hujipata katikati ya mapambano ya kung’ang’ania nani atawatunza, wakirushwa-rushwa kutoka kwa mshiriki mmoja wa familia hadi kwa mwingine hali wakijaribu kukabili msiba uliowapata na fedheha ya UKIMWI.”
UKIMWI kwa upesi unakuwa kisababishi kimojapo chenye kuongoza cha vifo miongoni mwa watoto na vijana waliokwisha kuwa watu wazima. Ndicho kisababishi cha tisa cha vifo miongoni mwa watoto kutoka umri wa mwaka mmoja hadi miaka minne, na kisababishi cha saba chenye kuongoza miongoni mwa matineja na watu wazima wa chini ya umri wa miaka 25. Kufikia miaka ya mapema ya 1990, UKIMWI ungeweza kuwa kimojapo visababishi vitano vyenye kuongoza cha vifo, likaripoti The AIDS/HIV Record, Septemba 1989. Ilhali, ripoti zaonyesha ukosefu wa kutojali ulimwenguni pote miongoni mwa wale wawezao kuambukizwa ugonjwa huu hatari. Fikiria mambo fulani ya hakika yenye kushtusha katika makala inayofuata.