Vijana Wanauliza...
UKIMWI—Je! Nimo Hatarini?
GAZETI Newsweek lilisema kwamba tangazo hilo ‘lilishtua ulimwengu.’ Mnamo Novemba 7, 1991, mwanariadha mashuhuri wa U.S. Earvin “Magic” Johnson alielezea watangazaji wa habari kwamba alikuwa amepatwa na virusi za UKIMWI. Baada ya kukiri huko kwenye kushtua, namba za simu za mashirika ya kutoa huduma juu ya UKIMWI zilisongwa na upigaji-simu. Hospitali nyingine zilisongwa na maombi ya watu wakitaka wapimwe kama wana UKIMWI. Watu wengine hata waliacha tabia yao ya kufanya ngono ovyoovyo—angalau kwa muda.
Labda vijana ndio waliopata pigo kubwa zaidi kutokana na tangazo hilo. Mkurugenzi wa huduma za afya katika chuo kikuu kimoja asema: “Wanafunzi walizingatia moyoni ujumbe wa kwamba ‘ulimpata, waweza kunipata’—kwa muda tu. . . . Kwa wanafunzi wengi, jambo lililompata Magic Johnson halitokezi mabadiliko katika tabia yao. Bado wanafikiri ‘hawawezi kuathiriwa.’”
Biblia ilitabiri kwamba nyakati zetu zingekuwa zenye “magonjwa ya kipuku,” yaani, maradhi ya kuambukiza yanayoenea upesi. (Luka 21:11) Kwa kweli UKIMWI unaweza kuitwa ugonjwa wa kipuku. Ilichukua miaka minane—kutokea 1981 hadi 1989—ili visa 100,000 vya kwanza vya UKIMWI vigunduliwe katika United States. Lakini ilichukua miaka miwili tu kwa visa 100,000 vya pili kuripotiwa!
Kulingana na Vituo vya U.S. vya Kudhibiti Maradhi, takwimu hiyo inayohuzunisha “inakazia mweneo wenye kuongezeka haraka wa [UKIMWI] katika United States.” Hata hivyo, UKIMWI ni ugonjwa unaoenea duniani pote, ukileta vifo na huzuni kupitia Afrika, Esia, Ulaya, na Amerika ya Latini. Ni jambo la maana kwamba Dakt. Marvin Belzer wa Hospitali ya Watoto katika Los Angeles aliuita UKIMWI kuwa “tatizo lenye kuogofya zaidi linalokabili vijana katika miaka ya 1990.”
Ambukizo Lenye Madhara Yaliyofichika
Maradhi hayo yasiyo ya kawaida ni nini, na kwa nini ni hatari sana? Madaktari waamini kwamba UKIMWI husitawi wakati kisehemu kidogo sana kinachoweza kuonekana tu kwa darubini—virusi iitwayo HIV (virusi ya ukimwi)—kinaposhambulia mkondo wa damu. Mara zikiisha kuingia humo, virusi hizo huanza kazi ya kutafuta na kuangamiza aina fulani ya chembechembe nyeupe za damu mwilini, zile chembechembe-saidizi aina za T za kinga. Chembechembe hizo hufanya kazi kubwa katika kusaidia mwili kupigana na maradhi. Hata hivyo, virusi za UKIMWI huzidhoofisha, na kuuharibu kabisa mfumo wa kinga.
Wakati mwingi waweza kupita kabla mtu aliyeambukizwa kujihisi mgonjwa. Wengine wanaweza kukosa dalili kwa karibu mwongo mmoja wa miaka. Lakini baadaye dalili kama mafua huanza kutokea—upungufu wa uzani na kupoteza hamu ya kula, homa, na kuhara. Mfumo wa kinga unapoendelea kupatwa na uharibifu wenye msiba, mgonjwa hupatwa kwa urahisi na maambukizo mengine mengi —kichomi, ambukizo la utando wa ubongo, kifua kikuu, au aina fulani za kansa—yanayoitwa ya kuotea kwa sababu yanatumia kikamili fursa inayotokezwa na kinga iliyodhoofishwa ya mgonjwa.
“Nahisi uchungu daima,” asema mgonjwa mmoja wa UKIMWI mwenye umri wa miaka 20. Ugonjwa huo umetokeza vidonda katika utumbo wake mpana na katika puru. Lakini, UKIMWI uliokomaa kabisa wamaanisha zaidi ya kukosa tu starehe na uchungu; kwa sababu huleta kifo kwa karibu wagonjwa wao wote. Tangu 1981 virusi hizo zimeenea kwa watu zaidi ya milioni moja katika United States pekee. Tayari watu zaidi ya 160,000 wamekwisha kufa. Wastadi wanatabiri kwamba kufikia mwaka wa 1995, idadi ya vifo itaongezeka maradufu. Kwa sasa hakuna tiba inayojulikana ya UKIMWI.
Vijana Wamo Hatarini
Kufikia sasa, ni asilimia ndogo sana ya visa vilivyoripotiwa vya UKIMWI—chini ya asilimia 1 katika United States—vinavyohusisha vijana. Kwa hiyo, huenda usijue binafsi vijana wowote waliokufa kutokana na ugonjwa huo. Jambo hilo halimaanishi kwamba vijana hawamo hatarini! Karibu sehemu moja kwa tano ya wagonjwa wote wa UKIMWI katika United States wamo katika umri wao wa miaka ya 20. Kwa sababu huchukua miaka mingi kwa dalili kutokea wazi, inaelekea sana kwamba wengi wa watu hao waliambukizwa wakiwa katika miaka ya utineja. Hali hii ya sasa ikiendelea, maelfu zaidi ya vijana watakuwa wagonjwa wa UKIMWI.
Kulingana na Vituo vya U.S. vya Kudhibiti Maradhi, virusi hiyo hatari huotea “katika damu, shahawa, na umajimaji wa uke wa watu walioambukizwa ugonjwa huo.” Kwa hiyo virusi ya UKIMWI hupitishwa kwa “kufanya ngono—ya kupitia uke, mkundu, au mdomo—na mtu aliyeambukizwa.” Watu wengi zaidi wamepatwa na ugonjwa huo kwa njia hiyo. UKIMWI waweza kupitishwa pia kwa “kutumia au kwa kudungwa sindano au sirinji ambayo imetumiwa na au kwa mtu aliyeambukizwa.” Na zaidi, “watu wengine wameambukizwa kwa utiwaji damu mishipani” ulio na virusi ya UKIMWI.—Voluntary HIV Counseling and Testing: Facts, Issues, and Answers.
Basi vijana wengi wamo hatarini. Idadi kubwa ya vijana (watu fulani wanasema kufikia kadiri ya asilimia 60 katika United States) wamejaribu kutumia dawa haramu za kulevya. Na kwa sababu baadhi ya dawa hizo za kulevya huingizwa mwilini kupitia sindano, kuna hatari kubwa ya kuambukizwa kupitia sindano zenye virusi. Kulingana na uchunguzi mmoja wa U.S., asilimia 82 ya wanafunzi wa shule za sekondari wametumia vileo, karibu asilimia 50 wakiwa wanafanya hivyo sasa. Huwezi kupata UKIMWI kwa kunywa chupa moja ya pombe, lakini baadaye inaweza kuathiri uamuzi wako na kukufanya uelekee zaidi kujiingiza katika tabia iliyo hatari zaidi—ngono ya ovyoovyo, ugoni wa jinsia moja au wa jinsia tofauti.
Katika 1970 chini ya asilimia 5 ya wasichana wenye umri wa miaka 15 walikuwa wamepata kufanya ngono. Kufikia 1988 idadi hiyo ilikuwa imeruka ikafika zaidi ya asilimia 25. Kufikia umri wa miaka 20, kama uchunguzi unavyoonyesha vilevile, asilimia 75 ya watu wa kike na asilimia 86 ya watu wa kiume katika United States hufanya ngono. Takwimu nyingine ya kuhofisha ni hii: Karibu kijana 1 kati ya vijana 5 amepata kufanya ngono na wenzi zaidi ya wanne. Ndiyo, vijana wengi zaidi na zaidi wanajiingiza katika ngono ya kabla ya ndoa, na wanaanza wakiwa wachanga kupita wakati mwingine wowote.
Hali ni mbaya kadiri iyo hiyo katika nchi nyinginezo. Katika nchi za Amerika ya Latini, kufikia robo tatu ya vijana matineja wamepata kufanya ngono ya kabla ya ndoa. Katika nchi za Kiafrika inaripotiwa kuwa wanaume wengi wamechagua wasichana matineja kuwa wenzi wa kingono katika jitihada ya kujikinga na virusi ya UKIMWI. Matokeo yakiwa nini? Ongezeko kubwa sana la visa vya UKIMWI miongoni mwa wasichana matineja wa Kiafrika.
Mweneo wa UKIMWI haujakomesha mwenendo huo wenye kudhuru sana. Ebu fikiria nchi moja ya Amerika ya Latini. Zaidi ya asimilia 60 ya “vijana waseja wenye kufanya ngono wamo katika hatari kubwa ya kupata virusi ya UKIMWI.” Hata hivyo, vijana chini ya asilimia 10 ndio wanaohisi kwamba wamo hatarini. Wanajiambia: ‘Sitapatwa nao.’ Lakini nchi hiyo ina “mojapo viwango vya juu zaidi vya ambukizo la virusi ya UKIMWI katika nchi za Amerika.”—Vituo vya U.S. vya Kudhibiti Maradhi.
Unaweza Kupatwa Nao!
Mweneo wa UKIMWI wathibitisha ukweli wa maonyo ya Biblia kwamba ‘mwisho wa’ ukosefu wa adili ya ngono “ni mchungu kuliko pakanga.” (Mithali 5:3-5; 7:21-23) Bila shaka, kwa msingi Biblia inarejezea uharibifu wa kiroho na kihisia moyo. Lakini si jambo la kutustaajabisha kwamba ukosefu wa adili za ngono pia una miisho mbalimbali yenye uharibifu wa kimwili.
Basi ni jambo la maana kwamba vijana wakabiliane kihalisi na hatari ya kuambukizwa UKIMWI na maradhi mengine yanayopitishwa kingono. Ule mtazamo wa kujiridhisha kwamba UKIMWI ‘hautanipata’ waweza kuwa hatari sana. “Unapokuwa na umri wa miaka kumi na mitano au kumi na sita au hata kumi na saba, kumi na minane, kumi na tisa, au ishirini, unataka kufikiri kwamba huwezi kuupata,” asema mwanamume mmoja kijana anayeitwa David. Hata hivyo, mambo ya hakika yathibitisha kinyume cha hilo. David alipatwa na virusi za UKIMWI akiwa na umri wa miaka 15.
Basi, tukisema waziwazi: Ikiwa unatumia dawa haramu za kulevya au unajiingiza katika ngono kabla ya ndoa, umo hatarini! Lakini vipi juu ya madai kwamba mtu anaweza kufanya “ngono salama”? Je! kuna njia halisi za kujikinga na ugonjwa huo wenye kuenea? Makala yetu itakayofuata katika mfululizo huu itazungumzia maswali hayo.
[Sanduku katika ukurasa wa 18]
Maradhi Mengine Yanayopitishwa Kingono
UKIMWI umekuwa ndio vichwa vikuu vya habari. Hata hivyo, The Medical Post laonya hivi: ‘Kanada imo katikati ya mweneo wa maradhi yanayopitishwa kingono miongoni mwa vijana.’ Na si Kanada pekee. “Kila mwaka vijana milioni 2.5 wa U.S. huambukizwa ugonjwa fulani unaopitishwa kingono,” chasema Kituo cha Mapendezi ya Umma chenye makao huko U.S. “Idadi hiyo yawakilisha kijana mmoja kwa kila vijana sita wenye kufanya ngono na sehemu moja kwa tano ya visa vya maradhi yanayopitishwa kingono.”
Kwa kielelezo, kaswende ambao wakati mmoja ulifikiriwa waelekea kutokomea, umerudi katika miaka ya karibuni, ukiambukiza vijana wengi zaidi ya wakati mwingine. Kisonono na klamdia (maradhi yanayopitishwa kingono yenye kuenea zaidi katika United States) pia yamekinza jitihada za kuyaangamiza. Na vijana wana kiwango cha juu zaidi cha kuambukiwa. The New York Times vilevile laripoti “ongezeko kubwa” la idadi ya vijana wenye ugonjwa wa madutu ya viungo vya uzazi. Maelfu ya vijana pia wana virusi za ugonjwa wa malengelenge. Kulingana na Science News, “watu wenye malengelenge ya viungo vya uzazi wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuambukizwa [virusi] zinazosababisha UKIMWI.”
Kituo cha Mapendezi ya Umma chasema hivi: “Ingawa vijana wana viwango vya juu sana vya maradhi yanayopitishwa kingono kuliko kikundi cha umri mwingine wowote, hawaelekei sana kutibiwa. Yakiachwa bila kutambuliwa na bila kutibiwa, maradhi yanayopitishwa kingono hudhuru sana kwa kutokeza maradhi ya kuchochota nyonga, kutoweza kuzaa, uchukuaji mimba wa nje ya tumbo la uzazi, na kansa ya shingo ya mji wa mimba.”
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Mtu yeyote anayejidunga dawa haramu za kulevya au anayejiingiza katika ngono ya ovyoovyo hujiweka katika hatari kubwa ya kupatwa na UKIMWI