Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada Yaimarisha Haki za Wazazi
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KANADA
MTOTO wenu anapokabili matatizo mazito ya kitiba, mkiwa wazazi wenye upendo kwa kawaida nyinyi huhangaika na kuona wasiwasi. Jinsi inavyowatia moyo na kuwafariji wakati madaktari wenye kuchukua mambo kwa uzito, wenye huruma wanapostahi uchaguzi wenu wa utibabu! Hata hivyo, hali huzuka ambapo hatua ya kishupavu huchukuliwa na matamanio ya wazazi hupuuzwa. Mara nyingi sana hili huongoza kwenye hali yenye kuumiza.
Katika Kanada sheria zinazolinda watoto hutoa mamlaka kwa maofisa wa serikali kuwa na mamlaka juu ya watoto. Wilaya nne zinaruhusu serikali kupuuza machaguo ya kimzazi bila usikizi wa kihukumu. Hili hutokeza masuala ya maana kwa wazazi na watoto wote. Wazazi wanaweza kufanya maamuzi kuhusu nini? Ikiwa serikali yachagua kuingilia uamuzi wa kimzazi, ni taratibu gani yapasa kufuatwa ili kuandalia wazazi na watoto haki ya kimsingi? Je, Katiba hulinda ufanyaji-maamuzi wa kimzazi?
Makala iliyotokea katika The Toronto Star la Machi 3, 1995, ambayo ilifanyia muhtasari masuala hayo kwa kuwa yalihusiana na kesi iliyohusisha mtoto msichana aliyezaliwa kabla ya wakati katika 1983. Wazazi wake walikuwa Mashahidi wa Yehova. “[Wao] wangekubali mengi ya matibabu ya kitiba lakini walikataa utiaji-damu mishipani. Madaktari waliomba amri ya mahakama. Hakimu alipatia Shirika la Msaada wa Watoto udhibiti juu ya huyo mtoto. Hakuna damu iliyopewa huyo mtoto hadi majuma matatu baadaye, na hili lilikuwa tu kwa ajili ya matayarisho ya uchunguzi wa jicho usio wa lazima na upasuaji ambao huenda ungefanywa. Wazazi walipinga hadi kesi ilipopelekwa kwa Mahakama Kuu Zaidi.”
Hukumu ilitolewa Januari 27, 1995, na ingawa Mahakama Kuu Zaidi haikutangua kile kilichokuwa kimefanywa katika 1983, watano wa mahakimu tisa walitoa miongozo ya kuzuia kutumia vibaya mamlaka ya serikali. Uamuzi wa Mahakama waimarisha haki za wazazi kufanya maamuzi ya kitiba kwa ajili ya watoto wao.
Kihususa, Mahakama ilifikiria ufanyaji-maamuzi wa kimzazi kwa upande wa uhuru wa kidini unaohakikishwa na Canadian Charter of Rights and Freedoms. Hakimu Gerard La Forest, akiwakilisha walio wengi, alitaarifu hivi: “Haki ya wazazi kulea watoto wao kulingana na itikadi zao za kidini, kutia ndani kuchagua matibabu ya kitiba na matibabu mengine, vilevile ni sehemu ya maana ya uhuru wa dini.”
Hii ndiyo mara ya kwanza ambapo mahakama kuu ya Kanada imeamua kwamba uhuru wa dini ulio chini ya Charter hutia ndani haki ya wazazi kuchagua utibabu wa kitiba kwa ajili ya watoto wao. Hakimu La Forest aliweka wazi kanuni hii alipotaarifu hivi: “Hii haimaanishi kwamba serikali haiwezi kuingilia inapoona likiwa jambo la lazima kulinda haki au afya ya mtoto. Lakini mwingilio kama huo lazima ufanywe kwa haki. Kwa maneno mengine, ufanyaji-maamuzi wa kimzazi lazima upate ulinzi wa Charter ili mwingilio wa serikali usimamiwe ifaavyo na mahakama, na lazima uruhusiwe tu wakati unapopatana na kanuni zifaazo zenye msingi wa Charter.”
Hakimu La Forest alikazia uhitaji wa kufanya kuwa haki mwingilio dhidi ya ufanyaji-maamuzi wa kimzazi wakati alipoitikia maelezo yaliyofanywa na wawili wa mahakimu wenzake: “Baadhi ya maelezo yao huenda yakaeleweka kuwa yanaunga mkono kutanguliwa kwa haki za mzazi kwa sababu tu mtaalamu wa kitiba anafikiri ni jambo la lazima kufanya hivyo. Ningehangaishwa sana ikiwa mtaalamu wa kitiba angeweza kutangua maoni ya mzazi bila kuonyesha ulazima wa kufanya hivyo.”
Ufanyaji-maamuzi wa kimzazi kuhusiana na utibabu wa kitiba ulitambulishwa kuwa wa haki kikatiba chini ya Canadian Charter of Rights and Freedoms. Hivyo, ujumbe wenye nguvu uliwasilishwa kwa maofisa wa utunzi wa afya ya watoto na mahakimu. Lazima watende kwa tahadhari na kwa staha ifaayo kwa haki za wazazi. Madaktari wanaohusika pia watakubali miongozo hii katika maana ya kwamba wataunga mkono chaguo la kimzazi la matibabu ya badala yafaayo, kutia ndani matibabu ya kitiba yasiyohusisha damu kwa ajili ya watoto.
Kwa kufikiria majadiliano ya sasa kuhusu utiaji-damu mishipani na hatari zao zijulikanazo, kutia ndani UKIMWI, mtu anaweza kuona umaana wa elezo la Hakimu La Forest alipoongeza hivi: “Wasiwasi uliotolewa na wenye kukata rufani katika rufani ya wakati huu unatokeza suala linalohusu kufaa kwa kuendelea na matibabu ambayo manufaa yayo ya kitiba ni yenye kutilika shaka sana . . . Hata hivyo, uthibitisho wa kitiba uliotolewa katika 1983 . . . hauturuhusu tutilie shaka uhitaji wa utiaji-damu mishipani, ingawa wengine huenda kwa kurudisha akili nyuma wakatamani sana kufanya hivyo. Hata hivyo, rufani hii yatukumbusha umaana wa kuendelea na utunzi wakati wa kutangua ukataaji wa kimzazi.”—Italiki ni zetu.
Makala iliyotajwa mbeleni iliyokuwa katika The Toronto Star ilimalizia hivi: “Ni nini kimetimizwa katika uamuzi wa Mahakama Kuu Zaidi? Kwanza, madaktari, wazazi, wafanyakazi wa umma na mahakimu sasa wana miongozo kwa ajili ya wakati ambapo tofauti ya maoni kati ya wazazi na madaktari itokeapo. Pili, mkazo juu ya matibabu ya badala ya kitiba wapasa kufanya kunyumbuka zaidi kuwezekane kuhusu suala la utibabu wa kutia damu mishipani katika wakati ambapo matibabu ya badala zaidi na zaidi yanatokezwa na kupatikana. Tatu, uamuzi unapofanywa wa kutafuta kutanguliwa kwa uamuzi wa wazazi, lazima kuwe na usikizi wa haki katika mahakama jukumu la ithibati likiwa juu ya serikali na madaktari kuthibitisha uhitaji wa mwingilio unaokusudiwa.”
Madaktari wa kitiba, mahakimu, na wazazi katika nchi nyinginezo bila shaka watapata miongozo iliyotolewa kupitia uamuzi wa walio wengi katika Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada, kuwa yenye misaada na ya kufaa. Inatumainiwa kwamba madaktari wa kitiba kila mahali wataendelea kuandaa utunzi wa kitiba katika njia ya kufikiria hisia na yenye huruma wakifikiria haki za watoto na pia za wazazi.