Wewe Una Haki ya Kuchagua
Njia ya kisasa ya kitiba (iitwayo uchanganuzi wa hatari/manufaa) inafanya iwe rahisi zaidi kwa madaktari na wagonjwa kushirikiana katika kuepuka utibabu wa kutumia damu. Madaktari hupima mambo kama vile hatari za madawa au upasuaji na manufaa zinazoweza kuwapo. Wagonjwa waweza pia kushiriki katika uchanganuzi huo.
Acheni tutumie kielelezo kimoja ambacho watu wengi wanaweza kujihusisha nacho—ugonjwa wenye kusedeka wa tezi za kooni. Kama ungekuwa na tatizo hilo inaelekea ungeenda kwa daktari. Kwa kweli, huenda ukawaona wawili, kwa kuwa mara nyingi wataalamu wa afya hupendekeza kupata wazo la pili. Huenda mmoja akapendekeza upasuaji. Atoa muhtasari wa kinachomaanishwa na hilo: Muda wa kukaa hospitalini, kiasi cha maumivu, na gharama. Kwa habari ya hatari, asema kwamba kutokwa damu sana si jambo linalowapata watu wengi na kifo kutokana na upasuaji huo chatokea mara chache sana. Lakini daktari anayetoa wazo la pili akuhimiza ujaribu utibabu wa dawa za kuua viini. Akufafanulia namna ya dawa, uwezekano wa kufanikiwa, na gharama. Kwa habari ya hatari, asema kwamba ni wagonjwa wachache sana wanaopatwa na matokeo mabaya yenye kutisha uhai kutokana na hiyo dawa ya kuua viini.
Yaelekea kila tabibu hodari alifikiria hatari na manufaa, lakini sasa wewe lazima upime hatari au manufaa hizo, pamoja na mambo mengine unayoyajua vizuri zaidi. (Wewe uko katika hali bora zaidi kufikiria pande kama vile imara yako ya kihisia-moyo na ya kiroho, fedha za jamaa, athari juu ya jamaa, na maadili yako mwenyewe.) Ndipo wafanya uchaguzi. Yawezekana watoa idhini baada ya kuaarifiwa upate utibabu mmoja lakini wakataa ule mwingine.
Ndivyo ingekuwa pia ikiwa ni mtoto wako ambaye angekuwa na ugonjwa huo wenye kusedeka wa tezi za kooni. Nyinyi mlio wazazi wenye upendo mnaoathiriwa sana moja kwa moja na ambao mtakuwa na daraka la kukabiliana na matokeo mngepewa muhtasari juu ya hatari, manufaa, na matibabu. Baada ya kufikiria pande zote, mnafanya uchaguzi baada ya kuarifiwa juu ya jambo hili linalohusu afya ya mtoto wenu na hata uhai wake. Labda nyinyi mwatoa idhini ya upasuaji, pamoja na hatari zao. Wazazi wengine huenda wakachagua dawa za kuua viini, pamoja na hatari zazo. Kama vile matabibu hutofautiana katika shauri lao, ndivyo wagonjwa au wazazi hutofautiana kwa habari ya wanachohisi kuwa ndicho kilicho bora. Hiyo ni sehemu inayoeleweka ya kufanya machaguo baada kuarifiwa (ya hatari/manufaa).
Namna gani utumizi wa damu? Hakuna yeyote achunguzaye mambo hakika kwa jinsi yalivyo awezaye kukana kwamba utiaji-damu mishipani unahusu hatari kubwa. Dakt. Charles Huggins, ambaye ni mwelekezi wa utumishi wa utiaji-damu mishipani kwenye Hospitali Kuu ya Massachusetts, alieleza jambo hili wazi sana: “Damu haijapata kamwe kuwa salama zaidi kama ilivyo sasa. Lakini bila kuepukika lazima ionwe kuwa isiyo salama. Ndicho kitu hatari zaidi tunachotumia katika utibabu.”—The Boston Globe Magazine, Februari 4, 1990.
Kukiwa na sababu nzuri, wafanya kazi wa kitiba wameshauriwa: “Inahitajiwa kabisa kukadiria upya pia ile sehemu ya hatari/manufaa ya utiaji-damu mishipani na kutafuta matibabu mengine.” (Italiki ni zetu.)—Perioperative Red Cell Transfusion, kongomano la Mashirika ya Afya ya Taifa, Juni 27-29, 1988.
Matabibu huenda wasiafikiane kwa habari ya manufaa au hatari katika kutumia damu. Huenda mmoja akatoa utiaji-damu mwingi na awe anasadikishwa kwamba unahalisi hatari hiyo. Mwingine huenda akahisi hauhalisi hatari hizo, kwa kuwa amekuwa na matokeo mazuri kwa kutibu bila damu. Hata hivyo, mwishowe kabisa, wewe, uliye mgonjwa au mzazi, lazima uamue. Kwa nini wewe? Kwa sababu mwili, uhai, maadili, na jambo la maana sana uhusiano wako (au wa mtoto wako) na Mungu wahusika.
HAKI YAKO INATAMBULIWA
Katika mahali pengi leo, mgonjwa ana haki isiyoweza kuhalifiwa ya kuamua atakubali utibabu upi. “Ile sheria ya idhini ya kuarifiwa ina msingi wa mambo mawili: kwanza, kwamba mgonjwa ana haki ya kupokea habari ya kutosha ili kufanya uchaguzi baada ya kuarifiwa kuhusu utibabu uliopendekezwa; na pili, kwamba mgonjwa aweza kuchagua kukubali au kukataa pendekezo la tabibu. . . . Isipokuwa wagonjwa wanaonwa kuwa wana haki ya kusema la, na pia ndiyo, na hata ndiyo pamoja na masharti, sababu nyingi za idhini baada ya kuarifiwa hutoweka.”—Informed Consent—Legal Theory and Clinical Practice, 1987.a
Wagonjwa fulani wamepata ukinzani wakati wamejaribu kutumia haki yao. Huenda ukinzani huo ulikuwa umetoka kwa rafiki aliye na hisia imara juu ya upasuaji wa kuondolewa tezi za kooni zenye ugonjwa au juu ya dawa za kuua viini. Au huenda tabibu akawa alikuwa amesadikishwa juu ya usahihi wa shauri lake. Huenda hata ofisa wa hospitali alikataa, kwa msingi wa mapendezi ya kisheria au ya kifedha.
“Madaktari wa mifupa wengi wanachagua kutofanya upasuaji kwa wagonjwa [Mashahidi],” asema Dakt. Carl L. Nelson. “Ni imani yetu kwamba mgonjwa ana haki ya kukataa namna yoyote ya utibabu. Ikiwa inawezekana kiufundi kuandaa upasuaji kwa usalama bila kutumia utibabu hususa, kama vile utiaji-damu mishipani, basi wapaswa kuwapo ukiwa wa hiari.”—The Journal of Bone and Joint Surgery, Machi 1986.
Mgonjwa mwenye ufikirio hatamsonga tabibu atumie utibabu ambao daktari hana ujuzi nao. Hata hivyo, kama Dakt. Nelson alivyosema, matabibu wengi waliojitoa wanaweza kukubaliana na imani za mgonjwa. Ofisa mmoja Mjeremani alishauri: “Dakt. hawezi kukataa kutoa msaada . . . akisababu kwamba matibabu mengine yote ya kitiba hayapatikani kwake ayatumie kwa Shahidi wa Yehova. Yeye angali ana wajibu wa kutoa msaada hata wakati njia zilizo wazi kwake kuzitumia zimepunguzwa.” (Der Frauenarzt, Mei-Juni 1983) Vivyo hivyo, hospitali ziko si ili zichume pesa tu bali ili kutumikia watu wote bila ubaguzi. Mwanatheolojia Mkatoliki Richard J. Devine ataarifu: “Ijapokuwa lazima hospitali itie jitihada nyingine zozote za kitiba kuhifadhi uhai na afya ya mgonjwa, ni lazima ihakikishe kwamba utunzaji wa kitiba hauhalifu dhamiri [yake]. Zaidi ya hilo, ni lazima iepuke namna zote za kushurutisha, kutoka kubembeleza mgonjwa hadi kupata agizo la mahakama kulazimisha utiaji-damu mishipani.”—Health Progress, Juni 1989.
BADALA YA MAHAKAMA
Watu wengi huafiki kwamba mahakama si mahali panapofaa kwa masuala ya kibinafsi ya kitiba. Ungehisije ikiwa wewe ungechagua kutumia utibabu wa dawa za kuua viini lakini mtu mwingine aende mahakamani ili kukulazimisha upate upasuaji wa kuondoa tezi za kooni zenye ugonjwa? Huenda daktari akataka kuandaa kile anachofikiria kuwa utunzaji bora, lakini yeye hana wajibu wa kutafuta utetezi wa kisheria ili akanyagie chini haki zako za msingi. Na kwa kuwa Biblia huweka kushika mwiko wa damu katika kiwango kile kile cha kiadili pamoja na kuepuka uasherati, kulazimisha damu juu ya Mkristo kungekuwa sawa na kulazimisha ngono—ugoni wa kinguvu.—Matendo 15:28, 29.
Hata hivyo, jarida Informed Consent for Blood Transfusion (1989) huripoti kwamba mahakama fulani husononeka sana wakati mgonjwa ana nia ya kupokea hatari fulani kwa sababu ya haki zake za kidini hivi “kwamba zinatunga tofauti fulani za kisheria—hadithi za kutungwa za kisheria, ukipenda—ili kuruhusu damu itiwe.” Huenda zikajaribu kuitolea udhuru kwa kusema kwamba mimba inahusika au kwamba kuna watoto wa kupewa riziki. “Hizo ni hadithi za kutungwa za kisheria,” chasema kitabu hicho. “Watu wazima walio hodari wana haki ya kukataa utibabu.”
Baadhi ya wale wanaosisitizia utiaji-damu mishipani hupuuza uhakika wa kwamba Mashahidi hawakatai matibabu yote. Wanakataa utibabu mmoja tu, ambao hata wataalamu husema unajawa na hatari. Kwa kawaida tatizo la kitiba laweza kutatuliwa kwa njia mbalimbali. Njia moja ina hatari hii, nyingine hatari ile. Je! mahakama au daktari kwa kutwaa daraka la ubaba aweza kujua ni hatari ipi ‘inayoyafaa masilahi yako bora’? Wewe ndiwe wa kuamua hilo. Mashahidi wa Yehova ni imara hivi kwamba hawataki mtu mwingine awafanyie uamuzi; ni daraka lao la kibinafsi mbele za Mungu.
Mahakama ikilazimisha juu yako utibabu wenye kukirihika, huenda hilo likaathirije dhamiri yako na lile jambo lenye umuhimu la nia yako ya kuishi? Dakt. Konrad Drebinger aliandika: “Hakika ingekuwa namna ya kujitakia makuu ya kitiba iliyoongozwa vibaya ambayo ingemwongoza mtu alazimishe mgonjwa apokee utibabu fulani, kuikandamiza dhamiri yake, ili kumtibu kimwili lakini uipe nafsi yake pigo la kifo.”—Der Praktische Arzt, Julai 1978.
UTUNZAJI WENYE UPENDO KWA WATOTO
Kesi za mahakamani kuhusu damu sana-sana zahusiana na watoto. Pindi fulani, wakati wazazi wenye upendo wanapoomba kwa staha kwamba utibabu usiotumia damu utumiwe, wafanya kazi fulani wa kitiba wametumia mahakama iwaunge mkono ili kumpa mgonjwa damu. Bila shaka, Wakristo huafikiana na sheria au hatua ya mahakama ili kuzuia mtoto asitendwe vibaya au asiachwe bila kutunzwa. Labda wewe umesoma juu ya kesi ambazo katika hizo mzazi fulani alimtenda mtoto kinyama au akamnyima utunzaji wote wa kitiba. Ni tanzia kama nini! Kwa wazi, Serikali yaweza na yapaswa kuingilia ili kumlinda mtoto asiyetunzwa. Na bado, ni rahisi kuona jinsi ilivyo tofauti wakati mzazi mwenye kujali anapoomba utabibu wa hali bora usiotumia damu.
Kwa kawaida kesi hizi za mahakama hukazia fikira watoto walio hospitalini. Mtoto huyo alipataje kuwa humo, na kwa nini? Karibu sikuzote wazazi wenye kuhangaikia walimleta mtoto wao apate utunzaji bora. Hata kama vile Yesu alivyopendezwa na watoto, wazazi Wakristo wanatunza watoto wao. Biblia hunena juu ya ‘mama mlezi atunzaye watoto wake.’ Mashahidi wa Yehova wana upendo huo wenye kina kwa watoto wao.—1 Wathesalonike 2:7; Mathayo 7:11; 19:13-15.
Kiasili, wazazi wote hufanya maamuzi yanayoathiri usalama na uhai wa watoto wao: Je! jamaa itatumia gesi au mafuta kupasha joto makao yao? Je! wataenda pamoja na mtoto wao wanapoenda safari ndefu kwa gari? Je! aweza kwenda kuogelea? Mambo hayo yanahusu hatari fulani, hata za uhai na kifo. Lakini jamii hutambua busara ya kimzazi, hivyo wazazi wanapewa nafasi kubwa ya uamuzi katika karibu maamuzi yote yanayoathiri watoto wao.
Katika 1979 Mahakama Kuu ya U.S. ilitaarifu waziwazi hivi: “Wazo la sheria juu ya jamaa hutegemea dhana ya kwamba wazazi wana kile ambacho mtoto anakosa kwa habari ya ukomavu, ujuzi, na uwezo wa kutumia busara nzuri unaotakwa ili kufanya maamuzi magumu ya maisha. . . . Kwa sababu tu uamuzi wa mzazi [juu ya jambo la kitiba] unahusu hatari [huo] hauhamishi mara moja nguvu za kufanya uamuzi huo kutoka kwa wazazi kwenda kwenye wakala au ofisa fulani wa serikali.”—Parham v. J. R.
Mwaka uo huo Mahakama ya Rufani ya New York ilitoa hukumu hii: “Jambo lililo la maana zaidi ya yote katika kujua kama mtoto ananyimwa utunzaji wa kitiba wa kutosha . . . ni kama wazazi wameandalia mtoto wao matibabu ya kutosha yenye kupokeleka kwa kufikiria hali zote zinazozunguka. Ulizio hili haliwezi kutokezwa kwa masharti ya kama mzazi amefanya uamuzi ‘unaofaa’ au ‘wenye kosa,’ kwa maana hali ya sasa ya utibabu, ijapokuwa maendeleo yao makubwa sana, huruhusu mara chache sana mikataa dhahiri kama hiyo. Wala mahakama haiwezi kujitwalia daraka la kuwa mzazi mlezi.”—In re Hofbauer.
Kumbuka kile kielelezo cha wazazi kuchagua kati ya upasuaji na dawa za kuua viini. Kila mmojapo utibabu ungekuwa na hatari zao wenyewe. Wazazi wenye upendo wana daraka la kupima hatari, manufaa, na mambo mengine ndipo wafanye uchaguzi. Kuhusiana na hilo, Dakt. Jon Samuels (Anesthesiology News, Oktoba 1989) alidokeza kufanya pitio la Guides to the Judge in Medical Orders Affecting Children, lililochukua msimamo huu:
“Maarifa ya kitiba hayakuendelea vya kutosha kumwezesha tabibu kutabiri kwa uhakika wowote wa kiakili kwamba mgonjwa wake ataishi au atakufa . . . Ikiwa kuna uchaguzi wa taratibu za kufuatwa—ikiwa, kwa kielelezo, daktari anapendekeza utaratibu fulani ulio na uelekeo wa asilimia 80 ya mafanikio lakini ambao wazazi wanakataa kukubalia, na wazazi hao hawakatai utaratibu fulani ulio na uelekeo wa asilimia 40 tu ya mafanikio—ni lazima daktari afuate mwendo ulio hatari zaidi kitiba lakini usiokatalika kwa wazazi.”
Kwa sababu ya zile hatari nyingi zenye kuleta kifo katika utumizi wa kitiba wa damu ambazo zimetokea na kwa sababu kuna matibabu mengine ya kutumia yenye mafanikio, je! kuepuka damu hakuwezi hata kukawa ndiko kwenye hatari zilizo za chini zaidi?
Kiasili, Wakristo hupima mambo mengi ikiwa mtoto wao anahitaji upasuaji. Kila upasuaji, uwe wa kutumia au kutotumia damu, una hatari. Ni daktari mpasuaji yupi ambaye hutoa mahakikisho? Huenda wazazi wakajua kwamba matabibu stadi wamekuwa na mafanikio mazuri katika upasuaji usiotumia damu juu ya watoto Mashahidi. Hivyo hata ikiwa tabibu au ofisa wa hospitali anapendelea utabibu mwingine, badala ya kusababisha pambano la kimahakama lenye kuleta mkazo na kumaliza sana wakati, je! si jambo la akili kushirikiana pamoja na wazazi wenye upendo? Ama sivyo huenda wazazi wakahamisha mtoto wao kumpeleka kwenye hospitali nyingine ambako wafanya kazi wana ujuzi wa kushughulikia visa kama hivyo na wana nia ya kufanya hivyo. Kwa kweli, utibabu wa bila kutumia damu utaelekea zaidi kuwa utunzaji bora, kwa maana unaweza kusaidia jamaa ‘ifikie miradi halali ya kitiba na isiyo ya kitiba,’ kama tulivyoona mapema kidogo zaidi.
[Maelezo ya Chini]
a Ona makala ya kitiba “Damu: Uchaguzi wa Nani na Dhamiri ya Nani?” iliyochapwa upya katika Nyongeza, katika kurasa 30-1.
[Sanduku katika ukurasa wa 18]
KUONDOA MAHANGAIKO YA KISHERIA
Huenda ukauliza, ‘Kwa nini madaktari na mahospitali fulani hufanya haraka kupata agizo la mahakama ili wampe mgonjwa damu?’ Katika mahali fulani sababu ya kawaida ni kuhofu kupasishwa daraka.
Hakuna msingi kwa hangaiko kama hilo wakati Mashahidi wa Yehova wanapochagua kushughulikiwa bila damu. Daktari mmoja kwenye Koleji Albert Einstein ya Tiba (U.S.A.) aliandika: “[Mashahidi] walio wengi hutia sahihi kwa utayari ile fomu ya American Medical Association, wakiondolea matabibu na mahospitali kupasishwa daraka, na wengi hubeba [kadi ya] Medical Alert. Fomu ya ‘Kukataa Kukubali Vitu Vilivyofanyiza kwa Damu’ iliyotiwa sahihi na kuandikwa tarehe, ni mwafaka-mkataba na inawapasisha wajibu wa kisheria kuifuata.”—Anesthesiology News, Oktoba 1989.
Ndiyo, kwa ushirikiano Mashaidi wa Yehova wanatoa uhakikisho wa kisheria kwamba tabibu au hospitali haitapasishwa daraka kwa kuandaa utibabu ulioombwa usiotumia damu. Kama ilivyopendekezwa na wataalamu wa kitiba, kila shahidi hubeba kadi ya Medical Document. Hii hujazwa upya kila mwaka na hutiwa sahihi na mtu huyo na mashahidi, mara nyingi mtu wa ukoo wake wa karibu.
Katika Machi 1990, Mahakama Kuu Zaidi ya Ontario, Kanada, ilitegemeza uamuzi uliotoa maelezo kwa kukubali juu ya hati hiyo: “Kadi hiyo ni julisho rasmi lililoandikwa la msimamo halali ambao mbebaji wa kadi aweza kuchukua kisheria katika kuweka kizuizi kilichoandikwa juu ya mkataba pamoja na daktari.” Katika Medicinsk Etik (1985), Profesa Daniel Andersen aliandika: “Ikiwa kuna taarifa inayoeleweka iliyoandikwa na mgonjwa ikisema kwamba yeye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova na kwamba hataki damu chini ya hali zozote, staha kwa hiari ya mgonjwa hutaka kwamba tamaa hiyo istahiwe, kama tu vile ingekuwa imesemwa kwa mdomo.”
Pia Mashahidi watatia sahihi fomu za hospitali za idhini. Moja inayotumiwa kwenye hospitali katika Freiburg, Ujeremani, ina nafasi wazi ambapo tabibu angeeleza habari aliyompa mgonjwa juu ya utibabu. Ndipo, juu ya sahihi za tabibu na mgonjwa, fomu hiyo huongeza: “Mimi mshiriki wa shirika la Mashahidi wa Yehova, ninakataa katakata utumizi wa damu ngeni au sehemu za damu wakati wa upasuaji wangu. Mimi najua kwamba utaratibu uliopangwa hivyo una hatari ya juu zaidi kwa sababu ya matatanisho ya kutokwa damu. Baada ya kupokea maelezo kamili hasa juu ya hilo, naomba kwamba upasuaji unaohitajiwa ufanywe bila kutumia damu ngeni au sehemu za damu.”—Herz Kreislauf, Agosti 1987.
Kwa kweli, kutibiwa bila damu huenda kukawa na hatari za chini zaidi. Lakini jambo kubwa hapa ni kwamba wagonjwa Mashahidi huachilia kwa furaha mahaingako yoyote ya bure ili kwamba wafanya kazi wa kitiba waweze kusonga mbele katika kufanya yale waliyojitoa kufanya, wakisaidia watu wapone. Ushirikiano huu hunufaisha wote, kama Dakt. Angelos A. Kambouris alivyoonyesha katika “Upasuaji Mkubwa wa Fumbatio Juu ya Mashahidi wa Yehova”:
“Mwafaka wa kabla ya upasuaji wapaswa kuonwa na daktari mpasuaji kuwa wa lazima na apaswa ashikamane nao bila kujali matukio yanayositawi wakati wa na baada ya upasuaji. [Hili] lawafanya wagonjwa wawe na maoni chanya kuhusu utibabu wa upasuaji, na linaondoa uangalifu wa daktari mpasuaji kutoka kwenye mafikirio ya kisheria na ya kifalsafa kuyaelekeza kwenye yale ya upasuaji na ya kiufundi, na hivyo, kumruhusu afanye vizuri sana na kutumikia masilahi bora ya mgonjwa wake.”—The American Surgeon, Juni 1987.
[Sanduku katika ukurasa wa 19]
‘‘Kutumia kupita kiasi tekinolojia ya kitiba ni jambo moja kubwa lenye kuleta ongezeko la sasa la gharama za utunzaji wa afya. . . . Utiaji-damu mishipani ni wenye umaana hasa kwa sababu una uwezekano mkubwa wa kuleta gharama na hatari. Kwa sababu hiyo, utiaji-damu mishipani uliainishwa na American Joint Commission on Accreditation of Hospitals kuwa ‘kiasi cha juu, hatari ya juu na wenye kuelekea kuwa na makosa.’”—“Transfusion,” Julai-Agosti 1989.
[Sanduku katika ukurasa wa 20]
United States: “Sababu ya uhitaji wa idhini ya mgonjwa ni lile wazo la kiadili la hiari ya mtu mmoja mmoja, kwamba maamuzi juu ya yatakayompata mtu mwenyewe yapasa kufanywa na mtu mwenyewe anayehusika. Sababu ya kisheria ya kutaka idhini ni kwamba tendo la kitiba linalofanywa bila idhini ya mgonjwa huwa ni kuumiza.”—“Informed Consent for Blood Transfusion,” 1989.
Ujeremani: “Haki ya mgonjwa ya kujiamulia mwenyewe hutangua ile kanuni ya kutoa msaada na kuhifadhi uhai. Kama tokeo: hakuna kutia damu mishipani dhidi ya hiari ya mgonjwa.”—“Herz Kreislauf,” Agosti 1987.
Japani: “Hakuna ‘kabisa’ katika ulimwengu wa kiti- ba. Madaktari waamini kwamba mwendo wa ki-siku-hizi wa tiba ndio bora zaidi na wafuata mwendo wayo, lakini hawapaswi kulazimisha kila jambo layo kuwa ‘kabisa’ juu ya wagonjwa. Wagonjwa pia lazima wawe na uhuru wa uchaguzi.”—“Minami Nihon Shimbun,” Juni 28, 1985.
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
‘‘Mimi nimepata kwamba jamaa [za Mashahidi wa Yehova] ni zenye kushikamana sana na zenye upendo,” aripoti Dakt. Lawrence S. Frankel. “Watoto ni wenye elimu, wenye kujali, na wenye staha. . . . Hata inaonekana kuna uwezekano wa kuwa na utii imara zaidi kwa miongozo ya kitiba, ambao huenda ukawakilisha jitihada ya kuruhusu kujiingiza kwa kitiba kwa kadiri imani zao zaruhusu.”—Department of Pediatrics, M. D. Anderson Hospital and Tumor Institute, Houston, U.S.A., 1985.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
‘‘Mimi ninahofu kwamba ni jambo la kawaida,” aeleza Dakt. James L. Fletcher, Jr., “kiburi cha ujuzi wa kazi kuchukua mahali pa busara nzuri ya kitiba. Matibabu yanayoonwa kuwa ‘yaliyo bora leo’ hurekebishwa au hutupiliwa mbali kesho. Ni jambo gani hatari zaidi, ‘mzazi mwenye kufuata dini’ au tabibu mwenye kiburi ambaye amesadikishwa kwamba utibabu wake ni muhimu kabisa?”—“Pediatrics,” Oktoba 1988.