Hospitali— Wakati Wewe Ni Mgonjwa
“Nilipoenda hospitalini mara ya kwanza, kwa ghafula nilihisi ni kama nilikuwa nimepoteza udhibiti wa maisha yangu, ni kama nimekuwa kitu kisicho cha maana.”—Marie G.
“Nakumbuka ziara yangu ya kwanza nikiwa mgonjwa. Nilijihisi mwenye kudhurika kwa urahisi sana na bila ulinzi.”—Paula L.
JE, WEWE umepata kuwa mgonjwa katika hospitali na kuhisi mambo hayo yaliyo hapo juu? Uwe umepata au hujapata, ni lazima ukubali kwamba watu wengi hutumia wakati mchache wakifikiria kuwa wagonjwa hospitalini. Na bado, taraja hilo huenda likawa halisi kwako siku moja. Katika 1987, kwa mfano, ripoti zinaonyesha kwamba 1 kati ya kila watu 7 hulazwa hospitalini katika United States. Tarakimu hizo hubadilika ulimwenguni pote. Bado, ukiwa mtu mwenye busara, ni matayarisho gani unayoweza kufanya ili kujiandaa kwa jambo hilo?
Njia moja iliyo ya maana zaidi ya kulinda afya yako ni kuhakikisha kama kulazwa hospitalini kunahitajika kweli kweli,” asema Dkt. Sidney Wolfe, mkurugenzi wa Kikundi cha Utafiti wa Afya ya Raia. Bila kujali unapoishi, unapokuwa mgonjwa, una haki na jukumu la kujulishwa juu ya mambo ya hakika ya afya yako. Mara nyingi daktari wako anaweza kukupatia majibu yenye kuridhisha.
Lakini iwapo kuna swali lolote, shauri la pili kutoka chanzo kingine linapendekezwa. Katika nchi fulani, kampuni za bima hata huhitaji maoni ya mtu wa pili kabla ya kulipia aina fulani za upasuaji mkubwa. Na si jambo lisilosikika kutafuta shauri la mtu wa tatu ili kusuluhisha tofauti za maoni ya uchunguzi wa ugonjwa na matibabu. Jambo la msingi ni: Mahali palipo na maoni mamoja au mawili au zaidi, mgonjwa mwenye hekima huchukua wakati kujiamulia mwenyewe uhitaji na hekima ya utibabu unaokusudiwa.
Kulazwa kwa Dharura
Bila shaka, katika hali ya dharura, huenda kusiwe wakati wa kupata mapendekezo mbalimbali ya kitiba. Mgonjwa huenda hata akawa amezimia, asiye na uwezo wa kusema au kuandika anapoletwa hospitalini. Wakati fulani ni lazima madaktari watende mara moja, hata kabla watu wa ukoo hawajafikiwa kuamua juu ya mapendezi ya mgonjwa au hiari zake. Hali kama hizo zinakazia kwamba kufikiri mapema na kufanya mipango ni mambo ya maana kabisa.a
Kwa mgonjwa ambaye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, hii inatia ndani kuchukua nyakati zote “Medical Directive/Release Document” (Hati ya Kitiba ya Mwelekezo/Ondoleo la Lawama) ya karibuni zaidi ikiwa imejazwa kabisa. Kwenye kadi hiyo mgonjwa anaonyesha kimbele mapenzi yake kuhusu utunzi wa kitiba na hutoa habari ya maana ili kwamba wafanya kazi wa tiba waweze kuwasiliana na watu wa ukoo au wengine ambao wajua mapenzi yake. Ingawa haiwezi kushughulikia hali zote, kadi hiyo ya maana hutumika kama hati halali ambayo husema wakati wewe huwezi kusema.
Pia ni jambo lenye msaada ikiwa rafiki wa karibu au mtu wa ukoo afahamuye mapendezi na masadikisho yako aweza kuja hospitalini kuwa tegemezo lako wakati wa dharura. Iwe hiyo yawezekana mara hiyo au la, “Medical Directive/Release Document” yenye tarehe ya karibuni zaidi huenda siku moja ikawa ndiyo njia pekee ya kupata ulinzi wa haki zako.
Hata ikiwa mtu si mtumishi aliyebatizwa wa Mashahidi wa Yehova na hana hati hii, anaweza kutayarisha taarifa kama hiyo kwa mkono (afadhali iandikwe kwa tapureta). Hii inapasa ionyeshe mapenzi yake kuhusu matibabu ya kitiba, ionyeshe mipaka yoyote ile, na ionyeshe yule anayepaswa kujulishwa iwapo kuna jambo la dharura.
Kujaza Fomu na Taarifa
Haki za mgonjwa zinatofautiana ulimwenguni pote. (Ona sanduku, ukurasa wa 17) Katika nchi fulani haki hizi zimeongezeka sana katika miaka ya majuzi; daktari hana ruhusa ya kutoa utibabu wowote bila idhini ya mgonjwa, kwa kawaida ikionyeshwa katika mwandiko. Hiyo ni sababu moja ambayo hufanya hospitali ziwe na fomu zao wenyewe ambazo hutaka wewe utie sahihi. Ikiwa hiyo ndiyo hali katika sehemu unayoishi, yafuatayo yanaweza kusaidia.
Unapaswa kusoma kwa uangalifu fomu zote kabla ya kutia sahihi kwa sababu sahihi yako inamaanisha kwamba unakubali, unaidhinisha, lolote ambalo fomu hiyo inasema. Usiruhusu yeyote akuharakishe kutia sahihi kwenye fomu ya kulazwa hospitalini, au fomu ya kutoa idhini ya matibabu, bila wewe kuisoma kwa uangalifu. Ikiwa hukubaliani na sehemu fulani katika fomu hiyo, piga kistari cha kufuta sehemu hiyo. Hata mtu fulani akiteta kwamba hiyo ni fomu ya hospitali na kwamba haiwezi kubadilishwa, bado huo ni mkataba wa kisheria, na huwezi kutakwa kutia sahihi kitu chochote ambacho hukubaliani nacho. Ingawa hutaki kuonekana usiyesababu mambo, ni jambo la maana usiridhiane kuhusu jambo hilo—una haki ya kukataa kukubali sehemu yoyote ya fomu.
Hasa kuhusiana na kukubali upasuaji au utumizi wowote wa damu, chunguza kila fungu kwa uangalifu. Baadhi ya Mashahidi wa Yehova wameshtuliwa na kile ambacho wameona katika fomu ya hospitali iliyotayarishwa eti kwa ajili yao. Ingawa hapo kwanza ilisema kwamba mapenzi ya mgonjwa kuhusu damu yataheshimiwa, fungu fulani la baadaye lilisema kitu kama, ‘Katika hali ya dharura au ikiwa daktari aona kwamba inahitajiwa, yeye anabaki na haki ya kutia damu mishipani.’ Zaidi ya hilo, kwa sababu Neno la Mungu huamuru Wakristo wajiepushe na damu, ni kawaida nzuri kuandika “Usitie Damu Mishipani” katika karatasi zote unazoletewa. (Matendo 15:28, 29) Hilo litaonyesha wazi wafanya kazi wote msimamo wako. Uhakika ni kwamba, idadi inayoongezeka ya wagonjwa wanakataa damu kwa sababu wanataka kuepuka hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa hepataiti, UKIMWI, au magonjwa mengine yenye kuua.b
Wagonjwa katika nchi fulani fulani wana haki chache kuliko zile ambazo zimeonyeshwa hapo juu. Kuna sehemu ambazo daktari ndiye sheria, na ni kama wagonjwa huonwa kuwa chini yake. Daktari mmoja kutoka nchi fulani ya magharibi alitembelea taifa moja la Kiafrika na akasema: “Wala sikuwa nimejitayarisha kwa njia ambayo madaktari na wagonjwa walitendeana . . . Wagonjwa wenyewe hawakusema kamwe hadi waliposemeshwa. Hawakuuliza madaktari wao maswali.” Ingawa desturi kama hiyo inaweza kufanya mambo kuwa magumu zaidi kwa mgonjwa, bado Mkristo mwenye hekima—kwa staha lakini kwa uthabiti—angeweza kusisitiza kwamba haki yake kwa msingi wa kibinadamu kuhusiana na adili yake ya kimwili na ushirika katika mazungumzo yanayohusu afya yake mwenyewe iheshimiwe.
Kuzungumza na Wafanya Kazi wa Kitiba
Daktari wako amepaswa awe ndiye wakili wako hasa na chanzo cha habari; hivyo, mengi huenda yatategemea umechagua tabibu kwa uangalifu wa kadiri gani. Asema mwandikaji mmoja: “Tambua kwamba madaktari ni kama mtu mwingine yeyote. Wao huonyesha wema wote na ubaya wote [ambao] sisi wengine wote huonyesha. Matabibu walio wengi hujaribu kufanya yote wawezayo kwa wagonjwa wao, lakini fikira za wengine [zimefanyizwa] na hali za kijamii kufikiri kwamba wao wana haki ya kukufanyia maamuzi. Ikiwa itikadi za daktari au utu wake unagongana na wako, tafuta daktari mwingine.”
Jaribu kupata majibu kamili kwa maswali yako na uradhi wako kabla hujakubali matibabu yoyote. (Ona sanduku, ukurasa wa 18.) Ikiwa huwezi kuelewa lolote, usione haya kusema hivyo. Omba kwamba maelezo yawe kwa usemi rahisi, usiotumia maneno ya kitiba. Lingekuwa pia jambo la busara ikiwa katika sehemu fulani ya mazungumzo yako na daktari, unaonyesha uthamini wa moyo mweupe kwa uelewevu wake juu ya msimamo wako unaotegemea masadikisho yako ya kidini.
Jaribu kusitawisha uhusiano wa kirafiki na wafanya kazi wa hospitali wanaokushughulikia, kama vile wauguzi, kwa maana wao waweza na wapaswa kuwa msaada mkubwa katika kutunzwa na kupona kwako. Wanapoleta dawa au sindano, hakikisha kwamba hizo ni zako kweli. Hiyo ni hatua ya hekima yenye kutumika, kwa maana hata kuwe na makusudio mema, makosa hufanywa.
Wafanya kazi wa hospitali huenda waonekane kuwa wenye shughuli nyingi, lakini kumbuka kwamba wengi wao walichagua kazi ya aina hiyo kwa sababu wao hujali watu na hutaka kikweli kusaidia. Unaweza kushirikiana nao ikiwa unajaribu kueleza mahitaji yako na mahangaiko yako kwa uwazi. Hakuna muuguzi (au yeyote yule wa wafanya kazi) aliye na haki ya kukudhulumu kwa maneno, kama vile: “Utakufa usipokubali utibabu huu.” Ripoti dhuluma yoyote kama hiyo kwa wasimamizi wa hospitali na watu wa ukoo au mhudumu wako; wanaweza kuwa katika hali ya kuzungumza badala yako.
Namna Gani Ikiwa Tatizo Latokea?
Kumekuwa na pindi ambapo, mashauri yote hayo yajapotumiwa, wagonjwa hujipata katika hitilafiano la kina kirefu pamoja na mfumo wa kitiba. Ingawa hali kama hiyo si ya kawaida, unaweza kufanya nini ukijipata kwa ghafula katika hali kama hiyo?
Kwanza, jaribu usibabaike. Kwa kawaida hicho ni kipindi kigumu kwa wote wanaohusika, huku hasira ikipanda upesi. Kwa hiyo kubaki ukiwa mtulivu, mwenye kusababu, na mwenye staha kwaweza kusaidia sana. Pili, fikiria na utumie njia zote zinazoweza kutumika. Hospitali huenda ikawa ina mwakilishi wa wagonjwa ambaye waweza kuwasiliana naye na kutafuta msaada kwake.
Mashahidi wa Yehova huliona kuwa jambo la maana kuwasiliana na wazee wao wa kundi. Washauri hao wenye hekima na ujuzi waweza hata kusaidia kupata makao yenye kushirikiana ikiwa hali ni nzito sana kadiri ya kuhitaji uhamisho.c Wakristo wa kweli hukumbuka pia kutegemea uwezo wa Yehova Mungu. Katika hali ngumu mara nyingi hakuna jibu moja, lenye kuhusisha mambo yote, na kwa nguvu zetu wenyewe huenda tusijue kwa usahihi ni wapi kwa kuelekea. Wengi wamepata kwamba baada ya kufanya yote yawezekanayo kibinadamu, kumgeukia Mungu kwa sala kumetokeza si faraja tu bali pia kupata masuluhisho yasiyotazamiwa.—1 Wakorintho 10:13; Wafilipi 4:6, 7.
Yatumainiwa kwamba hutapatwa na yoyote ya matatizo hayo, lakini ni vema kupanga kimbele. Pia kumbuka kwamba mambo fulani yatazamiwa uyafanye unapokuwa ukikaa hospitalini. Hospitali ni mahali pazuri pa kuonyesha sifa za Kikristo kama saburi, ushukuru kwa fadhili ulizoonyeshwa, na hasa shukrani kwa wenye kukusaidia. Barua fupi yenye kufuata baadaye kwa wafanya kazi wa hospitali, au hata zawadi ndogo inayotolewa kama wonyesho wa uthamini, huacha maoni mazuri yanayokaa kwa muda mrefu. Kukaa kwako hospitali huenda kukaandaa fursa ya kutoa ushahidi kwa mwenendo wako mwenyewe wenye mfano mzuri, hivyo ukichangia sifa nzuri ambayo Wakristo wa kweli huonea shangwe wakiwa wagonjwa.—1 Petro 2:12.
[Maelezo ya Chini]
a Zamani za kale mwandikaji wa Biblia aliandika mithali iliyovuviwa roho ambayo inakazia thamani ya kufikiri mapema: “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; bali wajinga huendelea mbele wakaumia.”—Mithali 22:3.
b Ona How Can Blood Save Your Life? (1990), iliyochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
c Kama ilivyoelezwa katika makala iliyo kwenye ukurasa wa 22, Mashahidi wa Yehova wana vyanzo vyenye thamani vya usaidizi katika kushughulika na matatizo ya kitiba na wafanya kazi wa hospitali.
[Sanduku katika ukurasa wa 15]
Ikitokea Uwe Mgonjwa Hospitali
Orodha ya mambo ya kuchunguza ulazwapo hospitalini:
◻ 1. Chukua “Medical Directive/Release Document” (Hati ya Mwelekezo/Ondoleo la Lawama) ya karibuni zaidi au taarifa iliyoandikwa na kutiwa sahihi kuhusu mapenzi yako.
◻ 2. Chagua daktari wako kwa uangalifu.
◻ 3. Hakikisha kwamba mlazo huo wa hospitalini unahitajika kabisa.
◻ 4. Soma na kujaza fomu za kulazwa kwa uangalifu. Ikiwa wewe ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, jitambulishe mara moja kuwa hivyo.
◻ 5. Lete kadiri ndogo iwezekanayo ya vitu vya kibinafsi vihitajiwavyo kabisa, kama vazi la kuendea bafuni, vifaa vya choo, na vya kusoma.
◻ 6. Acha nyumbani vito vyovyote vyenye thamani, vifaa vingi vya nguvu za umeme, na fedha za ziada.
[Sanduku katika ukurasa wa 17]
Haki za Mgonjwa
Mgonjwa anapoingia hospitalini, hapaswi kuogopeshwa mno na mazingira na kufikiri amekuwa kidude kisichokuwapo. Yeye ana haki ambazo hospitali nyingi na wafanya kazi wengi hufurahi kuzistahi. Haki zifuatazo zimefupizwa na zinategemea orodha ya haki kumi katika kitabu How to Stay Out of the Hospital, cha Lila L. Anastas, R.N.d
Mgonjwa ana haki ya:
1. Kupata utunzi wenye ufikirio na staha kutoka kwa wafanya kazi wenye uwezo.
2. Kupata kutoka kwa tabibu wake habari kamili na ya karibuni zaidi juu ya ugonjwa wake, matibabu, na maendeleo ya ugonjwa wake katika njia ambayo anaweza kuelewa.
3. Kupokea kutoka kwa tabibu wake habari inayohitajika kabisa ili atoe idhini yake mwenyewe kabla ya kuanza kwa hatua zozote na/au matibabu. Mahali ambapo njia nyingine ya kitiba yaweza kupatikana, mgonjwa ana haki ya kupata habari hiyo.
4. Kukataa matibabu kwa kadiri ambayo sheria yaruhusu.
5. Kila ufikirio wa faragha kuhusu programu yake mwenyewe ya utunzi wa kitiba.
6. Kutarajia kwamba mawasiliano yote na rekodi zinazohusu utunzi wake zitatunzwa kuwa siri.
7. Kutaraji kwamba, kwa uwezo wa hospitali, lazima hospitali iitikie vema kuhusiana na ombi la mgonjwa kupata utumishi au uhamisho kwenye utunzi mwingine iwapo hili laruhusika kitiba.
8. Kupata habari kuhusu uhusiano wowote wa hospitali na makao mengine ya utunzaji wa afya na elimu kwa kadiri utunzi wake uhusikavyo.
9. Kupashwa habari ikiwa hospitali inataka kufanya majaribio ya uchunguzi wa kibinadamu kuhusiana na utunzi wake au matibabu.
10. Kutarajia uendelevu mzuri wa utunzi na kujua mapema ni matabibu gani wanapatikana na mahali wanapopatikana.
[Maelezo ya Chini]
d Kitabu The Rights of Patients—The Basic ACLU Guide to Patient Rights (kitabu cha Chama cha Kiamerika cha Uhuru wa Wenyeji) chaorodhesha haki 25 katika “Kiolezo cha Haki za Mgonjwa.”
[Sanduku katika ukurasa wa 18]
Ulinzi na Ushiriki wa Mgonjwa
“Kama vile hakuna mshtakiwa yeyote apaswaye kwenda mahakamani bila wakili, ndivyo na mgonjwa asivyopaswa kuingia hospitali ya jiji kubwa bila mshiriki wa familia au rafiki wa karibu kuwa tayari kushughulikia faida za mgonjwa na kusema wazi bila woga iwapo kufanya hivyo kwahitajika kabisa.”—June Bingham, The Washington Post, Agosti 12, 1990.
“Muda wa enzi zote zilizopita, wazo la ushiriki wa mgonjwa katika maamuzi ya kitiba limekuwa geni katika fikira na utendaji wa matabibu. Na wagonjwa wamejifunza kutokana na maono yenye uchungu kwamba kuuliza maswali mengi mno yenye kuhoji huenda kukawatenganisha na sisi, kwa sababu mara nyingi mno sisi hatupendi maulizo hayo.
“Na bado, lile wazo la kwamba tunajua kile kilicho cha faida kwa wagonjwa wetu na hivyo tunaweza kutenda kwa niaba yao bila kuulizwa, laonekana wazi sana kuwa si la kweli hivi kwamba tunaweza tu kushangazwa na ile bidii ambayo kwayo wazo hilo limelindwa. . . .
“Tunaweza kukosa kukubaliana na wagonjwa, hata kubishana nao, hata kuwavuta kwa werevu, lakini lazima tufanye hivyo katika roho ya kuwajali. Mwishowe lazima tuheshimu kile ambacho wagonjwa wanataka au wasichotaka kutoka kwetu.”—Dkt. Jay Katz, daktari wa akili, profesa katika Chuo Kikuu cha Yale, The Medical Post, Kanada.
“Wagonjwa si vitoto vichanga na matabibu si wazazi. . . . Kwa kweli, yaonekana kuwa ajabu kulazimika kukumbusha wanafunzi wa tiba, na matibabu pia, kwamba wagonjwa wanapokabiliana na madaktari huwa na matarajio pia . . . kutumainiwa na kujitumaini wenyewe, kuruhusiwa wasimame kwa miguu yao wenyewe wala si kutumiwa vibaya kwa utegemeo wao, kuzungumziwa na kusikilizwa, kutendewa kwa usawa na si kutawalwa, kustahiwa mtindo wao wa maisha, na kuruhusiwa kuishi maisha katika njia zao wenyewe za kujichagulia.”—The Silent World of Doctor and Patient, cha Dkt. Jay Katz.
“Huduma huanza kwa kuonana kwetu na wagonjwa. Mionano na wagonjwa wapatao milioni 4 kila siku huwapa madaktari wa Amerika fursa ya kuonyesha si uwezo wetu tu, bali pia na huruma yetu ya kweli, kujali kwetu, na ujitoaji wetu kwa kila mgonjwa tumhudumiaye.”—James E. Davis, M.D., msimamizi wa Shirika la Kitiba la Amerika.