Bundi-Hudhurungi Aliye Kwenye Ukuta wa Hadrian
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
UKUNGU mwembamba ulifunika vilele vya miti wakati sauti yenye kuongezeka ya melodia yenye kupendeza ilipoondoa kimya cha alfajiri. Ndege wahamaji wa kiangazi walikuwa wamefika tu katika kaskazini mwa Uingereza ili kuongeza nyimbo zao kwa zile za ndege-weusi na mikesha wa mahali hapo.
Nilifuata kijito kilichojaa mimea iliyooza kilichopita kati ya kingo za mto zilizopambwa kwa maua aina ya primrose na maua-urujuani kuelekea makao ya kikale ya bundi-hudhurungi kwenye Ukuta wa Hadrian.a Nilijua kwamba kilometa 1.6 hivi upande wa juu zaidi wa mto, angekuwa karibu na kisiki cha mti mzee wa elm, akitunza makinda yake manne. Walikuwa wakifurahia makao yenye ujoto na salama katika uwazi wa kisiki cha mti aina ya ash uliooza.
Bundi—ni ajabu ya uumbaji kama nini! Mwono wake wa jicho usiku ni wenye kuona vizuri zaidi mara mia moja kuliko ule wa binadamu. Hata katika nuru iliyofifia ya mwezi, bundi anaweza kushika windo lake. Macho ya binadamu yana chembe ziitwazo pia ambazo hutenganisha rangi na chembe ziitwazo selifito ambazo hukusanya nuru, lakini macho ya bundi yamejaa pomoni selifito ambazo zina kemikali iitwayo zambarau-jicho. Kemikali hii hugeuza mwanga hafifu sana kuwa ishara ya kemikali ambayo humwezesha ndege huyo kuona vitu, ilhali binadamu huona tu kuwapo kwa nuru.
Bundi hawawezi kuzungusha-zungusha macho yao katika matundu ya jicho kama viumbe wengi wafanyavyo. Kila jicho halisogei kama taa ya mbele ya gari. Ili kushinda tatizo hilo, bundi—kwa sababu ya shingo iwezayo kunyumbuka kwa njia ya kushangaza—anaweza kugeuza kichwa chake angalau kwa digrii 270 ili kuona kila upande!
Imesemekana kwamba kutoka kiota chake meta 15 juu ya mti, bundi anaweza si kuona panya tu bali pia kusikia akifanya kelele za kutembea nyasini. Uwezo wake wenye kushangaza wa kusikia unatokana na ubuni wa masikio yake. Ukitazama uso wa bundi, utaona kwamba umeviringwa na manyoya magumu yaliyojipinda ambayo yanakusanya na kurusha mawimbi ya sauti hadi masikioni, yakidundisha sauti kwenye viwambo vya sikio vikubwa kuliko vyote katika ulimwengu wa ndege. Masikio yamewekwa moja likiwa juu kidogo kuliko jingine, ikiruhusu bundi kujua mahali inakotokea sauti kwa usahihi.
Mara bundi anapojua mahali windo lipo—iwe ni kwa kuona au kusikia sauti—ataruka chini kimya-kimya. Mwili wa bundi umefunikwa kwa manyoya yaliyo laini sana hivi kwamba sauti yote inazimwa. Hata manyoya ya bawa yana ncha laini ili kuondoa uvumi anaporuka. Wakati wa usiku wenye giza, watu wa mashambani nyakati fulani wameshtuliwa na umbo lenye kung’aa la bundi anayeruka chini-chini barabarani. Bila wao kujua bundi wanaweza kung’aa kwa mmetometo uliopakwa kwenye mabawa yake kutoka kuvu zenye kutoa nuru ambazo hukua juu ya mti unaooza wa kiota chake.
Niliendelea kusonga upande wa juu wa kijito na mara nikaona kisiki kizee cha mti kilichokunjika. Ujoto wa asubuhi ulikuwa umeleta mmoja wa ndege wachanga hadi kwenye kiingilio cha uwazi ili kuota jua kutokana na miale iliyoinama ya jua iliyopita matawi ya mti juu yaliyotandaa yenye majani mengi. Alikaa pale, akipepesa macho yake katika nuru ya jua iliyotapakazwa—mandhari yenye kufurahisha kwelikweli!
Akiwa amefichika mahali fulani katika matawi yaliyo juu, bundi-hudhurungi mzee alikuwa ametua na mwenzi wake, akichunguza yote yaliyo mbele yake kwa macho yaliyofungwa nusu. Nilijua kwamba angewatunza wachanga wake kwa uangalifu hadi waweze kujitegemea kwa hekima ya kisilika waliyopewa na Muumba wao Mtukufu.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa amri ya Maliki Mroma Hadrian, kati ya mwaka 120 na 130 W.K., Ukuta wa Hadrian ulijengwa kuwa kinga dhidi ya makabila ya Kaledonia yasiyotawalwa upande wa kaskazini mwa Uingereza. Ukuta huo huenda kilometa 117 kutoka Solway firth katika magharibi mwa Uingereza hadi mahali ambapo Mto Tyne huingia baharini kwenye pwani ya mashariki.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Kwa hisani ya English Heritage