Mahali Ambapo Tai Huenda Kula Samaki
WAO huja kwa maelfu, wakiwa wamevalia maridadi sana kwa ajili ya mlo mkuu, wakiruka kutoka sehemu zote za Alaska, British Columbia, na mbali kufikia jimbo la Washington. Ndege hao ni wenye kuvutia kwelikweli, na ni wenye kutokeza sana vichwa vyao vyeupe na mikia mishaufu ya manyoya ikipepea wanapotua. Wakiwa na miili ya kahawia nzito, wenye wastani wa uzani wa kilo 6, wale wa kike wakiwa wakubwa kidogo kuliko wa kiume, wao husafiri kwa mwendo wa kilometa 50 kwa muda wa saa moja, wakiwa na upana wa mabawa wa meta 1.8 hadi 2.4—lakini macho yao yakimwona samaki umbali wa kilometa moja, wanaweza kuruka kuelekea chini kwa mwendo wa kilometa 160 kwa muda wa saa moja na kumnyakua!
Hata hivyo, kwa karamu yao ya mlo mkuu katika Mto Chilkat, madaha ya angani kama hayo yenye kutazamisha hayahitajiwi. Milo yao ya salmoni haiendi popote. Hao wametapakaa kwa wingi mbele zao, wakingojea tu kunyafuliwa. Karamu hii yote wameandaliwa na Hifadhi ya Chilkat ya Furukombe wa Alaska, iliyoanzishwa katika 1982 na jimbo la Alaska “ili kulinda na kusitawisha mkusanyo mkubwa zaidi wa Furukombe ulimwenguni na mazingira yao muhimu.”
Hiyo hifadhi imeenea ekari 19,000 za sehemu ya chini ya mito Chilkat, Klehini, na Tsirku, na maeneo tu yaliyo muhimu kwa kuishi tai ndiyo yametiwa ndani. Eneo maalumu ambalo maelfu ya tai hujaa na watalii humiminika kuwaona ni kilometa nane kando-kando ya Mto Chilkat mpakani mwa Barabara Kuu ya Haines, katikati ya Haines na Klukwan.
Kikaratasi kimoja cha serikali chenye kichwa “Hifadhi ya Chilkat ya Furukombe wa Alaska” hueleza sababu kwa nini ukanda huu wa mto wa kilometa nane huweza kuandalia tai milo mitamu ya salmoni ambao wamekwisha kutoa mayai.
“Kawaida ya asili inayofanyiza maji yasigande katika kilometa nane za Mto Chilkat wakati wa miezi ya kugandana yaitwa ‘birika la kitope msonge.’ Msonge wa Tsirku, ambao ni mrundamano wa changarawe, mawe, mchanga, na kitope cha barafuto chenye muundo wa msonge, kwenye ndagano la Mito Tsirku, Klehini, na Chilkat huwa kama birika kubwa la maji.”
Kwa kawaida, mto hupunguza mwendo uingiapo ndani ya kitope cha tungamo la maji mengine, ukifanyiza delta, lakini bila kuacha nyuma birika la maji. Hata hivyo, mahali ambapo Mto Tsirku waingilia Mto Chilkat, miatuko ya ardhi na utendaji wa kibarafuto zilichimba jaruba kubwa lenye kina kipitacho meta 230 chini ya usawa wa bahari. Barafuto lilipoyeyuka, masalio ya kitope yalibaki, nayo mito iliongezea kitope cha mchanga na changarawe mpaka hatimaye jaruba likawa na kalio lenye kitope chenye upenyevu, ambalo lina kimo cha zaidi ya meta 230 kwenye mwamba-lalio walo.
Hayo masimulizi yaonyesha kwamba wakati wa misimu yenye ujoto ya vuli, kiangazi, na mapema katika vuli, maji kutoka kwa theluji na barafu iliyoyeyuka hutiririka kuingia ndani ya msonge wa kitope. Huo msonge hufyonza maji haraka zaidi kuliko yawezavyo kupita, ukifanyiza birika kubwa mno la maji. Kikaratasi cha hifadhi ya tai chaendelea kusema hivi: “Kipupwe kikiwasili, halihewa yenye ubaridi huanza na maji yaliyoko kandokando huganda. Hata hivyo, maji katika birika hili kubwa hubaki na halijoto ya kuanzia digrii tano hadi kumi Selsiasi kuzidi halijoto ya maji yaliyoko kandokando. Maji haya yenye ujoto ‘hupenya’ ndani ya Mto Chilkat na kuufanya usigande.
“Spishi tano za salmoni huzalia katika mito hii na mito na vijito vilivyoko karibu. Kukuru kakara za salmoni huanza katika kiangazi na huendelea hadi mwishoni-mwishoni mwa vuli ama mapema katika kipupwe. Salmoni hufa muda mfupi baada ya kutoa mayai na ni mizoga yao ambayo huandaa kiasi kikubwa cha chakula cha tai.”
Karamu ya salmoni huanza Oktoba na humalizika katika Februari, na muda mfupi baada ya hapo maelfu ya tai huanza kutawanyika kuelekea sehemu za mashambani za ujiranini. Hata hivyo, kwa mwaka mzima hiyo hifadhi huwa makao ya furukombe kati ya 200 na 400. Kwa kuongezea samaki wowote wanaoweza kushika, wao huongezea mlo wao kwa ndege wa majini, mamali wadogo, na mizoga.
Uchumba Wenye Kusisimua, “Ndoa” Zenye Kudumu
Wao huishi pamoja hadi kifo—wanaweza kufikisha umri wa miaka 40—lakini kwa kawaida hubaki pamoja wakati wa msimu wa utamio. Uchumba huanza katika Aprili na “waweza kuhusisha maonyesho yenye kutazamisha ya uchumba wa tai wenye kuruka chini wakiwa wameshikana makucha na kuruka kichwangomba hewani,” kulingana na faili Eagles—The Alaska Chilkat Bald Eagle Preserve. Yote hayo kwa kuongezea kushikana mikono? Salaala! yasikika ya kimahaba kwelikweli!
Viota 94 vimeonekana katika hiyo hifadhi. Kuanzia yai moja hadi matatu huanguliwa katikati ya mwishoni-mwishoni mwa Mei na mapema katika Juni, baada ya muda wa utamio wa siku 34 au 35. Wachanga huondoka kiotani kufikia Septemba, lakini ni lazima waridhike na vazi la manyoya lenye mapaku ya kahawia na meupe. Hawatapata zile rangi nyeupe maridadi vichwani na katika mikia mpaka wawe na umri wa miaka minne au mitano!
Hiyo faili pia hutoa historia ya uokokaji wa hao tai na kushauri watalii jinsi wanavyoweza kufurahia hiyo hifadhi kwa usalama:
“Hifadhi ya Chilkat ya Furukombe wa Alaska ina ekari 19,000 zilizotengwa kwa ajili ya ulinzi wa tai. Lakini tai hakulindwa sikuzote; wakati mmoja walikuwa windo la wawindaji wenye kulipwa. Ikitegemea ripoti za ule ukamio wa tai wa kula salmoni walio hai na wanyama wadogo, Bunge la Eneo la Alaska katika 1917 lilitoa bakshishi kwa wawindaji wa tai. Wale waliokuwa mashujaa wa vita wa Ft. William H. Seward katika Haines huelezea hadithi kuhusu jinsi walivyoongezea mshahara wao mdogo wa Jeshi na malipo ya dola moja (baadaye yalipandishwa hadi dola mbili) kwa kila jozi ya makucha.
“Uchunguzi wa baadaye ulipata kwamba madhara yaliyotokezwa na tai kwa salmoni yalikuwa yametiwa chumvi, na malipo ya tai waliouawa yaliondolewa katika 1953. Kufikia wakati huo, zaidi ya tai 128,000 walikuwa wamepigwa risasi ili kupata malipo. Idadi ya tai wa Kusini-Mashariki mwa Alaska wakati wa miaka ya 1940, wakati malipo yalipokuwa yakilipwa bado, ilikadiriwa kuwa nusu ya idadi ya tai katika miaka ya 1970.
“Wakati Alaska ilikuja kuwa jimbo katika 1959, furukombe katika Alaska wakaja kuwa chini ya ulinzi wa serikali chini ya Sheria ya Furukombe ya 1940. Kuua furukombe ni kuvunja sheria ya serikali, na kupatikana na tai walio hai au sehemu zozote (kutia ndani manyoya!), isipokuwa chini ya hali fulani hususa, ni kinyume cha sheria pia.
“Katika 1972 Bunge la Jimbo la Alaska lilianzisha Chilkat River Critical Habitat Area, ikisimamiwa na Idara ya Alaska ya Samaki na Wanyama wa Pori, ili kuhakikisha ulinzi wa mahali tai walipo wengi. Maeneo mapana ya mazingira ya tai yalibaki bila kulindwa, na pambano refu na mara nyingi kali liliendelea kati ya vikundi vya kuhifadhi mazingira na vile vya kusitawisha ardhi kuhusu masuala ya utumizi wa ardhi katika Bonde la Chilkat. Baada ya uchunguzi mwingi na Shirika la Kitaifa la Audubon na Uchunguzi wa Rasilimali wa Haines/Klukwan uliogharimiwa na serikali, wakata-miti, wavuvi, wanamazingira, wanabiashara na wanasiasa wa hapo hatimaye walifikia mwafaka. Katika 1982 bunge la jimbo lilifanya huo mwafaka uwe sheria kwa kufanyiza ekari 19,000 za Hifadhi ya Chilkat ya Furukombe wa Alaska.
“Kukata miti au kuchimba madini kulipigwa marufuku katika hiyo Hifadhi, lakini matumizi ya kitamaduni ya ardhi, kama vile kuvuna beri, uvuvi na uwindaji, yaweza kuendelea. Hiyo Hifadhi yasimamiwa na Idara ya Alaska ya Mbuga kwa msaada wa baraza la kushauri la washiriki 12 lifanyizwalo na wenyeji, maofisa wa serikali, na wanabiolojia.
“Jinsi ya kutumia maliasili ya hilo bonde bila kuharibu mazingira limekuwa swali la daima, na masuala ya utumizi wa ardhi bado yaweza kuamsha ubishi katika Bonde la Chilkat. Lakini wakazi wenyeji waona fahari kwamba suluhisho la hapo lilipatikana kwa ulinzi wa tai.”
Eneo kuu ambapo watalii wanaweza kuwaona hao tai ni kandokando ya Barabara Kuu ya Haines, ambayo iko sambamba na Mto Chilkat, na kuna maeneo yaliyotengwa kwa kusudi hili la kuwatazama.
[Ramani katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Chilkat River Chilkoot River
Klehini River KLUKWAN
Eagle Viewing Area
(alluvial fan)
▴
▴
Haines Highway
Tsirku River ▾ Chilkoot Lake
Chilkat Lake ▾
Chilkat River ▾ Lutak Inlet
Takhin River ▾
HAINES
[Hisani]
Mountain High Maps™ haki za kunukuu zimehifadhiwa na © 1993 Digital Wisdom, Inc.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Furukombe kwenye kurasa 15-18: Idara ya Utalii ya Alaska