Kioo—Watengenezaji Wacho wa Kwanza Waliishi Zamani za Kale
DIATOMU, viumbe hai vya chembe moja vya kihadubini, vyaelea katika uso wa maji ya bahari navyo hufanyiza sehemu sita kwa kumi ya viumbe hai ambavyo hufanyiza plankitoni za bahari-kuu. Neno “plankitoni” humaanisha “kile ambacho kimefanyizwa ili kwenda huku na huku,” na plankitoni zasemekana kuwa “ndogo sana na dhaifu kuweza kufanya lolote ila kufuata mikondo.”
Zaweza kuwa ndogo, lakini si dhaifu kamwe. Tufani zikorogapo virutubisho kwenye vilindi vya bahari, miani hii ya chembe moja inayoitwa diatomu huanzisha kukuru kakara za kujilisha, na kwa siku mbili zaweza kurudufisha idadi yazo. Na zinaporudufika, pia hurudufisha utokezaji wazo wa kioo. Kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? huzifafanua zaidi hivi:
“Diatomu, viumbe hai vya chembe moja, hufyonza silikoni na oksijeni kutoka kwa maji ya bahari na kutengeneza kioo, ambacho kwa hicho hujenga ‘visanduku’ vidogo vya kubebea klorofili zazo za kijani kibichi. Zasifiwa na mwanasayansi mmoja kwa umuhimu wazo pamoja na urembo wazo hivi: ‘Majani haya ya kijani kibichi yaliyofungiwa katika vito vya visanduku ni malisho ya sehemu tisa kwa kumi ya chakula cha kila kitu kinachoishi baharini.’ Kiwango kikubwa cha lishe ya chakula chazo iko katika mafuta ambayo diatomu hutengeneza, ambayo pia huzisaidia kuelea karibu na uso wa maji mahali klorofili yazo yaweza kufyonza miali ya jua.
“Vifuniko vyazo maridadi vya kisanduku cha kioo, mwanasayansi huyuhuyu hutuambia kwamba, hutukia katika ‘unamna wa vigezo vingi vyenye kutazamisha—miviringo, miraba, vigao, pembetatu, mviringo-yai, na mistahili—sikuzote mapambo ambayo ni marembo sana yakiwa katika vigezo vya jiometri. Haya hutengenezwa kuwa kioo safi sana kwa ustadi wa hali ya juu sana hivi kwamba unywele wa kibinadamu ungehitaji kupasuliwa kwa vipande mia nne ili kutoshea katikati ya hizo alama.’”—Kurasa 143-144.a
Kikundi kingine cha usanii wa viumbe vidogo kinachonawiri katika plankitoni za bahari-kuu ni radiolaria. Protozoa hawa wadogo sana—20 au zaidi wangeweza kuketi kwenye ncha ya sindano bila kugusana—pia hutengeneza kioo kutokana na silikoni na oksijeni katika bahari-kuu. Umaridadi tata na miundo yenye kustaajabisha inayopambwa na viumbe hawa usanii wao ni mzuri ajabu, kwani wapita hata diatomu. Chunguza kwa makini picha iliyoambatanishwa inayoonyesha moja ya radiolaria akiwa na vipira vitatu vikiwa vimeshikilishwa pamoja kama wanasesere wa Kirusi, vigongo vya protoplazimu vikifikilia kupitia mashimo ya kiunzi cha kioo ili kushika na kumeng’enya windo layo. Mwanasayansi mmoja atoa elezo hili: “Kuba moja ya jiodeski hailingani na usanii huu maridadi mno; ni lazima iwe kuba tatu za vioo vilijisokota, moja ndani ya nyingine.”
Kuna sifongo ambazo hutengeneza kiunzi cha kioo—moja yenye kushangaza ni ile iliyoitwa kikapu-maua cha Zuhura. Mara ya kwanza ilipoletwa Ulaya mwanzoni mwa karne ya 19, muundo wayo ulipendeza sana hivi kwamba sifongo hizi zilikuja kuwa vitu vyenye thamani sana vilivyowekwa katika hifadhi za kizuolojia—mpaka ilipogunduliwa kwamba hazikuwa adimu bali “zilifanyiza zulia kwenye lalio la bahari katika eneo la Kebu, Filipino, na kandokando ya pwani za Japani kwenye vina vya meta 200-300.”
Mwanasayansi mmoja alivutiwa sana nayo, na kuduwazwa nayo mno, hivi kwamba alisema: “Unapotazama kiunzi cha sifongo tata kama kile kilichofanyizwa na vianya vya silika inayoitwa [kikapu-maua cha Zuhura], chastaajabisha sana. Chembe ya kihadubini iliyo peke yayo ingeweza kujipangiliaje ili kunyesa vikanda milioni moja vya kioo na kutengeneza kimia tata na maridadi kama hicho? Sisi hatujui.”
Wala sifongo yenyewe haijui. Haina ubongo. Hufanya hivyo kwa sababu ilipangiliwa kufanya hilo. Ni nani alikuwa mpangiliaji? Si mwanadamu. Hakuwako.
Fungu la Mwanadamu Katika Historia ya Kioo
Lakini mwanadamu yupo sasa, na aonekana kuchukua sehemu kuu katika utengenezaji na utumiaji wa kioo. Kioo kiko kila mahali; chatuzingira. Unacho madirishani, katika miwani, katika kiwambo cha kompyuta, katika vyombo vyako vya kulia, na katika maelfu ya bidhaa nyinginezo.
Unyumbufu na umaridadi wa kioo zimesaidia kudumisha umaarufu wacho. Ingawa kwa kulinganishwa huenda kikavunjika kwa urahisi, kina nguvu nyinginezo. Bado chapendelewa kwa kuhifadhi vyakula. Kwa kielelezo, kinyume na metali hakifanyizi ladha katika chakula. Vibweta vingine vya kioo vyaweza kutumiwa kupikia. Huwezi kamwe kuwazia mkahawa uupendao ukiandika divai murua kwa vikombe vya plastiki.
Ayubu alilinganisha thamani ya kioo na dhahabu. (Ayubu 28:17) Hapana budi kwamba hakikuwa cha kawaida katika siku yake kama ilivyo sasa, lakini yaelekea kwamba tayari kilikuwa kikitumiwa kwa zaidi ya miaka elfu moja.
Ufundi wa kutengeneza kioo hatimaye ulifika Misri. Wamisri walitumia mbinu iitwayo kufanyiza-kiini. Kiini chenye muundo fulani kilifanyizwa kwa udongo na samadi, kioo kilichoyeyushwa kilimwagwa kukizunguka na kupata umbo ilipovingirishwa kwenye mahali laini. Kisha vinyuzi vya kioo vyenye rangi nyangavu vilizungushwa kwenye umbo la nje ili kufanyiza vigezo tofauti-tofauti. Mara kioo kilipopoa, kiini cha udongo kiliondolewa kwa kutumia kifaa chenye ncha kali. Tukifikiria mbinu za kikale, baadhi ya vifaa vya kioo vyenye kupendeza mno vilitokezwa.
Ilikuwa ni baadaye sana kwamba mbinu mpya, kupuliza-kioo, ingebadilisha utokezaji wa kioo. Ufundi huu huenda uligunduliwa mashariki mwa Pwani ya Mediterania, na bado ndiyo njia ya msingi ya kutengeneza kioo kwa kutumia mikono leo. Kwa kupuliza neli yenye shimo, mpuliza-kioo mwenye uzoefu aweza kutokeza kwa haraka miundo tata na ya kimapacha kutoka na “kidimbwi” cha kioo kilichoyeyushwa nchani pa neli yake. Ama sivyo, anaweza kupuliza kioo kilichoyeyushwa kuwa muundo fulani. Yesu alipokuwa duniani, kupuliza-kioo kulikuwa kunaanza tu.
Uvumbuzi wa kupuliza-kioo, pamoja na udhamini wa Milki ya Kirumi yenye nguvu, zilifanya bidhaa za kioo zipatikane kwa urahisi kwa watu wa kawaida, nazo bidhaa za kioo hazikuwa sasa vitu vya wenye cheo na matajiri tu. Kadiri athari ya Kirumi ilivyoongezeka, ndivyo ufundi wa kupuliza-kioo ulivyoenea katika nchi nyingi.
Kufikia karne 15, Venisi, ambacho kilikuwa kitovu muhimu cha biashara cha Ulaya, kilikuwa kimekuwa mtokezaji mkuu wa bidhaa za kioo katika Ulaya. Kiwanda cha kioo cha Wavenisi kilikuwa Murano. Watengenezaji wa kioo wa Venisi walistahiwa sana, lakini walikatazwa kuondoka kisiwa cha Murano, ili kwamba siri za ufundi wao wenye thamani zisijulikane kwa wengineo.
Bidhaa maridadi za kioo za Wavenisi zilichangia sana kuzidisha umaarufu wa kioo, lakini kutengeneza kioo haikuwa kazi rahisi kamwe. Kitabu A Short History of Glass hurejezea kichapo cha 1713 ambacho hufafanua hivi vile ilivyofanana: “Wanaume husimama daima wakiwa nusu-uchi katika halihewa yenye kung’ang’anaza kwa baridi karibu na tanuri zenye joto jingi . . . Wang’ang’amana kwa sababu mwili wao . . . umechomwa na kuharibiwa na joto la kupita kiasi.” Katika miaka ya baadaye wakata-kioo walilainisha kioo kwa kutumia gurudumu lizungukalo na poda za kusugulia.
Uvumbuzi wa Baadaye
Uingereza ilipata hadhi maalumu katika historia ya kioo. Mtengeneza kioo Mwingereza alihitimisha fomyula ya kutengeneza kioo cha risasi katika 1676. Ule mwongezo wa oksidi ya risasi ulitokeza kioo kizito ambacho kilikuwa thabiti, safi, na changavu.
Milki ya Uingereza ilikuwa katika upeo wayo wakati wa enzi ya Malkia Victoria, na kufikia wakati huu Uingereza ilikuwa pia mtokezaji mkuu wa kioo. Jambo lenye kutokeza hasa lilikuwa maonyesho makubwa ya bidhaa katika Crystal Palace katika 1851, wonyesho wa kwanza ulimwenguni, ambao ulivutia waonyeshaji bidhaa za kiviwanda na za kiufundi kutoka nchi zipatazo 90. Ingawa kioo kilitokeza sana katika hayo maonyesho, ilikuwa ni Crystal Palace yenyewe, ikiwa na kioo cha katikati chenye kimo cha meta 8.2, ambacho kilivuta uangalifu mkubwa. Karibu tani 400 za vipande vya kioo zilitumiwa kwa ajili ya kitu hiki kikubwa mno, ambacho kilikuwa na vipande 300,000 vya vioo vilivyotengenezwa kwa mkono.
Hata hivyo, ilikuwa ni katika Marekani kwamba badiliko kuu lililofuata katika kutengeneza kioo lilitukia. Hili lilikuwa kuhitimishwa kwa mashine ya kiufundi wa kutandaza kioo katika miaka ya 1820. Kitabu A Short History of Glass chasema hivi: “Kwenye mashine ya kutandaza, wanaume wawili ambao hawana uzoefu wa kazi wangeweza kutokeza mara nne vioo vingi kuliko kikoa cha wapuliza-kioo watatu au wanne waliozoezwa kazi.”
Mapema katika karne ya 20, mashine ya kupuliza chupa moja kwa moja ilihitimishwa katika Marekani. Katika 1926 kiwanda kimoja katika Pennsylvania kilitumia kidude ambacho moja kwa moja kilitokeza balbu 2,000 za umeme kwa muda wa dakika moja.
Wasanii na wabuni wengi wamevutiwa na yale wawezayo kufanya kiusanii na kioo. Hili limetokeza miundo ya kubuni kwa bidhaa za kioo na ubuni wa usanii zaidi katika kioo.
Kwa hakika kioo ni cha ajabu. Mbali na matumizi yacho yote ya nyumbani, ebu fikiria baadhi ya matumizi yacho mengine—katika Darubiniupeo ya Angani ya Hubble, katika lenzi za kamera, katika vinyuzi vya kuakisa vya mifumo ya kuwasiliana, na katika maabara ya kemia. Huenda kikawa chenye kuvunjika kwa urahisi, bali ni kinyumbufu na maridadi mno.
[Maelezo ya Chini]
a Kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Juu na Chini: The Corning Museum of Glass
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
The Corning Museum of Glass